Monday, February 15, 2010

UJUMBE WA KWARESIMA 2010

1.0 UTANGULIZI
Wapendwa Wanafamilia ya Mungu,
Mapadri, Watawa, Waamini Walei na watu wote wenye mapenzi mema:
Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo!
Tunafurahi kuwaandikia ujumbe huu wakati tunaingia katika kipindi maalumu cha Kwaresima, kipindi cha Neema, na kipindi chenye changamoto nyingi pengine kuliko vipindi vyote katika mwaka wa Liturujia. Ingawa katika mapokeo kipindi hiki kinajulikana kama siku arobaini za kusali, kufunga na kufanya matendo mema, huku msisitizo ukiwekwa kwa mtu binafsi kujinidhamisha na kuutesa mwili kwa matendo ya kujinyima, maana halisi ya Kwaresima siyo tu msisitizo katika kujinyima na kufunga labda pamoja na matendo kadhaa ya kiroho; siyo tu zoezi la nidhamu ya binafsi, ni kipindi maalumu kwa Kanisa zima, kwa ajili ya kufanyika upya. Ni kipindi ambacho Taifa zima la Mungu linapaswa kumwongokea Mungu. Ni kipindi ambacho Kanisa linapaswa kumwelekea Kristo na kumfanya awe Kiongozi wa maisha yetu. Na kwa kweli huu ni mchakato siyo tu wa kipindi cha Kwaresima, bali wa kudumu.

Kwaresima ni wakati wa kukua katika Kristo, ni wakati wa kuifanya mioyo yetu iwake mapendo ya Kristo, kama tunavyosali siku ya Jummane ya Juma la Kwanza la Kwaresima “Ee Bwana, utuangalie sisi watu wako tunaojitesa kwa kufunga; uifanye Mioyo yetu iwake Mapendo yako[1]”. Kwaresima ni kipindi ambacho mioyo yetu inatakiwa kumtamani Mungu zaidi na zaidi. Ni kitu gani kikubwa tunachopaswa kuomba katika kipindi hiki cha Kwaresima zaidi ya kuomba uongofu wa mioyo mioyo yetu ili imtamani Mungu?

Huo ndio ukweli aliotusisitizia hata Mtakatifu Agustino kwamba, ni Mungu pekee ndiye anayeweza kukidhi hamu ya mioyo yetu[2], ambayo ndiyo moja ya malengo makuu kabisa ya kipindi cha Kwaresima: kumtafuta Mungu, kukua katika kumtafuta, kuwasha mioyo yetu na Upendo wa Mungu. Tuombe ili Kwaresima hii itusaidie kukua katika Kumtafuta Mungu, kama Mzaburi anavyotukumbusha “Ee Bwana, usikie, kwa sauti yangu nalia, unifadhili, unijibu – Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta” ( Zab 27:8). Tafakari itakayotuongoza katika kipindi chiki cha Kwaresima mwaka huu ni “ Ninyi ni Chumvi ya dunia” (Mt 5: 13 ). Tunatafakari maneno haya ya Bwana wetu Yesu Kristo, kama Taifa la Mungu tukiwa katika Kipindi ambacho kuna matukio ambayo, kwa hakika, yanatugusa kama Waamini, vile vile kama – Raia wa nchi yetu ya Tanzania.

Kwanza kabisa, Baba Mtakatifu, Benedikto XVI alitangaza rasmi Mwaka wa Padri – mwaka aliouzindua Ijumaa ya tarehe 19 Juni 2009 na utafikia kilele chake hapo 19 Juni 2010. Ni mwaka ambao, Baba Mtakatifu analialika Kanisa zima kutafakari kwa namna ya pekee zawadi ya Upadri kwa Kanisa na kwa wanadamu wote. Hali kadhalika, Baba Mtakatifu anasema, mwaka huu ni fursa kwa Mapadri wenyewe kutafakari kwa kina wito wao na kuweza kufanya jitihada za kuwa Mashahidi wa kweli wa Injili katika Ulimwengu wa leo[3].

Pili tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Mkutano Maalum wa pili kwa ajili ya Afrika wa Sinodi ya Maaskofu, uliofanyika Mjini Roma tarehe 4- 25 Oktoba 2009 ukiwa na dhamira “ Kanisa katika Afrika na huduma ya Upatanisho, Haki na Amani: Ninyi ni Chumvi ya dunia….. Ninyi ni Nuru ya Ulimwengu…” (Mt 5:13. 14). Ni dhamira iliyobeba ujumbe mzito na ni vizuri wakati tunasubiri kupokea kwa mikono miwili matokeo ya Sinodi hii, kila mmoja wetu, kadiri ya ngazi yake, hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima, ajitafakari kuona anatoa mchango upi katika kuleta Upatanisho, Haki na Amani katika jamii yetu Barani Afrika.

Tatu, tunafatakari ujumbe wa “Ninyi ni Chumvi ya dunia” wakati Taifa letu likiwa katika mchakato kuelekea Uchaguzi Mkuu utakofanyika Oktoba 2010. Uchaguzi Mkuu ni tukio la Kisiasa / Kijami. Mafundisho ya Kanisa yamesisitiza siku zote ukweli kwamba, Waamini hawana budi kushiriki katika masuala ya Umma: ya kisiasa na kijamii, uongozi na utamaduni ambayo yana lengo la kujenga kwa pamoja na kitaasisi manufaa ya wote[4]. Hivyo basi, pamoja na kusali ili uchaguzi uweze kufanyika kwa amani, tungependa kuwahimiza kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi huo katika hatua zake zote, ili kuiwezesha nchi yetu kuwapata viongozi bora.

2.0 FUNDISHO LA JUMLA
“Ninyi ni Chumvi ya dunia…” (Mt 5:13) Katika muktadha yalipo maneno hayo yameelekezwa kwa wale wanafunzi wanaotajwa kuwa “ Wana heri,” “wapatanishi” na “wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki” n.k, (taz. Mt 5:1 n.k) wale wanaosikia maneno yake, wanafunzi wake, ambao wanathibitishiwa kwamba Ufalme wa Mbinguni ni wao. Ni maneno ambayo wanaambiwa vile vile wanafunzi wa Yesu wa nyakati zote. Chumvi ni kitu cha kawaida kabisa katika maisha ya kila siku. Bwana wetu Yesu Kristo anapotumia mfano wa kitu hiki cha kawaida kabisa na kuwafananisha nacho wanafunzi wake, hana maana ya kuwapongeza, bali kuwaonya kwamba upendeleo wanaoupata kama wana wa Ufalme wa Mbinguni, siyo kwa ajili ya manufaa yao tu, bali kwa faida ya wengine, na kwa utukufu wa Mungu Baba aliye mbinguni[5]. Kuwa Chumvi ya dunia ni mfano unaodokeza wajibu wa wanafunzi wa Bwana wetu Yesu Kristo[6].

Kadiri ya mafundisho ya mapokeo ya Wayahudi, hata kisayansi, chumvi haiwezi kupoteza nguvu yake ya kukoleza na ikabaki kuwa chumvi. Mwinjili Marko, katika Injili yake anataja ladha ya Chumvi na anasema kwamba ama Chumvi ni chumvi ama si Chumvi; hakuna kitu kingine: “Chumvi ni njema, lakini Chumvi ikiwa si Chumvi tena, mtaitia nini ikolee?” (Mk 9:50). Suala hapa ni kwamba, iwapo chumvi imekosa sifa ya kutumika tena, haifai kwa chochote, bali inaleta madhara ya kutokoleza na kutozuia uozo, kwa hiyo inapaswa kutupwa tu na kukanyagwa na watu.

Hivyo, kwa kulisikiliza neno la lake, wanafunzi wanapaswa, kwa matendo yao, kuwa katika dunia na sifa ya jinsi chumvi ilivyo katika chakula: kiungo cha lazima[7]. Ni mwaliko kwa Wanafunzi wake kuishi maisha ya ushuhuda[8]. Bwana wetu Yesu Kristo anaposema kwamba “Ninyi ni Chumvi ya dunia”, anawataka Wakristo wote kupenyeza ladha njema katika jamii wanamoishi na kusaidia kuhifadhi mambo mema katika jamii hiyo kwa kuzuia uharibifu. Watafanya hivyo kwa namna gani? Kwa uwepo wao hai katika nafasi mbalimbali za maisha. Jinsi matokeo ya Chumvi yanavyosikika tu pale inapochanganywa na chakula, hali kadhalika uwepo wa Bwana wetu Yesu Kristo duniani unaweza kutambulikana tu pale wafuasi wake wanapochanganyika na wengine. Kama vile chumvi isivyo kwa ajili yake yenyewe, hali kadhalika na Ukristo ndani ya mtu hauwezi kuwepo kama dini kwa ajili yake wenyewe. Ubatizo unatutuma kwenda kuwa mashahidi katika hali na mahali halisi tunakoishi na kufanya kazi: katika familia, sokoni, benki, hospitalini, shuleni, katika mambo yanayohusu siasa, jamii na utamaduni n.k. Haya yote ni maeneo ambako Wakristo wanatumwa ili kupenyeza ladha ya imani yao. Ni mwito wa kwenda kufanya alivyoamuru Kristo mwenyewe (rej. Mt 28: 19).

3.0 MAENEO MBALIMBALI YA UKOLEZAJI
3.1 Familia
Familia ni jumuiya ya msingi; ndicho chanzo cha uhai mpya wa binadamu, ndicho kituo cha kawaida ambamo mtu anaweza kupata maendeleo ya kiroho na kimwili kwa ukamilifu. Maisha ya kimaadili ya kibinadamu na uwezo wake wa kupenda, yanaamshwa kwanza na upendo wa wazazi. Kwa njia ya familia, kama chembe yake hai, jumuiya inajengwa na kuendelezwa. Mafundisho ya Kanisa yatwambia” Ustawi wa mtu binafsi na wa jamii ya kibinadamu na ya Kikristo, hufungamana kabisa na hali njema ya kindoa na kifamilia”[9]. Kwa hiyo, ujenzi wa Jumuiya yoyote ile ya kibinadamu unaanza na kufanywa upya kwa njia ya familia. Tunawaangaliza kujihami na virusi vya itikadi zenye sumu zinazotoka nje, zikidai kuwa ni utamaduni wa “kisasa” wa kukataa watoto[10].

Familia ya Kikristo ni maisha ya umoja na ushirika kati ya mume na mke. Kwa njia ya agano la ndoa, mume na mke siyo wawili tena bali ni mwili mmoja na wanaalikwa kila siku kukua katika ushirika wao kwa njia ya uaminifu wao kwa ahadi zao za ndoa kwa kila mmoja kujitoa kwa mwingine[11]. Hilo ndilo jambo la kwanza na la msingi kabisa katika ndoa ya Kikristo; kwamba wawili wanakuwa mwili mmoja (rej. Mwa 2:24; Mt 19:5-6).
Mkristo anayefunga ndoa, “anamwacha baba yake na mama yake” ili awe kwa ajili ya mtu mwingine. Anawekeza katika uhusiano huu mpya. Kwa namna hiyo, familia ya Kikristo inakuwa maskani ya Kiroho, maskani yaliyojengwa juu ya msingi wa upendo ambao Baba Mtakatifu Benedikto XVI anasema ”Upendo kati ya mume na mke, ambapo mwili na roho vinaungana na ambapo wanadamu wanaonja ahadi isiyozuilika ya furaha[12]”.

Ili kudumisha ushirika na muungano huu, wanandoa wanahitaji kuishi pamoja, kupanga mambo yao pamoja na kutekeleza kwa pamoja. Muungano wa ndoa maana yake ni mshikamano wa kweli katika mahitaji yote ya mwili na roho, katika machungu yote na katika furaha zote. Mahusinao haya ya pamoja, yanahitaji wanandoa wawe waaminifu kila mmoja kwa mwingine ili kujenga familia imara na yenye amani.

Ni jambo la kutafakari kwa kina kuona kama kweli familia zetu ni vitalu vya upendo. Kama kweli ndani ya familia zetu kuna umoja, ushirikiano, upendo na uaminifu, mambo ambayo ni chimbuko la furaha na amani katika familia. Pamoja na kumshukuru Mungu kwa ajili ya familia nyingi nzuri, kwa unyenyekevu wote mbele ya Mungu, yatupasa tukiri kwamba, umoja, ushirikiano, upendo na uaminifu kwa kiasi kikubwa vinakosekana ndani ya familia nyingi. Hicho ndicho kinakuwa chanzo cha migogoro inayosababisha janga la kusikitisha la kuvunjika kwa ndoa nyingi. Katika baadhi ya familia, bado yanaendelea matatizo ya unyanyasaji wa kijinsia, ukatili hasa Wanaume dhidi ya Wanawake, (ingawaje hatuwezi kukataa kabisa kwamba hakuna Wanawake wakatili dhidi ya Wanaume) na ubadhirifu ambao unasababisha umaskini katika familia. Mambo hayo yanazifanya familia nyingi zikose sifa ya kuwa familia za Kikristo kweli. Tunapotafakari ujumbe wa Kwaresima wa mwaka huu, “ Ninyi ni Chumvi ya dunia” hatuna budi, kujihoji na kujipekua ili kuona kinatakiwa nini ili tuzifanye familia zetu kuwa za Kikristo kwa kujenga upendo wa kweli, umoja, ushirikiano na uaminifu.

3.2 Wajibu wa Wazazi kwa Watoto
3.2.1 Malezi kwa ujumla
Wajibu wa wazazi kwa mtoto wao unatokana na ukweli kwamba wamemzaa na kwamba kiumbe huyu mpya anakuja ulimwenguni akiwa hana msaada wowote. Wajibu wa kwanza wa wazazi, ambao unatangulia kabla ya wajibu wowote ule, ni kuwajibika kwa kutwaa majukumu ya wazazi. Wanapaswa vile vile kuwa na upendo wa kweli kwa watoto, siyo upendo wa kibinafsi, ama upendo wa kupita kiasi unaosababisha kedekeza watoto. Kupenda kupita kiasi, kudekeza, kwaweza, kwa namna fulani, kuwa sawa na kukosa upendo. Juu ya hili, Maandiko Matakatifu yatwambia “Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe, bali yeye ampendaye humrudi mapema” (Mit 13:24).

Katika hayo, tunasema, kwa masikitiko makubwa, yale yanayotokea mahali pale wazazi wanapokosa kuwajibika kama wazazi, wanapokosa upendo wa kweli kwa watoto wao. Kwa toba tuwafikirie watoto wengi waliozagaa katika miji yetu, wale ambao, kwa bahati mbaya, wanajulikana kama ”Watoto wa mitaani” . Ongezeko la watoto hao siku baada ya siku, je, si kiashiria kwamba mahali fulani kama wazazi na kama jamii tumeshindwa kuwajibika? Tuseme nini juu ya habari tunazosikia kila siku juu ya unyanyasaji na ukatili dhidi ya Watoto? Na watoto wanaoitwa “machangudoa” je?

3.2.2 Malezi ya kiroho

Tunapenda kuwakumbusha wazazi, kwamba wana wajibu mkubwa kabisa wa kuwalea watoto wao kadiri ya uwezo wao, vile vile wakiangalia mafao (maendeleo) yao ya kiroho. Kazi kubwa na nzuri kabisa ya Wazazi ni kuhakikisha maendeleo ya nafsi ya Mtoto. Juu ya hili, Kanisa linatambua na kuthamini umuhimu wa malezi ya Kikristo kwa watoto kiasi kwamba, Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano umetenga hati nzima kwa ajili ya kuongelea jambo hili. Katika hili, Mtaguso watwambia “Wazazi, kwa sababu kuishi kwa wanao kumetokana nao, wanashika wajibu mkuu wa kuwalea watoto wao; hivyo, watazamwe kuwa walezi wao wa kwanza na wenye maana zaidi. Jukumu lao hilo la kuwa walezi ni muhimu sana, kiasi kwamba lisipotimizwa, ni vigumu sana kuziba pengo hilo. Ni juu ya wazazi kuandaa katika familia yao mazingira ya upendo na ya utawala kwa Mungu na ya huruma kwa watu, ambavyo vitasaidia kuwaelimisha kikamilifu Watoto wao kibinafsi na kijamii[13]”.

Ni wajibu wa wazazi kuwalea watoto wao katika njia za Mungu. Maandiko Matakatifu yanathibitisha hayo: “ Sikiliza, ee Israeli Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo” (Kum 6:4-7). Na Mtume Paulo atwambia “Ninyi akina baba, waleeni (Watoto wenu) katika adabu na maonyo ya Bwana..” (Efe 6:45). Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikano unaongeza: “ Katika familia iliyo kama Kanisa la kinyumbani, yawapasa wazazi kuwa watangazaji wa kwanza wa imani kwa ajili ya watoto wao“[14]. Wazazi wanapaswa kuwafundisha watoto wao elimu na uchaji kwa Mungu. Jambo ambalo tunaalikwa wote kulichukua kama changamoto kipindi hiki cha Kwaresima. Ni ukweli kwamba siku hizi, taratibu wazazi wengi wanaelekea kutotilia maanani sana wajibu wao wa kuifanya familia kuwa kweli Kanisa la nyumbani, lenye wajibu wa kurithisha imani ya mababu, kudumisha mapokeo ya kiimani na kuendeleza sala za pamoja kwa Mungu na kutafsiri kwa maisha ya kila siku misimamo yake ya kiimani, kama Kanisa linavyofundisha[15]. Wengi wanaelekea kuchukulia huo wajibu kama wajibu wa shule za Kanisa, ama wajibu wa Mapadri, Watawa na Makatekista. Lakini tujiulize, je, hata sala za kawaida tu za mapokeo ya Kanisa, watoto hawawezi kujifunza katika familia zao? Je, ni kweli kwamba, pamoja na majukumu mengi waliyonayo wazazi, hawawezi kupata muda wa kuwafundisha watoto wao mambo yanayowasaidia kumjua Mungu? Ifahamike kwamba, kadiri wazazi wanavyowafundisha watoto wao kumjua Mungu, ndivyo watoto watakavyowapenda zaidi wazazi wao.

3.3 Wajibu wa watoto kwa wazazi
Ni vema vile vile kutafakari wajibu wa watoto kwa wazazi wao. Kufuatana na imani na mapokeo ya makabila mengi, watoto wanao wajibu wa kuwapenda na kuwaheshimu wazazi wao kutokana na ukweli kwamba, baada ya Mungu, wazazi ni chanzo cha pili cha uhai, kukua na malezi . Hakuna shaka kwamba, katika familia ya kawaida, watoto wanapata vitu vingi kutoka kwa wazazi wao. Kwa hivyo, watoto wana wajibu wa upendo, heshima na shukrani.

3.3.1 Heshima
Kuhusu heshima, amri ya nne ya Mungu inasisitiza wajibu wa mtoto kuwaheshimu wazazi wake “ Waheshimu baba yako na mama yako, siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana , Mungu wako” ( Kut 20: 12; Kum 5: 16).
Bwana wetu Yesu, Kristo anainukuu amri hii mara mbili na anaithibitisha (Mt 15:4;19:19). Heshima kwa wazazi, inatoka katika fumbo la uhai ambalo wazazi ni washirika wa Mungu, na vile vile inatokana na wajibu mkubwa ambao wazazi wanao kwa mtoto wao mbele ya Mungu. Heshima hii, haipaswi kuishia tu katika hisia za ndani, bali pia inapaswa kujionyesha katika ishara za nje. Kwa bahati mbaya, wako watoto wengi ambao wanakosa heshima kwa wazazi wao kwa kuwaonea aibu, kuwakana kwa sababu ya hali yao duni, ama kwa sababu ya umaskini wao, na wakati fulani hata kutumia lugha mbaya dhidi yao na pengine kuwapiga hata kuwaua kabisa. Vitendo vya namna hii ni vya kusikitisha na ni vya aibu.

3.3.2 Utii
Kufuatana na Maandiko Matakatifu, mahusinao ya watoto kwa wazazi wao yanapaswa kuwa ya utii. Mtume Paulo anawataka watoto kuwaheshimu wazazi wao katika yote[16]; anataja kukosa utii katika orodha ya mambo yasiyompendeza Mungu[17] . Maendeleo yote ya mtoto yanategemea msaada na maongozi ya wazazi na walezi, na hivyo ni lazima mtoto awe mtii kwao. Kwa muda ambao watoto wanahitaji maongozi ya wazazi na bado hawana uwezo kamili wa kufanya maamuzi yao wenyewe, wanapaswa kuwatii wazazi wao katika mambo yote mema na halali yanayohusiana na malezi yao. Watoto wanakosa dhidi ya amri hii ya utii kwa wazazi wao ama wanapowatii wazazi wao kwa kinyongo, ama wanapowajibu kwa ukali, ama wanapodharau ushauri wao mwema.

3.3.3 Upendo na shukrani
Upendo wa mtoto kwa wazazi wao unapaswa kuwa upendo wa shukrani[18]. Kwa vile watoto wamepata uhai, matunzo, malezi na mambo mengine kutoka kwa wazazi wao, upendo na shukrani vinapaswa kuonyeshwa kwa maneno na matendo. Watoto wanapaswa kuonyesha kwamba wanahusika na mambo ya familia na wanapaswa kuwa tayari kutoa msaada. Watoto waliokwisha kuwa wakubwa, wanapaswa kuwasaidia wazazi wao wazee na wanapaswa kuwafurahisha angalau kwa kuwatembelea na kuwajulia hali mara kwa mara.

Tunapotafakari ni namna gani tunakuwa Chumvi ya dunia katika maisha ya familia, tunawafikiria wazee wengi vijijini waliotelekezwa na watoto wao, ambao wengi wao watoto hao wana uwezo wa kuwatunza wazazi wao, bali kwa kupuuzia tu wajibu wao, wanaamua kuwatelekeza. Tunasali na kuwaombea ili Neema za kipindi hiki cha Kwaresima ziguse mioyo yenu watoto na kuifanya iwaelekee wazazi wenu.

4.0 MWAKA WA PADRI
Tunapenda kuwakumbusha tena kwa namna ya pekee kwamba, tarehe 16 Machi 2009, Baba Mtakatifu, Benedikto XVI, akiongea na wahusika wa Kongregasio ya Makleri, alitangaza mwaka maalumu wa Padri ili wachuchumie ukamilifu katika maisha yao ya kiroho, jambo ambalo ni la msingi kabisa katika huduma na utumishi wao. Huduma yao ya kichungaji inategemea sana ni kwa jinsi gani wanavyochuchumilia ukamilifu. Kwa hiyo, mwaka wa Padri ni fursa muhimu kwa ajili ya kutafakari kwa namna ya pekee kazi ya Bwana, ambaye “usiku ule aliotolewa” (1Kor 11: 23) aliweka Ukasisi wa Daraja akiuunganisha, kwa namna ya pekee, na Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chemchemi na kilele cha maisha ya Kanisa lote. Kwa hiyo, ni mwaka ambao Kanisa linaalikwa kutambua upya, uzuri na umuhimu wa Upadri na wa kila Padri.

Dhamira ambayo Baba Mtakatifu ameichagua kwa ajili ya mwaka huu ni “ uaminifu wa Kristo, uaminifu wa Padri” nayo inaelekeza mawazo katika kutambua umuhimu wa pekee wa Neema: “Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza” (1Yoh 4:19). Na wakati huo huo ni jambo la lazima kumuelekea Kristo kwa uhuru wa upendo, ikikumbukwa kwamba, jina jingine la upendo ni “ Uaminifu[19]. Mtakatifu Yohane Maria Vianney alisema “Upadri ni Upendo wa Moyo wa Yesu”[20]. Maneno haya mazuri ya Mtakatifu huyu, yanatualika kwanza sisi kama Kanisa, tutambue, kwa unyenyekevu, zawadi kubwa ya Upadri siyo tu kwa Kanisa bali pia kwa wanadamu wote.

Kwa sababu hiyo, kwa njia ya ujumbe huu wa Kwaresima, tunaalikwa kutafakari kwa pamoja, maneno yale ambayo Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano ulisema juu ya Upadri katika utume wa Kanisa: “Kazi ya Mapadri, inashiriki mamlaka ya Kristo ambayo kwayo wenyewe hukuza, hutakasa na kuongoza mwili wake”[21]. Ndiyo sababu, ukuhani wa Mapadri, ijapo kuwa hudai kwanza Sakramenti zinazowaingiza katika Ukristo, lakini hutolewa kwa njia ile ya Sakramenti maalum ambayo kwa ajili yake, Mapadri kwa upako wa Roho Mtakatifu, hutiliwa muhuri wa pekee unaowafanya kuwa mfano wa Kristo kuhani, hivi kwamba wawezeshwe kutenda kwa jina la Kristo na katika nafsi yake (in Persona Christi) aliye Kiongozi[22]. Aidha, Mapadri wanashiriki, kwa kadiri yao, jukumu la Mitume. Ndiyo maana wanapewa kutoka kwa Mungu, neema inayowawezesha kuwa wahudumu wa Yesu Kristo kati ya mataifa kwa njia ya huduma takatifu ya Injili, ili sadaka ya mataifa iwe ya kupendeza na iliyotakaswa katika Roho Mtakatifu[23]. Maana kwa njia ya tangazo la Kitume la Injili, kweli Taifa la Mungu linaalikwa na kukusanywa hivi kwamba wote wanaoshiriki katika Taifa hili, madhali wanatakaswa kwa Roho Mtakatifu, wanaitoa miili yao iwe ” dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu” ( Rum 12:1).

Hivyo, shabaha wanayolenga Mapadri kwa huduma na maisha yao ndiyo utukufu wa Mungu Baba wanaopaswa kuutafuta katika Kristo. Nao utukufu wenyewe ni kwamba wanadamu wapokee kwa utambuzi, kwa hiari na kwa moyo wa shukrani kazi timilifu ya Mungu iliyotendeka katika Kristo na kudhihirishwa katika maisha yao yote.

4.1 Majukumu ya Padri
4.1.1 Padri, Mtu wa Mungu kwa ajili ya Watu
Padri anatwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu ili atoe matoleo na dhabibu kwa ajili ya dhambi[24]; naye anaishi kati ya wanadamu wengine kama ndugu. Ndivyo alivyoishi Yesu aliye Bwana wetu na Mwana wa Mungu, mtu aliyetumwa na Baba kwa wanadamu, ambaye alikaa nasi, akataka kuwa sawa na ndugu zake katika mambo yote, isipokuwa hakuwa na dhambi[25]. Mfano wake huo walikwisha kuufuata Mitume watakatifu. Mtakatifu Paulo, ambaye kwa Neema za Mungu, tumeadhimisha mwaka wake uliofikia kilele miezi michache iliyopita, Mwalimu wa mataifa, “ aliyetengwa kwa kuihubiri Injili ya Mungu” (Rum 1:1) anatangaza kwamba amekuwa hali zote kwa watu wote ili apate kuwaokoa wote[26]. Hivyo, Mapadri wa Agano Jipya wanatengwa kwa namna fulani ndani ya Taifa la Mungu kwa ajili ya wito wao na Daraja yao, ila si kwa lengo la kufarakana na Taifa hilo, wala na mtu yeyote, bali kwa kujitoa mhanga katika kazi aliyowaitia Bwana[27].

4.1.2 Padri, mhudumu wa Neno la Mungu
Taifa la Mungu hukusanywa, awali ya yote, kwa njia ya neno la Mungu aliye hai, ambalo watu wote wanayo haki kulitafuta mdomoni mwa Padri. Maadam hakuna anayeweza kuokolewa pasipo kwanza kuamini[28], Padri anawajibika kabla ya yote kuhubiri Injili ya Mungu kwa watu wote ili wausikie ujumbe wa Bwana wakaokolewe, kwa kufanya hivyo Padri anatimiza agizo la Bwana aliyesema: “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe “ (Mk 16:15). Maana, kwa neno liletalo wokovu, imani inawashwa mioyoni mwa wasioamini na kulishwa mioyoni mwa waaminio; vile vile, kwa imani, jumuiya ya waamini inajengwa na kukua. Paulo Mtume anasema “Imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo” (Rum, 10:17). Kwa hivyo, Mapadri huwiwa na watu wote ili kuwapelekea wote habari ya ukweli wa Injili walio nao katika Bwana[29]. Aidha wanaitwa kutoa mbele ya watu ushuhuda wa maisha yaliyo safi yenye kuwahimiza kumtukuza Mungu. Na kwa kweli ulimwengu wa sasa unawahitaji zaidi mashuhuda na si walimu wa maneno tu[30].

4.1.3 Padri, mhudumu wa Sakramenti za Wokovu
Mungu, ambaye peke yake ndiye Mtakatifu na mwenye kutakatifuza, alitaka kujitwalia wanadamu wawe washiriki na wasaidizi wake, ili watumikie kwa unyenyekevu katika kazi ya kutakatifuza. Ndiyo maana, mapadri huwekwa wakfu na Mungu, kwa njia ya Askofu, hivi kwamba washirikishwe, kwa namna ya pekee, ukuhani wa Kristo, na katika maadhimisho matakatifu watende kazi kama wahudumu wa yule anayetekeleza bila kukoma wadhifa wake wa kikuhani kwa ajili yetu kwa njia ya Roho wake[31]. Maana, wao kwa njia ya Ubatizo huwaingiza wanadamu katika Taifa la Mungu na Kanisa, kwa mafuta ya Wagonjwa huwatuliza wagonjwa, na hasa kwa adhimisho la Misa hutolewa, kwa namna ya Sakramenti, dhabihu ya Kristo[32]. Hivyo, kusanyiko la Kiekaristi ni kiini cha jumuiya ya waamini inayoongozwa na Padri.

Mapadri wanawafundisha waamini kutoa dhabibu ya Kimungu kwa Mungu Baba katika sadaka ya Misa, na kuunganisha na dhabibu hiyo toleo la maisha yao. Aidha, katika roho ya Kristo Mchungaji, Mapadri wanawafunza pia kuwa na moyo wa toba katika Sakramenti ya Kitubio, kusudi wapate kumwongokea Bwana kila siku zaidi na zaidi. Na ndivyo Kristo Bwana alivyoanza kuhubiri akisema “Tubuni, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia” (Mt 4: 17). Toba inakamilishwa na Padri aondoleaye dhambi “nami nakuondolea dhambi zako”.

4.1.4 Padri, mlezi wa Taifa la Mungu
Mapadri wanaendeleza kazi ya Kristo, Kiongozi na Mchungaji, kwa nguvu na mamlaka yanayowapasa na kwa jina la Askofu. Hivyo, Padri anaikusanya familia ya Mungu kama jumuiya inayohuishwa katika umoja na anayoiongoza kwenda kwa Baba kwa njia ya Kristo katika Roho Mtakatifu[33]. Kwa ajili ya huduma hii, kama vile kwa majukumu mengine ya Mapadri, inatolewa mamlaka ya kiroho ijaliwayo kwa lengo la kujenga[34]. Lakini, katika kulijenga Kanisa, Padri hupaswa kuwa na tabia ya ukarimu wa pekee kwa watu wote, akiiga mfano wa Bwana. Padri hana budi kutenda kwa mujibu wa matakwa ya mafundisho na maisha ya Kikristo, wala siyo kwa kuwapendeza watu[35]; tena awafunze na pia kuwaonya kama wana wapenzi[36], asemavyo Mtume Paulo “ Lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho” (2Tim 4:2).

4.2 Mazingira ya Huduma ya Padri leo

Sisi Maaskofu wenu, tunapowaandikieni Ujumbe huu katika kipindi hiki cha Kwaresima, tunataka kutafakari pamoja nanyi kwa kina wajibu huo mkubwa aliopewa Padri. Tunatambua mahangaiko yao ya kitume, huduma yao ambayo wakati fulani na katika mazingira fulani haitambuliki, lakini wanaendelea kuitoa pasipo kuchoka. Tunatambua vile vile upendo wao kwa watu wote. Tusemeje tena juu ya uaminifu wa kijasiri kabisa ambao Mapadri wengi wanauonyesha katika wito wao, licha ya matatizo mengi na pengine kutoeleweka vizuri na watu wanaowahudumia? Licha ya matatizo hayo yote, Mapadri wengi wanaendelea kuwa waaminifu kwa wito wao wa kuwa “marafiki” wa Kristo ”walioitwa naye kwa namna ya pekee wakachaguliwa, na kutumwa”[37]. Tunaamini kwamba, wengi wenu mna kumbukumbu nzuri ya Mapadri wenu, waliowabatiza, waliowafundisha kwa maneno na mifano yao mizuri ya kujitoa bila ubinafsi na wengine hata kutoa uhai wao kwa ajili ya huduma yao ya kipadri.
Pamoja na hayo, tunawaalika vile vile, katika kipindi hiki, tuwakumbuke Mapadri wenye shida maalumu na pengine wengine ambao wanakosewa hadhi yao, ama wazuiliwa katika kazi yao na wengine hata kuteswa, kudhulumiwa hata kufikia hatua ya kumwaga damu.

4.3 Upadri- Hazina ndani ya Vyombo vya Udongo

Tunapoadhimisha mwaka wa Padri wenye dhamira “ uaminifu wa Kristo,- uaminifu wa Padri” ni vema pia, kwa moyo wa unyenyekevu na majuto tutafakari hali ambazo, kwa bahati mbaya sana, Kanisa linasumbuka, linahangaika na hata kufadhaika kwa sababu ya baadhi ya Mapadri kukosa uaminifu katika Utume wao. Kwa bahati mbaya, kwa sababu hiyo, ulimwengu unapata sababu ya kukwazika na hata pengine kuwakataa Mapadri. Kinachotakiwa kufanywa na Kanisa katika mazingira kama hayo, siyo kufanya jitihada za kufunua udhaifu wa watumishi wake[38], bali kuwaombea na vile vile kutambua kwa dhamira yenye furaha ukuu wa zawadi ya Mungu inayowekwa kwa namna inayoonekana, kwa njia ya nafsi za viumbe wanadamu. Padri, pamoja na udhaifu wake na mapungufu yake, katika nafsi yake amebeba zawadi kubwa ya Mungu isiyo na kifani.

Juu ya hilo, tutafakari maneno ya Mtakatifu Yohane Maria Vianney aliyekuwa akisema: “Jinsi gani Padri alivyo na mamlaka makubwa…!, kama Padri angeelewa hilo, bila shaka angefariki kwa mshtuko, kwa sababu, hata Mungu Mwenyewe anamtiii: Padri anatamka maneno mawili na Bwana wetu anashuka toka Mbinguni, kwa sababu ya maneno ya Padri, na anakaa katika hostia ndogo” [39]. Na alipokuwa akiongea na waamini wake juu ya umuhimu wa Sakramenti, alikuwa akisema: ”Ukiondoa Sakramenti ya Daraja Takatifu, hatuwezi tena kuwa na Bwana. Ni nani aliyemweka pale katika Tabernakulo? Ni Padri! Ni nani aliyeipokea roho yenu kwa mara ya kwanza mlipopata uhai? Ni Padri! Ni nani anayelisha roho zetu ili tupate nguvu za kuendelea na safari yetu ya hija hapa duniani? Ni Padri! Ni nani atakayeiandaa roho yetu ili ifike mbele za Mungu, akiiosha kwa mara ya mwisho katika Damu ya Kristo? Ni Padri, siku zote ni Padri! Na kama roho hii ikifa ( kwa njia ya dhambi), ni nani ataihuisha, ni nani ataipa utulivu na amani? Vile vile ni Padri! … Baada ya Mungu, Padri ni kila kitu! Yeye mwenyewe hataelewa vizuri fumbo hili mpaka Mbinguni[40].

Mawazo haya, yanayotoka katika moyo wa kipadri wa paroko huyu Mtakatifu, yanaeleza heshima kubwa sana na upendo wa hali ya juu ambao Mtakatifu huyu alikuwa nao kwa upadri wake; na anaongeza tena ”iwapo tungalielewa vizuri Padri ni nani hapa duniani, hakika tungekufa, siyo kwa sababu ya mshtuko, bali kwa sababu ya upendo… Bila Padri, kufa na mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo visingalikuwa na maana yoyote. Ni Padri ndiye anayeendeleza kazi ya Ukombozi hapa duniani”…Nyumba iliyojaa dhahabu kubwa itasaidia nini iwapo kusingalikuwa na mtu yeyote ambaye anaweza kutufungulia mlango wake? Padri ana ufunguo wa hazina za mbinguni, ni yeye anayefungua mlango; yeye ndiye wakili wa Mungu mwema; ni yeye ndiye mtawala wa mali zake…. Iwapo mtaiacha parokia bila Padri kwa muda wa miaka ishirini, wanyama ndio watakaoabudu humo…padri siyo padri kwa ajili yake, bali kwa ajili yenu[41].”

4.4 Padri amewekwa Wakfu

Maandiko Matakatifu yatwambia kwamba “kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwaajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu” (Ebr 6:1 na katika sala yake ya kikuhani, Bwana wetu Yesu Kristo anawaombea Mapadri watakaswe, na watakaswe katika kweli. Juu ya hilo, Bwana wetu Yesu Kristo anasema “Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili nao watakaswe katika kweli” (Yn 17:19). Maana yake nini Bwana wetu Yesu Kristo kujiweka wakfu? Si Yeye “Mtakatifu wa Mungu” (Yn 6:69) kama vile Mtakatifu Petro alivyokiri? Ni kwa namna gani sasa anaweza kusema kwamba anajiweka wakfu, ama anajitakatifuza mwenyewe?

Katika Maandiko matakatifu, kuweka wakfu ama kutakasa kitu ama mtu maana yake ni kukifanya, ama kumfanya mtu huyo awe mali ya Mungu[42], yaani kukiondoa au kumuondoa katika mazingira yake na kukiweka/kumweka katika mazingira ya Mungu, kiasi kwamba kitu/ mtu huyo asiwe tena miongoni mwa vitu vyetu, bali awe mali ya Mungu mwenyewe. Kuweka wakfu ama kutakatifuza, kwa hiyo, ni kuondoa ulimwenguni na kuweka katika mikono ya Mungu aliye hai. Mtu hawi mali yake tena, bali anawekwa mikononi mwa Mungu; wala kitu chake hakiwi chake tena. Kwa maneno mengine, hiyo ni sadaka. Na hii ndiyo Sakramenti ya Daraja Takatifu. Ni kutoka ulimwenguni na kwenda kwa Mungu. Ni kutoka katika mazingira ya maisha ya kidunia na kuwekwa kando “ kwa ajili ya Mungu”. Na huu si ubaguzi! Kuwekwa katika mikono ya Mungu maana yake ni kuwekwa kwa ajili ya kuwawakilisha wengine. Padri anatolewa katika ulimwengu na kuwekwa kwa Mungu, na kwa namna hiyo kutoka kwa Mungu anapaswa kuwa kwa ajili ya wengine, kwa ajili ya wote[43].

4.5 Padri anatakaswa na Neno la Mungu
Tunaposoma katika Yohane 17:7, anaposema “Uwatakase kwa ile kweli” Bwana wetu Yesu Kristo anaongeza “Neno lako ndiyo kweli”. Neno hilo ni Yule “aliyefanyika mwili” (Yn 1:14), Yesu Kristo mwenyewe. Katika maana hiyo, wanafunzi wanawekwa katika mikono ya Mungu kwa kuzamishwa katika hilo neno la Mungu. Ndiyo kusema, neno la Mungu ni maji yenye kutakasa, nguvu ya uumbaji ambayo inawabadili na kuwaweka katika mikono ya Mungu.

Kwa hiyo, tunawaalika Mapadri wote kutafakari pamoja nasi na kujipima kwa njia ya maisha yetu ya kila siku kama kweli neno la Mungu linatugusa katika maisha yetu? Kama kweli neno la Mungu ni mkate wetu wa kila siku, ama mawazo na tamaa zetu ni Mkate wa ulimwengu huu. Tunalipenda neno la Mungu? Tunalijali kweli kutoka katika nafsi zetu kiasi kwamba linatugusa katika maisha yetu na kutuongoza katika fikra zetu? Si kweli kwamba mara nyingine tunaongozwa na mawazo ya ulimwengu huu katika matendo yetu? Tunapenda kweli kuacha neno la Mungu lituguse na kutusafisha?

4.6 Padri ni Mtu wa kujikana
Kuungana na Mungu kwa njia ya Kristo kunahitaji kujinyima, kujikana kwani Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe alisema “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate” (Mt 16:24). Kujikana maana yake ni kutotaka kufuata njia zetu na mapenzi yetu; maana yake si kuwa jinsi tunavyotaka sisi, bali kujisalimisha kwa Kristo mwenyewe kila mahali, na kwa namna yoyote ile, ili kwamba Yeye atutumie: “Lakini ni hai, wala si mimi tena, bali Kristo yu hai, ndani yangu” (Gal 2:20).

Padri siku anapopokea Daraja Takarifu anajikatalia kufanya kama anavyotaka yeye, anajiweka mikononi mwa Mungu. Lakini, ni lazima siku hadi siku aifanye upya ahadi hii ya kujiweka mikononi mwa Mungu. Kujikana huku kwa Padri, hakuwezi kuwa uchungu iwapo kama kweli Kristo ni msingi wa maisha yake; kama kweli anaingia katika mahusiano naye. Iwapo Padri anamjua, anampenda na ni rafiki wa kweli wa Kristo, hata katika kujikana na kujikatalia kwake, ambako wakati mwingine kwaweza kuonekana kama mzigo, ataweza kuonja faraja ya kuwa rafiki wa Kristo kwa njia ya ishara za upendo wake, ambazo kila siku anazionyesha katika mambo makubwa na madogo.

Tunawaaalika, kwa hiyo, waamini wote, katika kipindi hiki cha Kwaresima, kuwaombea Mapadri ili wawe kweli waaminifu katika wito wao, wauchuchumie utakatifu, watafute tunu za kweli za kujitoa kwa moyo wote kwa Kristo. Katika utendaji wa utume wao, wawe siku zote wameungana na sisi Maaskofu wao, nasi weneyewe tuungane nao na vile vile wakiwa wameungana miongoni mwao tena nanyi waamini Walei ambao tunawahudumia. Pamoja na matatizo yote wanayoweza kukumbana nayo katika kutekeleza utume wao, wayasikie siku zote maneno ambayo Bwana wetu Yesu Kristo aliwaambia Mitume; “………..Ulimwenguni mnayo dhiki, lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu” (Yn 16:33). Imani yao kwa Bwana na Mwalimu iwatie nguvu kuuangalia kwa matumaini wakati ujao wakitambua kwamba Kristo anawategemeza. Waufuate mfano wa Mtakatifu Yohane Maria Vianney kwa kumwacha Kristo ayatawale maisha yao ili katika ulimwengu wa sasa wawe wajumbe wa matumaini, wa upatanisho na amani.

5.0 FURSA NYINGINE ZA KUWA CHUMVI KATIKA DUNIA
Wapendwa Waamini, tunapofanya tathmini ya kina ya mambo yanayotokea katika jamii yetu, tunatambua kwamba, yako mambo mengi mazuri; kwa hayo hatuna budi kumshukuru Mungu. Nchi yetu ina amani ya namna ya fulani na waamini wake wanapenda amani, tuna umoja, mshikamano na upendo. Hata hivyo, hatuwezi kufumba macho na hivyo kushindwa kuona upande mwingine wa sarafu. Yapo mambo mengi vile vile yasiyopendeza mbele ya Mungu na yanayodhalilisha utu wa binadamu yanayotokea katika nchi yetu. Na katika hayo, sisi Maaskofu wenu tunawaalika kufanya tafakari ya unyenyekevu kabisa ili kuona kila mmoja anachangia namna gani na kwa kiasi gani katika mambo hayo yasiyompendeza Mungu. Pamoja na kwamba Uinjiliishaji katika nchi yetu, kama vile ilivyo katika nchi nyingi Barani Afrika, uko katika hatua zake za mwanzo, bado kuna watu ambao wamekwisha anza kumsahau Mungu, ama wanaona kwamba Mungu hana maana yoyote katika maisha yao, ama wanamkataa kabisa na kuanza kuabudu “miungu” wanayojitengenezea wenyewe ya uliwengu wa sasa: mali, madaraka, anasa n.k. Na hiki ndicho kiini cha tatizo kwa sababu, pasipo kumtambua Mungu, hata binadamu hawezi kutambulika, hawezi kuheshimiwa[44]. Kama vile Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikano unavyofundisha: “ Maana kiumbe bila Muumba hutoweka chenyewe kinatiwa giza“[45]. Miongoni mwa mambo ambayo hayapendezi ni kama vile: kuendelea kukua kwa tofauti kati ya walio nacho na wasio nacho, watu kutopewa haki zao za msingi, na mahali pengine mambo ambayo watu walipaswa kupewa kama haki zao za msingi yanageuzwa kuwa fadhili. Ujinga ambao taifa letu lilijitangazia mara baada ya uhuru kama adui anayepaswa kupigwa vita bado unaendelea pamoja na matokeo yake ya imani potofu kama vile mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, vikongwe n.k. Watu wanaendelea kukosa huduma za msingi za kijamii, hata pale ambapo mazingira yangeruhusu zipatikane, lakini, kwa sababu ya ubinafsi na uroho wa watu wachache, hazitolewi. Haya ni baadhi ya mambo machache ambayo hayampendezi Mungu na yanamdhalilisha binadamu, ambayo, kwa kiasi kikubwa, kwa unyenyekevu inabidi kusema kila mmoja ameshiriki kuchangia kwa namna yake.

Maandiko Matakatifu yanatwambia kwamba, baada ya Yohane Mbatizaji kuhubiri na kuwaambia makutano “itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake” (Lk 3:4), na kuwapa tisho la hukumu” na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti, basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni” (Lk 3:9), Makutano wakamwuliza, “Tufanye nini basi?” Akawajibu akiwaambia, “Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu, na mwenye chakula na afanye vivyo hivyo”. Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa, wakamwuliza, “Mwalimu tufanye nini sisi?” Akawambia, “Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa”. Askari nao wakamuuliza, wakisema, “Sisi nasi tufanye nini?” Akawaambia, msidhulumu mtu, wala msishtaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu” (Lk 3:10-14).

Tunapokuwa katika kipindi hiki cha Kwaresima, na hasa tunapotafakari mwito wa Kristo wa kuwa “Chumvi ya dunia”, ni vyema kila mmoja wetu akajitafakari ni kwa vipi na kwa namna gani amekuwa kweli Chumvi ya dunia katika nafasi yake, awe kiongozi wa dini, mwalimu, hakimu, askari, mwanasiasa n.k Je, anaamua kwa moyo wa dhati kabisa kutenda yanayompendeza Mungu na yanayojali hadhi ya utu wa binadamu katika eneo lake? Kwa unyenyekevu amwendee Bwana wetu Yesu Kristo na amulize “Nifanye nini basi?” Na Yeye atamjibu katika nafsi yake.

5.1 Chumvi ya Dunia na Ushiriki Katika Mambo ya Kijamii
Wakristo wote, kama raia, wanaalikwa kushiriki katika mambo yanayohusu jamii, na kuupa umuhimu ushiriki wao kama vile wanavyoupa umuhimu ushiriki wao katika mambo ya kiroho. Wakiwa wanaishi na kufanya kazi ulimwenguni, Wakristo wanaalikwa kufuata njia ya Kristo katika maisha yao ya kila siku, na hivyo kufanya tunu za matendo ya Kristo ziwepo katika jamii. Wakristo wanapaswa kumshuhudia Kristo na kufanya Ufalme wa Mungu uwepo kati ya watu. Kanisa limetumwa ili kuendeleza kazi ya ukombozi ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambayo kwa hulka yake inahusu kufanywa upya mambo yote ya ulimwengu. Katika maana hiyo, Kanisa limo ulimwenguni, ingawa si la ulimwengu huu[46]. Ni ukweli kabisa, Wanakanisa wote ni washiriki kamili wa kazi hii, ijapokuwa kwa namna tofauti. Kwa namna ya pekee, ushiriki wa waamini walei katika kazi hii una namna yake ya kuutekeleza kutokana na nafasi zao. Ushiriki wao katika masuala ya kijamii, ambayo mahala pengine huitwa “ Malimwengu”[47] una namna yake ya kuutekeleza kutokana na hali yao wenyewe. Hivyo basi kwa namna ya pekee, tunapenda kuwakumbusha Waamini Walei kwamba, katika masuala haya ya kijamii ndipo mahali ambapo mnatumwa na Mungu kuufanya utume wenu. Mnaishi katika jamii, katika “Malimwengu” yaani katika kazi mbalimbali mnazozifanya. Mnasoma, mnafanya kazi, mnaunda mahusiano kama marafiki, wanachama wa mashirika n.k. Neno aliyefanyika mwili, aliyatakatifuza mahusiano haya ya kibinadamu, hasa yale ya kifamilia, ambayo ndicho chanzo cha mahusiano yote ya kijamii, na kwa utashi wake mwenyewe alijiweka chini ya sheria za nchi yake. Alichagua kuishi maisha ya mseremala[48]. Nanyi hamuitwi ili kuacha nafasi mliyo nayo katika “ Ulimwengu”. Mungu anawakabidhi utume ambao unaendana na hali yenu katika ulimwengu. Manaitwa na Mungu ili, kwa roho ya Injili, muweze kuchangia katika kutakatifuza jamii mkiwamo ndani, kama vile chachu, kama vile chumvi katika chakula, mkitimiza majukumu yenu katika hali yenu ulimwenguni. Mungu anaonyesha mpango wake na anawapa wito wa kutafuta Ufalme wa Mungu kwa kuingia katika malimwengu na kuyaelekeza yafuate mpango wake.

5.1.1 Chumvi yenye Ladha ama Chumvi iliyopoteza Ladha?

Tunapokuwa katika kipindi hiki kitakatifu, cha Neema, sisi Maaskofu tunapenda kuwaalika waamini wote walei, kujitafakari na kujiuliza kwa makini, ni kwa namna gani uwepo wenu na ushiriki wenu katika masuala ya kijamii umechangia katika kuujenga Ufalme wa Mungu? Ni kwa namna gani uwepo wenu umesaidia katika kujenga haki, upatanisho, amani, upendo na mshikamano katika jamii? Huenda badala ya kuwa Chumvi inayokoleza katika jamii, mara nyingine mmekuwa kama chumvi isiyo na ladha kwa kuwa chanzo cha uozo katika jamii? Au wakati fulani na katika mazingira fulani mmekuwa ndio chanzo cha kueneza ubinafsi, uchu wa madaraka na hata wa mali? Tunaomba Neema za kipindi hiki kitakatifu ziwasaidie, ziwatie nguvu za kumwacha Mungu atawale katika mioyo yenu kwa kuzishika amri zake, kwa kutangaza ufalme wake na kuyaishi maisha yenu mkiwatumikia na kuwapenda watu wote bila ubaguzi, kama Kristo mwenyewe alivyofanya.

5.2 Uchaguzi Mkuu 2010

Kama tunavyofahamu, nchi yetu iko katika mchakato wa uchaguzi Mkuu, utakaofanyika mwezi Oktoba 2010. Uchaguzi huo utatupatia viongozi wapya: Madiwani, Wabunge na Rais wa nchi yetu. Uchaguzi huo ni tukio la kijamii na vile vile ni tukio la kisiasa. Ni tukio ambalo Wakristo wote wanapaswa kushiriki kama wajibu wao. Historia yatwambia kwamba, ushiriki wa Wakristo katika mambo ya ulimwengu umekuwa wa namna tofauti katika kipindi cha zaidi ya miaka 2000. Namna moja ya Wakristo kushiriki katika masuala ya kiulimwengu ni kwa njia ya kushiriki katika masuala ya kisiasa. Wakristo, kama vile mwandishi mmoja wa Kikristo alivyosema, wanaposhiriki katika masuala ya kisiasa “Wanatimiza wajibu zao za kiraia”[49]. Baadhi ya Watakatifu ambao Kanisa linawaheshimu ni wanaume na wanawake wengi ambao walimtumikia Mungu kwa njia ya kujitoa kwao kwa ukarimu katika mambo ya siasa na serikali. Mfano mzuri ni Mtakatifu Thomas More, ambaye alitangazwa kama msimamizi wa watawala na wanasiasa. Huyu alitoa ushuhuda wake kwa kifodini kwa ajili ya “ hadhi isiyoweza kunyang`anywa ya dhamiri ya kibinadamu”[50]. Pamoja na kwamba Mtakatifu Thomas More alipata namna tofauti za shinikizo la kisaikolojia, alikataa katakata kuikana imani yake. Pamoja na kwamba alikuwa mtiifu kwa mamlaka na taasisi halali, jambo lililomfanya kuwa mtu wa pekee, ni kwamba kwa maisha yake na kifo chake alifundisha kuwa, binadamu hawezi kutenganishwa na Mungu, wala siasa haiwezi kutenganishwa na maadili. Na ndilo jambo ambalo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye mchakato wa kumtangaza mwenyeheri unaendelea, alitufundisha kwamba, siasa lazima ijengwe katika misingi imara ya kanuni thabiti za kimaadili (ambazo hazina mjadala) zinazopaswa kuwa ndiyo mhimili wa maisha katika jamii. Tunatambua wazi kwamba katika nchi yetu hivi sasa kuna vyama vingi vya kisiasa ambamo waamini wana haki ya kujiunga na kushiriki katika kuchagua ama kuchaguliwa, na kwa kufanya hivyo wanashiriki kutimiza wajibu wao wa maisha ya umma ya nchi yao[51]. Hata hivyo, hali hii ya kuwapa uwezo na haki ya kushiriki katika vyama mbali mbali, haiwezi kuchanganywa na hali ya kushindwa kutambua na kuchagua kanuni za kimaadili na tunu za msingi zinazojali hadhi ya utu wa binadamu.

Ndiyo kusema, demokrasia ya kweli, ambayo uchaguzi ni sehemu tu ya kielelezo chake, itafaulu kuwa demokrasia ya kweli iwapo itakuwa imejengwa juu ya uelewa sahihi wa nafsi ya binadamu[52]. Ushiriki wa Wakristo katika siasa na hasa katika uchaguzi huu mkuu haupaswi kuipuuzia kanuni hii, vinginevyo, ushuhuda wa imani ya Kikristo ulimwenguni na muungano unaopaswa kuwepo kati ya yale ambayo Wakristo wanayaamini na maisha yao ya kawaida hautakuwepo.

5.2.1 Mambo ya Kuangalia

Wakati tunawaandikia barua hii, tunajua kwamba kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu zinaendelea. Tunajua kwamba wako watu wengi ambao wanatumia haki yao ya kiraia ya kugombea uongozi katika nafasi mbali mbali. Tunaomba sana, na kuwasihi wale wote wanaogombea katika nafasi hizo za uongozi, wafikiri na kutafakari kwa makini ni kitu gani kimewasukuma ili kuchukua hatua hiyo? Wanataka, kwa moyo radhi kuwatumikia Watanzania ili kila mtu katika jamii yetu apate hadhi yake ya kiutu ambayo ni stahili yake? Wana nia ya dhati ya kuwasaidia Watanzania ili kila mtu apatiwe mahitaji msingi ya kumwezesha kuishi maisha yanayomstahili mwanadamu? Wako tayari kuzifanya rasilimali za nchi yetu kuwa kwa ajili ya manufaa ya wote?
Wakati tunawahimiza waamini wote kushiriki katika zoezi zima la uchaguzi, tunaomba vile vile wale watakaoshiriki katika kuchagua, wawahoji na wapime udhati wa nia ya wagombea kwa kufuata vigezo vya hadhi ya utu wa mwanadamu na tunu za kimaadili.

Kamwe msichague mtu kwa sababu ya shinikizo, wala kwa sababu ya rushwa, au ubaguzi wowote ule kwani kwa kufanya hivyo mtakuwa mnakosea mbele ya Mungu. Muwachague viongozi mkiwa mumeongozwa na dhamiri safi mbele ya Mungu na hivyo muwachague viongozi ambao wataliongoza taifa hili kwa kujali maslahi ya wote, na ambao watatusaidia kujenga jamii yenye upendo, umoja, haki na amani.

6.0 MATOKEO YA SINODI KWA AJILI YA AFRIKA
6.1 Sinodi ya kwanza kwa ajili ya Afrika
Wapendwa Wanafamilia ya Mungu, takriban miaka kumi na nne iliyopita, tangu Aprili 10 mpaka 8 Mei 1994, Mkutano maalumu wa kwanza kwa ajili ya Afrika wa Sinodi ya Maaskofu ulifanyika ukiwa na wazo kuu “ Kanisa katika Afrika katika utume wake wa kuinjilisha kuelekea mwaka 2000: “Nanyi mtakuwa mashahidi wangu” (Mdo 1:8). Mtumishi wa Mungu, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, alieleza nia yake ya kuitisha mkutano huu muhimu kwa Kanisa tarehe 6 Januari 1989 ili kutoa nafasi ya kutosha kuuandaa.

Matukio yaliyoambatana na Mkutano huo maalum yalipokelewa kwa shauku kubwa, yakiwashirikisha waamini katika ngazi zote za Kanisa Katoliki katika Afrika kuanzia katika Majimbo, Parokia na Vikundi mbalimbali. Matukio hayo vile vile yalivuta hisia za Makanisa mengine ya Kikristo na jumuiya zake, pamoja na ya Wawakilishi wa dini zisizo za Kikristo, pamoja na watu wenye mapenzi mema kutoka katika kila Bara.
Barua Mausia ya Kitume aliyoitoaa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II baada ya mkutano huo maalumu, Ecclesia in Africa, ilikusanya matokeo ya mchakato mzima wa Sinodi kuanzia maandalizi mpaka maadhimisho ya Mkutano wenyewe: Sala, kubadilishana taarifa, kushirikishana furaha na uchungu, katika hali mbalimbali katika Kanisa, utamaduni, jamii, maisha ya kijamii na katika tafakari za kina juu ya kila mada zilizojadiliwa na Maaskofu wa Kanisa katika mazingira ya ushirika na utulivu kama ilivyo katika urika wa Maaskofu, wakiongozwa na Sinodi na Mchungaji wa Kanisa la Kiulimwengu.

Sinodi ya kwanza kwa ajili ya Afrika ilikuwa kama dira na mlango wa kuelekea maadhimisho ya Yubilei kuu ya mwaka 2000. Vile vile, Sinodi hii ya kwanza iliweka msingi wa kutengeneza ngazi mbalimbali za Kanisa, na wakati huo huo iliweka msingi wa kutengeneza hadidu za rejea kwa ajili ya kutathmini kazi ya uinjilishaji katika Afrika mintarafu vipaumbele vinavyopaswa kuwekwa kwa ajili ya mustakabali wa Bara la Afrika. Baadhi ya masuala yaliyopewa kipaumbele katika Sinodi hiyo ni kama: Afrika, kutoka Bara la Misioni kuwa Bara la Kimisionari, Malezi ya mawakala wa Uinjilishaji, uelewa mpya wa kulijenga Kanisa kama familia ya Mungu na utamadunisho.

6.2 Sinodi ya Pili kwa ajili ya Afrika
Mtumishi wa Mungu, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, akikubali matakwa na tamaa ya Maaskofu, Mapadri, watu wa maisha ya Wakfu na Walei, tarehe 13 Novemba 2004, alieleza nia yake ya kuitisha Mkutano wa pili maalumu kwa ajili ya Afrika wa Sinodi ya Maaskofu. Baba Mtakatifu Benedikto XVI alithibitisha mpango wa mtangulizi wake kwa kutangaza, mbele ya Baraza maalumu kwa ajili ya Afrika la Sekretariati ya Sinodi ya Maaskofu, uamuzi wake wa kuitisha katika mji wa Roma, mkutano wa pili maalumu kwa ajili ya Afrika wa Sinodi ya Maaskofu. Baba Mtakatifu alitaja maudhui ama dhana ya Sinodi hiyo kama “ Kanisa katika Afrika na huduma ya Upatanisho, Haki na Amani ” Ninyi ni Chumvi ya dunia, Ninyi ni nuru ya ulimwengu” ( Mt 5:13, 14). Wazo hili ni mwendelezo wa wazo la Sinodi ya kwanza kwa ajili ya Afrika na limetoa nafasi ya kutathmini yale yaliyotokea katika Kanisa la Afrika tangu Sinodi ya kwanza.

Sinodi hiyo imefanyika katika mji wa Roma tarehe 4-25 Oktoba 2009, na Kanisa la Tanzania lilipata bahati ya kuwakilishwa na Maaskofu 9 na waamini Walei 3. Wakiwa wameungana na Baba Mtakatifu, Mababa wa Sinodi wameweza kukabili hali halisi ya mambo katika Afrika ambayo si rahisi sana, wakitumia silaha za mwanga ( Rum 13:12) na upendo wa Kikristo, ambavyo vinatiwa nguvu na kuhamasishwa na matumaini ya Bwana Mfufuka Yesu Kristo. Pamoja na vikwazo vinavyozuia uinjilishaji, ambavyo chanzo chake chaweza kuwa sababu za kijinsia, kidini na kijamii, kuna matatizo makubwa ambayo yanahitaji ushiriki wa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema: hali ya umaskini, ukiukaji wa haki, magonjwa, unyonyaji, ukosefu wa mazungumzano, mgawanyiko, kutovumiliana, vurugu, uchafuzi wa mazingira, ugaidi na vita. Kanisa, likiwa na utii kwa amri ya Bwana wetu Yesu Kristo, linaalikwa kutangaza Habari Njema bila kuchoka, ili litoe, kwa njia ya huduma mbalimbali za kichungaji, utafutaji wa upatanisho wa kikanisa na kijamii kwa njia ya Kristo, amani yetu na upatanisho wetu, chanzo cha haki ya kweli kwa Bara zima la Afrika.

Sisi Maaskofu wenu, tunaungana nanyi katika kumshukuru Mungu kwa ajili ya Sinodi hii kwa ajilii ya Afrika, tunawaalika kuyapokea matunda yake, na tunawataka, hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima, msali na kuomba ili kila Mkristo awe kweli mjumbe wa Upatanisho, Haki na Amani.

7.0 HITIMISHO
Tunawatakia Neema na Baraka za Mwenyezi Mungu katika kipindi hiki kitakatifu cha Kwaresima. Tunawaombea ili Neema za kipindi hiki ziwasaidie kukua katika kumjua Mungu na kumwalika atawale katika maisha yenu. Tunashirikiana nanyi katika kuwaombea Mapadri wetu ili wawe kweli watumishi waaminifu mithili ya Kristo. Tunaiombea nchi yetu tukufu Upendo, Umoja na Mshikamano, Amani na Usalama. Mwenyezi Mungu atujalie kuwapata viongozi watakaojali maslahi ya wote na wenye kuheshimu utu na hadhi ya kila mwananchi. Tunaomba utekelezaji wa Sinodi ya pili kwa ajili ya Afrika ulete kweli matunda ya Upatanisho, Haki na Amani katika Bara letu la Afrika na katika nchi yetu ya Tanzania.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, na Pendo la Mungu, na Ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote.

Tunawatakia Kwaresima Njema na Pasaka yenye Heri tele!



Ni sisi Maaskofu wenu,

1. Mhashamu Askofu Yuda Thadei Ruwa’ichi, Ofm Cap,
Dodoma, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
2. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Dar es Salaam
3. Mhashamu Askofu Mkuu Norbert Mtega, Songea
4. Mhashamu Askofu Mkuu Josaphat Lebulu, Arusha
5. Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ruzoka, Tabora
6. Mhashamu Askofu Nestor Timanywa, Bukoba
7. Mhashamu Askofu Aloysius Balina, Shinyanga
8. Mhashamu Askofu Emmanuel Mapunda, Mbinga
9. Mhashamu Askofu Telesphor Mkude, Morogoro
10. Mhashamu Askofu Gabriel Mmole, Mtwara
11. Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Iringa
12. Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani, Lindi
13. Mhashamu Askofu Anthony Banzi, Tanga
14. Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Mahenge
15. Mhashamu Askofu Evaristo Chengula, IMC, Mbeya
16. Mhashamu Askofu Augustino Shao, Cssp, Zanzibar
17. Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi, Sumbawanga
18. Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Rulenge-Ngara
19. Mhashamu Askofu Jacob Venance Koda, Same
20. Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma, Singida
21. Mhashamu Askofu Method Kilaini, Bukoba
22. Mhashamu Askofu Damian Dallu, Geita
23. Mhashamu Askofu Paschal Kikoti, Mpanda
24. Mhashamu Askofu Ludovick Minde, OSS, Kahama
25. Mhashamu Askofu Alfred Leonard Maluma, Njombe
26. Mhashamu Askofu Castor Paul Msemwa, Tunduru-Masasi
27. Mhashamu Askofu Beatus Kinyaiya, Ofm Cap, Mbulu
28. Mhashamu Askofu Michael Msonganzila,, Musoma
29. Mhashamu Askofu Issack Amani, Moshi
30. Mhashamu Askofu Protas Rugambwa, Kigoma
31. Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza, Kayanga


[1] Taz. Misale ya Altare, TMP Book Department, Tabora, 1976, uk. 30
[2] Cfr. Confessions c 7:10
[3] Benedetto XVI, Lettera per l’indizione di un anno Sacerdotale, Libreria Vaticana,2009 ,p.3
[4]Cfr. Christifideles Laici, 42
[5] Francis Wright Beare, The Gospel according to Matthew, Basil Blackwell, Oxford 1981, p.136
[6] Georg Strecker, The Sermon on the Mount, An Exegetical Commentary, T&T Clark, Edinburgh, 1987, p. 49
[7] Ibid
[8] “Salt” in Dictionary of the Bible, John L. Mckenzie, S.J; Geofrey Chapman, London, 1965, p. 760; Hauck “ala” in Theological Dictionary of the New Testament, ed. Gerhard Kittel, vol. I, Eerdman, Grandrapids, (MI), 1995, p. 229.
[9] Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vaticano, Gaudium et Spes, 47
[10] L’Osservatore Romano, n. 43, 28 October 2009, Ujumbe wa Sinodi ya Pili ya Afrika, uk. 28
[11] Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 2207
[12] Deus Caritas Est, 2
[13] Gravissimum Educationis, 3
[14] Apostolicam Actuositatem, 11
[15] Lumen Gentium, 11 & Gravissimum Educationis, 3
[16] Taz. Efe 6:1; Kol 3:20
[17]Taz. 2 Tim 3:2
[18] Taz. Gaudium et Spes, 48
[19] Congregatio pro Clericis, Vatican City, 3rd April, 2009 – Letter.
[20] Benedetto XVI, Lettera per l’Indizione di un anno Sacerdotale, Libreria Editrice Vaticana, 2009, p. 3; Katekisimu ya Kanisa katoliki, Pauline, 2007, 1589.
[21] Presbyterorum Ordinis, 2
[22] Lumen Gentium, 10
[23] Taz. Rom 15:16
[24] Taz. Ebr 5:1
[25] Taz. Ebr 2:17; 4:15
[26] Taz. 1 Kor 9:19-23
[27] Taz. Mdo 13:2
[28] Taz. Mk 16:16; Rom 10:14-15
[29] Presbyterorum Ordinis, 4
[30] Taz. Evangelii Nuntiandi, 41 na 21
[31] Presbyterorum Ordinis, 5
[32] Presbyterorum Ordinis, 5
[33] Lumen Gentium, 28
[34] Taz. 2 Kor 10:8; 13:10
[35] Taz. Gal 1:10
[36] Taz. 1 Kor 4:14
[37] Benedetto XVI, Lettera per l’Indizione di un anno Sacerdotale, p. 4
[38] Benedetto XVI, Lettera per l’indizione di un anno Sacerdotale, p. 5
[39] Taz. Bernard Nodet, Le Cure’ d’Ars. Sa Pense’e- Son Coeur, ed. Xavier Mappus, Foi Vivante, 1966, p. 98
[40] Taz. Bernard Nodet, cit; p. 101.
[41] Taz. Bernard Nodet, cit. Pp. 98-100.
[42] Benedetto XVI, Il nostro essere Sacerdote: un Nuovo e Radicale Modo di unificazione con Cristo, Libreria Vaticana, 2009, p. 4.
[43] Benedetto XVI, il nostro Essere Sacerdote, cit. P. 5.
[44] Evangelium Vitae, 22
[45] Gaudium et Spes, 36
[46]Taz. Yn 17:16.
[47] Taz. Apostolicam Actuositatem, 5
[48] Taz. Mk 6:3.
[49]Letter to Diognetus, 5; taz. Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 2240
[50] John Paul II, Barua ya Kitume ya kumtangaza Mtakatifu Thomas More msimamizi wa Watawala na Wanasiasa, AAS 93 (2001) 76.
[51]Gaudium et Spes, 43 na 75.
[52] Gaudium et Spes, 25

No comments: