Monday, July 19, 2010

NIONAVYO MIMI LILIAN TIMBUKA


Mapambano ya UKIMWI yasigeuzwe mchezo wa kuigiza

Na Lilian Timbuka
ULE msemo kwamba matendo yana sauti kubwa kuliko maneno, una maana kubwa. Ni kwa kipindi kirefu sasa vyombo mbali mbali vya habari hapa nchini vimekuwa vikiandika na kutoa habari mbalimbali zihusuzo harakati za mapambana ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI miongoni mwa jamii ya Watanzania.
Jamii imekuwa ikishuhudia baadhi ya watu waishio na virusi vya UKIMWI wakijitokeza hadharani kwa lengo la kuielimisha jamii namna wanavyoweza kumudu kuishi na virusi vya Ukimwi.
Hata hivyo, Watanzania hao ambao wanaujasiri huamua kujitambulisha katika jamii ya Kitanzania kwa lengo la kuielimisha jamii. Lakini lengo hilo wakati mwingine linaonekana kuwa shubiri kwao kwa sababu jamii yetu bado inaonekana kukumbatia tabia ya unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu hao wanaoishi na virusi vya ukimwi.
Mara zote Waswahili husema “Vitendo vinaongea kuliko maneno.”
NIONAVYO MIMI; Msemo huo umejaa ukweli kwa sababu katika vita dhidi ya UKIMWI hapa nchini, bado uwingi na uzito wa maneno havijawa na uwiano na matendo.
Katika tafiti kadhaa zilizofanywa na Vyombo vya Habari hapa nchini ambapo zimeweza kukutana na hata na watu hao wanaoishi na VVU zimebaini kuwa miongoni mwa watu wanaowanyanyapaa watu wanaoishi na VVU na UKIMWI, ni pamoja na wafanyakazi wa sekta ya afya, ambao mbali na kuwanyanyapaa wagonjwa wanaowahudumia pia hunyanyapaana hata wenyewe kwa wenyewe pale inapotokea kwamba mmoja wao ni mwathirika.
Wazaramo husema “Zilongwa mbali, zitendwa mbali,” wakimaanisha “yanenwayo mengine yatendwayo mengine.”
NIONAVYO MIMI; Jamii inawategemea watu wa Sekta ya Afya kwa kuwa ndio waelimishaji wakuu ama chanzo kikuu cha elimu juu ya maambukizi na ugonjwa wa Ukimwi kwa ujumla.
Aidha, Jamii inawategemea viongozi wao, hususan wanasiasa ambao mara zote wanaongea sana juu ya upigaji vita unyanyapaa, ubaguzi na umuhimu wa kudhibiti maambukizi mapya dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, lakini maneno yamekuwa mengi zaidi ya vitendo.
Mfano rahisi ni pale Rais Jakaya Kikwete alipojitokeza kupima afya yake, kama mfano ili kwamba Watanzania wengine wajitokeze kupima, lakini tukio hilo ambalo lilipaswa kurudisha mwangwi kutoka kwa viongozi wote walio chini yake, kama Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na kadhalika, lakini badala yake suala zima likawa kama fujo za povu la soda zisizodumu.
NIONAVYO MIMI; Kushangiliwa kwa Rais Kikwete wakati alipojitokeza kupima afya yake kisha viongozi wenziwe wasipite njia ile ile aliyoipita ni sawa na ‘kumzomea’!
Nimeamua kuutumia mfano wa wananchi ambao hujitokeza hadharani ili kutahadharisha juu ya mambo kadhaa kwa kuwa kujitokeza kwao hadharani kuna maana kuliko maneno elfu ya ‘wapiga debe’ wasio na matendo.
Kuna haja ya kutenda zaidi ya kuongea.
NIONAVYO MIMI; Pia watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi kujitokeza bila hofu kutangaza hali zao, ili kuweka hali sambamba na wale ambao hawajapima ili waende kupima.
Pia kwa kuwa imebainika kwamba wale ambao watoto wao waliathirika kabla, wakati au baada ya kuzaliwa, hufichwa na wazazi wao kwa hofu ya kunyanyapaliwa na kubaguliwa na jamii, mtazamo huo sasa uwe kinyume chake.
Jambo moja ambalo ninaamini linaweza kumaliza kirahisi zaidi unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya wanaoishi na virusi na wagonjwa wa Ukimwi, ni wao kutojibagua na kujinyanyapaa wenyewe kwanza, wajitokeze, waonyeshe msimamo.
Kukubaliana na hali na kutojiona kuwa tofauti na wengine, kunaweza kuwa msaada mkubwa katika jitihada za kupunguza unyanyapaa na ubaguzi dhidi yao.
Mtakumbuka jinsi ambavyo wanafunzi wanavyowabandika wenzao majina, ikiwa aliyebandikwa jina atakasirika na kuhamaki bila shaka jina hilo litadumu kwake, lakini wale wanaodharau hufanikiwa kuyafuta majina, hivyo tunawashauri wale wanaoitwa majina mabaya ya kunyanyapaliwa wasiyatilie maanani na wawasamehe wanaowaita kwa sababu hawajui watendalo.
NIONAVYO MIMI; ni vema viongozi na wanataaluma wote wakiwemo wa sekta ya afya na ya habari, na wanajamii kwa ujumla, kuongea kwa matendo zaidi kuliko maneno.
Ni vema tukatambua kuwa, hatupaswi kuifanya vita hii ya ugonjwa wa Ukimwi ionekane sawa na mchezo wa kuigiza wa kusema mambo yasiyomaanishwa.

No comments: