Friday, November 20, 2009
Wahisani waiweka njia panda serikali wasema ufisadi unaitafuna nchi
Date::11/19/2009Wahisani waiweka njia panda serikali wasema ufisadi unaitafuna nchi Tausi Mbowe na Leon Bahati Mwananchi MZIMU wa ufisadi umezidi kuikosesha raha serikali baada ya mabalozi wa nchi wahisani ambao wanachangia bajeti ya serikali, kuonyesha dhahiri hawana imani na hatua zinazochukuliwa na serikali katika kukabiliana na suala hilo. Kutoridhishwa kwa wahisani hao ambao huchangia asilimia 33 ya bajeti, kunaweza kuiweka pabaya nchi. Mabalozi hao wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, wameonyesha wazi kuwa hatua zinazochukuliwa na serikali ni ndogo na kwamba, wameshindwa kulishupalia suala zima la mapambano dhidi ya rushwa nchini. Hii ni mara ya tatu kwa wahisani hao kuiwekea ngumu serikali kila inapofikia mwisho wa mwaka kwa kushindwa kutekeleza mambo yanayowavutia kutoa fedha. Mwaka jana wahisani hao waligoma kutoa fedha baada ya serikali kusuasua kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi wakiwemo wa fedha za EPA mpaka zilipofunguliwa kadhaa ambazo mpaka sasa zinanguruma mahakamani. Wakizungumza kwenye mkutano wa Nchi na Taasisi Wahisani wa Bajeti ya Serikali (DPG), uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, walisema takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania imezidi kudorora katika suala zima la uwazi na mapambano ya rushwa na kushika nafasi ya 24 katika orodha inayolinganisha nchi mbalimbali duniani. Akizungumza katika mkutano huo, ambao ulihusisha nchi wahisani na taasisi za kimataifa, Mwenyekiti wa Nchi Wahisani wa Bajeti ya Serikali (DPG), Peeter Dorst alisema kuwa nchi wahisani wanaamini kuwa ni muhimu kwa serikali kuonyesha wanachukua hatua katika suala zima la rushwa zikiwemo rushwa ndogo na kubwa. Alisema hali hiyo inatokana na habari za hivi karibuni kuonyesha kuwa Tanzania imeshuka nafasi 24 katika suala zima la uwazi katika mapambano dhidi ya rushwa. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Kupambana na Rushwa Duniani (CPI) mwaka 2006, Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 101, 2007 nafasi ya 94, mwaka 2008 nafasi ya 102 na mwaka huu ilikuwa nafasi ya 126. Mwenyekiti huyo alisema kutokana na takwimu hizo ni dhahiri kuwa Tanzania imeshindwa kupunguza rushwa na badala yake inaongezeka mwaka hadi mwaka. “ Hii inatufanya tuamini kuwa mitazamo ya watu kuhusu mambo ya rushwa inaongezeka badala ya kupungua, cha muhimu hapa ni kuhakikisha wananchi wa kawaida wanastahili kuwa na haki na kupata matunda ya maliasili zao, badala ya kutumiwa na watu wachache ambazo nyingi hupotea kwa sababu ya rushwa. Alisema serikali lazima ihakikishe inaweka mkazo katika uwazi na kutoa taarifa sahihi kuhusu masuala ya rushwa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha uchunguzi madhubuti unafanywa kwa rushwa kubwa na kuchukua hatua kali kwa kuwa ndio njia pekee ya kupunguza rushwa nchini. Mwenyekiti huyo alisema lazima serikali ihakikishe inaweka uongozi bora katika masuala ya fedha, ili kusaidia katika uwazi kwa lengo la kufanikisha mipango yake ya maendeleo na kupunguza umaskini kama Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yanavyosema hususan lengo la kwanza. Lengo la kwanza la MDGs linahusu kutokomeza umaskini uliokithiri na njaa kwa kupunguza kwa asilimi 50 idadi ya watu maskini, ambao kipato chao ni chini ya dola moja kwa siku na kupunguza kwa asilimia 50 idadi ya watu wanaokumbwa na njaa. Mwenyekiti wa kundi hilo la wahisani, Dorst alisema pamoja na serikali kusimamia ukuaji wa uchumi wa asilimia saba katika kipindi cha mwaka 2001/08, imeshindwa kushusha kiwango cha umaskini kwa kasi inayotakiwa. “Inatia moyo kuona kwamba, serikali imeweza kusimamia kidete ukuaji wa uchumi wa asilimia saba katika kipindi cha 2001-2008… Pamoja na kuweza kufanikiwa katika hilo, kiwango cha umaskini kimeendelea kuwa cha juu,� alisema Dorst. Dorst alisema katika kipindi cha mwaka 2001/07 kiwango cha umaskini kilishuka kutoka asilimia 35.6 hadi 33.6, ikiwa ni sawa na kushuka kwa asilimia mbili, kiwango alichosema hakiwatii moyo wao kama wafadhili wa bajeti ya serikali. Mambo mengine hapa nchini ambayo wahisani hawaridhishwi nayo, Dorst aliyataja kuwa ni kasi kubwa ya watoto wanaoshindwa kumaliza elimu ya msingi. Alitoa mfano kwamba, alipotembelea sekondari moja iliyopo wilayani Mpwapwa, aliwaona wanafunzi wengi wenye malengo mazuri kwa maisha ya baadaye kama vile kuwa madaktari, waandishi wa habari na mawaziri, hivyo aliitaka serikali isiwaangushe watoto hao pamoja na wengine nchini. Naye Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alionyesha kutofautiana nao akisema serikali imefanya juhudi kubwa sana na kwamba, lawama wanazotupiwa ziko zaidi kihisia. “Hapa lazima niwe mkweli na muwazi, hawa wenzetu wanotusaidia katika pato letu hawatuamini sisi kama serikali, kuna hisia suala la rushwa hatulishupalii ipasavyo,� alisema Waziri Mkulo. Waziri Mkulo alisema tofauti na hisia hizo za wahisani, serikali imekuwa ikipambana ipasavyo dhidi ya vitendo vya rushwa. Alisema hatua kadhaa zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa kadhaa wa ufisadi, wakiwemo waliobainika kuhusika katika kashfa ya uchotaji wa mabilioni ya fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na rushwa nyingine. “Serikali ilitoa ahadi ya kushughulikiwa rushwa kikamilifu. Kwa mfano mwaka 2005 jumla ya kesi za rushwa 58 zililifunguliwa na kufikia mwaka huu jumla ya kesi 1578 zimeshafunguliwa. Ongezeko la zaidi ya mara tatu, sasa hawa watu wanataka tulishughulikie kwa namna gani hasa,� alisema Waziri Mkulo. Waziri Mkulo alikiri serikali kushindwa kufikia malengo ya kupunguza umaskini kama ilivyojiwekea katika mikakati yake mbalimbali kwa mfano Mpango wa Kupunguza Umaskini na Kukuza Uchumi (Mkukuta) kwa Tanzania Bara na Mkuza kwa upande wa Zanzibar. Mkulo alisema kasi ya kupunguza umaskini haikuwa kubwa kutokana na mambo mbalimbali kama miundombinu mibovu, kushindwa kufikia lengo katika sekta ya kilimo na nishati ya umeme. Alisema serikali ilishindwa kufikia lengo katika sekta ya kilimo kutokana na mvua ya kutosha kushindwa kunyesha. Kukosekana kwa umeme wa uhakika pia kumechangia kushindwa kupunguza umaskini na matatizo mengine ya uchumi. Hata hivyo Waziri Mkulo alisema kuwa, kutokana na hali hiyo wamejaribu kuzungumza nao na kufanikiwa kuwashawishi wahisani hao na sasa wapo tayari kuongeza pesa nyingine kwa ajili ya Mkukuta na Mkuza ambao kwa sasa serikali inatayarisha awamu yake ya pili. Kuhusu matumizi mabaya ya pesa za wafadhili kwa kufanya makongamano badala ya kupeleka katika sekta husika kama kilimo, Waziri Mkulo alisema uwezekano wa kutumia fedha hizo tofauti na malengo yaliyokusudiwa ni mdogo. Alisema katika mkutano huo serikali yake imejipanga kujieleza kwa umakini kwa kutoa majibu yatakayowatosheleza wahisani hao, ili waweze kuwaelewa na kutoa fedha nyingine kama ilivyokuwa miaka mingine. Waziri Mkulo alijigamba kuwa serikali imetekeleza vizuri maeneo mengi ambayo walikubalina na wafadhili hao. Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Ramadhani Khijjah alisema mkutano huo una lengo la kujadili na kutathmini mambo yote waliokubaliana na wahisani hao. Alisema katika mkutano huo mambo mbalimbali yatazungumziwa ikiwa ni pamoja na kuangalia mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya umaskini, pato la taifa, bajeti ya nchi mazingira ya biashara pamoja na mpango wa ‘kilimo kwanza’. Watu mbalimbali waliohudhuria mkutano huo, wakiwemo wawakilishi wa nchi na taasisi wahisani, walipigwa na butwaa kuona sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kukaa mawaziri ambao karibu wote hawakufika
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment