Monday, November 30, 2009

HUYU NDIYE PADRI!



HUYU NDIYE PADRE
Na Padre Gaudence Talemwa

Padre ni mtu muhimu na mwenye kuhitajiwa na kundi la Mungu. Kwa kinywa chake anaweza kutamka maneno ya Bwana “Mimi ni njia, ukweli na uzima. Hakuna ajaye kwa Baba ila kwa njia ya mimi” (Yoh. 14:6).

Padre ni Mtumishi wa Mungu anayejitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa watu wa Mungu, “Kila padre ni kristo mwingine”. (“Alter Christus”). Ni mwanadamu kama wandamu wengine, aiyetwaliwa kati ya watu kwa mambo yamuhusuyo Mungu (Ebr. 5:1-3). Kumbe asiye binadamu hawezi kuwa Padre. Kwa hiyo padre hata baada ya upadrisho anaendelea kuwa binadamu. Na sote tunafahamu kuwa hali ya kibinadamu ni hali ya unyonge, uchovu, kushawishika kukata tamaa. Kumbe si halali watu kukasirika wanapomwona Padre mnyonge kama wao, si halali kuwadai mapadre kuwa na akili kama malaika, si halali kutaka upendo wao uyeyushe ugumu wa kila mkosefu au wawe na ufundi wa kutatua matatizo yote ya maisha. Ukweli ni kwamba wanaoteuliwa kuwa mapadre ni viumbe wanyonge wanaoshiriki unyonge wa ndugu zao. Na hii inawawezesha kuwaombea ndugu zao bila unafiki, vile vile ni wajibu wa waamini kuwaombea mapadre wao ili waishi kadiri ya wito wao kwani “hakuna mtu ajitwaliaye heshima hii yeye mwenyewe, ila yeye aitwaye na Mungu”. (Waebrania 5:4).

Tusikwazwe na unyonge wa padre, bali kinyume chake kiwe ndicho kweli. Unyonge wa padre uwe ni tumaini la wakosefu, uwe ni kitambulisho dhahiri kwamba Mungu hadharau unyonge wa binadamu. Mkosefu akikiri unyonge wake na kuomba msamaha Mungu atamjaza mema yake. “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki bali wenye dhambi”. (Lk 11:17). Hayo ni maneo ya kristo. Basi Padre kwanza ni binadamu kwa sababu ni mwakilishi na wombezi wa kweli wa ndugu zake, tushinde kishawishi cha kuwahukumu mapadre wetu, tuwaonee huruma, tuwaombee kama wanavyotuombea sisi; tuwaitikie, tuungane nao kwani ni wito wao kutuunganisha kwa jina la Bwana.

Yatubidi tufahamu kuwa Padre yuko nasi katika kipindi cha kuzaliwa kwetu, kufa kwetu, wakati wa furaha yetu na huzuni pia, katika nyakati na sehemu muhimu za maisha yetu Padre yupo. Mungu amempatia Padre uwezo mkubwa wa kuwatakatifuza watu.

Sakramenti ya upadre iliwekwa na kristo mwenyewe kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake pale alipowapatia wanafunzi wake Ekaristi Takatifu ambayo ingetolewa mpaka mwisho wa nyakati. Kazi hii huendelea kila katika ibada ya misa.

Katika mlima wa mizeituni kristo aliwapatia mitume wake uwezo wa kuondolea watu dhambi, kubatiza na kufundisha habari njema kwa watu wote. Padre anaendeleza wajibu huu yeye kama mtume wa kristo kwa mataifa yote.

Padre ana kazi ya kuwaelekeza watu kwa Mungu. Kwa uwezo aliopewa na Mungu, Padre hulisha roho za watu kwa chakula cha roho yaani Ekaristi Takatifu. Padre wa sasa huendeleza kazi ya mitume wa kwanza.

Sakramenti ya upadre humfanya “mkandidati” wa upadre kuwa kiumbe kipya na kumpatia alama isiyofutika – yeye ni kuhani milele.

Kazi ya kwanza ya padre kiujumla ni ya kiroho, yaani ya kutakatifuza watu. Kazi hii si ya siku moja, juma moja miezi au mwaka, bali ni kazi yake ya kila siku mpaka wakati wa kifo chake. Kazi ya Padre ni ya wakati wote. Maisha ya Padre yameungana na kristo na yametolewa kwa ajili ya watu wa Mungu. Tunamwita Padre “Father” yaani Baba, na kweli ndivyo alivyo.

Narudia tena Padre ni mwanadamu aliyepewa uwezo wa kutufanya watoto wa Mungu. Padre kweli kweli ni Mtumishi wa Mungu, lakini hata hivyo atakufa kama binadamu wengine. Kama Kristo mwingine hakuna mtu anayependwa sana na kuchukiwa sana kama Padre. Padre yuko katikati ya kila tatizo. Jitihada kubwa, kazi za ukarimu na sadaka mbalimbali vimekuwa majitoleo yake katika jumuia. Padre ni mtu wa ufahamu na mtu wa ukimya. Mtu anapoanguka kwa sababu ya ubinadamu husamehewa, lakini kwa Padre ni tofauti, hupigiwa kelele na kuhukumiwa hapo hapo. Ni akina nani wanaomwona Padre kuwa na kosa na kumuhukumu? Mara nyingi ni wale aliowasaidia kiaminifu na vizuri.

Katika uchanga wetu, Padre yupo ili apate kutubatiza. Kwa uwezo aliopewa na kwa mikono yake, dhambi ya asili inaondolewa kwa Mbatizwaji na anafanywa kuwa mtoto mteule wa Mungu

Katika uchipukizi na ujana wetu, Askofu ambaye ni Kuhani (Padre) hutupatia sakramenti ya Kipaimara ambayo kwayo tunajazwa mapaji ya Roho Mtakatifu. Aliyeimarishwa anapewa nguvu na kuwa askari amini wa Bwana.

Kila siku Padre hutupatia Ekarist Takatifu kwa ajili ya ustawi wa roho zetu. Kwani wakati maisha yetu yanapokuwa katika hatari, vishawishi na wasiwasi, tunahitaji mkate wa mbingu ili roho zetu ziimarike. Vijana na wazee, tajiri na maskini, wasomi na wasio wasomi wote wanaalikwa kumpokea Bwana wakiwa wamejitakasa.

Tunapokuwa wadhambi, tumezama katika dimbwi la utumwa wa shetani, tujongeapo kwenye kiti cha kitubio, sauti tulivu ya Padre ina nguvu ya Mungu kumtamkia Mdhambi “Nakuondolea dhambi zako kwa Jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu”. Maeneo haya humfukuza shetani na matokeo yake ni utulivu na amani ya roho anayopata mwenye kuondolewa dhabi.


Padre hubariki na kushuhudia makubaliano ya wawili wanaoahidi uaminifu katika sakramenti ya ndoa. Familia mpya, kiini msingi cha jumuia inapata baraka ya Mungu na kukua katika misingi ya imani kwa malezi elekezi ya Padre. Padre huunganisha jitihada zake na za wazazi katika kuelimisha watoto katika mambo ya imani na kuwaandaa kupokea sakramenti, Padre hachoki!. Hata wakati wa magonjwa tayari yuko pembeni mwa vitanda vyetu akitupatia Mpako Mtakatifu kwa kututuliza, kutuimarisha na kutuponya na uovu na ugonjwa pia.

Katika mazishi yetu Padre yupo tayari kupumzisha miili yetu katika shamba la Bwana. Na kila siku katika misa husali kwa ajili ya roho za marehemu walioko toharani.

Kazi afanyazo Padre zimepanuka katika uwanja mpana wa maisha ya binadamu, palipo na huzuni Padre huleta furaha, pasipo na haki hutetea haki, kwa vijana huwatia moyo na kuwafundisha fadhila mbalimbali, utii kwa watu, uaminifu, moyo wa uwajibikaji na heshima kwa watu. Huwakumbusha matajiri juu ya wajibu wao wa kusaidia wahitaji na waajiri kulipa ujira unaostahili. Kwa kuwa wito wake ni kazi ya ukweli, Padre ni chumvi ya dunia!.

Hakuna kazi yoyote njema na nzuri hapa duniani ambayo Padre hajatoa mchango wake wa usaidizi. Hujihusisha na kazi za elimu, sanaa, utafiti, huanzisha taasisi za ukarimu, vyuo na shule kwa ajili ya kutoa elimu, hospitali kwa wagonjwa na nyumba kwa wazee na wasiojiweza.

Padre hutoa zaidi na hupokea kidogo, zaidi hulipwa chuki na minongono. Kwa sadaka yake Padre inabidi apate heshima. Ni mtu anayemwakilisha Kristo. Kama Mtakatifu Francisko alivyosema “kama ningekutana na malaika pamoja na Padre, ningeweza kumsalimia kwanza Padre, kwani Malaika ni rafiki wa Mungu na Padre ni Mhudumu wa Mungu”.

Waamini wote wana wajibu kwa Mapadre wao. Jumuia bila Padre maendeleo yake ya kiroho ni haba!. Mtakatifu Yohana Maria Viane alisema: “Acha eneo na sehemu yoyote bila Padre kwa miaka ishirini, matokeo yake watu wataanza kuabudu wanyama”.

Kuna njia kuu mbili za kuwasaidia Mapadre wetu:
Waombee ili wawe watakafitu. Omba ili Kristo atume mapadre wengi katika shamba lake lenye mavuno mengi na wavunaji wachache. Wasaidie kwa mahitaji ya kimwili yaani kwa michango mbalimbali ya kuwezesha uimarishaji wa wito wa upadre katika seminari na kwa mapadre wenyewe. Tusaidie kuwaelekeza watoto wetu wa kiume katika wito huu mtakatifu wa upadre kwani anayetoa zawadi ya Padre kwa kanisa analipatia kanisa Kristo mwingine. Padre kwa kanisa ni zawadi kubwa kuliko zawadi zote zitolewazo.

No comments: