Sunday, November 28, 2010


NHC kupandisha kodi ya nyumba

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limesema litapandisha kodi za baadhi ya nyumba zake huku likiendelea na jitihada za kujenga nyingine. Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu (Pichani), alipozungumza na Jukwaa la Wahariri Tanzania kwenye hoteli ya White Sands, Dar es Salaam. Mchechu alisema NHC ina mpango wa kupandisha kodi kwa baadhi ya nyumba kwenye maeneo, lakini maeneo mengine itabaki palepale.
“Tutapandisha kodi kwa baadhi ya nyumba na hasa zinazotumiwa na watu wenye uwezo mkubwa kifedha...katika maeneo kama ya Tandika, Ilala na Keko, kodi itabaki palepale,” alisema Mchechu. Pia alitoa msimamo wa shirika hilo kuwa nyumba zake zilizopo maeneo ya Upanga, Kinondoni na Masaki katu haziuzwi na kuwa nyumba zinazoweza kuuzwa ni katika maeneo mengine.
Alisema licha ya hatua hiyo, uongozi umepanga kuhakikisha nyumba za shirika zinakuwa na hadhi inayostahili ikiwemo kufanyiwa matengenezo.
Kuhusu ujenzi wa nyumba, Mchechu alisema NHC inakusudia kujenga nyumba 10,000 za hadhi ya kati na ya juu kwa ajili ya kuziuza katika kipindi cha hadi kufikia mwaka 2015.
Alisema nyumba hizo zitajengwa na kuuzwa kwa utaratibu maalumu na ambao utatoa fursa kwa watu wengi kuzipata na kwa gharama nafuu, tofauti na hali ilivyo sasa.
Mchechu ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuongoza shirika hilo kongwe, alisema wana mpango wa kupunguza uhaba wa nyumba kwa kutekeleza miradi mbalimbali mikubwa na ambayo kwa sasa ipo kwenye mchakato.
NHC katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake, imepanga safu ya wakurugenzi wengi wapya wakiwemo waliokuwa wakitekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa nyumba huko Dubai.
Katik akipindi cha hivi karibuni, NHC imefanikiaw kufuta mikataba zaidi ya 50 ambayo imebainika kuwa na dosari ikiwemo kutolinufaisha shirika na badala yake kunufaisha watu wachache.

No comments: