Friday, November 26, 2010



Naibu waziri wa Viwanda na Biashara ambaye ni Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu akiangalia moja ya nyumba zinazojengwa kisasa wakati alpoizindua kampeni ya ujenzi wa nyumba bora kwa wakazi wa jimbo hilo unaojulikana ‘Operesheni Ondoa Tembe’ ili kuboresha makazi ya wananchi wake ambao asilimia kubwa wamekuwa wakiishi katika nyumba hizo za asili









Na Mwandishi wetu
Mbunge wa Singida Kaskazini, Mh. Lazaro Nyalandu amezindua kampeni ya kuondoa nyumba za Tembe jimboni mwake ijulikanayo kama ‘Operesheni Ondoa Tembe’.Operesheni hiyo ilizinduliwa na mbunge huyo pia ni Naibu waziri mteule wa Viwanda na Biashara, katika Kijiji cha Msange kata ya Ilongelo, jimboni humo ambapo aliwataka wananchi kuanza kubadili mfumo wa nyumba wanazioihi ili wawe na nyumba bora zaidi.
“ Kama tutashirikiana kwa pamoja inawezekana, hivyo kwa kuanzia kila mmoja aanze kufikiri kuwa na nyumba ya kisasa na tutahamasishana ili tuweze kubadilika” alisema Nyalandu.
Aliwaeleza wananchi wake kuwa nyumba za aina hiyo ambazo huezekwa kwa udongo pamoja na kuwa ni za asili lakini bado zina matatizo kwani hazina mwanga wa kutosha na hata hewa kwa watu wanaoishui huko.Nyalandu alisema opereshani hiyo itafanikiwa kwa juhudi za wananchi hao kwa kuhamasishwa na viongozi nasi kwamba yeye ndiye atakayelipa gharama hizo kama baadhi ya watu wanavyodhani.
“Hii ni operesheni ambayo inamgusa kila mmoja na hivyio tutashirikiana na viongozi wa kata na vijiji kuhamasisha wananchi kujenga nyumba bora ili kusiwe na tembe katika miaka kadhaa inayokuja” alisema.Akitembelea baadhi ya nyumba bora ambazo zimeanza kujengwa, Nyalandu alipongeza wananchi walioanza ujenzi wa nyumba hizo na tayari mwenyewe ameanzisha ujenzi wa nyumba ya kisasa ambayo itakuwa mfano kwa wapiga kura wake.
Mbunge huyo kijana alisema alianza kuhamasisha ujenzi wa nyumba bora katika kipindi kilichopita na watu wengi wamehamasika na kuanza kufyatua matofasli na kuchoma ili kuwa na nyumba bora na kusema kuwa operesheni hiyo ityasaidia kuboresha maisha ya watu.
Mkoa wa Singida ni moja ya mikoa ambayo imekuwa maarufu kwa ujenzi wa nyumba za tembe ambazo mbali na kuezekwa kwa udongo juu pia madirisha yake huwa madogo na hivyo kufanya wakazi wake kupata Mwanga mdogo ndani na pia hewa huwa haba. Mikoa mingine ni Dodoma na Shinyanga.

No comments: