Monday, February 15, 2010

TAFAKARI YA CPT
CHAGUZI HURU NA HALALI:

Mwananchi, ni haki yako na wajibu wako; tafakari

“KILA mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara mwasema; mvua inakuja, ikawa hivyo. Na kila upepo uvumapo kutoka kusini mwasema; kutakuwa na joto, na ndivyo ilivyo. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya?” (Lk 12: 54 – 56)
Chaguzi zijazo mwezi wa Oktoba 2010 si suala la utekelezaji rahisi rahisi wa haki na wajibu wa kwenda kwenye vituo vya kupigia kura na kupiga kura yako kisha kurudi katika shughuli za kawaida za maisha. Kuna hali fulani ya kisiasa ya watu kutojali chochote na kuwashuku viongozi wao wa kisiasa. Watu wanatambua kwamba kuna mambo mengi mazuri yanayofanywa lakini kwa kiwango fulani wamepoteza imani yao kwa baadhi ya viongozi wa siasa kwasababu ya mlolongo wa kashfa, maoni na matendo ya kubeza kutoka kwa wanasiasa na watendaji serikalini.
Ni jambo la muhimu kuelewa maana na ukubwa wa mwenendo wa raia wa kuwashuku viongozi na kutamani mabadiliko. Mwaka 1990 Mwalimu Nyerere alitambua tamaa ya aina hii ya watu kutaka kuwepo mabadiliko. Akiwahutubia vijana wa Mwanza alizungumzia juu ya hitaji la kuwepo mabadiliko kuendana na mahitaji ya nyakati.
Mwaka uliofuata Tume ya Jaji Nyalali katika taarifa yake ilipendekeza mabadiliko kadhaa katika miundo ya siasa na utawala ili kukidhi hitaji la watu kutaka kuwepo mabadiliko ili kupata fursa ya maendeleo chanya nchini. Kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini Tanzania ni kutokana na hitaji la mabadiliko lililopo.
Leo inapata miaka 18 tokea mfumo huo uanzishwe. Tunatathmini vipi matokeo ya mabadiliko hayo? Je, katika hali halisi ni dhahiri kwamba mfumo wa vyama vingi umeanzishwa? Je watu wamefundishwa maana ya mfumo huo, wamepewa nafasi ya kufikia maamuzi ya sera kwa njia mbadala kupitia vyama tofuati vya siasa na kutiwa moyo kudadisi kwa mitazamo na sera tofauti?
Au tumeshuhudia mwelekeo wa chama tawala kupanga mambo katika namna kwayo vyama shindani kutoweza kustawi kufikia kutekeleza wajibu wavyo itakiwavyo?
Ikumbukwe kuwa siasa sio tu namna ya kujipatia uwezo wa kutawala. Kwa bahati mbaya walio wengi wanao wania uwezo wa kisiasa ndivyo wanavyoona - ni njia ya kujipatia uwezo kwa faida yao hasa. Huo ni upotovu wa siasa yenyewe.
Kwa kadri ya mafundisho ya Kanisa kuhusu jamii, (SDC) siasa inahusishwa na utambuzi wa hadhi ya Utu wa kila binadamu. Siasa inahusishwa pia na kuipatia kila jumuiya ya binadamu uwezekano wa kushirikishana maisha yao kwa kuzingatia kanuni za maadili na tunu zijengazo ushirikiano katika moyo wa mapatano na umoja wa kitaifa.
Siasa zipo kwa kuhudumia msingi uliobainishwa wa kijamii. Sheria zote na sera za serikali lazima zikidhi sharti hilo la msingi la ubinadamu (taz. SDC no. 384,386,388). Maisha katika jamii yanakuwa na maana iwapo yamejikita juu ya msingi wa urafiki na udugu, kwa pamoja wakitafuta yale yaliyo mema kwa taifa lote (Social Doctrine of the Church – SDC no. 390).
Mamlaka ya kisiasa kwa asili yake ni chombo cha kuratibu na kuelekeza jamii kule kunakopatikana nyenzo na rasilimali kwa faida ya ustawi wa wote na wa kila mmoja (SDC no 294).
Kwa hiyo kutaka kuwa na uwezo kisiasa kwa faida binafsi, kama tulivyosema awali, ni upotovu wa asili ya siasa yenyewe. Tukitathmini miaka 18 iliyopita ya siasa ya vyama vingi hatuwezi kuficha msimamo wetu kwamba Chama tawala kimetumia siasa kushika mamlaka yote na ushawishi kwa manufaa yake chenyewe.
Wametumia mbinu nyingi za ujanja kushikilia mamlaka, lakini hawakujaribu ya kutosha kujenga utamaduni wa kweli wa demokrasia, na kubainisha nyenzo za kukuza vyama thabiti shindani na vyombo sawia vya kiraia.
Chama tawala kimehakikisha kwamba kinafaidika kikamilifu kwa kujitwalia yafuatayo: Katika nyanja za fedha, vitega uchumi vyote vya awali, mali zisizohamishika na hisa katika makampuni.
Kina ushawishi wote katika utumishi, utawala, kupitia uteuzi na vyombo vya habari vya umma. Pia kina ushawishi mkubwa katika taasisi muhimu rasmi, kwa mfano; mamlaka ya kodi; fursa za kuingia mikataba ya serikali na wafanyabiashara.
Vile vile katika makampuni ya kimataifa; mahusiano kongwe na wafadhili, Balozi, Asasi za Kimataifa na taasisi za kidini.
Watanzania wamekuwa wakiangalia kwa makini mambo yote yanavyoendeshwa, wengi hawaridhishwi na hawana furaha. Kama ilivyokuwa katika miaka ya 1990 wanataka mabadiliko.
Lakini mabadiliko gani wanayotaka? Mabadiliko yatakiwayo yanatekelezwaje? Mfumo wa siasa wa vyama vingi, awali ya yote, si suala la vyama vya siasa. Kimsingi, ni suala la kujipanga na kuhakikisha ushiriki wa wananchi katika kufanya maamuzi na kuwasilisha vipaumbele vya sera na kuwawajibisha wale waliopewa madaraka ya kuchukua maamuzi – ni juu ya mifumo ya ushirikishwaji na wajibu shirikishi (SDC 406).
Watu wanataka kushiriki katika kutoa maamuzi na lazima wasaidiwe itakiwavyo na watiwe moyo kushiriki.
Watu sharti wajionee dhahiri namna utawala unavyozingatia maoni yao katika ngazi ya jamii yao mahalia ngazi ya wilaya na kwenye ngazi ya taifa. Viongozi wafikie hatua ya kuachana kabisa na mwelekeo wa kuwaona watu kuwa ni wapokeaji wa maamuzi yaliyoshushwa kutoka kwa wale ati wanaotambua mema yafaayo kwa watu.
Watu wamechoka na mienendo ya matumizi mabaya ya mamlaka katika ngazi zote ambapo watendaji hujiona wana uwezo wa kumpa au kumnyima mtu huduma. Haki za watu mara nyingi zinapuuzwa na hili limewachosha. Wanawataka wale walio madarakani kuwatumikia wapiga kura wao, na siyo kujipendelea.
Upotovu wa siasa, yaani ubinafsi katika madaraka, ni moja ya dhambi kubwa ya jamii kwasababu huvunja si tu kanuni za maadili ya uongozi bali pia husababisha uvunjifu wa haki kwa jamii kitu ambacho chaweza kupelekea kuangamia kwa jamii yote. Matokeo ya hayo, ni jamii yote kutokuamini taasisi za umma na kujenga chuki ya kudumu kwa serikali na kwa taifa. Jambo hili huua kabisa utaifa.
Kwa kumalizia tafakari hii tunapenda kuongeza neno moja kuhusiana na muswada wa gharama za uchaguzi (Novemba 2009). Tunaunga mkono jitihada za kuratibu gharama za uchaguzi, kama tulivyoelezea katika Ilani ya Vipaumbele vya kitaifa mwaka 2009 – uk – 8 ”Pawepo kanuni za marekebisho na udhibiti (regulations) na kuwezesha uwazi kisheria kuhusiana na upatikanaji wa fedha za Chama ama mgombea.”
Tuonavyo sisi, Muswada uliopendekezwa unahitaji marekebisho makubwa na makini zaidi. Kwa kuzingatia tuliyo yaelezea awali, hatuoni kuwa muswada uliopendekezwa utaweka uwiano baina ya vyama vya siasa. Kinyume na dhamira hiyo, kuna uwezekano mkubwa sana muswada utazidisha tofauti zilizopo, kama sio kuua kabisa vile vyama vilivyopo.
Zaidi ya hayo, muswada una mianya inayoweza kutumiwa vibaya sana kirahisi tu.
Kwa hali ya mgawanyiko iliyomo ndani ya Chama tawala kwa wakati huu, tunahofia kwamba muswada uliopendekezwa utatumiwa vibaya sana na walio na uwezo na ushawishi (wawe ni kikundi cha wanasiasa walio na mawazo yanayofanana, au wafanyabiashara au ushawishi kutoka mataifa ya nje) dhidi ya wale wagombea uchaguzi wenye utashi mwema kwa taifa hata kuwaengua.
Mtazamo makini zaidi unadhihirisha kwamba uwezo wa kuongoza na kuratibu mchakato wote wa kudhibiti gharama za uchaguzi umo mikononi mwa watu wachache mno (msajili wa vyama vya siasa, makatibu wakuu wa vyama vya siasa) na hauzingatii ukubwa wa nchi (unawanyima madaraka walio wengi vijijini – wilayani).
Kwa kuanzia tunapendekeza linaloweza kufanyika: watakiwe kutangaza mahesabu ya gharama halisi zilizotumika na vyama vyote vya siasa katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na vyanzo vya fedha hizo. Kutokana na taarifa hizo tunaweza kupata fundisho la kutusaidia kuunda muswada unaozingatia uhalisia wa hali yetu ya kisiasa na kujijengea misingi ya haki na ya demokrasia shirikishi.

Mfululizo wa Tafakari hii inatolewa na:
Christian Professionals of Tanzania (CPT).
P.O. Box 9361, Dar es Salaam.
Namba ya Simu:
022-2127675
0713-329984Barua Pepe:
cptprof10@yahoo.com

No comments: