RPSP ilivyojipanga kulinda maadili ya manunuzi
Na Lilian Timbuka
PAMOJA na Sheria za Manunuzi ya Mali za Umma kuwekwa wazi, bado taasisi nyingi hazifuati kanuni za maadili katika kufanya manunuzi hayo.
Hii ni kutokana na ama taasisi nyingi zikiwemo za umma na zile za binafsi, kutotambua kanuni hizo za maadili au kuzipuuzia kanuni hizo.
Hali hii isipodhibitiwa ipasavyo, itaendelea kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa, huku jasho la walipa kodi hususan wale wa kipato cha chini, likiendelea kushereheshwa na wimbo wa ‘’hali ya maisha ni ngumu, afadhali ya jana kuliko leo...’’ ukiendelea kusikika kila kukicha.
Hata hivyo, Bodi ya Wanataaluma na Wataalam wa Manunuzi (RPSPT), imeliona hilo na hivyo kuamua kulivalia njuga ili kuhakikisha sheria hizi za manunu zinazingatiwa.
Msajili wa Bodi hiyo, Bw. Clemence Tesha, anakiri kutozingatiwa kwa kanuni za manunuzi na katika kukabiliana na hali hii, Bodi imeunda Sekretarieti ya Maadili, ambayo kazi yake ni kufuatilia na kuhakikisha kanuni na maadili ya manunuzi vinafanyiwa kazi kadiri inavyotakiwa.
Bw. Tesha alipata nafasi ya kuyazungumzia hayo katika Warsha iliyoandaliwa na Bodi ya Wanataaluma na Wataalamu wa Manunuzi (RPSPT), katika Hotel ya Blue Peal Jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Warsha hiyo iliwashirikisha Wataalamu wa Manunuzi walioko katika ajira na wale walioko vyuoni kwa sasa.
Bw. Paul Bilabaya anasema zaidi ya washiriki 500 walihudhuria warsha hiyo kutoka katika Vyuo Vikuu vya Mzumbe, Chuo Kikuu cha Mlimani, IPS Chanika, CBE Dar es Salaam na TAAA.
Washiriki hao kutoka vyuoni ni wale ambao wanatarajia kufanya mitihani yao mwaka huu.
Sanjali na hili, kwa mujibu wa Bw. Tesha, kwa sasa RPSP kwa kushirikiana na Sekretarieti hiyo ya maadili, inaendelea na utekelezaji mkubwa wa mradi wa kuhakikisha manunuzi yote yanaendana na fedha iliyotengwa kwa shughuli husika , huku manunuzi hayo yakifuata sera na taratibu za kisheria katika kulinda maadili.
“Mradi huu pia unaangalia taaluma ya manununuzi kama chombo cha kulinda na kuinua maadili katika jamii,”’ anasema.
Mradi huo ujulikanao kama FEAT ulionzinduliwa mwishoni mwa mwaka jana, unatarajia kutumia kiasi cha Shilingi Milioni 295 na kwamba, katika kuhakikisha elimu ya manunuzi inaeleweka vilivyo kwa taasisi mbalimbali, RPSPT inatarajia kuendesha semina mbalimbali katika kanda zote nchini ambapo watakutana na kuzungumza na wanataaluma wa manunuzi na usambazaji iwe ni kwa taasisi za serikali ama za binafsi.
“Tunajua kwamba kwa sasa maadili katika manunuzi ya mali za umma yamepewa kisogo, lakini sisi kama bodi haitatukatisha tamaa, tutazidi kushikamana katika kuhakikisha maadili yanazingatiwa ndani ya jamii,” anasema Bw. Tesha.
Ni kutokana na kutozingatiwa kwa kanuzi za maadili za manunuzi, taasisi mbalimbali nchini zikiwemo za serikali iwe ni serikali kuu ama Serikali za Mitaa kupitia Halmashauri mbalimbali, na hata mashirika binafsi, vimekuwa vikifuja fedha za umma kwa kulipa malipo hewa ama kulipa fedha nyingi zaidi kulinganishwa na manunuzi halisi.
Uzingatiaji wa kanuni ni nguzo muhimu katika kufanya manunuzi ya umma, kwani inaleta uwiano halisi wa thamani ya fedha (value of money) pale pesa inapoendana na uhalisi wa kitu kilichonunuliwa iwe katika ubora, ukubwa na hata uimara kwa bidhaa ma huduma husika.
Hii pamoja na mambo mengine, inahitaji uwazi katika ushindani, uwajibikaji na hata usawa.
Izingatiwe kuwa, masuala yote ya kiofisi ya ununuzi na usambazaji wa mali za umma, lazima yazingatie uadilifu na uaminifu na kuzingatia mazingira halisi ya usawa katika usambazji.
Zifuatazo ni kanuni za maadili ambazo hazinabudi kuzingatiwa katika masuala ya manunuzi ya umma:-
Uwazi, uaminifu na kujenga ushirikiano wa kibiashara kwa wafanyakazi na wasambazaji, utunzaji wa siri kwa masuala yote ya kiserikali na taarifa za kibiashara, kuepuka migogoro na kutojenga ubaguzi, kuhakikisha migogoro ya kibiashara inafikishwa kwa wakuu wa taasisi husika pale inapojitokeza na hatimaye uongozi kuchukua hatua haraka kuitatua.
Mengine ni uaminifu katika kupima utekelezaji wa zabuni, kuhamashisha utaalum wa hali ya juu katika masuala ya manunuzi pamoja na kwamba suala la upatikanaji wa faida lisipewe kipaumbele katika masuala ya utumishi wa umma.
Kulingana na Sheria za Manunuzi ya Umma (2004), Kifungu cha 72, ni marufuku kwa wafanyabiashara na watumishi wa umma kupokea na kutoa rushwa na sheria hii imeelezea rushwa kuwa ni pamoja na kuahidi, kutoa na kupokea kitu chochote cha thamani kinachoweza kumshawishi mtumishi huyo wa umma, ‘’kupindisha ukweli’’ katika masuala ya manunuzi.
Hata hivyo ni jambo la kawaida kabisa kusikia ama kuona baadhi ya wafanyabishara wakitumia uwezo wao wa kifedha katika kushawishi kupata zabuni katika mashirika ama makampuni fulani na hata wakati mwingine watumishi wa serikali wamekuwa wakijipatia sehemu ya malipo (10%) kutoka kwa wafanyabishara hao baada ya kuwapatia zabuni hizo.
Kufanya hivyo ni sawa na kupokea rushwa na pande zote mbili zinatakiwa kuchukuliwa hatua kwani kunayanyima makampuni na mashirika yenye sifa zinazotakiwa, nafasi ya kujishindia zabuni hizo.
Kufuatia kanuni za maadili kutozingatiwa, baadhi ya wazabuni licha kutokuwa na sifa zinazotakiwa, wamekuwa wakitumia uwezo wao wa kifedha kujipatia kazi ya usambazaji wa bidhaa mbalimbali katika mashirika, na mwisho wa siku ni kuiingizia serikali hasara kutokana na kutokuwa na viwango katika utendaji kazi.
Maadili katika ununuzi wa mali za umma, inajumuisha mambo mbalimbali likiwemo suala la kuangalia namna watu wanavyoshirikishwa katika manunuzi si tu kwa taasisi za umma, lakini pia kwa mashirika binafsi.
Ingawa kuna sheria inayowazuia watu kutojishirikisha katika vitendo vya rushwa, bado kuna haja ya kila mtu kujisahihisha katika nafsi yake na kuwa mwaminifu, akiongozwa na misingi imara ya imani yake ianyojengwa katika misingi ya maadili.
Njia pekee ni watu kubadilisha mienendo na mitazamo yao kwa kukutokubali kupokea na kutoa rushwa katika suala la manunuzi ya umma.
Haya yakizingatiwa, ni wazi kwamba kwa kiasi kikubwa Tanzania itakuwa imepiga hatua kwa suala la manunuzi ya umma hivyo kuleta maendeleo kwa wananchi kwa kuwapatia huduma na bidhaa zenye ubora wa hali ya juu, katika muda muafaka na kwa gharama nafuu.
Monday, February 15, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment