Monday, October 11, 2010

Elimu ya uraia mbadala wa siasa za Tanzania
Na Clecence Kunambi
MOJA ya mambo ambayo yamekuwa kwa muda mrefu yakielezwa kuwa ni chanzo cha kudumaa kwa demokrasia nchini Tanzania ni kukosekana kwa elimu ya uraia kwa wananchi wake.
Elimu ya uraia sio muhimu kwa Tanzania pekee bali kwa nchi yoyote ile, inayo lenga katika kumfanya mwananchi atambue haki yake ya msingi na hivyo kumfanya awe na maamuzi sahihi hasa kinapokuja kipindi cha kuchagua viongozi wake.
Miongoni mwa mambo ya msingi yanayosisitizwa katika elimu ya uraia ni pamoja na wajibu wa mwananchi kwa taifa lake,haki zake za msingi kama raia,kujiandikisha kupiga kura,kujitokeza kwenye mikutano mbalimbali ya kampeni kwa lengo la kusikiliza na kupima uwezo wa wagombea.
Hayo ni baadhi ya mambo machache tu kati ya mengi ambayo yanapatikana kwenye elimu ya uraia ambayo inaweza kutolewa na serikali na taasisi mbalimbali mfano vyombo vya habari.
Ni elimu muhimu inayopaswa kutolewa muda wote kwani kama nilivyosema hapo awali ina lenga katika kumfanya mwananchi ajitambue na kuelewa haki na wajibu wake katika taifa.
Ingawa katika mtazamo wa haraka haraka ukizungumzia elimu ya uraia basi hisia za wengi zinaenda katika kutoa elimu ya uchaguzi hasa kutokana na mshiko wa elimu hii kila muda wa uchaguzi hasa mkuu unavyokaribia.
Hakika ni hisia zinazojengwa zaidi na wanasiasa kwa malengo tofauti tofauti kubwa zaidi likiwa katika kuingia madarakani kwa nafasi mbalimbali za uongozi.
Aidha; wanasiasa kutokana na nafasi zao husimamia au hata kujenga ushawishi kwa taasisi mbalimbali katika utoaji wa elimu hii kwa raia.
Hapa pia ningependa kuchukua nafasi hii kuvipongeza vyombo vya habari kwa kazi kubwa vinayoifanya katika utoaji wa elimu hii.
Tokea mapinduzi ya vyombo vya habari ambayo yameenda sambamba na kuingia kwa mfumo wa vyama vingi, hakika kwa mtazamo wa kutoa elimu ya uraia hasa inayojikita katika masuala ya uchaguzi,vyombo vya habari vimefanikiwa sana.
Vituo vya luninga vimekuwa vikiendesha vipindi hata matangazo mbalimbali yanayohamasisha watu kujiandikisha na sasa vinafanya hivyo kuwahamasisha wajitokeze katika kupiga kura, vivyo hivyo kwa redio na magazeti.
Juhudi ambazo zimekuwa zikiungwa mkono na Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini kwa kudhamini matangazo hayo kwenye vyombo vya habari na kupata muitikio mkubwa kutoka kwa wananchi.
Muitikio umeonekana kuwa mkubwa kutokana na watu wengi ukilinganisha na chaguzi zilizopita, kujitokeza na kujiandikisha na wengine hivi sasa tunawashudia wanavyojitokeza kwa wingi katika kusikiliza kampeni zinazofanywa na wagombea mbalimbali.
Kwa hali halisi ya wananchi wa Tanzania,wanahitaji elimu ya uraia ili waweze kufanya maamuzi sahihi sio kwenye suala la uchaguzi bali kwenye mambo mbalimbali ya msingi na yenye maslahi ya taifa hili.
Wanahitaji ili wawe na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kuwa na nguvu kwa viongozi ambao wanawachagua.
Ukijaribu kufuatilia kwa kina vipindi au matangazo mbalimbali yanayotolewa na vituo vya luninga na redio, unaweza kufikiri kwamba baba wa taifa hayati Mwalimu Jullius Kambarage Nyerere hotuba zake zilikuwa zinahusu mambo ya uchaguzi tu.
Mwalimu Nyerere katika kipindi cha maisha yake alizungumza mambo mengi ya msingi, ambayo ni zaidi ya uchaguzi, na hotuba zake ni elimu tosha ya uraia ambapo kama zingekuwa zinawekwa kwa kiwango kikubwa, basi watanzania wengi hasa wa kizazi kipya, wangeelimika na kutambua haki na wajibu wao kwa taifa kwenye mambo mbalimbali.
Hivyo taasisi mbalimbali zilizo mstari wa mbele katika kutoa elimu ya uraia kipindi hiki, zinapaswa kutambua umuhimu wa elimu hii kwa watanzania hata baada ya uchaguzi mkuu. Na hii inapaswa tuitambue wazi kuwa, hii ni pumzi muhimu ya wanasiasa safi.



Kibakwe; Parokia iliyopata ‘mtoto uzeeni’
*Haikuwahi kupata Padri kwa miaka 99
*Ni parokia ya pili kwa ukongwe jimboni Dodoma

Na Damasus Mtalaze
KATIKA Kitabu cha Injili ya Mtakatifu Luka, sura ya kwanza, aya ya Tano hadi 19 (Lk.1:5-19), imeandikwa hadithi ya kuhani Zakaria na mkewe Elizabeth, na kwamba kipindi kirefu cha ndoa yao, wawili hawa hawakubahatika kupata mtoto.
Pamoja na wawili hawa kufikia umri wa uzee pasipokuwa na mtoto, lakini siku moja Malaika wa Mungu alimtokea Zakaria na kumpasha habari njema kuwa Mungu amesikia kilio chake, na mke wake atapata mimba.
Habari hii iliwashtua wanandoa hao kwani tayari Elizabeth alikuwa amefikia umri wa uzee na hatimaye neno hilo lilitimia, kwani Elizabeth alikuja kupata ujauzito na hatimaye mtoto.
Hadithi hii binafsi naifananisha na ile ya Parokia Katoliki ya Kibakwe Jimbo Katoliki la Dodoma, ambayo tangu Ukristo uingie parokiani humo miaka 99 iliyopita, haijawahi kupata Padri.
Huyu ni Padri Inocent Pius Mtawaka, OFM Cap, ‘mtoto wa uzeeni’ wa Parokia hiyo iliyopokea Ukristo tangu mwaka 1911, aliyepokea Daraja Takatifu, Julai 6 mwaka huu, huku ikijivunia kuwa na watawa zaidi ya 20 wanaotumika katika mashirika mbalimbali ya kitawa nchini.
Kabla ya kupatiwa Daraja hilo, Padri Mtawala aliweka Nadhiri za Kwanza kwa Shirika hilo la Wakapuchini, Oktoba 6, 2002 chini ya aliyekuwa Provinsyali wa Tanzania, Padri Beatus Kinyaiya (sasa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu), kabla ya kuweka nadhiri za daima hapo Agosti 2, 2009 huko Kola, Morogoro chini ya Provinsyali Padri Adelwald Itatiro-OFM Cap na baadaye Oktoba 31 mwaka jana, Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Mhashamu Telespol Mkude, kumpatia Daraja ya Ushemasi, tukio lililofanyika kwenye Chuo cha Wasalvatorian jimboni humo.
Tukio hili la upadri lililofanyika kwenye viwanja vya Parokia Katoliki ya Kibakwe likiongoza na Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Mhashamu Juda Thadeus Ruw’aichi na kuhudhuriwa na waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka maeneo kadhaa ya jimbo hilo.
Ninapozungumza haya, simaanishi kuwa Parokia hiyo haijawahi kuwa na wanafunzi wanaosoma katika shule mbalimbali za seminari nchini; inao wengi waliopitia kwenye shule hizo, lakini ukweli ni kwamba, hakuna ambaye amefanikiwa kufikia hatua ya kupatiwa Daraja ya Upadri katika kipindi hicho chote, kutokana na sababu mbalimbali.
Miongoni mwa sababu hizo kwa mujibu wa utafiti usiyo rasmi, ni baadhi ya wazazi kuwazuia watoto wao wasiendelee na wito wa Upadri, badala yake huwashauri na kuwashawishi kuoa ili wapate watoto kwa madai ya kuendeleza ukoo.
Hata hivyo, mawazo kama haya ni finyu kwani wazazi hao ndani ya Parokia hii ambayo ni ya pili kwa ukongwe jimboni Dodoma ikitanguliwa na Parokia ya Itololo-Kondoa iliyoanzishwa mwaka 1908, wanasahau kuwa na padri ni baraka ya pekee katika familia.
Shamrashamra za upadrisho zilianza Julai 4 Mwaka huu majira ya jioni, ambapo Padri Mtawala (wakati alikuwa bado shemasi), alipowasili Parokiani Kibakwe akiongozana na masista wa Huruma Miyuji, akitokea Dodoma mjini alikoshiriki Ibada ya Jumapili katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba.
Kesho yake shamrashamra zilizendelea kwa parokia hiyo kupokea ugeni wa Askofu Ruwa’ichi na Provinsyali wa Shirika la Wakapuchini Tanzania, Padri Adelwald Itatiro,OFM Cap, pamoja na wageni wengineo wakiwemo masista wa mashirika mbalimbali waliofika eneo hilo kwa ajili ya kushirikiana na Wanakibakwe katika tukio hilo muhimu la kihistoria.
Shamrashamra hizo zilinoga zaidi siku ya tukio lenyewe ambapo majira ya saa moja asubuhi, watu wakiwemo waamini na wale wenye mapenzi mema, tayari walikuwa wameanza kulisogelea jengo la Kanisa, wengi wakiwahi kukaa viti vya mwanzoni ili kuweza kulishuhudia vizuri tukio hili.
Ibada ya Misa Takatifu ilianza majira ya saa 4.10 asubuhi katika viwanja vya Parokia ambayo ndiyo iliyozaa Parokia za Mpwampwa, Lumuma, Mbuga, Kinusi , Rudi na Chipogoro.
Katika Ibada hiyo ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Mhashamu Ruwa’ichi, pamoja na mambo mengine, waamini walitakiwa kutambua namna Mungu anavyowapenda, kwani pamoja na kukaa muda wa miaka 99 bila kupata Padri mzawa, lakini neema imeshushwa kwao kabla ya kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Parokia.
Mhashamu Ruwa’ichi alisema, wazazi wamekuwa sehemu ya kikwazo kwa watoto wao kushindwa kufikia hatua ya Upadri, jambo aliloliita kuwa ni wahusika kutokuwa na sauti ya Mungu katika maisha yao.
Hata hivyo alimsisitiza Padri Mtawala kutambua kuwa, changamoto aliyonayo ni kuhakikisha anawatoa waamini wa parokia yake katika giza, huku akiwahubiria wazazi umuhimu wa watoto wao kupelekwa shule za malezi na hatimaye kumtumikia Mungu pindi watakapokuwa mapadri.
“Tunajua Parokia hii ya Kibakwe imepitia kwenye magumu mengi, lakini kwa kusikia sauti ya Mungu, leo hii imepata Padri, hivyo wewe kama mtoto wa parokia hii, watoe watu katika giza na kuwavuta vijana zaidi kuingia kwenye wito wa upadri,” alisema.
Aliwakumbusha wazazi kutambua kuwa, miito ya kumtumikia Mungu inaanzia katika ngazi ya familia, hivyo akawataka waamini kushirikiana katika kutoa malezi yaliyo sahihi kwa vijana wao.
“Kanisa lipo katika kipindi kigumu cha ukosefu wa mapadri na katika kuliondoa Kanisa katika tatizo hili, ni vema familia zikashirikiana katika kulea miito, huku tukitambua kuwa nafasi ya mtoto kwenda katika utawa ni yetu sote, tushirikiane kufanikisha hili,” alisisitiza.
Kwa upande wa watawa wa kike na kiume, Mhashamu Ruwa’ichi ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, anawataka kuwa wavumilivu licha ya kukumbana na changamoto mbalimbali katika utumishi wao lakini anasema hiyo isiwe kikwazo kwao.
Waamini kwa upande wao, wanasema, upatikanaji wa padri mzaliwa wa Parokia ya Kibakwe ni matumaini mapya ya upatikanaji wa miito mbalimbali ikiwemo ya upadri na watawa wa kike na kiume.
Katekista wa Kigango cha Wangi Zamani, Bw. Mathayo Walaza, anasema “kuzaliwa kwa padri ndani ya parokia yetu, ni ishara tosha kwamba imani sasa ipo juu tofauti na kipindi cha nyuma.”
Pamoja na kujivunia kupata padri mzawa, bado waamini wa Parokia Katoliki ya Kibakwe jimboni Dodoma wanayo changamoto ya kuhakikisha wanapata mapadri zaidi badala ya kutegemea wale wa kutoka nje na njia ya kufanikisha hili, ni kuhakikisha wanawalea watoto wao katika misingi ya kuipenda na kuitetea imani yao na hatimaye kuingia kwenye wito huo wa upadri.





KUELEKEA UCHAGUZI MKUU OKTOBA 31, 2010
Wagombea bado hawajagusa kero muhimu za watanzania
Na Dotto Bulendu
MWEZI mmoja umekwisha tangu kuanza kwa kampeni za kuwania kiti cha urais, ubunge na udiwani kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31, Mwaka huu.
Huku kwa upande wa Tanzania visiwani, kampeni zimeingia wiki ya pili baada ya kuchelewa ili kupisha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Wagombea karibu wote katika ngazi tofauti kwa sasa wanahaha kuwashawishi wapiga kura ili wawapatie ridhaa ya kuwawakilisha katika Bunge lijalo na Serikali ijayo.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi tayari imetoa tathmini yake juu ya mwenendo mzima wa kampeni ambapo inaonesha kwa kiasi kikubwa zinaonekana kufanikiwa, pamoja na kuwepo kwa dosari ndogondogo katika baadhi ya majimbo.
Kuna matukio ya baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa kuvamia mikutano ya vyama vingine na kusababisha vurugu, waandishi wa habari kubugudhiwa. Mfano ni tukio lililomkuta Mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi Fredrick Katulanda aliyekutana na kipigo kutoka kwa wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa chama Fulani cha siasa, kushushwa kwa baadhi ya waandishi wa habari katika msafara wa mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais.
Athari nyingine ambazo zimejitokeza katika kipindi hiki cha uchaguzi ni baadhi ya wagombea kuzidisha muda uliopangwa na Tume ya Uchaguzi, baadhi ya wagombea kuacha kunadi sera na kutumia muda mwingi kuzungumzia mambo binafsi ya wagombea wenzake, na si uwezo wa kuwawakilisha wananchi wa jimbo husika, mtego ambao baadhi ya waandishi wa habari wamenasa kwa kuacha kuandika na kutangaza sera za wagombea na ilani za vyama vyao na kuandika malumbano baina ya wagombea yaliyojikita zaidi katika maisha yao binafsi.
Mwezi mmoja umekwisha sasa, wagombea wengi wameshindwa kubainisha tatizo la msingi la elimu ya Tanzania, waliowengi wanazungumzia kero kama za mishahara midogo ya walimu, uhaba wa madarasa, nyumba za walimu, vifaa vya kufundishia na kuacha kulizungumzia tatizo la msingi la elimu yetu ambalo ni ubovu wa mitaala yetu kuanzia elimu ya msingi mpaka ile ya vyuo vikuu.
Elimu ya Tanzania kwa wanaoona mbali, ina mapungufu mengi, ni elimu inayotengeneza makarani wa maofisini, watu wasiojiamini, wasio na ubunifu, wenye tamaa na maisha ya starehe na kujirimbikizia mali hata kwa njia haramu. Kifupi mfumo wa elimu ya Tanzania hauna tofauti na ule wa enzi za ukoloni.
Elimu ya ukoloni haikulenga kuwafanya waafrika wawe wagunduzi na wataalamu, bali ililenga kuwajenga waafrika kama makarani na watafuta kazi za maofisini na katu wasije kuwa na uwezo wa kubuni mambo mapya, hususani ya kiteknolojia.
Leo hii mtanzania aliyemaliza elimu ya chuo kikuu katika masomo ya sayansi hana uwezo wa kugundua chochote zaidi ya kusubiri watu wa magharibi wagundue yeye aje kufundishwa namna ya kukitumia na kukikarabati.
Leo mtanzania aliyemaliza elimu ya chuo kikuu hana ujuzi wowote wa elimu ya ujasiliamali.
Asilimia kubwa ya wahitimu wa vyuo kikuu nchini, wanategemea kuajiriwa katika ofisi za serikali, taasisi za watu binafsi na mashirika, si kujiajiri wenyewe. Huwezi kuwalaumu, hali hii inasababishwa na elimu wanayoipata, imejikita katika mfumo wa kikoloni uliolenga kuandaa watafuta kazi na makalani, na si watengeneza kazi, na bado wagombea wetu hawaioni changamoto hii ambayo ni hatari kwa taifa letu kuwa na vijana wengi wenye elimu ya chuo kikuu isiyo na tija kwao, huku wote wakikazia macho kazi za maofisini, hususani za ukalani na uhudumu.
Leo Tanzania ina wahitimu wengi wa elimu ya chuo kikuu, lakini bado elimu ya Tanzania inategemea machapisho na mawazo ya wasomi toka nchi za magharibi. Tunapaswa tujiulize kuna udhaifu gani kwa wasomi wetu mpaka wanashindwa kuandika vitabu vinavyoweza kutumika katika mitaala ya elimu yetu?
Elimu ya Tanzania haimuandai muhitimu wa darasa la saba, kidato cha nne, sita na elimu ya chuo kikuu kujitegemea na kuwa wabunifu baada ya masomo, haya ni matokeo ya kuendelea kutegemea mitaala ya kikoloni iliyojikita zaidi katika nadharia na mawazo mgando na tegemezi, lakini wanaotuomba kura zetu hatuwasikii kulizungumza hili.
Leo vijana wetu wanamaliza darasa la saba hawajui kusoma na kuandika, rejea taarifa ya utafiti uliofanywa na asasi binafsi ya TUNAWEZA! inauma kuona idadi kubwa ya vijana ambao wanamaliza darasa la saba , lakini hawajui kusoma!
Vijana wetu wanamaliza kidato cha nne katika masomo ya sayansi hawajagusa kifaa chochote cha maabara zaidi ya kuviona katika vitabu, vijana wetu wanamaliza chuo kikuu, lakini uelewa wao katika fani waliyoisomea ni wamashaka na hawaoneshi tofauti na vijana walio makazini, lakini hawana elimu ya chuo kikuu.
Elimu ya Tanzania leo hii inashindwa kumtofautisha kijana wa darasa la saba, kidato cha nne, sita na chuo kikuu. Ukiwakuta pamoja huwezi kuwatofautisha kwani uwezo wao wa kufikiri na kujenga hoja hautofautiani, sasa ni elimu gani hii isiyomtofautisha aliyesoma na asiyesoma?
Nilitegemea wagombea wetu wangezungumzia tatizo la mfumo wa kutunga sheria nchini ambalo linasababisha matatizo mengi katika mfumo mzima wa sheria nchini.
Tanzania bado tunatumia sheria nyingi za kikoloni, wataalamu wetu wa sheria wanakariri sheria zilizotungwa katika mfumo mbovu wa kutunga sheria, Katiba inapigiwa kelele kila kukicha, lakini wagombea wetu hawajaliona hili.
Mikataba inayoingiwa na serikali yetu pamoja na wawekezaji imekuwa na hasara kwa watanzania na namna ya kuivunja mikataba hiyo bado ni shida kutokana na sheria za mikataba bado kuwa na udhaifu na hata wenye jukumu la kujadili mikataba hiyo, hawana uelewa wa kutosha na masuala ya kisheria za mikataba na kama wana uelewa huo, basi wanakosa uzalendo, mambo ambayo ni tatizo kubwa kwa maendeleo ya taifa letu.
Sera za maendeleo nchini bado zina matatizo mengi, wataalamu wetu tuliowapa dhamana ya kutunga sera wameonesha udhaifi mkubwa katika kutunga sera za maendeleo, mathalani sera ya madini ya Tanzania inasisitiza Tanzania kuongeza zaidi malighafi na si kubadilisha malighafi kuwa bidhaa za viwandani.
Sera ya maendeleo ya Tanzania inasisitiza kuzalisha tusichotumia na kutumia tusichozalisha, kitu ambacho ni moja ya tabia za uchumi wa kikoloni, sifahamu kwa nini wachumi na watunga sera wetu wanatupeleka huko.
Leo Tanzania imeua viwanda vyote alivyoviacha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, halafu wagombea wanazungumza habari za ajira kwa vijana bila kuzungumzia habari za viwanda ambavyo viataweza kutumia malighafi zetu.
Nchi yetu ina tatizo la nidhamu katika ukusanyaji wa mapato, ripoti ya Mkaguzi na Msimamizi wa Hesabu za Serikali kila siku analia na matumizi na upotevu wa fedha za serikali ambazo nyingi zinaishia mifukoni mwa wachache huku serikali ikiwa haina pesa.
Utajiri wa nchi hii unawanufaisha wawekezaji kutoka nje huku watanzania wakiendelea kulia na umasikini.
Rushwa imekithiri huku kipato kidogo,utofauti wa kipato,kushuka kwa thamani ya shilingi pamoja na kushuka kwa maadili kukitajwa kama moja ya sababu ya kukithiri kwa vitendo vya rushwa nchini.
Wagombea hawajazungumzia tatizo la watoto wasio na makazi,tatizo ambalo linakuwa kwa kasi nchini na kama taifa halitachukua tahadhari hili ni bomu ambalo tunalikumbatia,tatizo la maambukizi ya ugonjwa hatari wa ukimwi halizungumzwi kimkakati zaidi siasa kuchukua nafasi kubwa katika kampeni za mwaka huu.
Sijasikia mikakati ya dhati ya kupunguza ama kuondoa tatizo la ukiukwaji wa haki za binadamu katika baadhi ya maeneo nchini, mahusiano ya kimataifa, michezo, ujauzito kwa watoto mashuleni, maisha duni ya baadhi ya watumishi wa serikali, matatizo ya ardhi hususani maeneo ya vijijini, makundi ya watu maalum hususani walemavu, mafao ya wastaafu, bei ya mazao ya mkulima wetu, pembejeo na nyenzo za kilimo miongoni mwa wakulima na wafugaji wetu pamoja na mambo mengine mengi yenye tija na faida kwa watanzania.
Wagombea badilikeni zungumzieni ahadi zinazotekelezeka na zilizoko ndani ya ilani zenu, msitumie udhaifu wa watanzania wa kutokusoma kuwahadaa kwa ahadi kemkem ambazo hazimo kwenye ilani zenu na hazitekelezeki.
Watanzania hawahitaji kusikia maisha yenu binafsi, wanahitaji kujua ni kwa namna gani mtawatoa hapa walipo na kuwafanya wafaidi matunda ya utajili tuliozawadiwa na Mwenyezi Mungu.
Sina hakika kama yaliyomo katika ilani za baadhi ya vyama yameandikwa baada ya kufanyika kwa utafiti wa kina wa tatizo la watanzania hususani wanaoishi chini ya dola moja, kwani utitiri wa ahadi ambazo hazimo katika ilani za vyama, kunaleta shaka.
Leo mgombea akifika sehemu fulani akakuta kuna shida ya barababa, anaahidi hapohapo kuwa akipatiwa ridhaa ya kuongoza nchi ama jimbo, atajenga barabara.
Baadhi ya wagombea wameamuna kuvunja sheria ya gharama za uchaguzi bila hofu hii ni kutokana na ubovu na udhaifu wa sheria zetu. Ndiyo maana ninasema, Wagombea bado hawajagusa kero za Watanzania kwa kina katika kampeni zao.
Wawaeleze wazi Watanzania kuwa watawafanyia nini hasa kitakachotekelezeka pale watakapopatiwa ridhaa ya kuongoza.



Ardhi oevu muhimili wa uhai wa mazingira
Na Ismail Ngayonga
ATHARI za uharibifu wa mazingira zimekuwa zikiimeza dunia kila kukicha, hali inayosababisha kuwepo kwa baadhi ya viumbehai duniani kupotea, kutokea kwa mabadiliko ya tabianchi na hata kuhatarisha uhai wa binadamu.
Jambo hili limekuwa likichangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu katika harakati za kujiletea maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ambazo huathiri mazingira.
Wataalamu wanasema takribani mito 70 mikubwa duniani iliyokuwa na maji, imekumbwa na ukame na sasa haina maji tena. Hii ina maana kwa baadhi ya nchi kama Tanzania ambazo zimekuwa zikitegemea maji kwa ajili ya shughuli mbalimbali, zinaathirika.
Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na uharibifu wa mazingira unaondelea ambao umesababisha vyanzo vya maji kutoweka, vina vya mito, mabwawa, bahari na maziwa kupungua pamoja na magonjwa mbalimbali yanayotokana na uchafuzi wa mazingira.
Kinachotia hofu ni kwamba, huenda baadhi ya sehemu za Tanzania zikawa jangwa kutokana na kukithiri kwa kukatwa kwa miti. Takribani hekta 220,000 za misitu hufyekwa kila mwaka kwa mahitaji ya nishati hususan ile ya mkaa, kilimo kisicho endelevu na biashara ya magogo.
Miongoni mwa maeneo yaliyopo katika hatari za uharibu wa mazingira ni pamoja na maeneo ya ardhi oevu, ambapo kwa mujibu wa wataalamu wa mazingira, wanasema maeneo chepechepe (oevu) ni miongoni mwa mifumo mitatu mikubwa ya ikolojia duniani pamoja na misitu na bahari.
Maeneo oevu (Ramsdar), ni sehemu zenye umuhimu wa pekee duniani katika suala zima la uhifadhi wa mazingira. Ardhi oevu ni ile ardhi ambayo msimu wote wa mwaka huwa na unyevunyevu.
Jina la Ramsdar limetokana na mji wa Ramsdar uliopo nchini Iran ambapo ndipo mkataba wa kutunza maeneo ya ardhi oevu duniani ulisainiwa mwaka 1971. Kwa hiyo basi mwaka 1971 ndipo yalipofanyika maamuzi ya kulinda maeneo oevu dhidi ya uhalibifu, ili yaweze kutumika katika shughuli endelevu kama vile vyanzo vya maji.
Mpaka sasa kuna mataifa 152 duniani yaliyotia saini mkataba huo wa kulinda ardhi oevu. Kuna maeneo tengefu 1608 ya Ramsdar duniani yanayochukua ukubwa wa ekari Milioni 140. Tanzania imejiunga na Mkataba wa ardhi oevu (Ramsar) Agosti, 2000.
Kwa mujibu wa Wataalamu wa mazingira wanasema mfumo wa ardhi oevu unaofaa, ni sehemu muhimu ya mfumo wa taifa wa usalama wa ikolojia na msingi muhimu wa maendeleo endelevu ya uchumi, kwani mazingira endelevu yana uhusiano mkubwa na maisha ya binadamu pamoja na viumbe hai wengine. Binadamu anahitaji maji, chakula nishati na kadhalika katika kuendeleza maisha yake ya kila siku.
Wataalamu hao wanasema ardhi oevu ni moja ya bayoanuwai bora zaidi katika dunia, kwani ni makazi ya viumbe hai wengi, kama vile alga na mimea mbalimbali na wadudu, viumbe aina ya chura, ndege na samaki. Ardhi oevu inasaidia sana katika mchakato wa asili wa kuondokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Aidha, manufaa mengine yatokanayo na ardhi oevu ni pamoja na kusafisha sumu kutoka kwenye maji. Ni nzuri kwa kunyonya kemikali kwa mfano zile zinazotokana na sekta ya madini, ambazo zinajichuja katika migodi na kusafirishwa katika mifereji ya migodi.
Pia ni nzuri katika kusafisha kemikali kama nitrogen na phosphorous, ambazo zinapatikana kwa wingi katika mbolea za chumvi chumvi zinazotumika kwa kilimo na pia kuchuja maji taka.
Katika miaka ya hivi karibuni, maeneo ya ardhi oevu yamekuwa yakikabiliwa na changamoto mbalimbali za uharibifu wa mazingira zinazotokana na shughuli za binadamu ikiwemo kilimo, uvuvi, uwindaji, ufugaji na ukataji miti.
Mabadiliko ya hali ya hewa ni tishio jingine kubwa la ardhi oevu, inaelezwa kuwa hupunguza unyevu katika maeneo mengi na kuongeza myeyuko kutokana na joto kali na kusababisha mito mingi kutoweza kuhifadhi na kunyonya gesi joto zote katika misitu bila ya kuwa na mtandao wa nyongeza wa kutoka katika ardhi oevu na kanda ambayo ina misitu.
Katika Tanzania kuna maeneo manne ya ardhi oevu, ambayo ni ardhi oevu ya Muyovozi katika mto Malagalasi Kigoma, ardhi oevu ya Ziwa Natron- Manyara, ardhi oevu ya Bonde la mto kilombero- Morogoro, na ardhi oevu ya Bonde la Rufiji- Mafia hadi Kilwa.
Maeneo mengine ambayo taratibu zake bado hazijakamilika, ili yaweze kuhifadhiwa ni Mto Kagera na bonde la Mto Usangu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Batilda Burian anasema takriban asilimia 10 ya eneo la nchi ni ardhi – Oevu na lina umuhimu mkubwa kiuchumi, na kijamii kwani ni chanzo muhimu cha upatikanaji wa maji katika maziwa na mito na hivyo huwa nyenzo muhimu katika uzalishaji wa umeme.
Dkt. Batilda anasema wananchi wana kila sababu ya kutunza na kuyalinda maeneo ambayo ni ya ardhi oevu kwani yana umuhimu mkubwa hasa ikiwa ni pamoja na matumizi ya maeneo hayo katika shughuli za kilimo, uvuvi, uwindaji na matumizi ya kiikolojia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kwani huweza pia kudhibiti mafuriko na kuwa chanzo cha upatikanaji wa maji wakati wa ukame.
Kwa mujibu wa Dkt. Batilda anasema, pamoja na umuhimu mkubwa wa ardhi oevu kiuchumi, kijamii na kiikolojia, upo uharibifu mkubwa unaosababishwa na mambo ya uchafuzi unaotokana na utupaji wa taka ngumu na maji taka, kilimo kisicho endelevu, uchomaji moto na ufugaji usiozingatia uwezo wa malisho, hivyo ni budi kuwa na mipango endelevu ya kusimamia matumizi ya rasilimali zilizomo katika ardhi- oevu.
Naye Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Christopher Chiza, anasema Serikali ipo makini katika kuhakikisha mazingira yanatunzwa na maeneo hayo ya ardhi oevu yanaweza kutumika kwa shughuli nyingine za binadamu ambazo hazina athari kwa mazingira ya nchi.
Chiza alisema Serikali sasa imeandaa rasimu ya sera ya umwagiliaji ambayo itachochea kasi ya kuendeleza, kutunza na kuendesha skimu za umwagiliaji zitakazokuwa endelevu.
Alisema sera hiyo inayopendekezwa inalenga pia kuzielekeza sekta za umma na binafsi katika kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji, ambapo katika maandalizi ya rasimu ya sera hiyo, Serikali imezingatia maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwamo wabunge, wakulima, taasisi za elimu na baraza la mazingira.
Aidha, alisema uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuunda Wizara ya Maji na Umwagiliaji, unalenga pamoja na mambo mengine kuwa na sera ya umwagiliaji inayohusiana na sera nyingine kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuondoa migongano katika matumizi ya rasilimali za maji.
Aliitaja mikakati iliyowekwa na serikali katika kuhakikisha kuwa miradi ya umwagiliaji inakuwa endelevu, ni kusimamia utekelezaji wa sheria ya mazingira na sheria ya rasilimali za maji, ili kuhakikisha kwamba vyanzo vya maji vinatunzwa na kupeleka bungeni muswada wa sheria itakayosimamia sekta ya umwagiliaji.
Alisema mambo mengine ni kuainisha majukumu ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, sekta binafsi na taasisi zisizokuwa za kiserikali, kufanya utafiti wa kilimo cha umwagiliaji, kuzingatia tahadhari za utunzaji wa mazingira, kuweka mifumo ya vyombo vya watumia maji, kutenganisha majukumu ya serikali kuu na wakulima na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.
Kutokana na uhusiano usioweza kutenganishwa wa maisha ya binadamu na mazingira, juhudi mbalimbali lazima zichukuliwe kukabiliana na hali hiyo na kuitaka jamii kutambua umuhimu huo kwa kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali kuhifadhi mazingira
Miongozo madhubuti ya maendeleo na mipango, inahitajika kwa ajili ya matumizi endelevu na kuhifadhi ardhi oevu kwa faida ya binadamu na viumbe wa asili, kama ilivyowekwa katika mkataba wa Ramsdar, ambao unataka kila mwanachama aweke mikakati inayozingatia matumizi ya busara ya maeneo ya ardhi oevu.



Wananchi waelimishwe juu ya sheria ya ardhi

Na Lilian Timbuka
KAMA kuna mambo ambayo yanachukuliwa kwa unyeti wa hali ya juu nchini hasa wakati huu taifa linapozidi kuzama katika mikataba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni suala la ardhi.
Unyeti wa ardhi hautazamwi kwa maana ya tishio la wageni kutoka nje tu, bali pia jinsi sheria zetu za ardhi zinavyomlinda mwananchi wa kawaida ambaye anamiliki eneo lake, kisheria au hata kienyeji.
Mara nyingi kumekuwa na kilio cha wananchi katika maeneo mengi ambayo hutwaliwa ama na serikali kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kijamii; au hata pale yanapochukuliwa na wawekezaji binafsi.
Kwa ujumla, kilio kimekuwa juu ya fidia stahili ambayo wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa wanastahili kulipwa. Vilio ni vingi mno.
Ndiyo maana kwa kutambua machungu haya Taasisi ya Utafiti na Utetezi wa Haki Ardhi, imekuwa ikiendesha semina mbalimbali kuhamasisha wananchi ili wajue haki zao katika umiliki wa ardhi.
Katika semina hizo, maofisa wa Taasisi hii, pamoja na mambo mengine wamekuwa wakiwapatia wananchi changamoto itakayowasaidia kutambua fidia wanayostahili kulipwa ili kupisha maeneo yao yachukuliwe na serikali. Wamekuwa wakieleza na kuwasisitiza wananchi kuwa, kuyajua mambo haya ni haki yao kisheria.
Haki hiyo inaruhusu wanaohamishwa kuelezwa kiasi cha fidia watakayolipwa baada ya tathimini kufanyika, na si kusubiri kupokea hundi ambayo hawajui ni kitu gani wanalipwa.
Katika mada zao nyingi, zimekuwa zikijikita kwenye taratibu za sheria za ardhi katika utoaji wa fidia kwa wananchi wanaohamishwa katika maeneo yao. Wamekuwa wakiweka wazi kwamba wananchi wanapaswa kuhudhuria mikutano inayoitwa na baraza la ardhi la kijiji, ambalo linajukumu la kuwafahamisha wananchi juu ya ama kuchukuliwa na serikali kwa ardhi yao ama wawekezaji ambapo baada ya mkutano na wananchi juu ya kusudio la kuwahamisha, wahusika hupewa fomu namba 69.
Inaelezwa kwamba, fomu hiyo hupewa kila anayetakiwa kuhamishwa ili afanyiwe tathimini, hiyo ni kama kitambulisho chake, pamoja na mambo mengine fomu hiyo husainiwa na afisa ardhi mteule na inamtaka mmiliki wa ardhi ajaze fomu ya ardhi namba 70 pia.
Kulingana na elimu inayotolewa kwa wananchi wanaoshiriki semina hizo, imebainika kwamba wapo maofisa wa aina mbili katika kufikiwa kwa thamani ya eneo la mwananchi, hawa ni wathamini na mpima ardhi; kazi ya mthamini ni kukagua jengo ndani na nje ili kujua malighafi iliyotumika katika ujenzi na kuhesabu mazao yaliyopo.
Kwa upande wake mpima ardhi hupita katika mipaka ya ardhi, kuchukua vipimo vitakavyomsaidia kupata ukubwa wa eneo, kisheria shughuli zote hizi ni lazima zifanyike mbele ya mwananchi ambaye anamiliki eneo hilo.
Kazi hiyo ikikamilika takwimu za mthamini na mpimaji hujazwa kwenye fomu ya uthamini na ni lazima isainiwe na mthamini, mwenye eneo pamoja na kiongozi wa eneo husika.
Hakuna ubishi kwamba kama mchakato wa kuchukua eneo la mwananchi ndivyo unataka kwenda, hakika kusingekuwa na malalamiko kama ambayo tumeshuhudia yakitokea mara kadhaa kwa wananchi wanaohamishwa kwenye maeneo yao.
Ipo mifano hai juu ya malalamiko hayo, lakini ukitazama kwa makini, sheria inaweka wazi mchakato mzima wa kutwaa eneo la mwananchi, kwamba ni lazima ashiriki katika zoezi zima la kutathmini eneo lake kwa maana awepo wakati wa uthamini, lakini pia aweke saini kazi hiyo ikishafanyika kwa nia ya kujithibitishia kwamba haki kwa upande wake imetendeka.
Ni jambo la bahati mbaya kwamba, pamoja na utaratibu huu wa kisheria kuwa bayana hivyo, haijulikani ni kwanini tunaendelea kusikia malalamiko ya wananchi kupunjwa fidia, au wengine kuongezewa mno.
Ipo mifano hai, wapo wanaosema wazi kwamba baadhi ya mali zao, kama mimea, au nyumba na baadhi ya maendeleo yaliyofanywa juu ya ardhi yao huachwa, ni kwa kutambua ukweli huo, ni vema Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ikachukua wajibu wa kueneza elimu juu ya sheria ya ardhi kwa wananchi.
Nimeyasema haya kwa sababu baada ya kufunguliwa kwa mipaka ya soko la pamoja, ingawa bado suala la ardhi si sehemu ya soko la pamoja, lakini kupitia kigezo cha uwekezaji, ni rahisi zaidi wananchi kudhulumiwa haki zao kama watakuwa hawajui wanavyolindwa na sheria ya ardhi.
Tukubaliane kama taifa kuwa, zinatakiwa juhudi za dhati ili kuhakikisha kuwa Elimu kuhusiana na suala hili inawafikia wananchi wote ili kuhamasisha uwelewa wa wananchi juu ya haki zao kwenye miliki ya ardhi.

No comments: