Viongozi wa MBOMIPA wakumbwa na kashfa!
· Wadaiwa kuendesha umoja huo pasipo uelewa
Na Getrude Madembwe, Iringa
JUMUIYA ya MBOMIPA iko katika hatari ya kupatwa na mpasuko mkubwa baada ya baadhi ya wawekezaji wake kudai kwamba inaongozwa na viongozi mbumbumbu wasio na uelewa wa kutosha kuhusu sekta ya wanyamapori na utalii.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba hali hiyo, inayaweka katika hali ya wasiwasi mahusiano baina ya uongozi wa MBOMIPA, vijiji vinavyounda Mbomipa na wawekezaji wake.
MBOMIPA ni umoja wa vijiji 21 vya Tarafa ya Idodi na Pawaga wilayani Iringa, vinavyopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha, vilivyokubali kutoa sehemu ya ardhi yenye vivutio vya wanyama wa aina mbalimbali wanaotoka katika hifadhi za Taifa za Ruaha na Mikumi, kwa ajili ya matumizi bora na faida ya vijiji vyote.
Tangu isajiliwe kama jumuiya miaka mitatu iliyopita, MBOMIPA imefanikiwa kupata wawekezaji watatu ambao ni pamoja na Kilombero North Safaris Ltd, Merela Safaris Ltd na Tandala Tented Camp, waliowekeza sehemu ya eneo lao lenye ukubwa wa kilometa za mraba 776.4 na ambao kwa mwaka wamekuwa wakichangia zaidi ya Sh Milioni 150 kwa jumuiya hiyo.
Mmoja wa wawekezaji hao Bw. John Fliakos ambaye pia ni Meneja wa Kituo cha Tandala, alisema idadi kubwa ya viongozi wa MBOMIPA ni wakulima wanaoifanya jumuiya ijiendeshe kienyeji tofauti kabisa na wasimamizi wa hifadhi za taifa ikiwemo Hifadhi ya taifa ya Ruaha ambao ni wasomi.
Uchunguzi zaidi umebainisha kwamba uelewa mdogo wa viongozi hao umesababisha ugawanyike kulingana na matakwa ya wawekezaji ambao wao wenyewe hawaelewani kutokana na sababu za kimaslahi.
Pamoja na kukataa kuzungumzia udhaifu wa uongozi wa MBOMIPA, Mkurugenzi wa Kilombero North Safaris Ltd, Michael Mantheakis alisema kuna haja watendaji wa vijiji vinavyounda jumuiya wakawa wajumbe wa vikao vya MBOMIPA ili wasaidie kuimarisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya asasi hiyo.
Wakati baadhi ya wananchi wa vijiji vinavyounda jumuiya hiyo wakiulalamikia uongozi wao kwa kutokuwa na taarifa za kutosha kuhusiana na wawekezaji hao ambao baadhi yao hawana ushirikiano nao mzuri, viongozi wa MBOMIPA kwa upande wao wamedai kuwa madai ya kukosa elimu hayana msingi wowote kwasababu viongozi wa jumuiya hiyo wanachaguliwa kutokana na sifa zilizoainishwa kikatiba.
"Nikiri kwamba sifahamu chochote kuhusiana na mgawanyiko ndani ya jumuiya yetu unachangiwa na wawekezaji kutokana na mitazamo yao, lakini niseme kwamba uongozi wetu una kazi kubwa ya kufanya ya kurekebisha mambo ili kupunguza joto,” alisema Makamu Mwenyekiti wa MBOMIPA, Mashahuri Msavi nakuongeza kwamba uchaguzi ujao wa jumuiya hiyo utakaofanyika mwaka 2011 utakuwa wa ushindani mkubwa.
Hata hivyo alikanusha madai ya wawekezaji hao kwamba viongozi wa MBOMIPA hawajui sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza sekta ya wanyamapori na utalii.
”Niseme kwamba shida haiko kwa viongozi, shida kubwa iko kwa wananchi wa kawaida na kwa taarifa yenu ni kwamba tumeomba fedha zaidi ya Shilingi milioni kumi kutoka WWF ili zisaidie kutoa elimu kuhusiana na sekta hiyo,” alisema na kuongeza MBOMIPA ni wakulima zaidi si wataalamu na sisi tunahitaji wataalamu ambao watafanya kazi kitaalamu kadiri ya utaratibu wa hifadhi na tunatambua kuwa wanatakiwa kupatiwa elimu ili waweze kuwa wataalamu pamoja na kuboresha ufanisi wao ikiwa ni pamoja na kuimarisha vitendea kazi vyao.”
Alisema fedha hizo zikipatikana, zitaongeza kwa wananchi na kuchochea wajibu wao katika kuiendeleza sekta hiyo.
Thursday, November 19, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment