Monday, February 15, 2010


Kilimo; Lulu iliyotelekezwa!

Na DK. Sabbas Mbogo
TAKWIMU za kiuchumi zinaonyesha kuwa Uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua na kuongozeka kila mwaka. Inaonekana kuwa wakati uchumi ulikuwa kwa asilimia 4.2 mwaka 1995, ukuaji huu uliongezeka na kufikia kiwango cha asilimia 7.1 mwaka jana.
Kwa takwimu hizi, kila mtu ambaye hawajawahi kufika Tanzania na kuzuru sehemu kubwa ya nchi yetu, ataamini kwamba maisha ya wananchi ni ya kuridhisha kwa kiwango kikubwa. Ukweli ni kwamba, mambo yako kinyume kabisa. Asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi katika umasikini wa kutupwa!
Watanzania wengi wanaoishi vijijini hali zao ni za kusikitisha. Takwimu hizo hizo za kiuchumi zinabainisha kwamba, asilimia 34 ya watanzania waishio vijini, wana kipato cha wastani wa dola moja (sawa na shilingi 1,100/=) tu kwa siku, huku asilimia nyingine 17 ya wananchi hao, wakiishi chini ya kiwango hicho!
Inakadiriwa kuwa Watanzania milioni 13 wanaishi chini ya kiwango cha umasikini wa mahitaji muhimu. Hii ina maanisha kuwa idadi ya umasikini kwa Watanzania katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, imeongezeka kwa sababu, mwaka 2000, watu waliokuwa wakiishi chini ya kiwango cha umasikini na kukosa mahitaji muhimu walikuwa milioni 11.
Pengine sasa la kujiuliza kwa msomaji wa makala hii, ni inakuwaje uchumi ukue wakati hali ya umasikini kwa Watanzania ikiongezeka? Ukweli ni kwamba, uchumi umekuwa katika zile sekta chache za uzalishaji ikiwemo madini, ujenzi na pengine utalii. Mathalani, imeonesha kuwa sekta za ujenzi na viwanda iliongezeka kwa asilimia 10 kati ya mwaka 2003 na 2007.
Sekta za ujenzi na viwanda kamwe haziwezi kuleta maisha bora kwa Mtanzania, ikizingatiwa kwamba zinahusisha kundi dogo la watu. Mtu mmoja anaweza kuwa na viwanda hadi vitano, na hata kama vitatoa ajira kwa Watanzania wengi, bado faida kubwa itakwenda kwa mhusika na familia yake. Kuajiri idadi kubwa ya watu hakuwezi kuondoa umasikini kwa sababu uzoefu unaonesha kuwa mishahara inayotolewa na wamiliki we na matajiri wengi ni ile wa “Mkono kinywaji”, yaani wa kukidhi mahitaji ya chakula tu na kodi ya chumba.
Ubaya mwingine ni kwamba, sekta za viwanda na ujenzi zinachangia kidogo mno kukua kwa sekta nyingine zinazochukua kundi kubwa la wananchi. Kibaya zaidi, baadhi ya watu wanaotegemewa kusimamia kikamilifu hata kile kidogo kinachotolewa na sekta hizi, hutumia vibaya mapato yake kwa manufaa yao na familia zao.
Kumbe, umasikini umekuwa mkubwa kwa sababu sekta zinazohusisha Watanzania wengi zimetelekezwa ama kupewa kisogo kabisa na wahusika wakuu ambao walitarajiwa kuzisimamia. Sekta zilizotupwa na ambazo zingeweza kuinua maisha ya Watanzania wengi ni pamoja na Kilimo.
Utafiti umeonesha kuwa Tanzania ina ardhi yenye rutuba safi kuliko nchi nyingi duniani na ambayo haijatumiwa kabisa tangu kuumbwa kwa dunia.
Sekta ya kilimo ambayo ndio tegemeo kubwa la watanzania zauidi ya asilimia 80 imetupwa kapuni, kelele za kilimo uti wa mgongo na kilimo kwanza, zinaonekana kuwa za kisiasa zaidi kuliko uhalisia. Watu wale wale walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wakapewa mamlaka ya kutunza dunia na kuitiisha, wamegeuka kuwa wapiga porojo tu, huku wasiumizwe kamwe na uduni wa maisha ya watu.
Kilimo kimekuwa lulu ya mafanikio kwa nchi nyingi za mashariki ya mbali. Kwetu Tanzania, lulu hii imetelekezwa na kutupwa, na badala yake watu wazima wameaminishwa kwamba ili uibuke na maisha mazuri, lazima uwe mfanyabiashara! Ajabu yenyewe ni ile biashara ya uchuuzi wa vitu vidogo vidogo, kama pipi, maji ya kunywa, mitumba nakadhalika.
Hapa pengine nitoe mfano mdogo tu wa zao moja ambalo limeinua uchumi wa nchi nyingine, wakati sisi tumelipa kisogo -Kilimo cha Mpunga!
Hakuna asiyelijua Bonde la Mto Rufiji. Kwa wale tuliokuwa na akili timamu miaka ile ya mwanzoni mwa 70, tunakumbuka utafiti wa mtaalamu mmoja wa klilimo, aliyoufanya katika Bonde la Mto Rufiji na kubaini kwamba, lina rutuba nzuri mno kwa kilimo cha mpunga. Mtaalamu huyo ambaye sina haja ya kumtaja (sitaki kumkumbusha machungu), alibaini kwamba, Tanzania inaweza kujitosheleza kwa mchele, na hata kusafirisha nje ya nchi.
Utafiti huo ulibainisha kwamba, mchele ambao ungezalishwa baada ya kulima nusu tu ya bonde hilo, ungeweza kulisha bara zima la Afrika kwa mwaka mzima bila shida yoyote. Kwa lugha nyingine, Tanzania ingekuwa nchi inayoongoza Afrika nzima kwa uzalishaji wa zao hilo ambalo ni wazi lingeleta manufaa kwa wakulima wote wa ukanda huo wa Pwani.
Tofauti na Tanzania, nchi za wenzetu ambazo kwa bahati mbaya zaidi hazikujaliwa kuwa na ardhi kubwa na nzuri kama yetu, zimefanikiwa sana kukuza uchumi wao kutokana na kilimo.
Hapa nitaje nchi moja tu ya Thailand. Nchi hii, ndio inayoongoza duniani kwa kusafirisha mchele nje ya mipaka yao. Fikiria kwamba mchele wao umeanza kuwa maarufu hapa nchini tangu miaka ya themanini. Watu wamekula mchele wa kitumbo na aina nyingine kutoka Thailand, wakati sisi wenyewe tungeweza kuwalisha wao.
Inaaminika kwamba mchele wa Thailand ndio unaoongoza kwa bei katika soko la dunia! Kuna habari za kuaminika kwamba uchumi wa Thailand umekuwa kwa kasi kutokana na kilimo.
Wenzetu hawa, waliamua kwa dhati kabisa kukuza uchumi wao kwa kuwekeza kwa vitendo (sio kwa maneno kama yetu) katika sekta hii ambayo ndio inayobeba umati mkubwa wa watu.
Watawala wa nchi hiyo kwa nguvu na nia moja, waliamua kuwekeza kwa kuimarisha miundo mbinu, ikiwemo barabara zinazoweza kupitika kwa wakati wote na umeme. Waliondoa kila aina ya vikwazo vinavyoweza kuzorotesha sekta hii.
Walitumia uhamasishaji na ushirikishwa kwa serikali kuu, vikundi vya wananchi na wafanyabiashara, kwa maana ya masoko ili kuweka nguvu za pamoja kuimarisha sekta ya kilimo.
Haishangazi kusikia kwamba asilimia 97 ya watu vijijini wana umeme, wakati Tanzania hata huo wa mijini tu, ni mbinde! Hapa nchini, ni asilimia 2.5 ya wakazi wa vijijini wana umeme!
Idadi ya matumizi ya zana bora za kilimo yaliongezeka mno tangu mwaka 1960. Takwimu za kilimo zinabainisha kwamba, wakati nchi ya Thailand ilikuwa sawa na Tanzania katika sekta ya kilimo, leo hii, wenzetu hao wamefika mbali mno wakati sisi tunaendelea kusuasua.
Wakati wakulima wa nchi hiyo, wameongeza matumizi, mathalani ya matrekta kutoka matano, mwaka 1961 hadi 261 mwaka 2005, kwa Tanzania yameshuka kutoka matrekita 32 mwaka 1961 hadi kufikia 23 mwaka 2005!
Tukija katika matumizi ya mboleo, wakati Thailand yalipanda kutoka kilo 1.7 kwa hekta moja mwaka 1961 wakati tunapata uhuru hadi kufikia kilo 120.7, mwaka 2005, hapa Tanzania, yaliongezeka kutoka kilo 0.5 (yaani nusu kilo) kwa hekta mwaka 1961 hadi kufikia kilo 5.8 kwa hekta mwaka 2005.
Haishangazi basi kuona kwamba, nchi hizi mbili zilizokuwa zinalingana kiuchumi mwaka 1961, leo hii kwa kuinua sekta ya kilimo, kipato cha mwananchi wa Tanzania kinalingana na kipato cha mwananchi wa Thailand aliyeishi mwaka 1963!
Ingefaa sasa, wasimamizi wa majukumu ya maendeleo ya watu, kwa maana ya Serikali kuu, hususan wizara ya Kilimo na Umwagiliaji, ikajitazama upya. Wahusika wa wizara hii, wajiuliza, kwanini wapo. Na wapo kwa manufaa ya nani? Kwa nini Mungu kawachagua washike nafasi walizo nazo. Ni kwa sababu hakuna Watanzania wengine wenye weledi na utaalamu kuzidi wao. Wapo kwa sababu Mungu amewachagua ili watende mambo ya kuleta maendeleo ya watu?
Bado naamini kwamba, kama wahusika wataamua leo kutupilia mbali matakwa yao na kutimiza kile ambacho Mungu amewakabidhi, wakazama zaidi kuangalia maendeleo ya watu wao huko vijijini, Tanzania yenye kunuka umaskini itabaki kuwa simulizi katika historia ya nchi hii. Badala yake, itainuka historia yenye kujaa majina ya watu waliosimama imara kupambana na adui umaskini na hatimaye kuwezesha Watanzania kuishi maisha yenye neema tele!

No comments: