Thursday, April 9, 2009

KIPINDI CHA PASAKA

PASAKA NA MASWALI MAGUMU

Kwanini Damu ya Yesu ilijitenga na maji Msalabani?
*Shuhuda kuu sita za ufufuko hizi hapa

WAKATI waamini wa dini ya Kikristo nchini wakiungana na waamini wenzao kote duniani, kuadhimisha Sikukuu ya Pasaka, yapo mambo kadhaa ambayo yamekuwa yakiwatatanisha baadhi ya watu wakiwemo wakristo wenyewe juu ya mtiririko mzima wa matukio yaliyojiri, tangu kukamatwa hadi kufa kwake Bwana Yesu Msalabani.
Inaendelea Uk 3

Makosa yaliyopangwa kumtia Yesu hatiani, aina ya suluba aliyofanyiwa, sababu ya kuchomwa mkuki ubavuni, shahidi zilizopo kuhusu ufufuko wake na kama kweli alifufuka baada ya siku tatu; vikwazo vinavyoukumba ufufuko huo, na sababu hasa za kifo chake, ni miongoni mwa mambo muhimu yanayopaswa kujulikana vema kwa waamini wa Kikristo na watu wengine hususan wakati huu wa maadhimisho ya kumbukumbu ya mateso, kifo na hasa UFUFUKO wa Yesu Kristo.
Jumapili hii ambayo ni Siku ya Pasaka baada ya kupitia Juma Kuu yaani Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu, Jumamosi na hadi Jumapili hii, Yesu anafufuka na kuwa mshindi wa mauti huku Wakristo nchini, wakiungana na wenzao duniani kusherehekea siku hii.
Katika mazungumzo ya hivi karibuni na mmoja wa Wataalamu wa Biblia wa Kanisa katoliki nchini, Padri Titus Amigu ambaye ni Mkuu wa Seminari Kuu ya Peramiho iliyopo Jimbo Kuu Katoliki la Songea, anajibu maswali kadhaa yanayoulizwa na watu wengi ikiwa ni pamoja na tarehe rasmi yaufufuko wa Yesu.
Kwamba, mbona siku ya ufufuko wake yaani sikukuu ya PASAKA, haina tarehe maalumu? Hao, wanataka kujua tarehe hasa aliyofufuka Bwana Wetu Yesu Kristo.
Huku akirejea kitabu cha ZIJUE BARABARA SIKUKUU NOELI NA PASAKA kilichotolewa na BENEDICTINE PUBLICATIONS NDANDA- PERAMIHO, Padri Amigu ambaye pia ni Mkuu wa Seminaarin Kuu ya Peramiho iliyopo Jimbo Kuu Katoliki la Songeaa, alianza kwa kueleza makosa yaliyodaiwa kufanywa na Yesu na kutumika kumtia hatiani.
Anasema kwa kadiri ya sheria za Kiyahudi, Yesu alionekana na hatia ya kuidhihaki Nyumba ya Mungu, ndiko kudai kwamba angeliweza kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu. Anasema, “Kumbe Yesu alikuwa anazungumzia mwili wake mwenyewe.”
Kosa lingine kwa kadiri ya sheria ya Kiyahudi, lilikuwa kujiita Masiha, wakati alikuwa halingani na masiha waliyemtaka na kumsubiri wao, yaani masiha mkombozi wa kisiasa.
Padri Amigu katika mazungumzo hayo mintarafu sikukuu ya Pasaka anasema kwa kadiri yao Wayahudi, Yesu alikufuru kwa kujiita Mwana wa Mungu. “Haya ndiyo makosa makuu yaliyomfanya kuhani mkuu achane nguo yake kwa hasira,” anasema na kuongeza, “Kumbe makosa hayo yote hayakuwa ya msingi kwa kadiri ya sheria ya Kirumi.”
Inaelezwa na vyanzo mbalimbali kuwa, wakati kwa sheria ya Kiyahudi Yesu alipaswa auawe, katika sheria ya Kirumi hakuwa na hatia yoyote ya kumpasa kufa. Vyanzo vinasema, Wayahudi hawakuwa na uwezo wa kumuua mtu yeyote kwa vile sasa walikuwa wakitawaliwa na sheria mpya.

Kwa kuwa Yesu hakuwa na hatia ya kuuawa, Padri Amigu anafahamisha katika ZIJUE BARABARA SIKUKUU NOELI NA PASAKA alipaswa kuachiwa na ili viongozi wa Kiyahudi wasishindwe jambo, na ili waichemshe hasira ya Pilato dhidi ya Yesu, wanamsingizia makosa ya kisiasa ambayo kwayo, kwa sheria ya Kirumi, alipaswa auawe.
Anafahamisha akisema, “Wakamwambia kwa msisitizo Pilato, mkubwa wa Kirumi, kwamba Yesu amejiita mfalme wa Wayahudi, wakati Wayahudi wanatawaliwa na mfalme mmoja tu; Kaisari, na kwamba Yesu amewakataza watu kulipa kodi, wakati walikuwa wanapaswa kulipa kodi kwa Kaisari kila mwaka na halafu kwamba, Yesu aliwachochea watu kufanya mgomo.”
Anasema Wayahudi na wakuu wao kwa kuhakikisha Yesu anauawa, walimshinikiza Pilato na kumtisha kumshitaki kwa Kaisari yaani mfalme wa Dola Kuu ya Kirumi kwa kumwachia mtu kama Yesu aliyejiita mfalme.
Kuhusu sababu za Yesu kuchomwa mkuki akiwa msalabani, inaelezwa kuwa katika kipindi hicho wasulubiwa wenye mbinu za kuning’inia msalabani hawakufa haraka, hivyo wengine waliweza kuishi kwa siku kadhaa.
“Wao walikuwa wakipeleka miili yao juu na chini kwa ajili ya kukitanua kifua na hivyo kujiwezesha kupumua vyema. Kwa namna hii ya kupiga jaramba misalabani, waliweza kurefusha uhai wao,” alisema.
Hata hivyo watu wa namna hiyo kwa mujibu wa Padri Amigu, alipochoka walikufa baada ya dakika chache tu kwa vile vifua viliwabana na hivyo, kushindwa kupumua.
“Wasulibiwa wengine wawili waliosulibiwa pamoja na Yesu siku hiyo, walikuwa na nguvu na mbinu hiyo ya kupeleka miili yao juu na chini, ndipo wakakutwa jioni ile kabla hawajafa.”
Kumbe wakati huo, anasema, tayari Yesu alikuwa keshakufa labda kutokana na udhaifu wake, au kutokana na kutoamua kutumia mbinu ya kupiga jaramba msalabani. Miili ya wasulibiwa ilipaswa kuondolewa msalabani kwani hawakutaka kuichafua sikukuu au Sabato yao kwa kuwepo miili misalabani.
Basi, ndipo walipotakiwa wasulibiwa wote wawe wamekufa kabla ya kuingia kwa Sabato jioni ile. Anasema katika ZIJUE BARABARA SIKUKUU NOELI NA PASAKA kuwa, kwa kuharakisha kifo cha wasulibiwa, wale wezi waliokuwa hai hadi jioni, waliuvunjwa miguu ili wasiweze tena zoezi lao la kupiga jaramba misalabani. Kweli baada ya kufanyiwa hivyo, walikufa baada ya muda mfupi.”
Kuhusu Yesu, Mtaalamu huyo wa Biblia anasema, “Kwa upande wa Yesu, walipomwona amekufa walitaka wajue kama kweli amekufa, maana asije akajisingizia kufa tu. Ndipo kwa kadiri ya sayansi yao wakati ule, wakamtoboa ubavu waone kitatoka nini.”
“Ilipotoka damu na maji, walijua moja kwa moja kwamba Yesu alikuwa amekufa kidhati na wala hakujisingizia.”
Anazidi kufahamisha kuwa, kutoka kwa damu iliyotengana na maji, kwa Wayahudi ilikuwa alama muhimu ya mtu aliyekufa.
“Wahalifu waliokufa waliteremshwa chini ili mradi wasibaki wakining’inia msalabani. Hata hivyo, baada ya kushushwa msalabani wahalifu wengine walikoswa mazishi.
Ndipo miili yao iliachwa ioze yenyewe na hata pengine kuliwa na mbwa.”

Kwa upande wa Yesu, mambo yalimwendea vizuri na mwili wake ulipata mazishi mazuri kwa ruhusa ya Pilato
Kuhusu ukweli kwamba Yesu alifufuka baada ya Siku tatu, Mkuu huyo wa Seminari aliliambia Gazeti hili akisema kuwa, Yesu alifufuka Jumapili.
Anasema, Wayahudi waliita siku hiyo, Siku ya Kwanza ya Juma kwa kuwa hawakuwa na majina kama haya tunayotumia ya Jumapili, Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi.
Wao anasema, waliita Siku ya Kwanza ya Juma ndiyo Jumapili; Siku ya Pili ya Juma ndiyo Jumatatu hadi Siku ya Sita ya Juma ndiyo Ijumaa yetu na Siku ya Saba ya Juma, kwa jina maarufu Sabat, ndiyo Jumamosi yetu.
“Siku zote hizi zilianza jioni na kuisha jioni. Wayahudi hawakuzihesabu siku tangu saa sita usiku hadi saa sita ya usiku siku iliyofuata kama tunavyofanya sisi siku hizi. Siku aliyofufuka Yesu ilikuwa ni siku ya tatu, kama ilivyoandikwa kwa vile alizikwa Siku ya Sita ya Juma yaani Ijumaa; akabaki mle kaburini siku nzima ya Jumamosi yaani Sabato hadi mapambazuko ya Siku ya Jumapili,” anasema.
Hizo ni siku tatu yaani Ijumaa, Jumamosi na Jumapili. Mtaalamu huyo wa Biblia ansema, “Tunazihesabu siku tatu siyo kwa sababu saa 24, bali kwa kadiri ya majina ya siku yalivyo Ijumaa, Jumamosi na Jumapili; siku ya tatu.”
Hata hivyo, ufufuko wa Yesu unakumbwa na matatizo makubwa mawili yaani, wivu wa baadhi ya watu, pamoja na waandishi wasaka fedha.
Anasema, “Tatizo la kwanza ni wivu wa baadhi ya binaadamu. Watu wa aina hiyo, hapo kale hawakukubaliana na ukweli wa ufufiko wa Yesu. Hao, ndio waliowapa hongo askari waseme Yesu aliibwa na wanafunzi wake (Mt 28: 11-n 15)”
“Tatizo la pili, linasababishwa na waandishi wasaka fedha, yaani wenye uchu wa fedha. Hao, huandika vitabu vingi vyenye mawazo kama hayo ya kwamba, mwili wa Yesu uliachwa uoze au kwamba. walipewa mbwa waule.”
“Wengine huandika kwamba Yesu hakufa, bali aliendelea kuishi miaka mingi baadaye. Waislamu, hasa Waahmadiya hueneza habari kwa vitabu, majarida na vipeperushi kwamba Yesu hakufa, bali aliepuka kifo…”
Zipo shuhuda kuu sita zinazothibitisha ufufuko wa Yesu. Kwanza , kabla ya kufa aliishi maisha ya kiadilifu na ya muungano na Mungu.
Padri Amigu anasema, “Tena alisema waziwazi kwamba atafufuka, yaani hekalu la mwili wake litabomolewa, lakini katika siku tatu atalijenga tena na kama tujuavyo Yesu, kama Mwana wa Mungu alikuwa hasemi uongo kabisa. Ndipo mambo yalipodhihiri pale alipotoka kaburini kwa nguvu ya ufufuko. Ndipo maneno yake yakawa kweli kabisa.”
Anasema ushuhuda mwingine ni ule uitwao kisheria ushuhuda wa kimazingira. Huu ndio ushuhuda wa kaburi wazi. “Mwili wa Yesu haukuibiwa na yeyote maana kaburi lilitiwa muhuri na kulindwa na askari. Sasa mwili wake uko wapi?”
Anaongeza, “Amefufuka na ataonekana kwa wafuasi wake. Mtu aliyekufa kweli kweli, ukimwona anatembea tena na kula pamoja na watu maana yake ni nini? Maana yake amefufuka. Yesu alionekana na kula na wanafunzi wake tena. Basi kweli Yesu alifufuka kutoka wafu.”
Ushuhuda wa tatu kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali wa Biblia, ni ule wa watu ambao kiutamaduni, hawakuruhusiwa kuwa mashahidi wa jambo lolote. Wanawake hata kama walikuwa 100, katika utamaduni wa Kiyahudi, hawakuweza kusema chochote cha uzito wa kuwa ushahidi wa jambo lolote.
“Wafuasi bila kudanganya wala kutunga hadithi wanasema waziwazi kwamba, jambo hilo la ajabu la kufufuka kwa Yesu halikutegemea wanaume, ila kwamba Mungu kwa maajabu yake aliwateua wanawake wawe mashahidi wa tukio hilo …”
Ushuhuda mwingine ni ule wa kuundwa na kudumu kwa Kanisa la awali. Kama Yesu asingelifufuka, wanafunzi wangelitawanyika na Kanisa lisingezaliwa na kudumu kama lilivyotokea.
Mwingine ni ule wa Injili. Anasema, “Injili zote zinatangaza kwa anguvu moja kwamba, Yesu alikuwa mzima tena baada ya kifo chake. Hakuna Injili inayositasita kushuhudia ufufuko wa Yesu Kristo.
Ushuhuda wa sita, ni ule wa kubadilika kwa wafuasi. “Baada ya kufa, mitume walikuwa na woga mwingi, hata wakajifungia chumbani. Lakini, walipopata habari kwamba Yesu amefufuka, walijawa na nguvu na kutoa ushuhuda mbele ya watu bila woga tena. Laiti jambo hilo lingekuwa ni la uongo, wangezidi kuingiwa na woga badala ya kujawa na nguvu ya ajabu. Basi kweli Yesu alifufuka kutoka katika wafu.”
Hata hivyo, baada ya kufufuka, Yesu hakumtokea Pilato wala watetesi wake kwa kuwa hakuwa na nia ya kujigamba mbele ya adui zake.
Kuhusu tarehe maalumu ya kufufuka Yesu Kristo kama ilivyo kuzaliwa kwake Desemba 25, Mtaalamu huyo wa Biblia anasema ni kweli kwamba tunaamini na tuna uhakika kuwa Yesu Kristo alifufuka. Lakini hata hivyo, ni lini au ni tarehe gani maalumu lilipotokea tukio hilo zito, hilo hatujui.
“Hata hivyo, kutoijua tarehe rasmi ya ufufuko wa Yesu ni jambo dogo lilsilopasa kutunyima usingizi.”
Kuhusu tarehe ya kuadhimisha Pasaka, kuna historia ya namna yake. Kwa Wayahudi, siku hii ilisherehekewa tarehe 14 mpaka 15 ya mwezi uitwao Nissan. Kwa Wakristo, mambo haya yaliingia katika mgogoro.
Kabla ya utawala wa Papa Viktori kati ya mwaka 189 na 198, Makanisa ya Magharibi mwa Dola ya Kirumi, wakati ule, yalikuwa na kanuni ya kusherehekea Pasaka siku ya Jumapili, yaani siku ya kwanza ya juma, wakati makanisa ya upande wa Mashariki, walifuata kanuni ya Kiyahudi ya kusherehekea Pasaka tarehe 14 ya mwezi wa Kiyahudi Nissan.
Kwa juhudi ya Papa Viktori, ile kanuni ya kusherehekea pasaka tarehe 14 Nissan, ilipotea pole pole hivyo kusherehekewa Jumapili tu. Lakini, kukawa na swali: tarehe ya Jumapili hiyo ipangwe kwa vigezo gani?
Basi, mkutano mkuu wa Kanisa ambaohuitwa mtaguso uliofanyika huko Nicea mnamo mwaka 325 ulilima njia ya kumaliza tatizo hilo . Pale, iliamuliwa kwamba Pasaka isherehekewe na wote siku ya Jumapili moja.
Jumapili hiyo iwe ni ile inayofuata siku ya kumi na nne ya mwezi ule wa pasaka. Na mwezi wa pasaka uwe ni ule ambao, siku ya kumi na nne inatokea baada ya ikwinoksi ya majira ya kuchipukia majani (Vernal equinox) ambayo huko Ulaya huwa ni tarehe 21 Machi.
Lakini kutokana na tofauti za kalenda za watu wa mataifa mbalimbali, kauli ya Mtaguso wa Nikea haikufaulu kusawazisha mambo hayo na hivyo pia, haikupokelewa na Wakristo wote.
Katika enzi za Papa Gregory VIII, kulifanyika marekebisho ya Kalenda hapo mwaka 1582, mabadiliko ambayo yalileta misigano ya ziada.
Kwa upande wa Magharibi, kalenda iliyorekebishwa ilipokelewa na hivyo, Pasaka kusherehekewa kwa hoihoi Jumapili ya Kwanza , baada ya ikwinoksi ya majira ya kuchipua majani mpaka leo.
Kwa hali hii, Pasaka husherehekewa kati ya tarehe 22 Machi na 25 Aprili. Huko Mashariki, ile kalenda iliyopitishwa na Mtaguso wa Nicea haikurekebishwa kwa kadiri ya marekebisho ya mwaka 1582, na hivyo mara chache sana siku ya Pasaka huweza kuangukia katika tarehe sawa na upande wa Magharibi.
Kwa msingi huo, hebu sasa tujiulize kuwa, hivi hatuwezi kuamini ufufuko wa Kristo mpaka tujue tarehe kamili aliyoyofufuka? Je, makadirio waliyoyafanya wazeee wetu hayakidhi kiu yetu?
Hivi kwa mashaka hayo yanayotulazimisha kutaka kujua tarehe kamili eti ndipo tuamini ufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristo, tunawaona watu wa zamani kuwa ni wazembe kwa kutotutunzia tarehe tunazotamani kuzijua?

No comments: