Monday, July 26, 2010

MAISHA BORA!!!!!!


‘Maisha bora hayatapatikana kwa kushinda vijiweni’
Na Lilian Timbuka
WAKATI kumekuwa na mjadala juu ya kufanikiwa au kushindwa kwa kaulimbiu ya 'maisha bora kwa kila Mtanzania', iliyotumika kumnadi Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa kampeni mwaka 2005, kiongozi huyo amesema kuwa kauli hiyo haiwezi kutimia iwapo Watanzania wanabweteka na kushinda vijiweni bila kufanya kazi.
Rais Kikwete aliyasema hayo hivi karibuni Jijini Dar es Salaam wakati akizindua Kitabu cha Maadili kwa Kizazi Kipya, kilichoandikwa na Askofu Sylvester Gamanywa wa Wapo Mission (FPCT), chini ya Mpango wa Kitaifa wa Maadili kwa Kizazi Kipya.
Rais Kikwete alipokuwa akizungumza, alitumia mfano wa watu wanaoshinda wakicheza mchezo wa 'pool', bila kufanya kazi yoyote ile ya maana ya kuweza kuwaingizia kipato kwa siku, lakini mwisho wa siku wanadai kuwa Serikali imeshindwa kuwajengea mazingira ya kuondokana na umaskini ili hali wao hawajishughulishi. Aliwataka Watanzania kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.
Rais Kikwete alisema maadili ya jamii nchini yamemomonyoka kwa kiasi kikubwa, hali inayohitaji ushirikiano katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.
Hata hivyo, kwa muda mrefu sasa, kumekuwepo na mjadala juu ya kufanikiwa au kushindwa kwa kaulimbiu hiyo, ambapo wakati upande wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni chama tawala, wamekuwa wakiitetea kuwa imefanikiwa.
Lakini wachambuzi wa masuala ya siasa na uchumi nchini wamekuwa wakisema kuwa imeshindikana, kwani umaskini umezidi kuongezeka miongoni mwa Watanzania tofauti na miaka mitano iliyopita.
"Baba Askofu Gamanywa, suala hili la mmomonyoko wa maadili ni tatizo kubwa, linahitaji ushirikiano kupata ufumbuzi wake... ni tatizo la wengi duniani sasa, si Tanzania tu, halina mipaka ya nchi, dini, kabila, rangi wala familia... mmefanya kitu kizuri kubuni mpango madhubuti wa ufumbuzi. Hapa nchini tatizo hilo ni kubwa ndiyo maana tunakabiliwa na matatizo ya rushwa, ubadhirifu, wizi, mauaji, ulevi wa pombe, dawa za kulevya, ubakaji, mavazi yasiyofaa, haya yote yanaelezea ukubwa wa tatizo... linakuwa kubwa zaidi likichangiwa na dunia ya leo ya intaneti, ni vita ya wote bila kuchoka," alisema Rais Kikwete na kuongeza;"Baba Askofu Mkuu Gamanywa, katika kitabu chako hiki mbali na kuzungumzia maadili, pia kuna suala la mchakato wa kuwamilikisha watu uchumi, hili nafikiri linakwenda sambamba na ile kaulimbiu ya maisha bora kwa kila Mtanzania...maisha bora hayaji ukiwa umekaa unacheza pool, lazima ufanye kazi kwa bidii na maarifa,” alisisitiza Rais.
Mapema akizungumzia kitabu hicho kwa ufupi kabla ya kuzinduliwa, Askofu Gamanywa alisema kuwa kitabu hicho kinazungumzia masuala mbalimbali ya mmomonyoko wa maadili nchini katika awamu zote za serikali, tangu kupata uhuru, kikichambua falsafa yake, chanzo cha mmomonyoko huo nchini, namna ya kuinua uongozi wa kizazi kipya na mchakato wa kumilikisha uchumi kwa vijana.
"Mheshimiwa Rais tumeamua kujikita katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo la mmomonyoko wa maadili nchini badala ya kuendelea kulalalamika, mpango huu wa kitaifa wa maadili kwa kizazi kipya umelenga vijana kuanzia miaka 12 mpaka 35. Kitabu utakachozindua kimejikita katika maeneo kadhaa ikiwemo mkakati wa kurejesha maadili, kunoa vipawa vya uongozi kwa kizazi kipya, kumilikisha uchumi kwa kizazi kipya, maana umaskini nao ni chanzo kikubwa cha mmomonyoko wa maadili.”
Askofu Gamanywa alisema wangependa ifakapo Mwaka 2020, kizazi kipya kiachane na lugha ya “sisi ni maskini”.
Alisema ukuaji wa uchumi ni jambo la muhimu katika kila nchi kwa sababu ndio nguzo kuu ya maendeleo kwa kuanzia na ngazi ya familia mpaka Taifa. “Ndiyo maana tumejiandaa kupata maeneo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili vijana wapate kazi," alisema Askofu Gamanywa.
Akimuondoa hofu Rais, Askofu Gamanywa alisema kuwa viongozi wa Dini hawapaswi kuunga mkono vyama wakati wa kampeni, bali watafanya kazi na kukiheshimu chama kitakachoshinda.
"Viongozi wa dini hatuna vyama, vyama vyote ni vya kwetu, lakini tutakiheshimu na kufanya kazi na chama kitakachoshinda uchaguzi," alifafanua Gamanywa.

No comments: