Monday, January 18, 2010


Serikali yaambiwa: chagueni watu ama dhahabu.
· Filamu inayoonyesha ukweli migodini yasambazwa
· Wataka viongozi waliohusika wakamatwe
· Viongozi wa dini wasema heri kufa


Na Mwandishi Wetu.
UKWELI wa kile kilichofichwa kwa muda mrefu juu ya kinachotokea katika machimbo ya migodi ya dhahabu ya North Mara, wilaya ya Tarime mkoani Mara na Bulyanhulu, mkoani Shinyanga, umebainika.
Picha za miili ya watu waliokufa, wengine wakiwa wameungua, kubabuka, kujaa vidonda mwili na ukurutu, ni baadhi ya mambo ya kusikitisha yaliyomo katika filamu iliyorekodiwa na tume ya viongozi wa dini walioendesha uchunguzi katika mgodi wa North Mara na ule wa Bulyanhulu.
Wawekezaji wa kigeni wanaomiliki migodi hiyo, kwa muda mrefu wametuhumiwa kusababisha vifo vya watu na wengine kuachwa katika ulemavu wa maisha kutokana na vitendo vya kikatili, vikiwemo kutiririsha maji yenye kemikali katika mto unaotumiwa na watanzania wanaoishi katika maeneo yanayozunguka migodi hiyo.
Hali inayoonekana katika filamu hizo zilizoandaliwa na wataalamu waliotumwa na viongozi wa dini kutoka), Umoja wa Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), zimeonesha hali mbaya za watu walioathirika na maji yenye kemikali yaliyotiririka kutoka katika migodi ya North Mara inayomilikiwa na Barick kwenda katika mto Tigite, ambao maji yake yanatumiwa na wakazi wa vijiji kadhaa vinavyozunguka mgodi huo.
Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Wegita, Bw. Daniel Mwita anasema mdogo wake alifariki dunia baada ya kunywa maji ya mto huo baada ya kuvimba tumbo. Bw. Mwita anasikika katika filamu hiyo, akisema jinsi mdogo wake alivyoanza kulalamika juu ya maumivu ya tumbo na pamoja na juhudi zote walizofanya kuokoa maisha yake, mdogo wake huyo alifariki kesho yake, huku tumbo lake likiwa limevimba na ngozi ya mwili wake kugeuka rangi na kuwa nyeusi.
“Ingawa tulijaribu kutoa taarifa kwa viongozi wetu juu ya kifo hiki, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa hadi tunazika” anasema Bw. Daniel Mwita katika filamu hiyo, anapoelezea jinsi mdogo wake alivyofariki baada ya kunywa maji yam to Tigite.
Kadhalika, filamu hiyo inawaonesha Gati Mwita, wa kijiji cha Matongo ambaye mwili wake hautamaniki kwa jinsi ngozi ilivyochubuka na kuwa ngumu. Mwingine aliyeathirika vibaya ni Bibi kizee, Otaigo ambaye mwili wake umebabuka vibaya mithiri ya mtu aliyeungua moto.
Filamu hiyo ambayo dhahiri inasikitisha, licha ya kuonesha maji yenye kemikali yakitiririka kuingia katika mto Tigite, inawaonyesha Wambura Msamba mkazi wa Kijiji cha Matongo akieleza jinsi alivyopata upele mwili mzima baada ya kuoga maji ya mto huo, ambao picha zimeonesha baadhi ya viumbe wengine wa majini wakiwa wamekufa.
Jambo jingine la kusikitisha ni lile linalomwonyesha mtoto mdogo Betty Mwita, aliyeenea vidonda mwili, akilia kwa uchungu mbele ya wazazi wake. “mtoto amekuwa akilia usiku na mchana tangu aoge maji hayo. Kwa kweli ni mateso makubwa yanayotupata” anasikika akisema mama yake anayemshikilia kwa makini, huku mtoto huyo akiendelea kulia akionekana kuwa na maumivu makali.
Wakazi wa vijiji vya Wegite na matongo waliohojiwa na tume hiyo, wanataka mgodi huo uondolewe kwa sababu kama utaachwa, baada ya muda vijiji hivyo vitageuka makaburi ya watu.
“Mimba zinatoka, mifugo inakufa yote. Hawa wamekuja kuangamiza watu kwa sababu mto Tigite una sumu. Bora kuwa masikini kuliko hivi” anasema Bw. Mwita Nyamoraka katika mahojiano hayo.
Pamoja na ukweli huo, wakazi wa maeneo hayo, wanalalamika kupuuzwa kwao na viongozi wa serikali tangu ngazi ya wilaya hadi mkoa. Bw. Paulo Mhega, anasikika akilalamika; “hapa ni kifo tu, hakuna anayetusikiliza”. Mkazi mwingine wa Matongo, Esta Mungui ambaye ni mmoja wa waathirika wa maji hayo, anasema; “ hakuna anayetusikiliza wala kutusaidia”.
Naye Diwani wa Kata ya Kemambo, Bw. Agostino Sasi, maarufu kwa jina la Neto, anasikika akisikitikia hali mbaya ya watu katika Kata yake na anataka viongozi wa dini na mabalozi wan chi za nje waingilie kati kuokoa maisha ya watu wake.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Mbunge wa Tarime, Mhe. Charles Mwera ambaye anataka wale wote walioidanganya serikali na kudai kwamba maji ya mto Tigite ni safi na salama, wachukuliwe hatua za kisheria.
Jambo la kusikitisha katika filamu hiyo, ni kitendo cha maafisa wa serikali ngazi ya wilaya kutoonesha kujali kwao na hali inayotokea katika vijiji vilivyoathirika. Mmoja wa maafisa wa Wilaya ya Tarime, anasikika bila wasiwasi akisifia kampuni ya Barick kwa kazi nzuri ya kujenga shule za msingi na sekondari katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo.
Aidha, afisa huyo, anasifia pia jinsi kampuni hiyo, ilivyoweza kuilipa Halmashauri ya Wilaya kiasi cha shilingi milioni 250 kama sehemu ya mchango wao katika shughuli za maendeleo na kuongeza ajira kwa wakazi wake.
Akizungumza na KIONGOZI, mmoja wa viongozi wa dini kutoka Umoja wa Makanisa ya Kikristo Tanzania, Mchungaji John Magafu, anasema hali waliyoikuta katika vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara, iliwasikitisha mno kiasi kwamba walishindwa kujua kama wako Tanzania ama ni nchi inayotawaliwa na makaburu.
“Hawa wawekezaji ni wanyama. Inahitaji moyo wa jiwe kuwatazama wananchi ambao Mungu amewapa ardhi na madini kuwa mali yao ya asili, wakinyanyaswa na kuuawa kimya kimya ndani ya ardhi yao huku viongozi wa serikali wakiwa kimya ”anasema Mchungaji Magafu.
Mchungaji huyo aliyeshiriki kusimamia utengenezaji wa filamu hiyo, anasema maisha ya wananchi wanaozunguka mgodi huo, ni mabaya na wako hatarini kuteketea iwapo hatua za lazima na za haraka hazitachukuliwa mapema iwezekanavyo.
“Ukimya wa Serikali unatupa wasiwasi juu ya nia yao. Hakuna anayesikiliza kilio cha watu wale. Wamekuwa kama yatima na watumwa ndani ya nchi yao. Ni kama Neno la Mungu linavyosema; “tumekuwa watoto yatima tuliofiwa na nbaba urithi uko mikononi mwa wageni” anasema akinukuu kitabu cha Maombolezo 5:1-4.

….. viongozi wa dini watishiwa maisha
Wakati huo huo, watu wasiojulikana wameanza kuwatisha baadhi ya viongozi wa dini waliohusika kuchunguza tuhuma za migodi hiyo.
Akithibitisha jambo hili, Mchungaji Magafu amesema, amepokea baadhi ya simu zikimtaka aache kusambaza mikanda ya filamu inayoonesha unnyama waliotendewa wananchi wanaoishi jirani na migodi hiyo.
“Bila aibu watu hawa nao wanajaribu kututisha sisi viongozi wa dini na wanataka eti hata filamu hizi zisitolewe. Sisi katika kufanya kazi ya Mungu, hatuogopi vitisho na afadhali kufa kwa kulinda kondoo wa Mungu kuliko kuishi”
Amesema tangu awali walipata vikwazo hata walipokuwa katika ziara hiyo, lakini hawakuvitilia maananani sana. “Lakini kadri siku zinavyoongezeka, hali inabadilika. Nataka niwambie, wasijaribu kututisha. Tunajua wanaofanya hivi wanataka kuwagopesha watu ili wasiseme na wao wapate nafasi ya kuendeleza ukatili wao kwa Watanzania

Kadhalika, anasema” viongozi wa dini kwanza hawakuelewa sababu zilizowafanya baadhi ya viongozi wa Serikali kuficha ukweli wa kile kilichotokea katika mgodi huo na hata kuwatisha wale waliojaribu kueleza ukweli. Kwa hatua yao ya kutaka kututisha, sasa tumejua sababu yake wanataka kuficha uozo.
Mchungaji Magafu, amesema filamu zote mbili, ile ya Tarime na Shinyanga, zitasambazwa nchi nzima kwa watu wa kada mbalimbali ili watu wajue ukweli wote na wasikubali kudanganywa tena.
“Tunataka watu wajue kilichotokea na kinachoendelea kuwakuta watanzania wenzetu wa huko. Tunataka wajue namna baadhi ya wawekezaji wanavyokuja kuchota mali za Watanzania na kwenda kuzitumia nchini mwao”
Pamoja na kusambaza kwa filamu hizo, wameitaka serikali, kuwakamata na kuwashitaki viongozi wote waliohusika na unyama huu kama wanavyofanyiwa wahalifu wa kimataifa.
“Nabii Isaya alitabiri vema kabisa aliposema ..nchi yenu inaliwa na wageni mbele ya macho yenu, na hata kumbukumbu la Torati limesema litakuja taifa geni tusilojua ulimi wake, ambalo litachuma mali na kuteketeza mali zetu na watu wetu hadi tutakapoisha kabisa. Haya ndiyo tuliyoyaona huko Tarime na Sinyanga” anasema Mchungaji Magafu.
Anasema viongozi wa dini, wameshangazwa na ujasiri wa ajabu uliooneshwa na viongozi na wasomi waliopewa dhamana ya kulinda maisha ya watu na mali zao kwa kukosa huruma na kushirikiana na wawekezaji walio tayari kuangamiza maisha ya watu bila huruma.
“Kama wawekezaji hawa wanafikia hatua ya kumdanganya waziri, kwa kumtembeza katika maeneo mengine na kuficha kule maji yalikokuwa yanatiririka, kuna sababu gani ya kuwaamini tena wao na waliowasaidia? Anasema Mchungaji huyo akikumbushia tukio la Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Khamis Kagasheki, ambaye katika ziara ya kufuatialia tukio hilo, alioneshwa na uongozi wa Barick sehemu tofauti na kufichwa kule kulikokuwa kunatiririsha maji yenye kemikali zenye sumu hadi pale alipoelezwa ukweli na wenyeji na kujionea hali halisi.
Sakata la migodi hiyo, limevuma sana mapema mwaka jana kabla halijatulia kwa muda. KIONGOZI, lintachapisha ripoti kamili ya kamati ya viongozi hao katika matoleo yake hajayo.

No comments: