Monday, February 15, 2010

Mwanzo wa Mwaka na mbwembwe zake!!!!!!

Na Lilian Timbuka
Kama Januari ikichukuliwa kama sampuli ya hali ya mambo itakavyokuwa kwa miezi mingine 11 iliyobaki, basi kuna kila sababu ya kusadiki kwamba mwaka huu utakuwa na changamoto nyingi na ngumu kuliko kawaida.
Januari imekatika huku matukio ya ujambazi yakiwa yametikisa nchi kwa kiwango kikubwa, tukio la mauaji ya raia 14 kisiwani Ukerewe likiwa ndilo limeshikilia rekodi ya juu kabisa pengine kwa miongo kadhaa iliyopita kuwahi kutokea nchini.
Yamekuwapo pia matukio mengine mengi ya ujambazi, lakini kibaya zaidi ni kule kuhusishwa kwa baadhi ya askari polisi na tuhuma za ujambazi.
Kwa kifupi wapo polisi waliotajwa kuhusika katika matukio ya ukiukaji wa maadili ya kazi yao mkoani Mara, Mwanza, Arusha na Rukwa katika kipindi cha Januari pekee. Wapo waliotajwa kushirikiana na majambazi kuwapora na pengine kuwaua raia, wapo waliotajwa kukodisha silaha kwenda kufanyiwa uhalifu, lakini wapo walioamua kuwa vibaka na kukwapua fedha za raia kwenye ATM.
Hatuwezi kusema kwamba askari hawa wachache ndio jeshi zima la Polisi limeoza, ila tunapochukulia hawa kama sampuli, basi hofu inajaa miongoni mwa wananchi. Kwani kama kipindi cha mwezi mmoja tu mikoa zaidi ya minne askari polisi wamehusika katika uhalifu, ni hatari kubwa.
Mwezi uliopita wahariri walipata bahati ya kukutana na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, katika kile alichojaribu kuwasilisha ‘kutafuta ubia wa dhati kati ya wahariri na polisi’.
Kwa IGP huu ni mkakati wa Jeshi la Polisi kukuza ulinzi shirikishi, ili kukabiliana zaidi na uhalifu nchini. Ulinzi shirikishi si dhana ngeni, ila ni msisitizo kwa sasa unaelekezwa huko kwa kuwa changamoto za uhalifu nazo zimekuwa nyingi.
Katika mkutano huo, IGP Mwema alipokea baadhi ya maswali kutoka kwa wahariri, mengine yalikuwa mepesi lakini mengi yalikuwa mazito na magumu.
Kwa ujumla wake, yalilenga kumpa ujumbe mmoja tu kwamba kuna urafiki wa mashaka kati ya askari polisi na raia. Mwema alielezwa inakuwaje polisi aliyebeba bunduki, kavalia sare za jeshi, anayelipwa mshahara kwa kodi za wananchi, lakini anadiriki kufyatua risasi kumuua raia asiyekuwa hata na rungu.
Mwema alielezwa kwamba zaidi ya mwaka mmoja sasa umma unasubiri kusikia hatua zilizochukuliwa na jeshi hilo dhidi ya askari polisi wake walioua raia (cold blood) Tunduma, Kyela, Arusha, Dar es Salaam Kimara Temboni na Ilala Shariff Shamba.
IGP alielezwa kwamba kwa taarifa zilizopo askari walioua raia kwa sababu tu wana bunduki waliopewa kuwalinda raia hao, bado wapo kazini wanaendelea na kazi kana kwamba hakuna cha ajabu kilichotokea.
Alielezwa pia kwa ujumla askari polisi wake wamegeuza raia migodi midogo midogo. Hakuna asiyejua kuwa kuingia kituo cha polisi ni bure, lakini kutoka ni lazima mkono uzame mfukoni. IGP Mwema alikumbushwa kwamba askari wake ni mabingwa wa kuwabambika kesi raia kwa sababu za kipuuzi kabisa.
Nikiri tu kuwa nafasi hii haitoshi kuorodhesha vielelezo vinavyothibitisha pasi na shaka yoyote kwamba maadili katika jeshi hili yameporomoka mno. Ni kwa jinsi hiyo sauti za kumtaka aanze upya ilipazwa kwenye mkutano huo kwa sababu ilivyo imani ya wananchi kwa chombo hiki ambacho dhima yake kuu ni kulinda maisha na mali zao, imeporomoka mno.
Nikiri tu hapa kwamba IGP Mwema tangu achukue usukani wa Jeshi la Polisi amefanya kazi kubwa walau kurejesha nidhamu kwa kiwango fulani, lakini nisiwe mnafiki niseme wazi kwamba kazi ya Mwema ni ngumu zaidi kuliko inavyoweza kuelezwa kwa sababu amerithi matatizo sugu ya kushuka kwa uadilifu na weledi katika jeshi hilo.
Kuna askari polisi walizoezwa kusema uongo, na hadi leo wangali wanasema uongo, ripoti zao za uhalifu wanazowasilisha kwa wakubwa nyingi ni za kutengeneza.
Umma unakumbuka vilivyo jinsi aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe, alivyojitahidi kuusadikisha umma kwamba wafanyabiashara wa madini waliokuwa wameporwa fedha zao na polisi na kisha kuuawa walikuwa ni majambazi. Umma unaelewa ukweli wa jambo hili. Huyo alikuwa kiongozi wa ngazi ya Kamanda wa Polisi Mkoa!
Wiki iliyopita Polisi mkoa wa Dar es Salaam wameibuka na sakata la Jerry Muro, mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC). Muro anadaiwa eti ametishia kwa silaha ili apewe rushwa ya Sh. milioni 10 kwa kujifanya ofisa wa Takukuru. Lakini cha kushangaza hatuhumiwi kwa unyang’anyi wa kutumia silaha!
Habari za kukamatwa kwa Muro zilisambaa vyumba vya habari kama moto wa nyika, na waliokuwa wanasambaza kwa kasi kubwa ni askari polisi waliokuwa wanasema kwamba kigogo mmoja ametiwa mbaroni, kulikuwa na kila juhudi za kutaka kumshikisha adabu Muro.
Niseme tu kwamba Muro hadi sasa ni mtuhumiwa tu hakuna chombo chochote cha kisheria ambacho kimekwisha kumtia hatiani, yote yanayosemwa dhidi yake ni tuhuma tu tena zenye utata wa hali ya juu.
Lakini kwa akili ya kawaida, Muro ambaye utendaji kazi wake umesababishia zaidi ya askari wa usalama barabarani 40 matatizo kutokana na kukamatwa wakipokea ‘kitu kidogo’ kutoka kwa madereva, hawezi kuepuka kutegwa na kusakwa ili aangamizwe na polisi hao hao.
Ukitafakari kwa kina jinsi habari za Muro zilivyoenezwa, kwamba alikuwa anataka kupewa rushwa, kwamba alitumia silaha yake kumtishia mtu, kwamba amekuwa akimwandama mhusika ili ampe rushwa; lakini hakuna juhudi yoyote ya kitaalam (kiweledi) kwa polisi kufanikisha ukamatwaji wa Muro akiwa anapewa fedha hizo; basi yanayobaki ni maswali zaidi kuliko majibu.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, amesema kwamba wana ushahidi kamili juu ya kuhusika kwa Muro katika tukio la kuomba rushwa ya Sh. milioni 10, tunaamini kwamba ushahidi huo utapelekwa mbele ya vyombo vya sheria ili Muro apate nafasi ya kujitetea.
Lakini wakati tukisubiri Muro, mwandishi aliyeshinda tuzo ya mwaka jana ya mwandishi bora Tanzania, afikishwe mahakamani, hebu Kova atueleze ni weledi wa wapi wa polisi wa ngazi yake kuchukua silaha ya mtu anayomiliki kihalali na kuianika hadharani? Anataka kuwasilisha kwa watu nini, kwani umiliki wa silaha si jambo binafsi ndiyo maana mtu haruhusiwi kuionyesha ovyo hadharani kadri mtu atakavyo?
Nguvu hizi nyingi kiasi hiki anazotumia Kova kusisitiza uhalifu wa Muro za nini? Na kwa nini sasa?
Wapo watakaojitokeza kusema kwamba tunampigia debe Muro kwa sababu ni mwandishi wa habari mwenzetu, lakini ni vema wakosoaji wa namna hiyo wakajua wazi kwamba kwa miaka mingi sana, polisi wamejijengea ngome kongwe ya kusukia raia kesi, mara nyingi kwa nia ya kumkomoa kama si kumnyamazisha mtu.
Itoshe tu kusema weledi wa polisi umetiliwa shaka siku nyingi, imani ya watu wengi juu ya uadilifu wa askari wengi imeshuka mno. Kwa mtazamo wa wengi polisi wanaweza kuwa wanasumbuliwa na kile kinachoitwa ‘kikulacho ki nguoni mwako’ ni kwa jinsi hii mtu anapoitafakari Januari na mwenendo wa mambo ndani ya Jeshi la Polisi na akipima hali hiyo na matarajio ya IGP Mwema kwamba huu ni mwaka wa mabadiliko kwa jeshi hilo, hakika kinachorajiwa ni miujiza tu kama watu wenyewe watabakia kuwa walewale

No comments: