Na Waandishi Wetu
WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdori Shirima kuzuia haraka matibabu ya magonjwa sugu yanayoendeshwa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la KKKT, Ambilikile Mwasapile katika Kijiji cha Samunge, Tarafa Sale, Loliondo.
Dk Mponda alisema hayo jana alipokuwa akijibu swali la waandishi wa habari baada ya kumaliza kuzindua matumizi ya Bajaji kwa ajili ya kusafirishia wagonjwa.
MCHUNGAJI Mstaafu Ambilikile Mwasapile akiendelea na kazi ya kutoa dawa
Alisema amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha kumzuia mchungaji huyo kuendelea na utoaji wa dawa mpaka serikali itakapojiridhisha na hali ya usalama pamoja na uwezo wa dawa hiyo.
“Kutokana na hali halisi ya usalama wa kiafya kwa sasa katika eneo hilo, kuna hatari ya kuwepo kwa milipuko ya magonjwa kwa kuwa idadi ya watu inazidi kuongezeka,” alisema Dk Mponda.
Hata hivyo, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Raymund Mushi alisema hajapata taarifa yoyote kuhusiana na hatua hiyo ya Wizara ya Afya... "Hadi jioni hii mpaka ninatoka ofisini sijapata taarifa yoyote kuhusiana na uamuzi huo."Baadhi ya wananchi waliohojiwa kuhusiana na hatua hiyo ya Serikali walisema badala ya kuchukua hatua hiyo, ilipaswa kusimamia mchakato mzima wa utoaji wa dawa hiyo kwa kuhakikisha kwamba inatolewa katika mazingira mazuri na kuhakikisha huduma muhimu za kijamii zinapatikana kijijini hapo ikiwa ni pamoja na kuwabana wamiliki wa magari kupunguza nauli na kukarabati barabara.
Mkazi wa Karatu, Reurent Bortha, alisema anashangazwa na serikali kuibuka sasa wakati mchungaji huyo alianza kutoa dawa hiyo tangu Agosti mwaka jana... "Tunaiomba serikali kusaidia upatikanaji huduma muhimu kama mahema na kukarabati barabara na siyo sasa kuibuka na kusema dawa haijafanyiwa utafiti."
Bortha ambaye amedai kwamba ndugu zake wamepona maradhi mbalimbali kutokana na dawa ya mchungaji huyo, alisema serikali imechelewa kufanya utafiti wa kuthibitisha dawa hiyo kitaalamu na inachopaswa kufanya ni kuweka mazingira bora ya utolewaji wake.Mwananchi mwingine, Peter Ngoi alisema kama serikali inatilia shaka dawa hiyo, inapaswa kuwafuata watu waliokunywa na kupona na siyo kuhangaika kuipima na kuichunguza... "Hawa watu wa Serikali ni wa ajabu hawajazungumza na sisi wagonjwa wanakaa Dar es Salaam na kutangaza kusitisha dawa."
Dk Mponda alisema serikali ilishaanza kuchukua hatua za awali ikiwepo ya kupeleka wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), ambao alidai kuwa wamewasili eneo hilo tangu Jumanne iliyopita na kuanza kufanya uchunguzi.
Alisema utaratibu wa kisheria wa utoaji wa dawa unamtaka atakayegundua dawa ya aina yoyote anatakiwa kufuata taratibu zilizopo ikiwemo kuthibitishwa na TDFA ili kuangalia ubora na madhara yake kwa watumiaji.“Sheria zipo, tatizo lililopo ni katika usimamiaji. Hata hivyo, inachukua muda mpaka utaratibu wa kuithibitisha dawa kama inafaa au haifai kwa matumizi ya kutibu magonjwa ya binadamu," alisema Dk Mponda.
Akizungumza katika uzinduzi wa matumizi ya pikipiki hizo, Dk Mponda alisema zimenunuliwa na serikali kwa ajili ya kubebea wagonjwa. Alisema katika awamu ya kwanza, Serikali imenunua pikipiki 400 maalumu kwa ajili ya kubebea wagonjwa zenye thamani ya dola za Marekani 5,900 kila moja.
Waziri huyo alisema pikipiki hizo zitagawiwa katika mikoa yenye matatizo ya usafiri hasa maeneo yenye milima ikiwamo Rukwa, Mbeya, Pwani, Morogoro na Dodoma.Dk Mponda alisema pikipiki hizo zimekuwa usafiri wa uhakika kwa wagonjwa katika nchi za Afrika ya Kusini, Sudani, Kenya na Senegal, Malawi, Ethiopia na Guinea.
No comments:
Post a Comment