Sunday, November 28, 2010

Yaliyosemwa na Mawaziri siku walipoapishwa

Magufuli: Nitafanya kazi kwa kasi ya juu
Shamsi: Tutajitahidi kudhibiti majambazi
Hawa: Nitasahihisha dosari za awamu iliyopita
Nundu: Heshima ya ATC itarudi hivi karibuni

RAIS Jakaya Kikwete amewaapisha mawaziri na naibu mawaziri aliowateua wiki hii, huku wenyewe wakiahidi kutowaangusha Watanzania. Hafla ya kuwaapisha mawaziri hao ilifanyika viwanja vya Ikulu mjini, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mabalozi, viongozi wa serikali, dini na vyama vya siasa.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti baada ya kuapishwa, mawaziri hao walisema utendaji katika miaka mitano ya ijayo utakuwa wa ari kubwa ili kutowaangusha Watanzania katika kuwaletea maendeleo.
Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli, alisema lengo la Rais kuunda baraza la mawaziri lililo na mchanganyiko ni kuhakikisha linaleta maendeleo katika kasi itakayokubalika na wengi.
Alisema kwa upande wake ameupokea uteuzi wa Rais kuwa ni heshima kwake, hivyo atahakikisha analipa kwa kuwatumikia Watanzania kwa kufanya kazi katika kasi ya juu.
Dk. Magufuli alisema katika wizara hiyo, atasimamia kikamilifu ustawi wa barabara kwa kuwa ni kiungo muhimu kinachohitajika ili kuwa na maendeleo katika sehemu zote nchini.
"Siwezi kueleza mambo mengi kwa kuwa hata ofisini sijaingia lakini, kitu kikubwa ninachoweza kusema ni kwamba tunakwenda kutekeleza yale tuliyoyaahidi katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM," alisema Dk. Magufuli.
Kwa upande wake, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, aliwataka Watanzania kwa sasa kumpa nafasi ila awahakikishie kuwa atawatumikia kikamilifu.
Sitta alisema ameupokea uteuzi na kwamba anaamini mambo yatakwenda vizuri.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, alisema anaingia katika wizara hiyo akijua bado kuna changamoto zinazohitaji kutatuliwa na kuahidi kuwa atafanya hivyo.
Nahodha alisema moja ya changamoto hizo ni tatizo la ujambazi, japo limefanikiwa kudhibitiwa kwa kiasi fulani, lakini bado kumekuwepo na matukio ambayo yatadhibitiwa.
"Uzuri ni kwamba miongozo ipo na dhamira tunayo kuhakikisha ujambazi unatoweka, kwa kushirikiana na wenzangu tutasimamia sheria na taratibu ili kufanikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao,î alisema.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, aliwataka Watanzania kufurahia uteuzi wake katika kwa kuwa atasimama usiku na mchana kuhakikisha maendeleo yanakuja.
Dk. Mwakyembe alisema kwa kushirikiana na waziri wake, Dk. Magufuli, watasimamia kikamilifu wizara hiyo kuhakikisha maendeleo yanapatikana.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, alisema atapambana kuhakikisha yale yanayodaiwa kuwa ni matatizo katika sekta ya utalii na uwindaji yanapatiwa ufumbuzi na kuona marekebisho ya sheria za uwindaji yaliyofanywa yanatoa nafasi kwa Watanzania kunufaika.
Alisema kwa kuwa amepewa nafasi ya kuongoza wizara muhimu inayoongoza katika kuliingizia taifa fedha za kigeni, atahakikisha anafanya vizuri kaw kadri ya uwezo wake.
Naye Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, alisema moja ya changamoto kubwa anazokabiliwa nazo na ambazo angependa kuzitafutia ufumbuzi ni upatikanaji wa maji maeo yaliyo karibu na watu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, alisema atahakikisha katika awamu yake hi ya pili, anashughulikia changamoto zilizojitokeza miaka mitano iliyopita hususan mahusiano na wafanyakazi.
Waziri Hawa, alisema kazi yoyote huwa na changamoto kama ilivyotokea kwa wizara hiyo lakini changamoto hizo ni chachu ya kufikia maendeleo ya nchi na wafanyakazi kwa ujumla.
Omary Nundu ambaye ni Waziri wa Uchukuzi, alisema atahakikisha analirudishia heshima Shirika la Ndege Tanzania (ATC).
Alisema nchi zote zina mashirika ya ndege yanayosimamiwa na serikali na kuwa hilo linawezekana kwa Tanzania na atakachofanya ni kushirikiana na watumishi wa sekta hiyo kuona jinsi ya kulifanikisha.
Kwa upande wake , Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alisema anaingia kwenye wizara ambayo kazi zake anazifahamu kwa kina.
Alisema anafahamu changamoto nyingine zinazoikabili wizara hiyo, hivyo anaamini kwa kushirikiana na wananchi na kwa kufuatata sheria na taratibu, atafanikiwa kuleta mabadiliko.
Naye naibu wake, Goodluck Ole Medeye alisema anatambua kwamba wizara hiyo ni nyeti, hivyo kwanza atahakikisha anajifunza kutoka kwa watumishi wa wizara hiyo.
ìKuanzia mhudumu hadi Katibu Mkuu wa wizara watakuwa walimu wangu, na nitatekeleza majukumu yangu kwa kufuata sera, sheria na kanuni kuleta mabadiliko ya kimaendeleo,îalisema.
Ole Medeye ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa miongoni mwa wabunge watakaolikisha Bunge la Tanzania katika Jukwaa la Wabunge wa SADC, alisema majukumu hayo hayataathiri utendaji wake serikalini.
Naye Waziri wa Nishati na Madini , William Ngeleja, alisema katika kipindi cha pili cha awamu ya nne, wamejipanga kumaliza tatizo la mgao wa umeme nchini.
Alisema serikali ipo katika utekelezaji wa mpango wa ununuzi wa jenereta kubwa za kuzalisha umeme ambapo megawati 100 zitatumika kwa mkoa wa Dar es Salaam na megawati 60 kwa mkoa wa Mwanza.
Ngeleja alisema katika mwaka huu wa fedha, sh. bilioni 103 zimetengwa kwa ajili ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika mikoa 16.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umenza na wakandarasi wapo maeneo ya mradi wakiendelea na kazi.
Pia, alitaja mradi mwingine wa umeme unaofadhiliwa na Mfuko wa Kushughulikia Changamoto za Milenia (MCC) ambao utatekelezwa katika mikoa sita ya Mwanza, Dodoma, Morogoro, Iringa, Mbeya na Tanga.
Mradi mwingine ambao utaanza kuzalisha umeme wa gesi asilia ni mradi wa Mnazi Bay mkoani Mtwara ambao utazalisha megawati 300, Somanga megawati 200, Kiwira megawati 200 zitakazotokana na makaa ya mawe.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema anatambua changamoto za kushamiri kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto hivyo ni mambo ambayo atayasimamia vyema.
Alisema nafasi aliyopewa ameifanyia kazi kwa miaka sita katika ubalozi wa Denmark akiwa Ofisa Mipango, Utawala na Jinsia, hivyo atatumia uzoefu wake kuleta ufanisi.
Naibu waziri huyo alisema, hivi karibuni serikali imeridhia mikataba ya kimataifa ya haki za watoto, hivyo atafuatilia kwa kina maeneo yenye matatizo na kuyafanyia kazi.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema elimu ni kipaumbele kikubwa katika serikali ya awamu ya nne na atajitahidi kuhakikisha mipango yote iliyopo kwenye ilani ya uchaguzi inatekelezwa.
Alisema ni lazima vyuo vya elimu ya juu viwezeshwe kutoa elimu kwa kiwango ambacho mhitimu ataweza kushindana katika soko la ajira hususan katika nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, alisema katika uongozin wake atahakikisha kero za wafanyakazi zinamalizwa kabisa, badala ya kuvutana.
ìTunakusudia kufanya kazi bega kwa bega na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) , serikali haitakiwi kuvutana na shirikisho hilo, tunatakiwa kuzungumza na kushirikiana kuboresha mahitaji ya wafanyakazi,îalisema.
Naye Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, alisema atakanya kazi kubwa ya kumsaidi waziri wake ili kuhakikisha wizara inafanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yake.
ìNatambua ajira kwa vijana bado ni changamoto kwa wizara, hivyo ni suala ambalo tutaliwekea kipaumbele kwa kuwezesha vijana kupata ajira,î alisema.
Alipotakiwa kueleza ni kwa nini baadhi ya wananchi wanaponda uteuzi wake, alisema ni chuki za kisiasa na pengine watu hawapendi jina na sura yake, lakini anaamini amefanya kazi vizuri kipindi kilichopita ndiyo maana ameteuliwa tena.
Wengine walioapishwa na wizara zao kwenye mabano ni Waziri wa Nchi (Utawala Bora) Mathias Chikawe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Stephen Wassira.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Samia Suluhu na Dk. Terezya Hovisa (Mazingira).
Katika Ofisi ya Waziri Mkuu, walioapishwa ni William Lukuvi (Sera, Uratibu na Bunge) na Dk. Mary Nagu (Uwekezaji na Uwezeshaji).
Wengine ni George Mkuchika, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa ambao ni naibu mawaziri.
Mawaziri wengine ni Mustapha Mkulo (Fedha na Uchumi) na manaibu wake Gregory Teu na Pereira Ame Silima. Balozi Khamis Kagasheki (Mambo ya Ndani) Celina Kombani (Sheria na Katiba), Bernard Membe (Mambo ya Nje) na naibu wake Mahadhi Juma Mahadhi.
Dk. Hussein Mwinyi (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) Dk. Mathayo David Mathayo (Kilimo, Chakula na Ushirika) na naibu wake Benedict ole Nangoro. Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia) na naibu wa wizara hiyo Charles Kitwanga maarufu Mawe Matatu.
Wingine ni Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara) na naibu mawaziri Adam Malima (Nishati na Madini) Dk. Athumani Mfutakamba (Uchukuzi) na Lazaro Nyalandu (Viwanda na Biashara).
Philipo Mulugo ambaye ni naibu waziri (Elimu na Mafunzo ya Ufundi) Dk. Haji Hussein Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii) naibu wake Dk. Lucy Nkya, Sophia Simba (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto).
Emmanuel Nchimbi, (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo) Profesa Jumanne Maghembe (Kilimo, Chakula na Ushirika) na naibu mawaziri Dk. Fenella Mukangara, Abdallah Juma Abdallah (Ushirikiano Afrika Mashariki) Injinia Christopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika) Injinia Gerson Lwenge (Maji).
CHANZO GAZETI LA MZALENDO

No comments: