Muswada gharama za uchaguzi ‘unakusanya usipotawanya’
Na Joseph Sabinus
MUSWADA wa Sheria wa Gharama za Uchaguzi kama ninavyoulewa ndivyo hasa ulivyo, ni kituko ambacho kinanichekesha hata kunifanya nione aibu kutamka kwani sijui unataka nini. Kama ninavyouelewa ndivyo ulivyo, ni aibu lakini kama sivyo, msinishangae maana aulizae, anataka kujua.
Kama ninavyouelewa muswada huo, kifungu chake cha 12 (1) na (3) kinazuia mtu, asasi, shirika au kampuni kuingiza nchini fedha toka nje na ndani ya siku 90 kabla ya Uchaguzi Mkuu au ndani ya siku 30 kabla ya Uchaguzi Mdogo.
Sijui na nazidi kusema sijui kama kweli wadau wote wanauelewa na wanajua wazi kuwa muswada huu unalinda maslahi ya taifa, au unalinda maslahi ya wateule wachache wanaotaka kuogolea juu ya asali na maziwa, huku wengine wakitembea juu ya misumari ya moto milele na milele.
Nijuavyo mimi, ingawa yamefanyika mabadiliko kadhaa yanayoweza kumithilishwa na viraka juu ya kaniki, ni wazi muswada haujaeleweka kwa Watanzania na wala hawajapata fursa ya kuujadili na kutoa mapendekezo yao. Hii ni kupora haki yao ya Utanzania.
Ninajua dhahiri kuwa wabunge wanafanya kwa niaba ya wananchi wao lakini, katika mambo nyeti kama hilo, wabunge si tu watu wa kuamua kufanya walitakalo, bali lile wanalotumwa na waliowaweka madarakani.
Ni kwa msingi huo, maslahi ya taifa yangetangulizwa, muswada huu ungepewa muda wa kutosha wananchi waupitie, waujadili na waamue kuwatuma wabunge cha kwenda kusema juu yake huko bungeni, lakini hili halikuonekana na kama lilifanyika, basi limefanyika kwa “kubip” ili kudanganya toto.
Ni wazi lengo la muswada huu ni kutaka kuona kunakuwapo udhibiti wa fedha chafu zinazoweza kutumika katika chaguzi. Hili sina ugomvi nalo, lakini Serikali itambue nafasi kubwa iliyo nayo katika kuufanya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010 uwe wa kidemokrasia zaidi kuliko ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita.
Kimantiki, naona wazi kabisa huu haukuwa mwaka au kipindi mwafaka kwa Watanzania kujadili muswada huu labda, kama kuna njama ya kuviumiza baadhi ya vyama, na kuutumia kuvibeba baadhi ya vyama au chama fulani hususan chama tawala chenye wabunge wengi.
Kwangu mimi, kung’ang’ania kujadili muswada huu sasa, ni kujaribu kutunga sheria kwa ajili ya tukio lijalo la uchaguzi, au kwa ajili ya kikundi au mtu fulani na hii ni hatari kwa nchi inayojinadi kuwa ni ya kidemokrasia kama Tanzania.
Hata hivyo, wabunge wameupitisha kwa madai kuwa ni hatua ya kupiga marufuku matumizi makubwa ya fedha katika uchaguzi. Kwa madai yake, muswada ulitaka fedha haramu, misaada, michango na ufadhili wenye shaka vipigwe marufuku.
Kwa mantiki hiyo, wagombea sasa watatakiwa waeleze vyanzo vyao vya fedha ili kuepusha nchi kuongozwa na watu waliowekwa madarakani kwa nguvu za fedha za ndani au kutoka nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu na Bunge, Philip Marmo, matumizi makubwa ya fedha zikiwamo zinazopatikana kwa njia isiyo halali, yanadhibitiwa kuanzia Uchaguzi Mkuu ujao mwaka huu.
Pamoja na madoido mengi ya malengo ya muswada huo uliopitishwa, ni wazi kuwa ulilenga kuwadhibiti na kuwabana wagombea wa vyama vya upinzani ambao wengi vyama vyao havina ruzuku na kwa mfumo huo, ni wazi huo unakuwa mtego wa kuwaminya wapinzani pale watakapoonekana kukitikisa chama tawala katika kinyang’anyiro.
Iweje mtu usiyempa pesa, utake kujua matumizi yake? Huu ni ubabe dhidi ya demokrasia unaopakwa mafuta ili ung’ae na kuonekana machoni kuwa ni mzuri. Kama kweli Serikali kupitia chama tawala imenuia kudhibiti hali hiyo, basi itoe ruzuku sawa kwa wagombea wote wa vyama kisha, ione nani atakiuka kinyume chake, tunajaribu kubaka demokrasia kwa kupulizia manukato yasiyoua mbu.
Nalazimika kukumbuka namna Sheria ya Uchaguzi nchini isivyokidhi mahitaji ya mfumo wa vyama vingi. Katiba pia, ni ugonjwa unaozua magonjwa mengi ya kidemkrasia nchini.
Nchi inatawaliwa na mfumo wa chama dola. Kwamba chama tawala kinakuwa na mamlaka kupindukia. Watu wanajilimbikizia vyeo na madaraka kiasi cha kuiminya demokrasia ya vyama vingi isipate kupua.
Iweje Rais wa nchi, huyo huyo awe mwenyekiti wa chama kitaifa? Katiba yetu imetoboka. Iweje Rais anapozunguka kufanya kazi za chama chake, aongozane na wakuu wa mikoa na wilaya wakitumia rasilimali kama magari ya serikali badala ya chama achilia mbali kuwa wanawakosea haki Watanzania ambao sio wanachama wa chama hicho wanaohitaji huduma zao kama viongozi wa serikali kwa wakati huo.
Kwa mahitajhi ya sasa, ni vyema Watanzania tukiri na kuchukua hatua za marekebisho ya katiba ya nchi kwani sasa ni wazi imetoboka na inavuja; asali na maziwa vyote vinadodondka inabaki barafu katika karatasi la nailoni.
Nirudi kwenye muswada wa sasa ulio mezani, kwamba unataka mtu, taasisi au chama kutoa hesabu za gharama za uchaguzi! Hivi vyama vyote vya siasa hususan vinavyoshiriki uchaguzi vinapewa ruzuku? Kama vinapewa ruzuku, ni haki na wajibu serikali kuwa na nguvu za kisheria za kujua ruzuku hiyo imetumikaje, lakini nijuavyo, vyama vingi vya upinzani, havina ruzuku.
Vinatembeza bakuri kwa wanachama na pengine wahisani kama ilivyo serikali ili kujiendesha. Sasa, inapofikia hatua kukawa na mkakati wa kudhibiti mapato wakati wa uchaguzi, unakuwa ni ujanja wa watu wachache, kuvibana vyama vya upinzani ili vishindwe kushiriki kikamilifu katika uchaguzi na hiyo, itoe ushindi wa bure kwa baadhi ya vyama.
Serikali ijue dhahiri kuwa, kama haitoi ruzuku au gharama za uchaguzi kwa vyama vyote, haina haki kutaka kujua matumizi ya vyama hivyo, huo ni ukatili wa kidemkrasia. Ndiyo maana ninasema, hoja hiyo ingekuwa na maana endapo, kila mgombea anayepitishwa na chama, atapewa ruzuku toka serikalini vingivevyo, hapana. Hii ni janja ya nyani. Ni ukandamizaji na ubabe dhidi ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa.
Tunajua suala hili limekwenda bungeni, limejadiliwa na kupitishwa, lakini ikumbukwe kuwa Chama Tawala (CCM) kina wabunge wengi zaidi hivyo, kwa mfumo wa kulindana, ipo hatari ya wazi hata lisilo na maslahi kwa taifa, linapitishwa ili mradi limeletwa na chama chao.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kipo madarakani kinapata takriban shilingi bilioni 24 kama ruzuku na kwa maana hivyo, kwa miaka mitanio, ni taktiban bilioni 124.
Hicho, kinaweza kuunga mkono juhudi za makusudi kudhibiti hicho kinachoitwa fedha chafu za uchaguzi ili kibaki chenyewe dhidi ya akina NCCR-Mageuzi, akina TLP na vingine visivyo na ruzuku na hata CUF kwa mfano, nacho kinaponea kwenye tundu la sindano kutokana na nguvu yake visiwani Zanzibar.
“Hivi mtu kama huyu CCM, unataka umwambie aende katika uchaguzi na mtu ambaye humpi na hana hata senti moja?”, anahoji kwa mshangao na kuongeza, “Katika mazingira hayo, unaendaje kwenye ushindani wa haki kupambana na chama dola!”
Mbatia anasema katika mazungumzo na waandishi wa habari katikati ya juma kuwa, endapo muswada huo wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi utapitishwa bila kufanyiwa marekebisho yenye maslahi ya taifa, chama chake kitatinga mahakamani kuzuia usianze kutumika.
Kwa busara za kawaida tu, ni wazi muswada huo kwa jinsi ulivyo ukipitishwa bila marekebisho makini na ya dhati na kuwa sheria, utavikandamiza vyama vya upinzani na utakuwa unaifanyia ubabe demokrasia nchini.
Mbatia kuhusu Katiba anasema, “Tatizo la Tanzania ni Katiba. Katiba hii iliundwa na kikundi cha wachache ndiyo maana hata inatoa mianya ya ufisadi.”
Kiongozi huyo na baadhi ya wengine wa upinzani, mara kadhaa wamekuwa wakiasa kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba ili kupata Katiba inayolinda maslahi ya watu, taaasisi, vikundi na vyama vyote kwa faida ya taifa.
“Kwanini tusikubali kuandaa Katiba kwa maslahi ya wote, hadi tusubiri tutembee juu ya maiti kama ndugu zetu wa Kenya walivyofanya baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007. Mimi nimuombe Rais Kikwete kwa nia njema, aruhusu Watanzania wazungumzie hatima ya taifa lao na bahati nzuri, hatujafikia hatua ya kutoana ngeo wala kutosalimiana. Tusiombe wala kusubiri kufika huko,” anasema Mbatia.
Ni kwa msingi huo, anasema kisiwepo kikundi cha wateule wachache wanaojitengenezea mazingira ya kumiliki utawala wa nchi na rasilimali za umma sambamba na suala la elimu bora kwa wachache, ili hao hao, baadaye waje kuchukua madaraka.
Anasema, “Hata mfumo wa elimu uliopo hapa nchini, unajenga tabia ya walio nacho waendelee kuneemeka, na wasio nacho waendelee kuumia… pamoja na hayo, Watanzania bado wanafungwa midomo maana mtu anaposema uozo aliouona, anaambiwa ametumwa na nani. Uhuru wa habari na mawazo uko wapi?”
Mwenyekiti huyo wa NCCR-Mageuzi anasema, katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, anajua yapo mengi yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne, lakini pia, mengine yamekuwa ni simulizi za vitabuni na majukwaani, bila utendaji wala nia ya dhati.
“Mfano, wakati anazindua Bunge, rais Kikwete alisema atatengeneza mazingira bora ya zaidi ya kisiasa, lakini mara ngapi Rais Kikwete amekaa na wapinzani kujadili hatima ya taifa lao kama Watanzania na matokeo yake, miaka mitano inakwisha kwa agenda ya ufisadi.”
Anasema na kuongeza kuwa, ili kuliweka taifa katika hali nzuri zaidi, ni bora iundwe tume ya maridhiano ili “wachafu waende watubu” na kuonesha namna wanavyojirudi. Tuzaliwe upya na Tanzania iwe mahali pema pa kuishi.
Monday, February 15, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment