Monday, July 19, 2010

MAKALA YA JINSIA




Afrika na changamoto ya mimba za utoto
Na Lilian Timbuka
BARA la Afrika, hasa maeneo ya Ukanda wa Jangwa la Sahara na Asia ndiyo yanayoongoza kwa idadi kubwa ya vijana walio chini ya umri wa miaka 15.
Katika maeneo haya, takwimu zinaonyesha kuwepo na idadi kubwa ya wasichana wanaopata mimba kabla ya wakati unaopendekezwa kitaalamu.
Sehemu kubwa ya vijana hao, tayari wako kwenye hali ya kukua kimaumbile na kiakili, hali iliyopelekea wengi kuingia kwenye vitendo vya ngono mapema.
Mwaka 2009, taasisi ya kimataifa inayojihusisha na takwimu za idadi ya watu duniani, (World Cencus Bureau) ilitoa takwimu zinazoonyesha kuwa idadi ya vijana chini ya miaka 15, sasa imefikia bilioni 1.2
Hii ina maana kuwa, idadi hii ni asilimia 20 ya watu wote duniani.
Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, inaonyesha kuwa maeneo ambayo kuna idadi kubwa ya vijana wenye umri chini ya miaka 15, ndiko pia kwenye idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na matatizo ya uzazi.
Hii inatokana na watoto wengi wa kike katika umri mdogo kuingia kwenye vitendo vya ngono kwa ridhaa yao wenyewe, au ushawishi unaotokana na sababu mbalimbali.
Kwa mfano, uchunguzi uliofanywa sehemu mbalimbali na (WHO) kwa Ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, (Tanzania ikiwemo), asilimia 28 ya wanawake wenye umri wa miaka 20 - 24, walishika mimba kabla ya umri wa miaka 15.
Ripoti mbaya zaidi iliyoelezwa kwenye ripoti hiyo inaihusisha nchi ya Niger ambayo ndoa za mapema kwa wasichana wadogo zinaonekana kuwa utamaduni uliozoeleka kiasi cha kufikia asilimia 51.
Nigeria nayo ni miongoni mwa nchi zenye takwimu mbaya za vijana kuingia kwenye vitendo vya ngono mapema.
Nchi hii ni miongoni mwa zile za Afrika zenye idadi kubwa ya wanawake wanaoolewa na kushika mimba mapema, ambapo sasa imeripotiwa kuwa ongezeko limefikia asilimia 28 kwa mujibu wa takwimu za mwaka jana.
Nigeria ina vijana chini ya umri wa miaka 24 wapatao milioni 45, sawa na idadi ya watu wote Tanzania kwa mujibu wa sensa ya Mwaka 2000.
Nchi nyingine zenye mfano kama huo ni pamoja na Nicaragua (asilimia 28), na Bangladesh (asilimia 46).
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Chama cha Madaktari wanawake nchini (Mewata), Marina Njelekela, kitaalamu wakati mzuri wa kushika mimba ni miaka 18 na kuendelea.
Kimaumbile inabainika kuwa wanawake wanaoshika mimba katika umri mdogo, wanakuwa kwenye hatari ya kukumbana na matatizo wakati wa kujifungua mara nne zaidi kuliko kama wangefanya hivyo baada ya miaka 18.
Tafiti za wataalamu zinabainisha kuwa, imani za kidini, ukosefu wa haki sawa baina ya Mwanaume na Mwanamke, utajiri wa haraka haraka, msukumo wa maamuzi kutoka kwa baadhi ya jamii unaomuona mtoto wa kike kama mzigo, ni moja ya mambo yanayosababisha ndoa za mapema.
Dhana potofu ya hamu ya uzazi wa mapema ili kujenga familia kubwa, ni mambo ambayo jamii imeyafungia macho kwa muda mrefu na hivyo watoto wadogo wa kike kujikuta wakiozeshwa.
Aidha, imani potofu kwa baadhi ya wanaume kwamba wasichana wenye umri mdogo kuolewa mapema ni baraka 'utajiri' ni mambo mengine yanayokwamisha jitihada hizi za kukabiliana na tatizo hili.
Kwa upande wao, wazazi ambao kimsingi ndio wabebaji wakubwa wa jukumu la malezi kwa watoto wao, wamekuwa sehemu kubwa ya tatizo hili kutokana na kuruhusu binti zao kuolewa katika umri mdogo.
Hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na umaskini unaowashawishi wazazi kuwakatiza masomo watoto wao na kupokea mahari ili kukidhi mahitaji ya maisha ya kila siku.
Kibaya zaidi ni kwamba, wazazi wamekuwa wakifanya hivyo huku wengine wakijua fika athari zinazoweza kutokea kutokana na maamuzi hayo.
Lakini pia ndoa za mapema zinawanyima uhuru wasichana kuendelea na masomo, jambo ambalo kama wangekuwa na nafasi, nalo wangeweza kujiendeleza na hivyo kuipa jamii 'utajiri' wa wanawake wengi wenye elimu.
Wasichana wengi hasa sehemu za mijini, wamejikuta wakirubuniwa kirahisi kwa ushawishi wa pesa au vitu vingine vya thamani, na hii si tu imewafanya kupata mimba mapema, baadhi yao wameambukizwa ugonjwa hatari wa Ukimwi.
Vifo ni athari nyingine kubwa, huku baadhi vikitokana na utoaji wa mimba kiholela unaofanywa na madaktari waliokosa sifa.
Kwa mujibu wa Njelekela, jamii inaweza kuepuka tatizo hili iwapo mifumo ya maisha inayokandamiza jinsia ya kike itaondolewa na hamasa kubwa ikawekwa katika kutetea haki za mtoto wa kike.
Bila kufuata mifumo hiyo ya maisha, bado watoto wa kike wataendelea kupata taabu ndani ya jamii.
Aidha, jambo lingine muhimu ni jamii kubadilika na kufuta dhana potofu inayolenga kumuona mtoto wa kike kama mzigo.
Wazazi pia watambue wajibu wao katika suala la malezi ya watoto na kuepuka vishawishi vya kuwaoza mabinti zao mapema kwa lengo la kupata mahari au utajiri wa haraka haraka.
Aidha, elimu ya kutosha kuhusu athari za kutumbukia kwenye vitendo vya ngono mapema sambamba na athari za ugonjwa wa Ukimwi, ni mambo muhimu ambayo jamii inabidi kuyaangalia kwa mapana zaidi.
Wasichana pia wanapaswa kuepuka tamaa za kuishi maisha ya kisasa katika umri mdogo kwani kwa kufanya hivyo, kutawaepusha na vitendo vya ngono


No comments: