Monday, July 26, 2010

KIPINDU PINDU CHA MWENDAWAZIMU!

WILAYA ya Temeke, Mkoani Dar es Salaam, imesikika mara nyingi ikikumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu. Watu mbalimbali wamepoteza maisha na serikali imetumia fedha nyingi kutibu wagonjwa.
Mbali na kipindupindu, ajali za barabarani zinazotokea hasa mijini, zinashika kasi ambapo maisha ya watu yaameangamia kila siku. Na siku hizi basi, ajali za pikipiki nazo zinatishia maisha ya watu kama Simba ndani ya Mbuga ya Serengeti.
Hata hivyo, katika matukio yote mawili, ya ugonjwa wa kipindupindu na ajali za barabrani, wanaokumbwa na janga hilo ni watu wazima wenye akili timamu. Wanaugua wasomi, wanagongwa wenye viungo kamili;macho na miguu isiyo na dosari.
Ajabu ni kwamba sio rahisi kumkuta mtu mwenye ugonjwa wa akili- mwendawazimu, akiwa mmoja wa wagonjwa wa kipindupindu ama aliyegongwa na gari!
Tunajua mazingira yanayomzunguka mwendawazimu (mgonjwa wa akili). Kwake usafi ni bidhaa adimu sana. Hafui, haogi kila siku na anachokula ni kile kilichotupwa jalalani, akishirikiana na inzi na wadudu wengine. Kumbe, kwa mazingira hayo, tungetarajia awe wa kwanza kukumbwa na kipindupindu. Kinyume chake, katika kundi la wanaougua, huyu hayumo!
Hivyo hivyo katika ajali, kugongwa kwa mwenzawazimu, ama lugha ya heshima, mgonjwa wa akili ni jambo la nadra sana. Badala yake wanaogongwa na kugonga ni watu wenye akili njema kabisa.
Swali la kujiuliza ni je, hawa hawasikiki kwa sababu ni wachache? Ama ni kwa vile hawana mtu wa kufuatilia maisha yao kwa kuwa wanahesabika kama waliotupwa? Lakini hata katika hilo, kwa nini tusisikie walao mara moja moja?
Kama watu wasomi, wanaoishi mijini kuliko endelea na wanaojua maana ya afya; namna ya kuwa waangalifu katika uendeshaji wa magari na matumizi ya barabara wanafanya mambo yanayohatarisha maisha yao, kuna sababu gani ya kutumia neema ya uzima na akili kuwadharau wagonjwa wa akili –wendawazimu?

No comments: