Monday, October 11, 2010

Dini bila Imani

BINADAMU anajiangamiza mwenyewe kwa: siasa zisizo na kanuni, starehe bila dhamiri, utajiri bila kufanya kazi, maarifa bila tabia nzuri, biashara bila maadili, sayansi bila utu, dini bila imani na upendo bila sadaka. Haya ndiyo mambo yanayo tuangamiza.
Haya ni mafundisho yenye uzito wa pekee kutoka kwa muasisi wa ukombozi wa taifa la India, kutoka kwa utawala wa Waingereza, Mahatma Gandhi aliyeuawa na mtu mwenye siasa kali huko New Delhi mwaka 1948.
Mafundisho haya ni ya kweli na yanafaa hata katika siku zetu hizi ambamo kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili, kuna ubinafsi na maisha ya kiroho ambayo hayajajengwa juu ya misingi imara.
Kanuni nane ambazo Gandhi anatufundisha, zinafaa kwa mtu binafsi na kwa jamii nzima pia.
Siasa ambayo haijikiti katika mizizi ya maadili, bali imejengwa juu ya misingi ya maslahi binafsi na udanganyifu, inawafanya hata watu binafsi kuwa fedhuli. Starehe isiyo na kipimo, inayotangazwa mara nyingi kwa kupitia vyombo vya habari, inamfanya mtu kukosa adabu.
Utajiri mkubwa ambao mtu ameupata kwa njia zisizo halali, unaoambatana na ubadhirifu wa kutisha, vinafanya fedha kuwa ndama wa dhahabu, na hivyo kuwafanya watu wawe tayari kutoa sadaka yoyote ile alimradi tu wapate fedha. Kiburi na dharau katika maarifa vinafanya dhamiri kuwa tupu ama ipambwe kwa upuuzi na porojo. Uchumi usiojali kanuni zozote za maadili ama mshikamano wowote ule, unakuwa mtambo wa kuwagandamiza wanyonge, kuwanufaisha wenye nguvu na kuwapeleka watu katika ubinafsi , dhuluma na hali ya kutojali shida za watu wengine. Sayansi ikichukuliwa kama mwamuzi wa mwisho wa kila kitu, inaharibu uhai inaangamiza ulimwengu inaendelea kufuata njia za ajabu bila kujali kwamba ina mipaka yake na kwamba inabidi ifuate mpango wa Mungu. Hata dini ikichukuliwa kama ibada za mapokeo tu ama siasa kali, ama mkusanyiko tu wa watu, inapoteza sifa yake muhimu kabisa ya imani na mapendo. Mapendo ambayo kielelezo chake cha juu kabisa ni kuutoa uhai kwa ajili ya rafiki (Yn 15:13).



Daladala za Tanga tiketi vipi?

Nisemayo sija-zua, ni kweli nime-tafiti
Mwanzo mimi nilijua, kakauka kwa ku-nyuti
Sasa nimesha tambua, wote hawana tikiti
Daladala Tanga vipi, mbona hamna tikiti?

Kote nimesha chungua, hakunayo tofauti
Nauli waki-chukua, sarafu na au noti
Usidhani wa-dengua, kukupati tikiti
Daladala Tanga vipi, mbona hamna tikiti?

SUMATRA wanalijua, kuwa hazipo tikiti
Hawajafanya hatua, japo wanayo ripoti
Kwa hili wana-rembua, hawaja-valia njuti
Daladala Tanga vipi, mbona hamna tikiti?

Ndiyo maana hupangua, nauli kwa kila ruti
Asubuhi inakua, mia tatu kila siti
Jioni inapungua, hiki kizungu-mkuti
Daladala Tanga vipi, mbona hamna tikiti?

Mchana wana amua, kui-jaribu bahati
Noti ukiwapa hua, chenji wakupiga buti
Ni vigumu kutambua, ipi nauli ya dhati?
Daladala Tanga vipi, mbona tikiti hamna?

Ni jiji limesha kua, na sheria madhubuti
Mambo msije chagua, ya kuyapa u-dhibiti
Hili jambo lita-zua, mambo mbele na kahati
Daladala Tanga vipi, mbona tikiti hamna?

Abiria kutambua, nauliye ithibati
Konda anapo pangua, hui-haribu bajeti
Aweza mtu ugua, sababu ya ndogo shoti
Daladala Tanga vipi, mbona tikiti hamna?

Ambao wana dengua, kuyafwata masharti
Kiapo wana tangua, hima wapigwe penalti
Sheria wataijua, litakuwa ni parati
Daladala Tanga vipi, mbona tikiti hamna?

Raphael Meshack Mwamwejo,
Kiwalani-D’salaam,
0765/0713 937378,
adammwambapa@ymail.com.


Shirika la Roho Mtakatifu matumaini ya imani Bagamoyo
· Kuwa mwenyeji Mkutano Mkuu wa dunia
· Shule za Marian, Epiphany zachangia mil.120 za maandalizi

Na Dalphina Rubyema
MIONGONI mwa maeneo yanayorudisha kwa kasi hadhi yake ambayo ilikuwa imeonyesha dalili za kupotea, ni Mji wa Bagamoyo ambao umebeba historia ya Tanzania katika nyanja tofauti.
Ni eneo hili la Bagamoyo ilipoanzia historia ya Ukristo Ukatoliki na kupenya maeneo kadhaa wa kadha nchini, huku Kanisa la kwanza likijengwa Afrika katika eneo hilo la Bagamoyo, likiendelea kuwa kivutio kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.
Katika kulinda historia na heshima ya eneo hili, Mapadri wa Shirika la Roho Mtakatifu wamekuwa mstari wa mbele kulienzi eneo hili kwa kufanya mambo mbalimbali ya kiroho na kijamii.
Miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na kulitunza kwa kulifanyia ukarabati wa mara kwa mara Kanisa la kwanza barani Afrika ambalo limejengwa hapo Bagamoyo, kutunza makaburi ya kihistoria na makumbusho ya nyaraka mbalimbali za Kanisa Katoliki pamoja na kueneza Injili katika sehemu mbalimbali nje na ndani ya nchi.
Hata hivyo, juhudi za Mapadri hawa wa Shirika la Roho Mtakatifu lenye Makao yake Makuu jimboni Arusha, haziishii tu kwenye huduma za kiroho, bali pia zimeweka mizizi katika utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu.
Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Marian, ni miongoni mwa shule zinazoendeshwa chini ya usimamizi wa shirika hilo, shule ambayo imekuwa tishio kitaaluma kwa kuwa miongoni mwa shule tatu bora nchini.
Shule hii ya Wasichana ya Marian ambayo ina wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, kwa sasa imekomaa na kuzaa shule ya Wavulana inayojulikana kwa jina la Marian pia, yenye kidato cha kwanza hadi cha pili, achilia mbali ile Shule ya Msingi ya Epiphany yenye mchanganyiko wa wanafunzi wasichana na wavulana wapatao 500, wanaosoma kuanzia shule ya awali hadi darasa la saba.
Katika kuhakikisha wanamuenzi kwa vitendo Mwanzilishi wa Shirika hilo la Roho Mtakatifu Padri Claude Francois, aliyezaliwa Februari 26 mwaka 1679 na kufariki dunia Oktoba 2 mwaka 1709, wazazi na wafaunzi wanaosomoa kwenye shule hizo, walijumuika na mapadri wa Shirika hilo katika kuadhimisha miaka 300 tangu kufariki kwa mwanzilishi huyo.
Tukio hilo la aina yake lilialoacha simulizi mjini Bagamoyo na maeneo jirani, lilifanyika Oktoba 2 mwaka huu kwenye eneo la Msalabani, ambapo wanafunzi wote kutoka shule hizo tatu, mbali na kuelezea wadhifa wa mwanzilishi huyo, lakini pia walionesha michezo mbalimbali katika kumuenzi.
Tukio hilo lililoanza majira ya saa tisa alfajiri, lilianza na mbio ndefu kutoka Kerege ilipo shule ya wavulana hadi Kosovo, kabla ya kuanza matembezi ya hisani yaliyowashirikisha wanafunzi, walimu na watumishi wengine pamoja na Mapadri na baadhi ya wazazi, yaliyoanza majira ya saa 2.00 - 3.00 asubuhi kutoka Kosovo hadi eneo hilo la Msalabani.
Baada ya kufika Msalabani, wanafunzi hao pasipo kuonesha uchovu, walishiriki katika michezo ikiwemo ngoma, sarakasi, ngonjera, mashairi, muziki na maigizo na hatimaye shamrashamra hizo kuhitimishwa na Ibada ya Misa Takatifu iliyoanza majira ya saa 11.30 jioni na kuongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardina Pengo.
Ilikuwa majira ya saa 6.30 mchana ulipoanza mchakato wa harambee ya uchagiaji wa pesa kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa Kidunia wa Shirika hilo la Roho Mtakatifu, unaotarajiwa kufanyika nchini mwaka 2012.
Mkuu wa Shirika la Mapadri wa Roho Mtakatifu Kanda ya Tanzania, Padri Joseph Shio, anasema, katika mkutano Mkuu huo ambao hufanyika kila baada ya miaka nane, shirika lake linatarajia kupokea takribani watu wapatao 120 kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni
Anasema, huu ni ugeni mkubwa na kwamba, shirika linahitaji si tu mchango wa sala, bali pia mchangowa fedha na vitu vingine ili kuwezesha shirika kufanikisha mkutano Mkuu huo unaotarajiwa kufanyika katika eneo hilo la Bagamoyo.
Katika kuunga mkono maandalizi na hatimaye ufanisi wa mkutano huo, Mkurugenzi wa Shule za Marian na Epiphany, Padri Valentino Bayo, anasema kwa kushirikiana na wanafunzi na wazazi, shule zake zimeona umuhimu wa mkutano huu, hivyo kufikia muafaka wa kuchangia sehemu ya gharama.
Anasema, kila shule imejiwekea utaratibu wake katika kufanikisha lengo hilo na kwamba, wanaosimamia zoezi la ukusanyaji wa michango, ni walimu na kamati za shule husika.
Katika kuudhihirishia umati huo kwamba Padri Bayo yupo sahihi, Mwenyekiti wa Kamati ya Wazazi Shule ya Wavulana Marian, Bw. David Luago, hakusita kusimama mbele na kutamka bayana kuwa katika tukio hilo linalozidi kuifanya Bagamoyo izidi kufahamika zaidi katika anga za kidunia, shule yake inachangia kiasi cha shilingi Milioni 60.5.
“Sisi wazazi wa watoto wanaosoma kwenye shule ya Wavulana ya Marian, tulikaa hivi karibuni Msimbazi na kuamua kuchangia shilingi milioni sitini na laki tano,” anasema Bw. Luago.

Anabainisha kuwa, hadi sasa zaidi ya shilingi milioni 22 zimeishachangwa na kukabidhiwa kwa uongozi wa shule na kuahidi kwamba, kiasi cha takribani shilingi milioni 37 kilichobaki, kinatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa Novemba mwaka huu.
Kwa upande wa Shule ya Wasicha Marian, hawa waliahidi kuchangia kiasi cha shilingi milioni 36 ili kufanikisha mkutano huo na kama sehemu ya kutekeleza ahadi yao, waliandaa mnada wa vitu mbalimbali ambapo kivutio cha aina yake ilikuwa ni picha ya shule ambayo ilitengenezwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia magazeti na vipande vya bati, ambayo katika mnada huo ilinunuliwa kwa shilingi 780,000.
Shule ya Msingi Epiphany pamoja na wanafunzi wake kuwa ni wenye umri mdogo ikilinganishwa na shule za Marian, lakini hawakubaki nyuma katika kuudhihirishia umati uliokuwa umekusanyika katika eneo la Msalabani wakiwemo, mapadri wanashirika, watawa wa kike na kiume, wazazi, walimu na watumishi wengine wa shule hizo, pia waliandaa mchoro maalum ulioonesha majengo na mazingira ya shule yao, mchoro ulionadiwa na hatimaye kuuzwa kwa shilingi 1,577,500.
Mbali na hilo, wanafunzi wa shule hiyo pia waliandaa chakula maalum kwa ajili ya wazazi wao, ambapo kila mzazi alitakiwa kuchangia shilingi 50,000, mchango ambao ulikuwa ni walazima bila kujali kama mzazi, amekula ama hakula chakula hicho.
Kutokana na hilo, shule hiyo yenye wanafunzi 500 ilitarajia kupata shilingi Milioni 25 kutokana na chakula hicho cha hisani.
Hatua ya shule hizi kukubali kuchagia zaidi ya shilingi milioni 120 (kutoka kwenye shule zote tatu), kunaonesha ni jinsi gani wazazi wanakubali na kuunga mkono mchango unaotolewa na Mapadri hawa wa Shirika la Roho Mtakatifu nchini hususan katika Sekta ya elimu.
Bw. Fidelis Mgasha, ambaye ana watoto wawili wanaosoma Epiphany, anasema “Kwa vile nina watoto wawili kwenye shule hii, nimetoa shilingi 100,000 kwa ajili ya kuchangia mkutano huu na wala sioni shida kutoa kiasi hiki kwani najua nawekeza ili wanangu waweze kupata elimu bora si bora elimu kama baadhi ya shule zinavyofanya.”
Mzazi huyu ambaye alikuwa ni miongoni mwa wazazi waliohudhuria tukio hilo la aina yake kwa kuwakutanisha pamoja wazazi, walimu na wafanyakazi wa shule zote tatu , shule hiyo ipo juu si tu kitaaluma, lakini pia kwa upande wa malezi ya kiroho na kwamba, licha ya watoto wake hao kuhamia shuleni hapo kwa takribani miezi mitano, lakini wameonesha mabadiliko makubwa.
“Siwezi kusema walikuja hapa mbumbumbu, lakini ukweli ni kwamba wamebadilika mno kwani naona kitaaluma wanazidi kupaa tena sana achilia mbali kujisimamia wenyewe kusali sala pasipo kukumbushwa, na hata nidhamu yao sasa hivi iko juu...hakika ni shule nzuri sana acha tu tuchangie,” anasema Bw. Mgasha.
Ni kutokana na mchango wa shirika hili chini ya usimamizi wa Padri Bayo, historia ya Bagamoyo ambayo ilikuwa nyuma kielimu, sasa imebadilika na badala yake imekuwa na sifa ya pekee kwa kuwa na shule bora nchini, shule ya wasichana Marian, ambayo kwa mujibu wa Padri Bayo, zaidi ya wanafunzi 3,000, walijitokeza kufanya mtihani maalum kwa ajili ya kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.
Kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Mapadri wa Shirika la Roho Mtakatifu katika eneo hilo la Bagamoyo si tu kutakuwa kunaendeleza historia ya Kanisa kama eneo hilo kuwa kitovu cha Ukristo Ukatoliki, bali pia utazidi kuleta mbinu mpya za kufanya shule hizo zizidi kulinda kiwango chake cha ufaulu na nidhamu kwa ujumla.

Uhaba wa vyoo changamoto inayozikabili Manispaa

Na Hyasinta Kiwori
HAPA nchini, hasa sehemu za miji mikubwa ikiwamo Dar es Salaam na kwingineko, kumekuwapo na ongezeko la kasi ya uchafuzi wa mazingira.
Zaidi ni ile tabia ya wakazi wa miji hiyo kujisaidia ovyo, katika maeneo yasiyo rasmi kama vile kandokando ya barabara, kwenye bustani za miti, pembeni mwa bahari pamoja na kwenye baadhi ya kuta za majengo.
Tabia hii imeonekana kumea na kuota mizizi kiasi cha kuifanya miji hiyo ionekane kuwa ni yenye sura chafu kadri wahusika wa manispaa wanavyojitahidi kupambana na mazingira yake.
Katika uchunguzi wangu nilioufanya kwenye maeneo mengi, nimeweza kubaini kuwa, ukosekanaji wa vyoo vya kutosha vya umma katikati ya miji hiyo ni kati ya sababu zinazochangia uharibifu huo wa mazingira.
Miji mingi hapa nchini imekuwa ikikabiliwa na tatizo hilo la kukosekana kwa huduma ya vyoo vya umma, ambako kwa namna moja ama nyingine vingesaidia kulitatua.
Kutokana na hali ilivyo, inaonyesha dhahiri kuwa endapo kungekuwa na idadi kubwa ya vyoo vya umma, hasa katika maeneo ya katikati ya miji, uchafuzi huo wa mazingira ungeweza kupungua ama kwisha kabisa.
Nasema hivyo kwasababu, wakazi wengi wawapo katika shughuli zao mbalimbali za kujitafutia riziki, iwe mchana ama usiku huangaika mno kutafuta mahala pa kupata huduma hiyo muhimu ya vyoo.
Wakazi hao huangaika kutafuta huduma hiyo kutokana na kwamba vyoo vya umma ni vya kuhesabika ama kwa lugha nyepesi inayoweza kueleweka kwa urahisi ni vichache.
Imekuwa si jambo la kushangaza kabisa kutembea na kumaliza hata zaidi ya vitongoji vitatu vya mji, tena mji mkubwa bila kukuta japo choo kimoja tu cha umma.
Kwa sababu hiyo, wakazi wengi huishiwa na ustahimilivu wa haja zao na kujikuta wakisahau wajibu wao wa kutunza mazingira na kuamua kuchepuka mahala penye uficho na kujisaidia haja ndogo.
Hasa ikizingatiwa kila mmoja wetu anafahamu kuwa makali ya haja ya kutaka kujisaidia yanapoukabili mwili, maumivu yake hushinda hata ya kiu na njaa.
Katika hili, nafikiri iko haja ya manispaa husika kufanya jitihada za hali na mali na kuchukua hatua za haraka zinazoweza kuleta tija kwa wakazi, mazingira yenyewe pamoja na taifa zima kwa ujumla.
Jitihada hizo si nyingine bali ni kuhakikisha kuanza ujenzi wa vyoo katika maeneo yao, kwa nguvu na kasi ya hali ya juu kama harakati za kujikomboa kutoka katika uchafuzi huu unaoitia aibu nchi.
Nimeamua kuandika kwa sababu, uhaba huu wa vyoo ni kilio kinachosumbua wananchi wenye nia safi ya mapinduzi ya kimazingira katika taifa letu.
Zaidi ya yote hayo, kilio changu hiki napenda zaidi kiwafikie wakuu wa mikoa wote nchini pamoja na mameya katika manispaa zetu. Si tu kukisikia na kukitupilia mbali kilio hiki, bali wakifanyie kazi kama sehemu ya majukumu yao na kwa manufaa yetu sisi ambao ndio wana mazingira wa kwanza katika maeneo yetu.

No comments: