Monday, February 15, 2010

Matatizo hospitali ya Ndolage yatafutiwe ufumbuzi wa kina

Na Arodia Peter
NDOLAGE, moja ya hospitali kongwe nchini zinazoongozwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kanda ya Magharibi, hivi sasa iko taabani kutokana na matatizo mbambali ikiwemo kupanda kwa gharama za matibabu pamoja na kukimbiwa na wataalamu wa fani mbalimbali.
Hospitali hii ambayo ilianzishwa na wafadhili kutoka Serikali ya Ujerumani Mwaka 1928 na baadaye kukabidhiwa kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Kanda ya Bukoba (Kagera), hivi sasa imedorola kiasi cha kutisha na kama hakuna mipango ya dharula ya kuinusuru hospitali hiyo, basi wananchi walio wengi watakufa kutokana na kukosa fedha za matibabu.
Ndolage ni moja ya hospitali za Taasisi za Dini zinazopata ruzuku ya serikali ili kutoa huduma ya matibabu kwa bei nafuu kwa wananchi wa vijijini ambao uwezo wao wa kifedha ni mdogo mno.
Kutokana na kupanda kwa gharama za matibabu, baadhi ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo hutoroka kabla ya kupona kwa kuogopa gharama za matibabu ambazo kwa ujumla ziko juu kupindukia.
Kutokana na tabia hiyo ya kutoroka inayodaiwa kukithiri, hospitali hiyo imeweka masharti mapya kwa wagonjwa wanaotakiwa kulazwa. Masharti hayo ni pamoja na kulipia kabla gharama za dawa atakazotumia mgonjwa muda wote atakaokuwa amelazwa. Hizi ni mbali na gharama za vipimo vingine pamoja na kitanda ambacho kinalipiwa kila siku shilingi 2000.
Hali ni mbaya zaidi kwa wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo, kwani hutakiwa kulipia kwanza gharama zote za dawa atakazokuwa akitumia wakati wote akiwa kitandani. Lakini pia mgonjwa anatakiwa kulipia shilingi elfu mbili kila siku kwa ajili ya kitanda alichokilalia. Hii ni mbali na gharama nyingine za vipimo na hata kuongezewa damu ikibidi.
Kwa matibabu yanayohitaji upasuaji, mgonjwa anatakiwa kuwa na kati ya shilingi 40,000 kwa upasuaji mdogo na ule mkubwa unagharimu kati ya shilingi Elfu 60 hadi Laki Tatu.
Aidha, hospitali hiyo imeondoa utaratibu wa kuwahudumia bila malipo watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na akina mama wajawazito kama taratibu za serikali zinavyoelekeza. Uchunguzi unaonyesha kuwa viwango vinavyotozwa kwa wajawazito wanaojifungua kawaida ni shilingi elfu 15 na 25 wanaojifungua kwa njia ya upasuaji.
Kutokana na hali ya umasikini wa wananchi walio wengi katika maeneo mengi ya Wilaya ya Muleba, wajawazito wanakwenda kujifungulia kwa wakunga wa jadi ambao hawana utaalam wa kutosha katika masuala ya uzazi, ambapo baadhi yao wanadaiwa kufia kwa wakunga hao huko vijijini.
Wakizungumza kwa kupokezana wananchi wachache waliokutwa wamefika kuwajulia hali ndugu zao waliolazwa hospitalini hapo, walisema licha ya kupanda kwa gharama za matibabu, uongozi wa hospitali hiyo hauna huruma na masikini, kwamba watu wasiokuwa na uwezo wanafia majumbani kwa kukosa fedha za kujitibu.
Retisia Aporinary , mkazi wa kijiji cha Itongo moja ya vijiji vilivyo karibu na hospitali hiyo alisema mtoto wake aitwaye Patianus Aporinary alinusurika kufa baada ya
wahudumu wa hospitali hiyo kumtelekeza eneo la mapokezi kutokana na familia yake kushindwa kulipa shilingi elfu 45 za matibabu.
“Mtoto wangu ameokolewa na msamaria mwema aliyemkuta mapokezi amezirai bila huduma yoyote, familia nzima tulihangaika kutafuta kiasi hicho cha fedha bila mfanikio, tulibaki mapokezi zaidi ya saa 4 bila mgonjwa wetu kupokelewa. Alikuja mama mmoja alipoona hali ya mwanangu aliamua kutusaidia kwa kutupatia kiasi hicho cha fedha, ndipo tulipohudumiwa,” alisema mama huyo na kuongeza kuwa .
