Nimezaa na dada yangu bila kujua; nifanyeje?
NIMEZALIWA katika familia ya watu wenye uwezo wa kati. Wazazi wangu walikuwa watumishi wa Serikali na tuliishi maisha mazuri sana. Jirani na sisi kulikuwa na familia nyingine ambayo ilikuwa rafiki wa familia yetu. Wazazi wetu waliishi kwa upendo na maelwano makubwa kiasi kwamba tulikuwa kama ndugu.
Sisi watoto tulielewana sana na mahusiano hayo mema yaliendelea hata baada ya familia zetu mbili kuachana kwa sababu za kikazi.
Miaka kadhaa baadaye, nilikutana na mtoto mmoja wa kike wa ile familia rafiki, na kwa kuwa tulifahamiana vema, tulijikuta tukiangukia katika mahusiano ya mapenzi.
Kwa kweli mapenzi yetu yalikuwa ya dhati kabisa na kama walivyo vijana wengi wa siku hizi, tulianza kuishi pamoja kama vile tungekuwa mke na mume.
Katika mahusiano hayo, mchumba wangu alishika ujauzito. Niliwataarifu wazazi wangu kuwa nimepata mchumba na nikawahakikishia kwamba watampenda kwa sababu anatoka katika ukoo na familia wanayoijua vema. Hata hivyo, sikuwaambia kuwa mwenzangu ni mjamzito kwa sababu wangechukia sana.
Hatimaye, mwenzangu alijifungua mtoto mzuri wa kiume, na hapo ndipo tukaona vema sasa kuwataarifu wazazi wetu nia yetu ya kufunga ndoa. Tulikubaliana na mwenzangu kwamba kila mmoja akawaambie wazazi wake ili maandalizi ya ndoa yaanze mara moja.
Wazazi wangu walikuwa na hamu ya kumjua mchumba wangu. Nikiwa nimejawa furaha, niliwaambia kwamba ni mmoja wa binti za ile familia rafiki. Kitendo cha kutaja tu jina la binti yule, baba alipokea jambo hilo kwa furaha kubwa na kunipongeza kwa kuchagua binti kutoka kwa familia wanayoijua kikamilifu.
Lakini hali ilikuwa tofauti kwa mama. Yeye alikosa raha ghafla, na bila kutarajia alisema haungi mkono kwa sisi kuoana.
Mimi na baba tulijaribu kuuliza kulikoni apinge wakati tunaotaka kufunga ndoa ni watoto wa familia mbili zilizo marafiki na zinazojuana kwa muda mrefu. Lakini mama alishikilia msimamo wake huo huo. Kwanza, tulidhani anafanya utani, lakini ukweli ni kwamba huo ndio ulikuwa msimamo wake wa kutotaka tufunge ndoa. Lakini nilipomwambia kwamba tayari tuna mtoto, mama aliangua kilio kikubwa na kusema hata kama imetokea hivyo, bado hawezi kukubali tuoane.
Baba ambaye kwa tabia ni mpole sana na hupenda mara nyingi kumsikiliza mama, alijaribu kumshawishi mama akubaliane na chaguo langu na kama hataki aseme ni kwa sababu gani hataki tusifunge ndoa. Pamoja na kuulizwa kwa muda mrefu, mama hakuwa tayari kusema sababu zaidi ya kudai tu kwamba hataki.
Mama ambaye kwa wakati huo alikuwa anafanya biashara na mwenye fedha za kutosha, alisema yuko tayari kunipa chochote, lakini sio mimi kufunga ndoa na mchumba wangu. Jambo hilo lilinipa wakati mgumu sana kwa sababu kwanza, tayari tuna mtoto, pili tunapendana sana na mwenzangu, na tatu, mama hasemi sababu gani hataki tufunge ndoa. Nilijaribu kutafuta sababu labda ya kuwepo kwa ugomvi baina yao nikashindwa. Katika kukaa kwao na familia wakwe zangu watarajiwa, sikuwahi kusikia wakisemana vibaya ama wakigombana. Sasa tatizo nini?
Nilimtafuta mchumba wangu kwa njia ya mawasiliano na nilipompata, nilitaka kumwambia ukweli kwamba mama hataki tufunge ndoa ingawa nilihofia matokeo ya habari hiyo kwa sababu kama angeniuliza sababu, ningeshindwa kujibu.
Hata hivyo, wakati nataka kumweleza hali halisi, naye alisema wazazi wake hawajaafiki wote sisi kuoana! Nilipouliza ana maana gani kuwa hawajaafiki wote, mchumba wangu alisema wakati mama yake amepokea kwa furaha kubwa taarifa ya sisi kutaka kufunga ndoa akisema kuwa sasa familia hizi mbili zitakuwa si rafiki tena bali ndugu, baba yake amepinga kwa nguvu zote kwamba tusioane!
Nilishituka sana kusikia habari hii. Kwangu mama hataki, ila baba anataka. Kwa mwenzangu, baba yake hataki, lakini mama yake anaunga mkono. Kulikoni?
Ilibidi nami niweke mambo hadharani. Mchumba wangu alishikwa na butwaa aliposikia kisa kama hiki kwa upande wetu pia.
Kwa zaidi ya mwezi tulibaki katika giza tusijue sababu halisi za mama yangu na baba wa mchumba wangu kupinga, wakati mama baba yangu na mama wa mwenzangu walituunga mkono.
Lilikuwa jaribio kubwa na lililotupa wakati mgumu. Ilibidi vikao vya ndugu wa pande zote mbili kila kimoja kwa namna yake, vikao kujadili suala hilo. Hata hivyo, vikao hivyo havikuzaa matunda. Tulichukua uamuzi mgumu na wa mwisho. Tuliamua kwenda kanisani ambako Mchungaji wa Kanisa letu aliwaita wazazi wangu kila mmoja kwa wakati wake. Mwezi Septemba, mwaka huu, jioni moja, Mchungaji alitukutanisha mimi na wazazi na katika kikao hicho, Mchungaji baada ya kutoa maneno magumu na yaliyomtaka kila mmoja wetu kupokea taarifa atakazotoa kwa moyo wa ujasiri, hatimaye alisema kile kilichomfanya mama asitake sisi tufunge ndoa.
“Kwa kweli kila mwanadamu chini ya jua ana mapungufu yake na katika jambo hili, hakuna haja ya kushambuliana na kuchukiana, bali Mungu asimame na atupe moyo wa subira” alisema Mchungaji huyo, huku akimwangalia kila mmoja wetu kwa zamu. Baada ya kuona sote tumetulia na tunamwangalia kwa makini hatimaye alisema;
“Mama yetu amekiri mbele zangu na mbele za Mungu na ameomba toba kwa kosa hilo, kwamba hataki kijana wenu afunge ndoa na yule binti kwa sababu wao ni ndugu wa damu moja”
Awali sio mimi wala baba aliyeelewa maana ya kauli hiyo, na hilo likawa dhahiri machoni mwa Mchungaji wetu. Hakusubiri aulizwe na mmoja kati yetu. “Najua bado hamjaelewa. Ni kwamba, wakati ule mnaishi pamoja na ile familia, mama alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mzee wa ile familia na huyu kijana wenu (mimi) ni mtoto wa kuzaa wa yule mzee na siyo mtoto wako!”alisema huku akimtazama baba usoni.
Sitaki kusema kilichoendelea. Kila mmoja aliondoka ofisini kwa mchungaji akiwa amechanganyikiwa. Yaani, mimi ni mtoto wa yule mzee; kwamba mimi na mchumba wangu ni watoto wa baba mmoja!
Hadi wakati huu, nimeshindwa hata kumwambia mchumba wangu (dada yangu) kwa sababu najua inaweza kuhatarisha maisha yake. Lakini pia, kukaa kimya hakutaleta faida kwani hakuna siri ya watu wawili, iko siku itajulikana kama ilivyokuwa kwa siri ya mama kuzaa nje ya ndoa.
Pili, moyo wangu umekufa ganzi na mapenzi kwa mama yangu yametoweka kabisa. Nimehama nyumbani na nimechanganyikiwa kwa sababu sijui sasa nianze kujitambulisha kwa ubini upi. Kama mama amekiri kwamba mimi si mtoto wa ndoa, nitaendelea vipi kujiita ubini wa mtu asiye baba yangu? Na nitaanzaje kujiita ubini ambao utawachanganya watu? nifanyeje jamani wa kipindi cha MARIDHIANO?
Ndugu msomaji, unakaribishwa kuchangia mada hii ya msikilizaji wa RADIO MARIA KATIKA KIPINDI CHA MARIDHIANO kwa kutuma ujumbe wako wa maneno machache kwa email; kiongozi news &yahoo.com.
Monday, November 30, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment