Wednesday, August 8, 2012

NANENANE YA MAJONZI, BASI LAUA 17 PAPO HAPO TABORA


Na El - hadji Yuusuf, Tabora
WATU 17 wamefariki dunia baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Tabora kwenda Mbeya kupinduka eneo la Kitunda wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.

Ajali hiyo, ilitokea umbali wa kilomita 200 kusini mwa mji wa Tabora, ikilihusisha basi la Sabena aina ya Scania lenye nambari za usajili T 570 AAM.
Katika ajali hiyo, watu wanne wamejeruhiwa vibaya na wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Kitunda wakisubiri kuhamishiwa katika Hospitali ya Mkoa ya TaboraKitete, kwa ajili ya matibabu zaidi.
Abiria wengine 54 waliokuwa katika basi hilo walinusurika na kuomba kuendelea na safari, baada ya kufanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa hawakuwa na madhara makubwa katika miili yao. Miongoni mwa watu walikufa ni watoto 6 wanawake 5 na wanaume 6 ambao miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Kitete kwa ajili ya kutambuliwa na ndugu na jamaa zao.
Hata hivyo, hadi kufikia jana mchana, miili ya watu saba ilikuwa imetambuliwa na baadhi ya ndugu, ukiwemo wa askari Polisi Konstebo Kheri, wa Kituo Kikuu cha Polisi cha mjini Tabora.
Marehemu wengine waliotambuliwa ni Vitus Tulumanye, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), tawi la Tabora na Farah Inga raia wa Zimbabwe aliyekuwa akifanyakazi Tabora.
Wengine waliotambuliwa ni Ikamba Thadeo, Damalu Goma, Beatrice Kalinga ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi Igoko wilayani Uyui mkoani Tabora na Madirisha ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi iliyoko wilaya Mpya ya Kaliua.
Mwalimu Madirisha anadaiwa kufuatana na watoto wanne na mkewe ambaye bado hajatambuliwa najuhudi zinaendelea za kubaini familia ya mwalimu huyo.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na dereva wa basi hilo kwa mwakilishi wa basi hilo mkoani Tabaro, Shaaban Mnyema, chanzo cha ajali hiyo ni lori aina ya Fuso lililokuwa limeegeshwa katika kona. Alidai kuwa dereva wa basi hilo alipojaribu kulikwepa 'Stearing Road' ilikatika na gari kuacha njia na kupinduka.
Dereva huyo Ali Nassoro, ambaye alitoroa baada ya kutoa taarifa za ajali na maelezo hayo kwa njia ya simu, alisema ajali hiyo ilitokea jana saa 6.30 mchana katika eneo ambalo halina mawasiliano ya simu za mkononi.
Nassoro alisema hata katika kijiji cha Kitunda kulikuwa hakuna mawasiliano na hivyo kumlazimi kumtuma mtu kwenda Sikonge kutoa taarifa za ajali hiyo.
Baadhi ya majeruhi waliotambuliwa ni Grace Mbunga, Kayungilo Nsungu, Zena Shigela, Ndisi Ngosha, Kulwa Kija, Feni Salum, Shinje Kayogole na Emmanuel Charles.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Anthony Ruta, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na alipouwa akiwasiliana na Mwandishi alikuwa njiani kuelekea eneo ilipotokea ajali.

No comments: