Monday, July 26, 2010

HATA MASHAIRI YANAVIJIMAMBO!! SOMA HAPA!

ELIMU YA UCHAGUZI
Nikiwa Mtanzania, wajibu nauchukua,
Elimu takupatia, ni wewe utaamua,
Moyo ulojaa nia , hatua bora chukua,
Viongozi wenye sifa, twapaswa kuwachagua.

Waja na nyingi ahadi, tena zisizo mashiko,
Wale wote mafisadi, watapata mishitiko,
Kama utajitahidi, kura yako kuwa yako,
Ustawi wa taifa, upo mikononi mwako.

Ustawi wa taifa, upo mikononi mwako,
Watalihodhi taifa, kiuza shahada yako,
Nawe tapoteza sifa, iliyo halali kwako,
Mafisadi twawajua, hakuna kuwachagua.

Wanayo mingi misomo, kuonyesha wanaweza,
Uongozi si mdomo, kama matendo vilaza,
Mwaka huu ni kikomo, chali wote twawalaza,
Nchi sio mali yao, viongozi mafisadi.

Nibora wakae kando, sheria iwatafune,
Hodari kula magendo, na jela wakaione,
Tusije regeza mwendo, lazima watafutane,
Ni kura yangu na yako, tusije poteza njia.

Uongozi sio pesa, kama wanavyo dhania,
Nyerere mfano hasa, ni mengi katufanyia,
Porojo za kisiasa, ndizo wameng’ang’ania,
Shule mwalimu mmoja, elimu gani tatoa?

Twataka maendeleo, na sio porojo zao,
Heshima na utu leo, si hoja vichwani mwao,
Nchi pasi mwelekeo, walinda rafiki zao,
Japo wabaya si wote, wazuri tuwachague,

Si kwa dini wala rangi, tutapata viongozi,
Ukabila si msingi, kupata wachapakazi,
Rafiki wasiku nyingi, si hoja kumpa kazi,
Twataka watu makini, tena wawajibikaji.

Kisa eti ni Mkara, kura hutompatia,
Dhambi ilo tia fora, ndugu yangu wajitia,
Taifa takosa dira, vizazi vitajutia,
Nimaneno ya Nyerere, mimi nimekumbushia.

Na viongozi wa dini, shime nanyi nawatia,
Elimu safi makini, kwa waumini kutia,
Kwani hata wapagani, waweza onyesha njia.
Twataka watu makini, tena wawajibikaji.

Mwalimu Theophil P. Mlungwa
Parokia ya Nyakato-Mwanza
0784 499590/0767 499590

No comments: