Wednesday, August 22, 2012


TUPAMBE KWA MAPAMBO YETU YA ASILI
MITUNGI ambayo imebakia kuwa mapambo ya barabara baada ya kukosa wateja, tatizo ambalo linakwamisha juhudi za wajasiriamali wa sekta inayojiajiri katika kujiendeleza kiuchumi.
TASWIRA YA BAADHIYA VITUO VYA MABASI DAR ES SALAAM

VIBANDA vya kupumzikia abiria katika vituo vya daladala mkoani Dar es Salaam, vinakabiliwa na tatizo la ukosefu wa matunzo. Pichani, abiria akisubiri usafiri katika kibanda ambacho kimeanza kuanguka, eneo la Karume, jana. Hali hiyo, inayotishia walengwa imedumu kwa zaidi ya wiki tatu sasa.


BENKI ya NMB, imeanzisha mpango wa Financial Fitness, unaolenga kuwahamasisha wanafunzi kuitumia benki hiyo katika kujiwekea akiba ya fedha. Pichani, wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Mkapa, mkoani Mbeya, wakiangalia jarida linaloelezea mpango huo, uliotambulishwa shuleni hapo.


Monday, August 20, 2012

MUONEKANO WA MAGAZETI JUMATATU YA LEO
















Diwani afuturisha wafanyakazi wa Kampuni ya Uhuru Publications Ltd
DIWANI wa Kata ya Kwadelo,wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, Omary Kariati (wa pili kushoto), akitoa neno wakati wa futari aliyowaandalia wafanyakazi wa Kampuni ya Uhuru Pulbications Limited (UPL), wachapishaji wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, ofisi za UPL, Lumumba, Dar es Salaam, Mwishoni mwa wiki iliyopita.


Mapishi ya Biriani ya kuku iliyopambwa kwa mayai

Birini ni moja ya chakula ambacho watu wengi hupenda kukitumia nyakati za sikukuu kama chakula maalumu.
Wengi katika siku kama hizi, hawapendi kukisa kabisa.
Hata hivyo, upishi wa chakula hutofautiana. Mimi leo nawapikia biriani ya nyama ya kuku ambayo nitaipamba kwa mayai.


MAHITAJI;
Mchele kilo moja aina ya Pishori/Basmati
Kuku aliyechinjwa mmoja, mkate vipande vya kawaida
Paketi moja ya maziwa ya mtindi
Vitunguu maji vikubwa sita, vikate vipande vikubwa vya mviringo
Mayai sita
Vitunguu swaumu vilivyopondwa kijiko kimoja cha chai.
Tangawizi mbichi iliyotwangwa kijiko kimoja cha chai.
Malimao makubwa mawili
Papai bichi moja, limenye, toa mbegu, kata vipande na kisha lisage kwenye blenda kwa kutumia jagi linalotoa chembe kubwa kubwa.
Viazi mviringo vikubwa kama 5, vimenye uvikate nusu.
Nyanya ziloiva, zisage pia kisha uzichuje
Tomato paste kiasi, mafuta ya kupikia, kiasi, Chumvi kiasi, Cinnamon, Pilipili manga kiasi, Karafuu kiasi, Hiliki kiasi na Zafarani kiasi, iloweke katika maji ya moto nusu glass.

NAMNA YA KUPIKA;

Weka ndani ya blender Tangawizi, papai ilosagwa na kitunguu swaumu na maziwa mgando, uvisage mpaka viwe mchanganyiko mzito, Weka pembeni
Osha nyama ya kuku kisha ipake chumvi ukamulie malimao, mwagia mchanganyiko wa papai na tangawizi na vitunguu swaumu kisha weka jikoni uchemshe mpaka iive iwe laini (kama ni kuku ya kienyeji), ikiwa ni kuku wa kizungu usiichemshe sana itavurugika.
Kisha saga tena viungo vyote vilivyosalia pamoja, na umiminie kwenye nyama ya kuku ikiwa inachemka.
Weka nyanya iliyosagwa kwenye blender na ile ya paste kwenye kuku inayochemka, ukoroge ichanganyike kwenye nyama.
Menya vitunguu maji uvioshe uvikate. Weka sufuria jikoni uweke mafuta yachemke.
Kisha tia vitunguu maji ukaange mpaka vibadili rangi na kuwa ya udhurungi, baada ya hapo viipue na uvichuje mafuta uviweke pembeni vipoe.
Menya viazi mviringo uvikaange kwenye mafuta mpaka viive, ipua weka pembeni vipoe
Kama kuku imeiva, isikauke iwe na rojo, chukua vitunguu ulivyokaanga uvimiminue kwenye kuku, na viazi pia, changanya, acha ichemke kiasi halafu ipua weka pembeni tayati kwa kuliwa.
Bandika tena sufuria jikoni utie maji na chumvi, yakichemka tia mchele na mafuta.
Pika kama wali wa kawaida unavyopikwa. Ukishaiva nyunyizia yale maji ya zafarani huku unageuza ili rangi isamba.
Kama huna zafarani basi tumia rangi ya chakula ya orange. Funikia na uweke moto mdogo sana mpaka wali ukauke vizuri (hii ni kama haupalii na mkaa kwa juu.


NB: Kama utapenda unaweza kuweka zabibu kavu pia wakati unaweka mchele kwenye maji ya moto zinaivia humo.

Chemsha pia mayai yakishaiva, yamenye na uyagawanye katikati, yaani vipande viwili, bila kuvuruga kiini cha ndani.
Wali ukiiva, sasa waweza pakua kwenye sinia kubwa na juu ukapanga vipande vya mayai, ili kuleta muonekano mzuri mezani.
Chakula chako mpaka hapo kitakuwa tayari kwa kuliwa.


Karibu sana mezani, na ninawatakia sikukuu njema ya Eid El Fitri.


Wednesday, August 8, 2012

NANENANE YA MAJONZI, BASI LAUA 17 PAPO HAPO TABORA


Na El - hadji Yuusuf, Tabora
WATU 17 wamefariki dunia baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Tabora kwenda Mbeya kupinduka eneo la Kitunda wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.

Ajali hiyo, ilitokea umbali wa kilomita 200 kusini mwa mji wa Tabora, ikilihusisha basi la Sabena aina ya Scania lenye nambari za usajili T 570 AAM.
Katika ajali hiyo, watu wanne wamejeruhiwa vibaya na wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Kitunda wakisubiri kuhamishiwa katika Hospitali ya Mkoa ya TaboraKitete, kwa ajili ya matibabu zaidi.
Abiria wengine 54 waliokuwa katika basi hilo walinusurika na kuomba kuendelea na safari, baada ya kufanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa hawakuwa na madhara makubwa katika miili yao. Miongoni mwa watu walikufa ni watoto 6 wanawake 5 na wanaume 6 ambao miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Kitete kwa ajili ya kutambuliwa na ndugu na jamaa zao.
Hata hivyo, hadi kufikia jana mchana, miili ya watu saba ilikuwa imetambuliwa na baadhi ya ndugu, ukiwemo wa askari Polisi Konstebo Kheri, wa Kituo Kikuu cha Polisi cha mjini Tabora.
Marehemu wengine waliotambuliwa ni Vitus Tulumanye, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), tawi la Tabora na Farah Inga raia wa Zimbabwe aliyekuwa akifanyakazi Tabora.
Wengine waliotambuliwa ni Ikamba Thadeo, Damalu Goma, Beatrice Kalinga ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi Igoko wilayani Uyui mkoani Tabora na Madirisha ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi iliyoko wilaya Mpya ya Kaliua.
Mwalimu Madirisha anadaiwa kufuatana na watoto wanne na mkewe ambaye bado hajatambuliwa najuhudi zinaendelea za kubaini familia ya mwalimu huyo.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na dereva wa basi hilo kwa mwakilishi wa basi hilo mkoani Tabaro, Shaaban Mnyema, chanzo cha ajali hiyo ni lori aina ya Fuso lililokuwa limeegeshwa katika kona. Alidai kuwa dereva wa basi hilo alipojaribu kulikwepa 'Stearing Road' ilikatika na gari kuacha njia na kupinduka.
Dereva huyo Ali Nassoro, ambaye alitoroa baada ya kutoa taarifa za ajali na maelezo hayo kwa njia ya simu, alisema ajali hiyo ilitokea jana saa 6.30 mchana katika eneo ambalo halina mawasiliano ya simu za mkononi.
Nassoro alisema hata katika kijiji cha Kitunda kulikuwa hakuna mawasiliano na hivyo kumlazimi kumtuma mtu kwenda Sikonge kutoa taarifa za ajali hiyo.
Baadhi ya majeruhi waliotambuliwa ni Grace Mbunga, Kayungilo Nsungu, Zena Shigela, Ndisi Ngosha, Kulwa Kija, Feni Salum, Shinje Kayogole na Emmanuel Charles.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Anthony Ruta, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na alipouwa akiwasiliana na Mwandishi alikuwa njiani kuelekea eneo ilipotokea ajali.
Naibu Waziri Wizara ya Afrika Masharika apata ajali

Mzimu wa ajali kwa wabunge na viongozi wa Taifa umeendelea kushika kasi hapa nchini baada Naibu waziri wa Afrika Mashariki, Abdullah Juma Abdalla Saddallah (Pichanai aliyejeruhiwa) na familia yake kupata ajali mbaya eneo la Tumbi Kibaha wakati akitoka Bungeni na familia yake.
Ajali hiyo mbaya ilitokea majira ya jioni hii wakati naibu waziri huyo akitokea Bungeni kuelekea jijini D'salaam akiwa na mkewe pamoja na watoto wake wawili na a dereva wake ambaye aliumia vibaya na kukimbizwa hospital yaTumbi-KibahaMashuhuda wa ajali hiyo akiwemno Abdulaziz Video amedai kuwa chanzo cha ajali hiyo inasemekana alikuwa analikwepa Lori alilokuwa akipishana nalo na hivyo gari lake kuhama njia na kupinduka .


Imeelezwa baada ya ajali hiyo umati wa wananchi wakiwemo vibaka walifika eneo hilo kutaka kupora mali mbali mbali ila hawakuweza kufanikiwa baada ya raia wema kusaidia kuepusha hali hiyo.

Gari la Naibu waziri wa Afrika Mashariki,Abdullah Juma Abdalla Saddallah likiwe limepinduka


Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Taifa Mohamed Mpinda alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo baada ya kuhojia na mwandishi wa habari hizi na kuwa hali ya naibu waziri huyo si mbaya sana zaidi ya dereva wake ambaye ameumia kichwani.

MALAWI HAWATUTISHI, TUPO TAYARI KWA LOLOTE
KAMATI ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imesema Tanzania imejiandaa kiakili na kivifaa kuingia vitani na Malawi kama italazimika kufanya hivyo.
Akizungumza mjini Dodoma jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Edward Lowassa alisema kamati yake imeridhishwa na maandalizi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
“Tumepewa maelezo na jeshi letu na tumeridhika kuwa ikibidi kuingia vitani jeshi letu liko vizuri sana na limejipanga vizuri sana kwa uhakika, kiakili na kivifaa,” alisema Lowassa.
Kabla ya Lowassa kuzungumza na waandishi wa habari, alifanya kikao cha faragha kilichohusisha pia wajumbe wa kamati hiyo na makamanda wa JWTZ walipofika bungeni kutoa taarifa kwa kamati hiyo.
Hata hivyo, katika tamko hilo Lowassa alisema Tanzania inatarajia mgogoro huo utamalizika kwa njia za kidiplomasia kwa sababu Watanzania na Wamalawi ni ndugu wa muda mrefu.
“Ikibidi kuingia vitani jeshi letu liko vizuri sana na kama ilivyo ahadi yao (JWTZ), wako tayari kulinda mipaka ya nchi yetu hadi tone la mwisho.
Tunasali sana tusifike hapo,” alisema Lowassa na kuongeza: “Tunategemea hatutafika huko, lakini kwa heshima ya nchi yetu kama ikibidi kufika huko (vitani) tutafika kulinda mipaka yetu”.
SAKATA KUFUNGIWA MWANAHALISI

Wafanyakazi Tigo wakaangwa
KUTEKWA, kupigwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chama cha Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka na hatimaye kufungiwa kwa Gazeti la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana, kumeleta kizaazaa katika kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Habari kutoka ndani ya kampuni hiyo ya simu yenye mtandao mpana nchini, zinasema kuwa zaidi ya wafanyakazi 30 wamefukuzwa kazi na wengine wako kwenye uchunguzi wakituhumiwa kuvujisha mawasilino ya siri ya simu za wateja kwa Gazeti la MwanaHalisi.
Kwa mujibu wa habari hizo, taarifa za mawasiliano za simu zinazodaiwa kuvujishwa na wafanyakazi hao, zilikuwa kati ya Dk. Ulimboka, Afisa Usalama wa Ikulu na watu aliowasiliana nao kabla ya kutekwa.
Rais Jakaya Kikwete amepata kuliambia taifa mara mbili kwa njia ya televisheni, mwishoni mwa Juni na alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari wiki iliyopita, kwamba serikali yake haihusiki kuteka, kutesa na kumtupa daktari huyo porini.
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda amepata kuliambia Bunge kuwa, serikali yake haihusiki na utekaji, utesaji na kuhoji, “...serikali imteke ili iweje?”
Hivi karibuni serikali ililifungia Gazeti la MwanaHalisi baada ya kuandika habari iliyomtaja ofisa mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa Ikulu (TISS), kuwa ndiye aliyetekeleza mpango wa kumteka, kumpiga na kumtesa hadi kumjeruhi Dk. Ulimboka, ambaye kwa sasa anaendelea na matibabu kwenye hospitali moja nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa habari hiyo ambayo serikali inadai kuwa ni ya uchochezi, MwanaHalisi ilianika namba ya simu ya ofisa huyo pamoja na watu wengine wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo linaloendelea kuchunguzwa na kamati maalumu iliyoundwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Vyanzo vya habari kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi waliokumbwa na sekeseke hilo, zinasema kuwa waliofukuzwa wengi ni wafanyakazi wa kitengo cha IT ambao wanadaiwa kuhusika kutoa taarifa za siri ya mawasilino kati ya Dk. Ulimboka na watu wanaoaminika kuwa ni wabaya wake.
Mmoja wa wafanyakazi kutoka Kampuni ya Tigo, aliliambia gazeti hili kuwa mbali na kutuhumiwa kutoa siri kwa Gazeti la MwanaHalisi, wafanyakazi wengine wametimuliwa kwa madai ya kufanya udanganyifu kwenye huduma za Tigo Pesa na kujipatia fedha.
“Kweli watu wengi wamefukuzwa wakituhumiwa kutoa siri kwa Gazeti la MwanaHalisi, lakini wengine walikuwa wakishirikiana na mawakala wa Tigo Pesa kuiibia kampuni.
“Kwa mfano mfanyakazi alikuwa anakubaliana na wakala kumwingizia kiasi kama cha sh milioni moja, lakini anaweza kuingiza hadi sh milioni 1.5 na kati ya hizo sh 500,000 ni mali yake,” alisema mfanyakazi huyo.
Akizungumzia na Tanzania Daima Jumatano, Mhariri Mkuu wa Gazeti la MwanaHalisi, Jabir Idrissa alishangazwa na taarifa za Tigo kuwafukuza wafanyakazi wake kwa sababu ya habari iliyochapishwa na gazeti lake.
“Chanzo chetu cha habari hakikutoka kwa wafanyakazi wa Tigo. Kama wamefukuzwa kwa sababu ya MwanaHalisi, wamewaonea bure. Kama Tigo ndio waliotupa taarifa na zile za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), zilitoka wapi?” alihoji Jabir na kusisitiza wafanyakazi hao wameonewa bure.
Ofisa Uhusiano wa Tigo, Edward Shila, alipohojiwa kuzungumzia tukio hilo, hakukubali wala kukataa madai hayo na kumtaka mwandishi kumtumia maswali kupitia e-mail yake ili aweze kuyatolea majibu kiofisi.
“Kama una maswali naomba uniandikie kupitia e-mail yangu ambayo nakutumia sasa hivi…maana siko tayari kutoa kauli yoyote isiyokuwa ya kiofisi,” alisema.
Naye Omary Matulla ambaye amejitambulisha kuwa ni ofisa wa kitengo cha kumbukumbu katika kampuni hiyo, alikanusha kuwapo kwa taarifa za kufukuzwa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Alisema kuwa kila mfanyakazi ana mipaka ya kufanya kazi katika kampuni hiyo, na pia ni wajibu wa kila mtumishi kutunza siri kubwa.
“MwanaHalisi ana mbinu zake za kupata habari wala haiwezekani kupata habari kupitia kampuni yetu na hata hivyo jambo hilo si rahisi hata kidogo kutokea,” alikanusha Omary.
Dk. Ulimboka alitekwa usiku wa Juni 26, kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Tangu kutokea kwa tukio la kutekwa kwa Dk. Ulimboka, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, wamekuwa wakiinyoshea kidole serikali kwamba ndiyo iliyohusika.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi mkoani Dar es Salaam, Suleiman Kova, hivi karibuni alitangaza kumfikisha mahakamani mtu mmoja aliyedai kukiri kuhusika na utekaji wa Dk. Ulimboka.
Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa, polisi wamekamata mtu aitwaye Joshua Malundi kutoka Kenya ambaye amekiri kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka.
Alidai kuwa mtuhumiwa alikwenda kutubu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kawe, Dar es Salaam.
Lakini hata hivyo, mchungaji wa kanisa hilo, Josephat Gwajima alikana kauli ya Kova juu ya mtuhumiwa huyo, akisema hajakwenda kutubu kwao.
CHANZO; TANZANIA DAIMA
VITI VYA UKUMBI WA NUNGE KENYA

VYAGHARIMU DOLA 3,000 KILA KIMOJA

Bunge la Kenya lililokarabatiwa na ambalo limekuwa gumzo kubwa kwa sababu ya gharama ya viti vya bunge hilo, hatimaye limefunguliwa rasmi na rais wa nchi hiyo Mwai Kibaki.

Viti hivyo vimegharimu dola 3,000 za kimarekani kwa kila kiti kimoja vikiwa jumla ya 350 vimetengenezwa na kitengo cha magereza nchini humo.

Zabuni ya kwanza ya kutengeneza viti hivyo ilitolewa kwa kampuni moja ya nje lakini ilifutwa baada ya baadhi ya wabunge kugundua kila kiti kingegharimu dola 5000 za kimarekani.

Maafisa wanasema ukarabati huo uliogharimu dola milioni 12 utaliweka bunge katika mfumo mpya wa kisasa wa komputa."Mabadiliko tunayoyafanya yataleta mabadiliko chanya katika uongozi," spika wa bunge Kenneth Marende ameiambia BBC.

Amesema mfumo wa kupiga kura wa elektroniki utawawezesha wabunge kupiga kura kwa uhuru wao binafsi kuliko kulazimika kupiga kura kwa kuhofia vyama vyao.

"sasa mbunge atakuwa peke yake, huru kabisa binafsi, atafanya maamuzi yake na kubonyeza tu kitufe."Mwandishi wa BBC Odeo Sirari mjini Nairobi, anasema baadhi wanaona viti hivyo kuwa ni vya gharama kubwa sana kuliko mabunge mengine katika jumuiya ya madola.

Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga na rais Mwai Kibaki pamoja na wabunge ni miongoni mwa wanaolipwa mshahara wa juu sana barani Africa.Wabunge walifurika katika jengo hilo lililokarabatiwa wakati rais na spika wakiongoza utaratibu wa sherehe za ufunguzi.

Ukarabati huo ulianza mwezi Aprili mwaka 2010 na ulikuwa umepangwa kuchukua mwaka mmoja kumalizika lakini ulichelewa kwasababu ya utata ulioghubika zabuni yake, mwandishi wetu anasema.

Mbunge John Mbadi, katika kamati ya uwekezaji aliongoza upinzani juu ya zabuni ya kwanza,"hatukuweza kuelewa ni kwa vipi wabunge wangekuwa wanakaa katika viti vinavyogharimu karibu shilingi 400,000 za Kenya kama dola 5,000, ambazo kwa kiwango chochote cha kawaida zingeweza kujenga nyumba kwa wananchi kadhaa," ameiambia BBC.

"ilikuwa ni upuuzi," amesema.Mwandishi wetu anasema watu wengi wamelalamika kuwa gharama za sasa bado ni juu. David Langat, anayesimamia uzalishaji katika magereza nchini Kenya, amesema vifaa vyote vilivyotumika vilitoka nchini Kenya lakini gharama za viti zimekuwa kubwa sana.

Ameiambia BBC kuwa viti hivyo vyenye uzito wa kilo 50 kila kimoja vina kinga dhidi ya moto na vina dhamana ya miaka 30. Kwa sasa, Kenya ina jumla ya wabunge 220 lakini ukumbi huo umewekwa viti 350 idadi ambayo watachaguliwa katika uchaguzi ujao mwezi Machi kwa mujibu wa katiba mpya.
Mwenyekiti wa Azam FC mzee Said Mohamed Said akihojiwa na waandishi wa habari baada ya kumtangaza rasmi kocha wa timu yake ya Azam FC ya jijini Dar es salaam, ambapo pia alisema kuhusu mchezaji Redondo ambaye anadaiwa kusajiliwa na timu ya Simba kwamba wao hwamzuii mchezaji huyo kwenda Simba isipokuwa Simba ifuate utaratibu wa Usajiri tu hawana tatizo na hilo
KOCHA WA AZAMU FC

Boris Bunjak kocha mkuu mpya wa timu ya Azam FC akiipia picha wakati alipotambulishwa rasmi na uongozi wa timu hiyo leo jijini Dar es salaam, Boris Bunjak raia wa Serbia aliyezaliwa mwaka 1954 amesaini mkataba wa kuitukimia Azam FC kwa muda wa miaka miwili akiiitumikia timu hiyo, Boris Bunjak amefundisha timu mbalimbali katika nchi za kiarabu na amewahi kuchezaea timu ya taifa ya Serbia na vilabu mbalimbali huko Ulaya Mashariki amewahi kufanya kazi pia katika chama cha soka cha Yugoslavia mwaka 1993-1994 na kazi nyingine nyingi kuhusiana na masuala ya soka.
Dk. Fenella awafunda vijana



Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara akipokea tuzo kutoka kwa Katibu Mkuu wa International Youth Fellowship Bw. Lee Hunmok jana wakati wa ufungaji wa kambi ya kimataifa ya vijana Jijini Dar es Salaam. Tuzo hiyo ilitolewa kwa Wizara kama ishara ya kutambua mchango wake katika kuhakikisha kuwa maendeleo ya vijana yanastawi kikamilifu.



Maendeleo ya vijana ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa letu, na ni muhimu vijana wakatambua hilo kwa kutimiza wajibu wao kwa jamii inayowazunguka.


Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara wakati akifunga kambi ya kimataifa ya vijana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyokaa kwa muda wa siku saba kwa lengo la kuzungumzia mstakabari wa maendeleo ya vijana hususan kuwajengea vijana fikra chanya kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Mukangara alisema kuwa vijana wanatakiwa kuwa na moyo wa kujituma, kujitolea na kufanya kazi kwa bidii ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya ujana.


‘Fanyeni kazi kwa bidii, kwa kujitolea, kwa kuzingatia muda na kujitegemea ili kutimiza ndoto zenu za kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kiafya’. Alisema Dkt. Mukangara.

Aidha, amewaasa vijana kuachana na fikra za kulalamika, kudai haki bila wajibu na kunyosheana vidole na badala yake kijana mwenyewe ajiulize amefanya nini kutatua kero inayomzunguka.


Vijana kataeni vitendo vya uchochezi, chuki na kejeri kwa viongozi kwani kufanya hivyo kunaweza kuwaingiza katika misuguano isiyo na tija na mkumbuke kuwa maendeleo ya vijana hayawezi kushamiri na kustawi pasipo na amani, lindeni amani kwa nguvu zenu zote na kusimamia sheria wakati wote’ Alisema Dkt. Mukangara.


Alisema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa vijana na kupitia Wizara yake imeweka mipango ambayo inatoa vipaumbele kwa maendeleo ya vijana.


Naye Katibu Mkuu wa International Youth Fellowship (IYF), Bw.Lee Hunmok aliwataka vijana kuwatumikia wenzao na kuwa mabalozi kwa vijana ambao hawakupata fursa ya kuingia kambini.


Bw. Vitus Faustin Mzale ni kijana aliyeshiriki kambi hiyo kutoka mkoani Kagera alisema kuwa ameweza kujifunza mambo mbalimbali kambini hapo na amewataka waandaaji kushirikiana na Serikali ili kuwapa vijana mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kujikwamua kiuchumi.


Kwa upande wake Bi Mariza Vargas kijana kutoka Peru alisema kuwa amefungua moyo wake kwa ajili ya kujitolea na ameweza kujua namna ya kufanikisha malengo yake ya kujiletea maendeleo kama kijana.


Kambi hiyo ya kimataifa iliyoandaliwa na International Youth Fellowship ilishirikisha nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Kenya, Korea, Malawi, Peru na China.

SERIKALI KUWALIPA WANANCHI

WA MASWA NG'OMBE ZAO


Serikali imeahidi kutoa kiasi cha sh. milioni 6 kulipa fidia ya ng’ombe 22 wanaodaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na askari wa wanyamapori wa pori la akiba Maswa wilayani Meatu, mkoani Simiyu.


Inadaiwa ng,ombe hao walipigwa risasi na kuuawa Desemba 2009 baada ya kuingizwa kuchungia ndani ya hifadhi hiyo, kitendo ambacho ni kinyume na sheria zinazolinda hifadhi za wanyama pori .


Ahadi hiyo imetolewa juzi na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wakazi wa kata ya Sakasaka jimbo la Kisesa.


Alisema lengo la uamuzi huo ni kuimarisha mahusiano mazuri kati ya askari wa wanayamapori na wakazi wa vijiji vinavyozunguka akiba ya pori hilo.





Mkuu wa wilaya ya Meatu, Rosemary Kirigini akitoa taarifa yake ya maendeleo ya pori la akiba Maswa kwa naibu Waziri Maliasili na Utalii Mh. Lazaro Nyalandu aliyetembelea pori hilo.


“Pia ni sehemu ya mikakati inayochukuliwa na serikali ya kuhakikisha mgogoro wa muda mrefu kati ya uongozi wa pori la akiba Maswa na wananchi wakazi wa vijiji vinavyozunguka pori hilo,unamalizika na kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo,” alisema Nyalandu.


Katika hatua nyingine, Nyalandu ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Singida kaskazini, alisema kuwa serikali inatarajia kuunda kamati huru ambayo itashughulikia kutafuta ufumbuzi wa mgogoro uliopo kwa muda mrefu katika akiba ya pori la Maswa.


“Katika kamati hii,kutakuwepo na mwakilishi mmoja kutoka wizara ya mali asili na utalii na wajumbe watakaobaki watakuwa ni watu huru ambao watazitendea haki pande zote mbili.


Ni matarajio yetu kwamba taarifa itakayotolewa na kamati hiyo haitaionea au kupendelea upande wo wote, itakuwa timilifu,” alifafanua naibu waziri huyo.


Nyalandu alisema kamati hiyo itatoa taarifa yake wizarani mapema kabla bunge la sasa kuhairishwa.


Katika hatua nyingine, alitumia fursa hiyo kuagiza wananchi waendelee kuelimishwa vya kutosha juu ya sheria zote za hifadhi za wanyama pori ili waweze kuzitii bila ya kushurutishwa.

“Napenda kukumbusha kuwa marufuku kuchungia,kulima,kuingiza au kufanya shughuli zo zote za kijamii ndani ya hifadhi la wanyama pori.

Mfugaji au mtu yeyote atakayevunja sheria halali ailizowekwa atachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Nyalandu. Awali Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Rosemary Kirigini, alisema hifadhi ya pori la akiba Maswa ipo kwa mujibu wa sheria.


“Kwa hiyo, wananchi kuigiza mifugo yao ndani ya hifadhi hiyo kwa madai ya kutokuwa na maeneo ya malisho ni kuvunja sheria.



Naibu Waziri wa Maliasli na Utalii Lazaro Nyalandu (kushoto), akibadilishana mawazo na mbunge wa jimbo la Kisesa mkoa wa Simiyu Mh. Mpina muda mfupi baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa pori la akiba la Maswa.


Tunashauri wananchi wenye mifugo wanaopakana na pori la akiba la Maswa watafute maeneo mengine ya kupeleka makundi yao ya mifugo, au washauriwe kupunguza mifugo yao kwa kuanzisha ufugaji wa kisasa,” alisema DC Kirigini.


Aidha, alisema kuwa wataendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa madai kwamba hifadhi zilizopo, ni hazina kwa vizazi vilivyopo sasa na vya baadaye kwa nchi ya Tanzania na dunia kwa ujumla.


Wakati huo huo, DC Kirigini ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kubadilisha jina la akiba la pori la Maswa na kulipa jina la akiba ya pori la Meatu.


Alisema kuwa kwa vile sasa wilaya ya Maswa imegawanywa na kuwa na wilaya wilaya tatu baada ya kuanzishwa kwa wilaya ya Bariadi na Meatu,akiba ya pori hilo ambalo sehemu kubwa ipo wilaya mpya ya Meatu,hivyo kuna ulazima wa kuitwa pori la akiba la Meatu.


Kwa upande wake Nyalandu alisema ombi hilo la kubadilisha jina la pori hilo linazungumzika.
RAIS JAKAYA KIKWETE, YOWERI MUSEVENI, JOSEPH

KABILA NA PAUL KAGAME WAKUTANA UGANDA

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete,Rais Paul Kagame wa Rwanda(kushoto),Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda(Watatu kulia) na Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo wakiwa katika mkutano wa viongozi wan chi za Maziwa Makuu unaofanyika jijini Kampala Uganda jana jioni.


Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda wakifurahia jambo wakati wa mkutano wa Viongozi wa nchi za Maziwa Makuu unaofanyika jijini Kampala Uganda (picha na Freddy Maro)





Monday, August 6, 2012

NAREJESHA FOMU


Mgombea nafasi ya Mwenyekiti UWT Taifa, Halima Mohamed Mamuya, kulia, akirudisha fomu ya kuomba kugombea nafasi hiyo kwa Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni UWT Makao Makuu Dar es Salaam Riziki Kingwande leo.
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUWEPO KWA MGONJWA WA
EBOLA, WILAYA YA KARAGWE MKOA WA KAGERA, TANZANIA


Utangulizi



Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu tetesi zilizokuwa zimeenea hapa nchini kutoka kwenye vyombo mbali mbali vya habari kuhusu kuwepo kwa mgonjwa wa Ebola,wilayani Karagwe mkoa wa Kagera.



Mnamo tarehe 3 Agosti 2012, Wizara ya Afya na Ustawi Wa Jamii ilipokea taarifa kutoka kwa mganga mkuu wa wilaya ya Karagwe ya kuwepo kwa mgonjwa aliyekuwa anahisiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola, katika hospitali ya Wilaya ya Nyakahanga.


Aidha,taarifa hiyo ilibainisha kuwa mgonjwa huyo alikuwa ni mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka (6) kutoka katika kijiji cha Nyakatundu wilayani Karagwe.


Mgonjwa huyu alikuwa na dalili za homa kali, kulegea, kutokwa damu puani, kutapika damu, na kukojoa damu.


Maelezo kutoka kwa mama mzazi zilieleza kuwa mtoto huyu alianza kuugua kuanzia tarehe 30 Agosti 2012, ambapo alipatiwa dawa ya Septrin baada ya hospitali binafsi kuonyesha kuwa ana ugonjwa wa“Typhoid”.



Uchunguzi wa awali katika hospitali ya Nyakahanga ulionyesha kuwa mtoto huyu alikuwa anasumbuliwa na uambukizo kwenye haja ndogo (Urinary Tract Infection).Vile vile alifanyiwa uchunguzi wa kimaabara na Vipimo vya malaria, Hepatitis na Typhoid havikuonyesha kuwepo kwa magonjwa haya.


Hospitali inaendelea kumpatia matibabu mtoto huyu na imewaweka mgonjwa na mama yake anayemtunza kwenye chumba maalum (Isolatiom room) kwa ajili ya uangalizi zaidi.



Aidha mnamo tarehe 4 Agosti 2012, timu za wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na timu ya mkoa wa Kagera imeweza kufika na kumfanyia uchunguzi wa kina pamoja na kuchukua sampuli za damu kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika maabara ya Taifa ya uchunguzi wa magonjwa na Maabara za nje ya nchi, ili kubaini kama ameathirika na ugonjwa wa Ebola.


Timu hiyo ya wataalamu imetoa taarifa kuwa hali ya mgonjwa huyu kwa sasa imeimarika ikiwa pamoja na kutokuwa na homa, kutapika na kukojoa damu kumekoma pia, uchunguzi uliofanywa kwa mama wa mtoto umeonyesha kuwa hana dalili zozote za ugonjwa wa Ebola.


Vile vile hakuna taarifa ya mtu mwingine yeyote kwenye familia hiyo au kwenye maeneo ya kijiji hicho au cha jirani kuwa na dalili za ugonjwa huo.



Kufuatia taarifa hii, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Mkoa wa Kagera imechukua hatua zifuatazo;



Imepeleka timu ya wataalamu mbali mbali kutoka Wizarani na mkoa kwa lengo la kwenda kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu kuwepo kwa ugonjwa huo.



Imetoa elimu ya Afya kuhusu njia za kuzuia kuenea ugonjwa wa Ebola pamoja na dalili za ugonjwa huu, kwa wananchi na watumishi wa afya katika hospitali ya Nyakahanga
kupeleka vifaa kinga katika hospitali ya Nyakahanga pamoja na maeneo ya mipakani
kutoa matangazo kwa jamii kwa kutumia vipaaza sauti na kupitia radioni (Radio Karagwe) kuhusu ugonjwa huu. Aidha, vipeperushi pia vimetolewa.

HITIMISHO:
Wizara inapenda kuufahamisha umma kuwa mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola hapa nchini.


Aidha, Wizara ya Afya imejiaanda kikamilifu kukabiliana na ugonjwa huu iwapo utatokea hapa nchini.



Kwa sasa timu za wataalum zipo katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro na Arusha, kutoa elimu juu ya ugonjwa huu kwa wataalamu na kwa wananchi na vilevile kufuatilia ugonjwa huu sehemu za mipakani.



Wizara inaendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa haraka kwenye kituo chochote cha kutolea huduma za afya, mara wanapoona dalili za ugonjwa huu.

Imetolewa na:
kitengo cha Mawasiliano
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
Tarehe 6 Agosti, 2012

NAZINDUA MASHINE ZA KUVUNIA MPUNGA





Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza laMapinduzi,Dk. Ali Mohamed Shein, akiwasha Mashine ya KuvuniaMpunga, (Combine Harvester) ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Mashine hizo 14 zilizonunuliwa na Serikali ya Mapinduzi kwa lengo la kuboresha Mapinduzi ya Kilimo, katika Shamba la Mbegu Bambi, Wilaya ya Kati Mkoa waKusini Unguja. (Picha na RamadhanOthman, IKulu)





Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza laMapinduzi,Dk.Ali Mohamed Shein,(kushoto) akiangalia Mpunga Ukitokakatika mashine ya Kuvunia Mpunga,(Combine Harvester) baada yakuzindua mashine hizo katika shamba la Kilimo la Serikali huko BambiWilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja leo





Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza laMapinduzi,Dk.Ali Mohamed Shein,(kushoto) akiangalia Mpunga Uliovunwakwa kutumia mashine ya Kuvunia Mpunga,(Combine Harvester) baada yakuzindua mashine hizo katika shamba la Kilimo la Serikali huko BambiWilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja leo.
TANZANIA SASA KUKAGUA HESABU
ZA UMOJA WA MATAIFA

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) ambaye pia ni Mkaguzi wa hesabu za Umoja wa Mataifa (UN) Ludovick Utouh akiongea na waandishi wa habari kuhusu Taasisi 10 za UN ambazo zitafanyiwa ukaguzi chini ya usimamizi wake ambapo watumishi 60 kutoka ofisini yake watafanya kazi hiyo. Kwa kipindi cha miaka sita nchi za Tanzania, China na Uingereza zimepewa jukumu la ukaguzi wa hesabu za UN.






Edwin Rweyumamu kutoka ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) akimkaribisha CAG ambaye pia ni Mkaguzi wa Hesabu za Umoja wa Mataifa (UN) Ludovick Utouh ili aweze kuongea na waandishi wa habari kuhusu Tanzania kupata nafasi ya kukagua hesabu za UN kwa kipindi cha miaka sita. Watumishi 60 kutoka ofisi ya CAG watafanya kazi ya kuzikagua taasisi 10 za UN. (Picha zote kwa hisani ya Anna Nkinda – MAELEZO)







NAREJESHA FOMU Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa akimkabidhi fomu anazorejesha za kugombea nafasi ya ujumbe wa UVCCM-NEC, Katibu wa UVCCM mkoani Mwanza Elias Mpanda jana, katika ofisi za CCM Mkoa wa Mwanza. Mstahiki Meya huyo anagombea nafasi ya ujumbe wa UVCCM-NEC ngazi ya Taifa.
Uozo Zimamoto

* Vigogo wajinufaisha kwa stika feki
* Aliyefanya madudu ahamishwa kituo


NA MWANDISHI WETU, MWANZA

SERIKALI inaibiwa mamilioni ya shilingi kutokana na uuzwaji wa stika feki za vifaa vya kuzimia moto kwenye magari, viwandani na ofisini, unaofanywa na baadhi ya vigogo wa Jeshi la Uokoaji na Zimamoto Tanzania, imefahamika.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, unaonyesha baadhi ya vigogo wa jeshi hilo makao makuu, jijini Dar es Salaam, wana mtandao wa kuuza stika hizo mikoani, ikiwemo Mwanza, Mara na Geita.

Kwa mujibu wa uchunguzi, vigogo hao wanashirikiana na watumishi wa jeshi hilo, wakiwemo maofisa kadhaa walioko kwenye mikoa hiyo.

Jijini Mwanza, uchunguzi unaonyesha stika hizo zimemwagwa na kuuzwa kwa wingi kwenye viwanda kadhaa, vikiwemo vya samaki na vinywaji na kwamba, mhusika mkuu wa biashara hiyo ni ofisa mmoja wa jeshi hilo.

Ofisa huyo anadaiwa alihusika katika biashara hiyo kwenye viwanda hivyo kabla ya kuhamishwa kituo cha kazi.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya jeshi hilo, mwishoni mwa wiki iliyopita, zilidai Machi, mwaka huu, ofisa huyo alibambwa na kitabu cha stika feki akiwa katika harakati ya kuziuza kwa wenye magari.

“Alitozwa faini ya sh. 800,000 na alizilipa pale pale,” kilidai chanzo chetu cha habari na kuhoji alizipata wapi fedha hizo, ambazo ni nyingi ikilinganishwa na kipato cha mtumishi huyo.

Habari kutoka kwa mtu aliye karibu na ofisa huyo zilisema fedha hizo alitumiwa na kigogo anayedaiwa kuendesha mtandao huo.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, mkoani Geita, stika hizo zimeuzwa katika migodi kupitia kwa ofisa (jina linahifadhiwa) anayefanya kazi katika mgodi wa Geita Gold Mine (GGM).

Mkoani Mara, uchunguzi unaonyesha zinasambazwa na ofisa wa jeshi hilo (jina tunalo) ambaye inadaiwa hutumiwa moja kwa moja na kigogo aliye makao makuu, Dar es Salaam.

Julai 18, mwaka huu, dereva wa idara hiyo makao makuu alikamatwa na kitabu cha stika feki akikisafirisha kwenda uwanja wa ndege kwa ajili ya kukisafirisha kwenda mkoani Mara, kupitia Mwanza.

“Dereva huyo alipobanwa alikiri kuwa katumwa na kigogo mmoja kukituma kitabu hicho kwenda kwa... mkoani Mara, kupitia Mwanza,” kilidai chanzo kingine kutoka idara hiyo mkoani humu.

Chanzo hicho kilidai bosi huyo alipopata taarifa za kukamatwa kwa dereva, aliwajia juu askari wa idara hiyo waliomkamata, huku akitamba hawana mamlaka ya kuhoji kitu kinachotumwa na bosi wao.

Mkuu wa Zimamoto jijini Mwanza, aliyejitambulisha kwa jina moja la Bulambo, hivi karibuni akizungumza kwa simu, alishindwa kukanusha tuhuma za kukamatwa kwa mtumishi huyo na kudai suala hilo hawezi kulizungumza kwenye simu hata kama lipo.

Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili, Naibu Kamishna wa Zimamoto Makao Makuu Dar es Salaam, aliyefahamika kwa jina moja la Shija, alikiri kuwepo kwa dosari kama hizo.

Alisema kutokana na kasoro mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza, waliamua kubadili utaratibu ambapo hivi sasa stika hizo zinasimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

"Hivi sasa sisi hatuhusiki tena na uuzaji wa stika kutokana na kasoro mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza, kazi hiyo hivi sasa inafanywa na TRA," alisema.

Hata hivyo, TRA inahusika na uuzaji wa stika kwa ajili ya vyombo vya moto pekee, wakati zingine kama vile za viwanda bado zinauzwa na jeshi hilo.

CHANZO GAZETI LA UHURU AGOST 6, 2012