Mtoto wake alianguka na kupoteza fahamu kutoka juu ya mti aliokuwa amepanda akitafuta kuni na majani kwa ajili ya chakula cha mifugo. Alisema licha ya kupoteza fahamu pia alikuwa na majeraha sehemu za kichwani na mgongoni ambapo alikuwa akivuja damu nyingi mfululizo.
Kuna malalamiko mengi ya wagonjwa wanaotibiwa kwa kutumia kadi maalum za Bima ya afya, kwamba wanapokwenda hospitalini hapo huchelewa kupatiwa huduma kwa sababu hawatoi pesa taslimu, kwamba wahudumu hutangulia kuwahudumia wale tu wenye pesa kwakuwa malipo ya bima ya afya yanachukua muda mrefu.
“Sisi wenye bima ya afya hatupewi huduma kama wale wanaokuja na pesa taslim, Kwakuwa malipo yetu yanapitia katika mlolongo mrefu wa kiserikali, kwa hiyo wahudumu wanatupita tu na kuwapa vipaumbele wale tu wenye pesa taslimu” alilalamika mwalimu wa Shule ya Msingi Kagabiro.
Licha ya viwango hivyo vikubwa vya matibabu, huduma katika hospitali hiyo zimedorola kutokana na madaktari, wauguzi na wataalamu wa vitengo vingine kuikimbia kutokana na uongozi wa hospitali hiyo kushindwa kuwalipa viwango vya mishahara vilivyowekwa na serikali.
Aidha, inadaiwa pia kuwepo kwa matabaka kati ya wafanyakazi wanaolipwa kutokana na ruzuku ya serikali na wale ambao wanalipwa na hospitali. Kwamba wale wanaolipwa na hospitali wanapata mishahara mikubwa tena kwa wakati muafaka, lakini wanaolipwa na hospitali mishahara yao ni midogo na inachelewa sana.
Wakati mwingine tunapata mishahara katikati ya mwezi mwingine, mshahara wa Mwezi wa Septemba 11 tumeupata siku chache kabla ya sikukuu ya Krismas, hayo ndiyo maisha yetu hapa Ndolage,” walisema baadhi ya wauguzi.
Taarifa za kukimbiwa na wafanyakazi tayari zilithibitishwa na Katibu wa hospitali hiyo Sospeter Kabululu, ambaye alisema wataalam wake wanakimbia kutokana na mishahara kuwa midogo ikilinganishwa na ile ya serikali na taasisi nyingine..
Kabululu alitaja sababu nyingine kuwa ni kutokana na baadhi ya Taasisi za Dini kutokuwa na utaratibu wa kuwalipia wafanyaksi wake malipo ya uzeeni (Pensheni) kwenye mifuko ya hifadhi za jamii kama (NSSF) kama yalivyo mashirika na taasisi nyingine nchini. Kwamba hali hiyo imechangia wataalam wengi kuondoka kwani wanahitaji kuwa na uhakika wa maisha ya uzeeni pindi watakapo staafu kazi zao.
Mganga Mkuu Mstaafu wa Hospitali hiyo Dr. Kalisti Twagilayesu anayefahamika na wengi kama ‘ Dr.Twagila’ anasema kinachoikuta hospitali hiyo kwa sasa ni matokeo ya kutegemea wafadhili wa nje kuhudumia wanachi kwa muda wote tangu ianzishwe miaka mingi iliyopita.
Alisema kudorola kwa huduma pamoja na wataalamu wengi kuikimbia hospitali hiyo kunapaswa kuangaliwa kwa jicho la kipekee na serikali pamoja na taasisi zinazohusika ili kuokoa maisha ya wanajamii wanaoitegemea hospitali hiyo kupata huduma za matibabu kwa kutegemea wataalam na huduma nafuu.
Dr. Twagilayesu ambaye alikuwa mtumishi wa hospitali hiyo hadi kustaafu kwake miaka 19 iliyopita, alisema suala la wafanyakazi wa hospitali hiyo kukosa malipo ya uzeeni kupitia Mifuko ya kijamii inayoeleweka ni tatizo kubwa na lisipoangaliwa kwa umakini basi hospitali hiyo itaendelea kukimbiwa na wataalam kila kukicha.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Muleba Dr. Fidelis Mabula alipoulizwa kuhusu kupanda kwa gharama za matibabu hospitalini hapo, alikiri kuzifahamu taarifa hizo na kusema kuwa mara kwa mara amekuwa ukiushauri uongozi wa hospitali kurekebisha viwango hivyo vya gharama za matibabu bila mafaniko.
Dr. Mabula ambaye pia aliwahi kuwa Mganga Mkuu wa hospitali ya Ndolage miaka ya nyuma, aliulaumu uongozi wa hospitali hiyo kwa kupandisha mno viwango na gharama za matibabu huku wakijua jamii inayowazunguka ni masikini na hawawezi kwa namna yoyote kumudu gharama hizo.
Mabula alisema licha ya Serikali kuipatia mgao wa fedha na mishahara kwa baadhi ya madaktari na wauguzi, lakini hospitali hiyo imeshindwa kujirekebisha jambo ambalo linazidi kuiathiri jamii katika suala zima la haki ya kupata matibabu.
“Hiyo hospitali inapata ruzuku ya serikali kupitia mfuko maalum unaojulikana kama ‘Busket Fund’ na hii ni mbali na kulipiwa mishahara kwa baadhi ya madaktari na wauguzi, bado pia wanapata fedha zinazotokana na Bima za afya za wafanyakazi lakini sijui tatizo liko wapi” alihoji na kuongeza
“Hebu waandishi tusaidieni, mimi nimekwishaueleza uongozi wa Dayosisi mara nyingi wapitie viwango hivyo vya gharama, na si kweli kwamba hawapati fedha, wanapata kama nilivyokueleza ila wanataka kupata zaidi, lakini kwa hali ilivyo wanawaumiza wananchi ambao wengi ni masikini” alibainisha. Hata hivyo Mabulla hakutaja kiwango halisi kinachotolewa na Busket Fund kwa mwaka kwa hospitali hiyo.
Kwa upande wake alipoulizwa nafasi ya serikali na hata wafadhili wengine wa ndani na nje ya nchi katika hospitali hiyo ni ipi, Kabululu alisema kuwa wafadhili wapo lakini ufadhili wao ni katika baadhi ya miradi kama vile Ukimwi na huduma kwa watu wenye magonjwa sugu wanaougulia majumbani ikiwemo kansa.
Kiongozi huyo wa hospitali alisema kuna Mfuko mwingine unaojulikana kama Poor Penshen Fund unaofadhiliwa na Taasisi ya United Evangelical Mission (UEM) ya Marekani maalum kwa ajili ya kuchangia gharama za matibabu kwa watu ambao ni masikini sana ili wapate matibabu bure. Kwamba taasisi hiyo inachangia jumla ya Euro 8000 kwa mwaka katika hospitali hiyo.
Aidha, Kabululu alisema kuna miradi iliyoanza mwaka jana ambapo wafadhili kutoka Denmark wanachangia miradi miwili ijulikanayo kama ‘Delivary Fund’ ambao unachangia asilimia 40 tu katika gharama za matibabu ya akina mama wajawazito, na asilimia 60 inayobaki inachangiwa na akina mama wenyewe pamoja na hospitali.
Mradi mwingine aliutaja kuwa unaitwa ‘fifty fifty’ ambapo sehemu ya msaada huo ni kwa ajili ya kulipa mishahara ya wafanyakazi na nusu iliyobaki ni kwa ajili ya kununulia madawa. Hata hivyo Kabululu alisema kiasi kinachotolewa katika miradi hiyo miwili ni shilingi milioni 30 kwa mwaka. Na kuongeza kuwa licha ya misaada hiyo bado hospitali inaendelea kupata hasara.
Naye Askofu Mkuu Mstaafu wa KKKT nchini Dr. Samson Mushemba akizungumzia madai ya kudorola kwa huduma na kupanda kwa gharama za matibabu hospitalini hapo alikuwa na haya ya kusema.
“Mambo mengi ya Ndolage hivi sasa siyajui sawa sawa kwa sababu nimestaafu, Lakini uongozi wa dayosisi unaweza kukupa majibu sahihi, isipokuwa nina taarifa za kuondoka kwa wafanyakazi kwa sababu ya kulipwa mishahara midogo” alisema na kuongeza
“Lakini hili la gharama kubwa za matibabu bila shaka viongozi wanaongeza ili kuweza kuziba pengo kubwa lililokuwa likitolewa na wafadhili kwa muda mrefu, na pia hili la udhaifu wa uongozi wa hospitali nitakwenda huko Ndolage nione udhaifu uliopo.”
Hata hivyo kiongozi huyo aliushauri uongozi wa Dayosisi kutafuta mbinu za kufidia gharama za matibabu kwa kutafuta wafadhili ili iweze kuhudumia jamii ambayo wengi ni masikini.
“Watu wetu ni masikini, hizi gharama hawawezi kuzimudu, nashauri uongozi wa
Gharama hizi zimethibitishwa na Katibu wa Hospitali hiyo Sospeter Kabululu wakati wa mahojiano na mwandishi wa makala haya.
Kama tulivyosema awali, kwa ujumla huduma katika hospitali hii ni mbaya, na kama hatua za haraka hazitachukuliwa na KKKT Kanda ya Kaskazini Magharibi pamoja na Serikali basi wananchi wanaotegemea huduma ya matibabu hospitalini hapo wataangamia.
Ikumbukwe kwamba wananchi wanaoishi kuzunguka eneo hili pamoja na Mkoa wa Kagera kwa ujumla wana umasikini wa kipato unaotokana na zao tegemeo pekee la biashara (Kahawa) kushuka bei katika soko la dunia. Wakati huo hakuna hospitali nyingine mbadala kwa wananchi hao.
Hospitali ya Wilaya inayotegemewa na wilaya nzima ya Muleba ni Rubya ambayo nayo ni ya Kanisa Katholiki. Hata hivyo kutokana na jiografia ya nchi yetu, wananchi ambao awali walikuwa wakiitegemea Ndolage wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa 50 kufuata matibabu ya gharama nafuu kwenye hospitali ya Rubya.
Kutokana na umbali huo mrefu, wananchi ambao ndugu zao wanafia kwenye hospitali ya Rubya wanalazimika kubeba maiti kwenye baiskeli kwa kilometa tajwa hapo juu. Kwani kama wamefuata matibabu ya bei nafuu watawezaje kumudu gharama za kusafifirisha maiti kwa gari?
Hospitali ya Ndolage ilianzishwa Mwaka 1928 katika Kijiji cha Bushagala, Kata na tarafa ya Kamachumu Wilaya ya Muleba mkoani Kagera ikiwa chini ya Mjerumani aliyefahamika kwa jina la Fredrich Kroeber.
Sababu za kujengwa hospitali katika eneo hilo, inasemwa kuwa ni kutokana na kuwepo kwa maporomoko makali ya maji kutoka mto Bugonzi kwa ajili ya kuzalisha umeme wa uhakika kwa matumizi ya hospitali. Hadi sasa umeme huo bado unatumika licha ya kuwepo ule wa Tanesco ambao ni wa gharama kubwa.
Tangu kuanzishwa kwake, hospitali ilikuwa ikipata misaada na wataalam kutoka Mission ya Kilutheri ya Ujerumani. Mwaka 1939 Kroeber alirudi kwao Ujerumani kwa ajili ya kusomesha watoto wake, ambapo wakati huo hapa nchini shule hazikuwepo.
Hata hivyo, hakuweza kurudi kutokana na kuwepo Vita ya Pili ya Dunia na nchi hiyo ikiwa ndiyo kinara wa vita hiyo.
Baadaye Ndolage ilichukuliwa na Mision ya Uingereza kabla ya kukabidhiwa kwa Church of Sweden Mission ya (Sweden) ambao waliendelea kwa muda mrefu hadi wakati wa uhuru Mwaka 1961. Tangu wakati huo wameendelea na ufadhili ambapo matibabu na huduma nyingine zilipatikana kwa bei nafuu sana.
Kutokana na umuhimu wa hospitali hiyo, ndiyo maana serikali ilipoamua kuzipatia ruzuku hospitali zinazomilikiwa na Taasisi za dini, Ndolage ilikuwa mojawapo, lengo likiwa ni kuzisaidia hospitali za vijijini kutoa huduma bora ambako serikali haina hospitali zake.
Katika miaka ya karibuni wafadhili wengi wanadaiwa kujitoa na kubakia wachache ambao hata hivyo kutokana na gharama zilivyo, ni vigumu kuamini kama kuna ufadhili wowote ama wa serikali au wafadhili kutoka nje kama Katibu wa hospitali anavyosema.
Hapa kuna maswali mengi ya kujiuliza, ni kwa vipi hospitali hiyo imebadilika na kuwa ya kulipia (Private) moja kwa moja tofauti na awali. Je wahusika ambao ni uongozi wa KKKT Mkoa wa Kagera wanakubali hali hii iendelee? Na je nafasi ya ruzuku ya serikali kwa hospitali hii inadhihirika wapi?
Mwandishi anapatikana kwa simu: 0755-456270,kemmyp2@yahoo.com

No comments: