Monday, November 30, 2009

AJALI! AJALI! AJALI!!!!!


Ajali za barabarani zinaua zaidi ya malaria kwa mwaka!
Na Lilian Timbuka
IMEELEZWA kuwa ajali za barabarani zimekuwa zikichangia vifo vingi vya watoto na vijana duniani, walio na umri kati ya miaka 10 mpaka 24 na ni chanzo cha tatu kwa vifo vya watu walio na umri kati ya miaka 30 na 44.
Hayo yameelezwa na Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Kimataifa ya kuwakumbuka waathirika wa Ajali za Barabarani kwa mwaka 2009, Tanzania.
Siku ya kuwakumbuka waathirika wa ajali za barabarani huadhimishwa kila ifikapo 15, Novemba ya kila mwaka.
Maadhimisho hayo yalianzishwa na Umoja wa Matafa kwa kupitia katika Azimio lake la namba A/60/5(2005), ambapo iliifanya itambulike kama siku rasmi ya kimataifa ya kuwakumbuka waathirika wa ajali hizo za barabarani na familia zao na kuzitaka nchi wanachama pamoja na jumuia za kimataifa kuitambua siku hiyo.
Siku hii pia inatoa fursa kwa jamii nzima kuwa na mwitikio katika ajali za barabarani, madhara, gharama, na hatua zinazoweza kuchukuliwa katika kuzuia ajali zisitokee, na ni siku ambayo pia inatoa nafasi ya kuikumbusha serikali wajibu wake na jamii nzima katika suala la kuzifanya barabara kuwa sehemu salama.
Katika bara la Afrika, maadhimisho haya yamekwishafanyika katika nchi za Afrika ya Kusini, Uganda na Nigeria katika miaka iliyopita.
Imeelezwa pia kuwa kila baada ya dakika 6, mtu mmoja hufa au kujeruhiwa kutokana na ajali za barabarani duniani kote, wakiwemo madereva, abiria, waendesha pikipiki, baiskeli na watembea kwa miguu.
Takwimu za dunia zinaonesha kuwa watu milioni 1.2 hufa kutokana na ajali za barabarani kila mwaka na kuacha mamilioni ya watu na ulemavu wa kudumu. Idadi hii ya watu ni kubwa ukilinganisha na idadi ya watu wanaokufa kutokana na malaria.
Watoto 260,000 hufariki kila mwaka kutokana na ajali za barabarani duniani kote. Shirika la Afya Duniani linaonyesha kuwa ifikapo mwaka 2015, ajlai za barabarani zitakuwa chanzo kikuu cha vifo na uolemavu kwa watoto.
Kutokana na hilo, asilimia 90 ya vifo hivyo hutokea katika nchi zenye pato la kati na la chini na Tanzania ikiwa miongoni mwa kundi la pato la chini kabisa na kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kati ya mwezi Januari na Juni mwaka huu, tayari watu 1460 wamefariki na watu 8,373 wamejeruhiwa kutokana na ajali za barabarani hapa nchini ambapo inaonyesha kuwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, kutakuwa na jumla ya vifo 3000.
Jamii inapaswa kutambua kuwa, madhara yote haya nimzigo mkubwa kwa nchi kama Tanzania. Mwaka 2006, ilkadiriwa kuwa ajali hizo zilileta hasara ya asilimia 3.4 ya pato la ndani la Taifa.
Hata hivyo, iwapo kama jamii na serikali itakuwa makini, vifo hivi vinaweza kuepukika, kwani zaidi ya robo tatu ya vifo vyote husababishwa na makosa ya kibinadamu, kwa maana ya kwamba, madereva, waenda kwa miguu, waendesha baiskeli na watumiaji wengine wa barabara, hufanya makosa ambayo huishia kupoteza maisha yao au ya wengine.
Lakini kwa kutoa elimu, uhandisi na usimamizi wa sheria za barabarani, kutasaidia kupunguza vifo visivyokuwa vya lazima.
Lakini tukirudi katika maandiko Matakatifu yanasema Mungu amesema damu ya watu hawa inamlilia katika nchi na mbinguni. Hapa tunapata fundisho ambalo si la kawaida sana kusikika , lakini ni muhimu. Kwani pale ambapo damu ya watu inamwagika ovyo ovyo bila hadhi ya mwanadamu, na mara nyingine vibaka nao hukusanyika pale kumalizia wanaopumua ili kuokota mali zao, ni mahali pa pekee kabisa.
Panastahili kukumbukwa kama sehemu ambapo ajali zinatokea na kumwagika ardhini damu ya watu wenfi na wasio na hatia.
Aidha ni vema kuwaombea marehemu walifariki kutokana na ajali na kwa namna ya pekee, kuwaombea msamaha kwa niaba ya wote waliosababisha vifo vyao.
Monsinyori Julian Kangalawe Katibu Mtendaji wa Idara ya Liturujia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), anasema siku kama hiyo kila mmoja ambaye anaendesha vyombo vya usafiri, ajitafakari namna anavyoweza kukiendesha chombo chake, na ni kwa namna gani anamjali Mungu muumba wa wote na jinsi anavyowahudumia wale ambao wanapata huduma katika vyombo hivyo vya usafiri.
“Na hatimaye tujifunze na tufundishe hata watoto wetu kujali uhai, kulinda kwa kila namna maana uhai unatoka kwa Mungu na ni mali ya Mungu peke yake aliye Bwana wa Mbingu na nchi,” amesisitiza Monsinyori Kangalawe.
Aliongeza kuwa, Mungu peke yake ndiye mwanzo wa uhai, hakuna mazingira yoyote yanayoweza kujitwalia haki ya kuharibu moja kwa moja kiumbe cha kibinadamu kisicho na hatia.
Alisema binadamu anapofikiria vyombo vya usafiri, anapaswa kuona umuhimu wa kuwa na kiasi, kwa kuwa fadhila hukaa katikati.
Fadhila ya kiasi inamuandaa binadamu kuzuia kila kitu kinachopita kiasi. Hivyo wale ambao wanasababisha vifo vya wenzao kwa jnjia ya ajali za barabarani, watambue kuwa wanafanya kosa kubwa.
Akinukuu Amri ya Mungu isemayo USIUE ambayo ni Amri ya Tano, Monsinyori Kangalawe anasema wale wote wanaoendesha vyombo vya abiria, inawapasa kujua amri hiyo na kukumbuka kuwa kila wanapozembea na kuendesha vyombo vya abiria kwa kasi isiyokubalika na kisha kusababisha ajali, watambue kuwa wanamkosea Mungu.
Anasema ajali nyingi za barabarani zinaonesha kusababishwa na mwendo kasi wa madereva, ama kujaza abiria na mizigo kupita kiasi. Ni rahisi sana kusema ajali ilitokea, lakini matokeo ya ajali hizo ni vifo vya watu.
Biblia inasema “Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake kupokea damu ya ndugu yako kutoka kwa mkono wako (Mwa. 4:10-11).”
Damu ya Habili peke yake inakuwa ni sababu ya kupata laana kwa namna hiyo inayotisha na kwa mtu anayesababisha ajali na kuwaua watu wengi wasio na hatia, Mungu atamwambia “Damu ya watu wote hawa inanililia kutoka katika nchi.”
Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA-CCC), limesema maadhimisho hayo mwaka huu yatafanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Na baadaye Tanzania inatarajia kutuma ujumbe wake nchini Moscow kuhudhuria mkutano wa kwanza wa Kimataifa wa Mawaziri unaohusu usalama barabarani.
SUMATRA imesema katika mkutano huo, Mawaziri wote wa usafirishaji kutokana katika nchi zote duniani, watapata nafasi ya kusaini Muongo wa Utekelezaji kuhusu usalama barabarani kwa lengo la kunguza kwa asilimia 50, vifo vinavyokadiriwa kufikiwa ifikapo mwaka 2020.
Taarifa hiyo ya SUMATRA imesema endapo Muongo wa Utekelezaji utathibitishwa, Serikali ya Tanzania inatarajiwa kuongeza nguvu katika sekta ya usalama barabarani, kufanya ubunifu madhubuti wa miundo mbinu, kubadili tabia ya watumiaji wote wa barabara na kutoa huduma nzuri baada ya ajali kutokea.
Hata hivyo imesisitixza kuwa jukumu la usalama barabarani si la Askari wa usalama barabarani au Serikali peke yake, bali ni jukumu la kila raia wa nchi hii kwa matumizi yasiweza kuhatarisha maisha ya watu wengine na wale wanovitumia vyombo hivyo.

No comments: