Monday, February 15, 2010

Tanzania ya leo na mipango ‘mfu’!
Lilian Timbuka
UKIANGALIA historia ya nchi hii utakuta imejaliwa kuwa na mipango mingi na mizruri, ambayo kwa namna moja au nyingine imebakia kuwa ndoto katika ofisi fulani au kama imetekelezwa basi ndivyo sivyo na mafanikio yake bado ni alama ya kiulizo.
Sio sahihi kwa hiyo kuzungumzia mipango kama tatizo la Kitanzania. Tumebobea katika kupanga mipango, lakini tatizo letu liko katika kufanya maamuzi sahihi kwa wakati na kwa maslahi ya wengi na vilevile kudhibiti kila linaloamuliwa litekelezwe kama ilivyokubalika na sio vinginevyo.
Hebu tujaribu kuangalia mipango mbalimbali na jinsi ambavyo hukosa maamuzi na udhibiti. Tumeanguka au tumejiangusha wenyewe, ingawa jambo lenyewe lilikuwa zuri na linalofaa ndani ya uwezo wetu pamoja na umasikini wetu.
Mathalani elimu ya Watu Wazima; huu ni mpango uliotufanya tuonekane tofauti kabisa na nchi nyingine za Kiafrika. Lakini kutokana na kushindwa kubadilika na kufanya maamuzi sahihi kwa wakati wake, leo nchi yetu iko nyuma ya wale tuliowapita kwa mbali miaka michache iliyopita.
Katika dunia hii ya Teknohama inawezekana kuirudisha elimu ya watu wazima kwa nguvu mpya na kuwafundisha watu kusoma, kuandika, ujasiriamali, biashara na menejimenti kirahisi kabisa na kwa namna ambayo itakuwa inavutia watu na kwa muda mfupi tofauti na kumrudisha mtu akae darasani kwa masaa mengi zaidi kama ilivyo sasa.
Pengine hii inatokana na kushindwa kuoanisha elimu na kazi. Maana laiti ingelieleweka kwamba madhumuni ya elimu sio tu kufuta ujinga bali kumpa mtu uwezo wa kujipatia na kudhibiti maisha yake mwenyewe, hili lingelikuwa jambo jepesi kueleweka na kutekelezeka.
Kwenye miaka ya sitini na sabini Watanzania walihamasishwa kuchangia kwa lazima au kwa hiari uanzishwaji wa mashirika ya umma na mashirika na yakaanzishwa na kuendeshwa na Watanzania wenyewe.
Jambo la kujiuliza iweje leo hii Watanzania hao hao wanashindwa kufanya kitu kama hicho, pamoja na kuwepo kwa masoko ya mitaji na hisa ambayo ingeweza kuwachochea Watanzania kuungana na kuendesha mashirika na biashara zao kwa maendeleo ya Taifa? Tunabaki kualika wawekezaji toka nje kila kuchapo!!
Tatizo ambalo binafsui nimelibaini toka kukua kwangu, tunashindwa kuoanisha umuhimu wa kuwa na taasisi za kiuchumi kwa maendeleo ya nchi na mashirika ya umma, hata kama mashirika hayo ni ya watu binafsi.
Shirika binafsi halianzishwi tu kwa ajili ya kumsaidia au kumtajirisha mtu binafsi, bali ni kwa ajili ya faida ya uchumi wa nchi na wananchi pia. Na ni wajibu wa wanasiasa na watumishi wa umma kutoa huduma yao inayohitajika kwa mikono miwili kwa sekta binafsi.
Matumaini ya Watanzania yalikuwa makubwa sana wakati wa kuanzishwa kwa Shirika la Nyumba. Ndoto ya wakati huo ilikuwa eti siku moja kila Mtanzania maskini kwa tajiri atakuwa na nyumba yake kulingana na ukubwa wa familia yake.
Lakini hali haiku hivyo hivi sasa, kuyumba kwa shirika hili hapa katikati, kulichangia kudhoofisha uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa.
Maana ukitembelea katika nchi yoyote ukakuta ujenzi unaendelea basi ujue hapo kuna maendeleo, lakini ukikuta ujenzi huo umelenga katika mji fulani tu, basi hayo ni maendeleo bandia.
Lengo la vijiji vya Ujamaa lilikuwa ni kurahisisha kupiga vita umasikini, ujinga na maradhi. Lakini kwa sababu moja au nyingine maamuzi yaliyofanyika baada ya miaka ya 80, hayakuzingatia hili na ukawa ndio mwanzo wa kuzuka sera na mipango mipya ambayo haikutofautiana zaidi ya majina mapya katika mipango iliyotakiwa kutekelezwa chini ya sera na mpango wa ujamaa vijijini.
Aidha, kuna waliopigia debe kuanzishwa kwa maeneo huru ya kiuchumi, na kweli hilo likafanyika, lakini ufuatiliaji na kuona kwamba mipango iliyokuwepo ndiyo iliyofanikishwa sio jambo yakinifu kujua kama linafanyika au la.
Kinachoonekana leo ni baadhi ya majengo katika maeneo huru yakigeuzwa maghala ya bidhaa ikiwemo magari ya mtumba.
Lengo la Maeneo huru ya kiuchumi kama sikosei lilikuwa kununua bidhaa mpya toka nchi mbalimbali duniani na Tanzania kujigeuza soko kubwa la bidhaa upande wa Afrika Mashariki na ya Kati.
Hata hivyo, hapakuwa na kuoanisha masuala muhimu yaliyostahili kufanyika ili hilo lifanikiwe. Badala ya kuwa na ndege na meli za mizigo, tumejikuta tukijiingiza katika manunuzi ya vitu vingine vya anasa!
Wakati Tanzania tunaendelea kujikongoja kiuchumi, wenzetu huko Botswana, Namibia, Uganda na Rwanda jambo hilo nililolianisha hapo juu limewanyua kiuchumi.
Hata hivyo0 ni vema nikalisema hili, kuwa, katika maamuzi yenye faraja yaliyofanywa na Serikali hivi karibuni ni yale ya kurejesha jeshi la Kujenga Taifa. Uamuzi huu ni wa busara, kwa kuwa umerudisha mawazo ya kuona mbali zaini na mbele kuliko ule wa kulifuta Jeshi hilo kama nilivyokuwa nikilifikiria mimi ambaye hata JKT sijaipitia bali ninapata masimulizi tu ambayo huwa yakinipa tama ya kupitia huko!!!.
Ni vema ikatambulika kuwa, JKT sio chombo cha kujenga umoja wa kitaifa kwa vijana wetu tu, bali ni chombo kinachoweza kutumika kukabiliana na matatizo yetu mbalimbali ya kiuchumi, kijamii, kiteknolojia na kiutamaduni.
Yahitaji kongamano zima kuonesha jinsi JKT inavyoweza kuwa na manufaa ndani na nje ya nchi.
Uamuzi wa kuwa na Madaraka Mikoani ni uamuzi uliofanywa kwa kuzingatia ukubwa wa nchi yetu na jinsi ambavyo viongozi wa juu walivyokuwa na wakati mgumu wa kuitembelea yote na kuharakisha maendeleo mikoani.
Mpango huu ukawa hautekelezeki na zipo habari za juu juu tu kwa wananchi kuhusu mbadala wake unaoitiwa 'devolution'- ambao binafsi nadhani ni sawa na dhana ya kuweka mvinyo mpya katika kiriba kikuukuu. Tumeshindwa kutekeleza lililopaswa kute3kelezwa na sasa tunabuni jina jipya na biashara inaendelea kama kawaida.
Ilikuwepo mipango mingi kama vile ya Siasa ni Kilimo, Maji ni Uhai na Kilimo cha Umwagiliaji Maji. Hivi tofuati yake na Kilimo Kwanza ni nini? Kauli mbiu hii mimi ninaiona kuwa ni sawa na mipango ile ile iliyofeli awamu zilizopita.
Haya azma njema ya kuanzisha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ililenga kuwaondolea Watanzania mzigo wa upatikanaji wa nishati mbadala kwa matumizi ya binadamu na viwanda.
Lakini lengo hilo hivi sasa linavurugwa na matatizo ya uendeshaji wa shirika lenyewe kama ilivyo katika uendeshaji wa rShirika la Reli ya Kati na ile ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Udhaifu katika maamuzi, udhibiti na ufuatiliaji umetufikisha mahala pabaya na sasa kushoto na kulia vilivyotarajiwa kuwa mkombozi wa mwananchi sasa ni mzigo unaowadidimiza katika dhiki na mapungufu ya kila aina.
Sera na Mipango ya Maendeleo Vijijini iliyochangiwa si haba na Benki ya Dunia, haieleweki ilikopotelea na badala yake sasa tuna mpango unaoitwa MKUKUTA na MKURUBITA na ndugu zao, ambao inaonekana kuwa ni moja ya vipande vipande vya maazimio na makusudio ambayo hayana mwelekeo wa kugeuka kuwa kitu kinachoweza kuleta mabadiliko yoyote makubwa na ya maana katika maisha ya mwananchi wa kawaida zaidi ya umangimeza wa wachache ambao wananufaika na kujinasua wao binafsi na umaskini.
Sera ya michezo na burudani bila shaka zipo, lakini kamuulize mwanamichezo au msanii yeyote nchini; siamini kama kwanza atajua kuwepo kwake achilia mbali, kwa yeye kujua mchango wake katika kufanya michezo na burudani kama ajira na lengo katika maisha ya kijana wa Tanzania.
Upo uwezekano wa kuzifanya hospitali, shule na vyuo vyetu kuingiza fedha za kigeni, lakini nani afanye maamuzi nanani adhibiti na nani afuatilie?
Katika miaka ya sasa ni muhimu kuchanganya elimu, ushauri na utafiti kwa kuwapa vijana wetu ajira ya muda ili wafanye yale yanayowezekana ikiwa ni sehemu ya kuhitimu kwao.
Nalo hili tunalifanyia mzaha na halioneshi kama linapewa uzito unaotakiwa na hivyo nchi inapoteza kile ilicho nacho tayari.
Ili kuimarisha na kuendeleza elimu na sayansi ya maamuzi, udhibiti na ufuatiliaji, upo umuhimu wa kutenga siasa na masuala ya uchumi kwa kiasi fulani.
Inavyoonekana mpaka sasa nchi hii inaongozwa zaidi kwa misingi na kanuni za kisiasa kuliko zile za kiuchumi na biashara. Matokeo yake ndiyo hali iliyopo karibu katika kila sekta, serikali na wanasiasa wana mkono.
Vilevile ufanyaji maamuzi sahihi, udhibiti na ufuatiliaji ni utamaduni. Na kama utamaduni mwingine wowote unahitaji muda na gharama kuujenga. Lakini faida au manufaa yake siku zote ni kubwa kuliko gharama za kuanzisha, kuulea na kuujenga ndani ya jamii husika.

No comments: