Je ni kweli Tanzania inakwamisha juhudi za EAC?
Na Lilian Timbuka
KATIKA toleo lililopita la Gazeti hili, iliandikwa habari moja iliyokuwa na kichwa kilichosomeka kuwa “vitambulisho vya uraia kikwazo EAC.
Katika habari hiyo, ilionekana kuzungumzia nchi za Uganda na Tanzania kuwa zinaendesha taratibu sana zoezi la upatikanaji wa vitambulisho vya uraia kwa wananchi wake, hali inayosababisha kukwama kuanza kwa soko la pamoja kama ilivyoazimiwa na nchi washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Soko hilo la pamoja lilipaswa kuanza rasmi Tarehe Moja Julai Mwaka huu, lakini ilionekana kuwa kuna raia wengi ambao walipata matatizo pindi walipojaribu kuvuka toka nchi moja kwenda nyingine, siku ambayo ndiyo ilikuwa mwanzo wa taratibu hizo kuanza kutumika.
Hata hivyo ilibainika kuwa, raia wengi wa nchi za Uganda na Tanzania, walikuwa hawana vitambulisho hali iliyosababisha zoezi hilo kukwama.
Hali hii ilithibitishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Bibi. Beatrice Kiraso ambaye alisema wamepata malalamiko mengi kuwa kuna watu walipata matatizo siku hiyo pale walipohitaji kuvuka toka nchi moja kwenda nchi nyingine. Hata hivyo alisema ushapu wa nchi ndio utasaidia zoezi hilo kuanza mapema.
Lakini wakati Naibu Katibu Mkuu huyo Bibi Kiraso akisema hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi, anasema kuna shutuma ambazo zimeelekezwa kwa Tanzania kuwa ndiyo inayokwamisha kufikiwa kwa makubaliano baina ya nchi hizo za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Profesa Paramaganda anasema shutuma zinazotolewa na nchi za Afrika Mashariki kuwa Tanzania inakwamisha kufikiwa kwa baadhi ya makubaliano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki siyo za kweli.
Prof. Kabudi, ambaye pia ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Tanzania ya majadiliano katika ushirikiano wa nchi za jumuiya hiyo, anasema kimsingi, shutuma hizo zinatokana na msimamo wa Tanzania katika kulinda maslahi ya Taifa ili fursa za kiuchumi na raslimali zilizopo nchini ziwanufaishe Watanzania na wageni, badala ya kusababisha vurugu nchini.
Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi na miongoni mwa mambo yaliyopo kwenye ushirikiano huo ni pamoja na Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, Sarafu Moja na Shirikisho.
Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, anasema kuna hofu kwa Watanzania kuhusu ushirikiano huo, hofu ambayo anasema ni ya msingi kwa sababu wanaufuatilia ushirikiano huo kwa umakini mkubwa kutokana na athari zilizojitokeza na kusababisha Jumuiya ya kwanza ya Afrika Mashariki kuvunjika Mwaka 1977.
Alipoulizwa na Mwandishi wa makala haya ni kwanini anasema hivyo, Profesa huyo nguli katika masuala ya Sheria, anasema katika majadilino yanayofanyika kila nchi inaangalia maslahi yake na iko tayari kupinga au kukataa kufungua milango ya ushirikiano kwenye jambo lolote endapo itaona kuna athari yoyote ya kiuchumi au kiusalama.
"Siyo kweli kwamba tumekuwa kikwazo, tunapinga kila jambo, hapa tupo katika kulinda maslahi ya taifa, hivyo kama tunaona jambo hili lina athari, lazima tutapinga na lile lenye manufaa kwa taifa tunalikubali, hatuwezi kukubali au kukataa kila kitu kinacholetwa na kila nchi Afrika Mashariki inafanya hivyo," amefafanua.
Akitoa mfano, Prof. Kabudi anasema wakati Tanzania ikiwa tayari imekwishafungua milango ya fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo ajira kwa wageni hasa katika maeneo ya utalii, sekta ya elimu na maeneo mengine, nchi nyingine zikiwemo Kenya na Uganda zimeendelea kusogeza mbele muda wa kuruhusu fursa zao hadi mwaka 2015.
Kwa msingi huo, anasema malalamiko yanayotolewa hivi sasa na nchi hizo yanatokana na kukerwa kwao na msimamo wa Tanzania katika kulinda maslahi ya raia wake kwa sababu zinataka kufaidika na raslimali zilizopo nchini kupitia ushirikiano huo.
Hata hivyo mpaka sasa imebainika kuwa nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa ardhi kutokana na ama sera mbaya za kumiliki ardhi au eneo dogo lililopo, hivyo zinataka kutumia vyema fursa ya ushirikiano huo ili kukidhi mahitaji yao, jambo ambalo tayari Tanzania imekwishalibaini na imeweka mikakati ya kukabiliana nalo ili kulinda maslahi ya wananchi wake.
Kutokana na hali hiyo, Prof. Kabudi amewataka Watanzania kuwa makini na taarifa zinazotolewa na nchi hizo hasa kupitia vyombo vyao vya habari kuwa Tanzania ni kikwazo katika ushirikiano huo, kwa kuwa taarifa hizo ni propaganda zinazotokana na hasira za kushindwa kwa mikakati yao ya kuhodhi raslimali zilizopo nchini.
Amewahakikishia Watanzania kuwa, timu ya majadiliano ya Tanzania ipo imara kulinda maslahi ya taifa na raia wake hivyo amewataka wananchi kutokuwa na hofu yoyote katika suala hilo.
Monday, July 26, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment