Monday, July 26, 2010

Kwa nini kila mtu anataka ubunge?


Na Padri Babtiste Mapunda
" NI haki yangu ya kikatiba kugombea ubunge, ndiyo kwa maana nimekuja kutangaza nia ya kugombea katika jimbo hili. Mkinichagua nitawajengea uwanja wa ndege katika Jimbo hili la Endeleeni kulala."
Haya ni baadhi ya maneno tunayoendelea kuyasikia wakati huu wa mchakato wa kuchukua fomu na kuzirejesha za kugombea Ubunge ama Udiwani.
Ni kweli kila mwananchi ana haki ya kikatiba ya kugombea na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania. Halikadhalika ana haki ya kuchaguliwa kuwa Diwani. je nani hapendi cheo hiki?
Naendelea kujiuliza je!, kila mtu anaweza kuwa Mbunge au Diwani? Hivi ni suala la Katiba, uhuru na haki ya mtu kugombea au kuna kitu kigine cha ziada? Naendela kushangaa na kujiuliza; "Kwa nini watu wengi siku hizi wanapenda kugombea Ubunge?" Inashangaza kuona majimbo mengine kuna watu zaidi ya 12 kama namba ya Mitume wa Yesu, najiuliza kulikoni?
Je inawezekana kwamba hii ni alama ya kukua kwa demokrasia nchini Tanzania? Sijui! Kinachonishagaza zaidi ni kile cha hata Wasomi wa Vyuo Vikuu, Madaktari wa hospitali, Maaskari na hata baadhi ya viongozi wa Dini, kupata hamasa ya kupenda Ubunge. Inaonekena kuna kitu huko!
Pamoja na ukweli kwamba uongozi siku hizi umekuwa ni wa kununua kwa njia ya rushwa kama alivyojisemea Mzee Warioba, bado kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaokipenda cheo hicho. Au ni ile heshima ya kuitwa "Mheshimiwa Mbunge?" Sijui! Cha kushangaza zaidi inasemekana hata wale wenzangu ambao kisomo chao kipo chini, yaani cha Kidato cha Nne, wanazidi kuwania. Mbaya zaidi kuna watu ambao wanasemekana wamegushi hata vyeti na sasa wanajiita "MaDks" yaani madaktari, wanawania pia. Kwa kweli dhana nzima ya mchakato wa kuwania uongozi huo inanipa shaka kubwa na inanitisha.
Enzi za Mwalimu Nyerere, waliogombea uongozi katika siasa walikuwa wanajipima kwanza, je naweza, na je ninakipaji hicho? je, nina sifa gani ya kutaka kuwa Mbunge? Je ninaweza kutumikia wananchi bila ubaguzi? Lakini leo, hii inaonekana kila mtu anaweza tu kuwa Mbunge bila matatizo. Najiluza ni nini kimetokea katika uwanja huu wa siasa?
Ukweli unaoonekana wazi ni huu kwamba, kazi ya ubunge ambayo ni ya siasa ni mtaji wa kupata pesa kirahisi. Ninaona hii ndiyo sababu kubwa sana ya watu kumiminika kutafuta ajira hiyo.
Ubunge ni biashara nzuri na ya haraka sana katika kujipatia kipato. Ndiyo maana watu wengi hivi sasa wameamua kuiisaka kwa udi na uvumba, hata kama ikibidi kwenda kwa waganga wa kienyeji, kuloga, kutoa rushwa kubwa kubwa na pengine hata kuua ili mradi tu ahakikishe kuwa anaupata ubunge; ataufanyia nini na ubunge huo, unaambiwa hii si hoja ya kuhoji!
Millioni 40 kuipata baada ya miaka mitano ya kutumikia kama mbunge si pesa ndogo. Watanzania wengi wanaitumikia nchi hii kwa zaidi ya miaka 20 na hata 30, lakini hawapati kiinua mgongo cha pesa hiyo wanayopata waheshimiwa wabunge.
Kwa mtu asiyeshika pesa za mamilioni, hayo ni mafanikio makubwa sana. Leo ukiwa mbunge unapta marupu rupu mengi sana, ya gari, matibabu kwa familia yako, pesa ya simu, kusimamia mfuko wa maendeleo wa jimbo lako maarufu kama CDF.
Heshima kubwa unayoipata ya kuitwa "mheshimiwa mbunge wa jimbo la Nipeni nile”, inaonekana ni kitu kikubwa sana ambacho watu wanakitafuta kwa udi na uvumba hasa katika miaka ya hivi karibuni.
Kadiri ya misigi iliyojengwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wengi walijichuja wenyewe. Lakini leo vyama mbali mbali vya siasa hapa nchini, vina kazi kubwa ya kuwachuja wagombea hao.
Mwaka huu kuna kazi kubwa sana hasa ndani ya chama tawala cha CCM kwa vile kina wagombea wengi sana ambao wanawania nafasi za ubunge kupitia chama hicho.
Sheria mpya ya gharama za uchaguzi na tishio la kuwachukulia hatua watoa na wapokea rushwa, linaonekana kupuuzwa kila kukicha. Hapa ndipo ninapoona kwamba kuna nini huko bungeni kiasi cha watu kupuuza sheria iliyosainiwa na Rais wa nchi!
Ama sheria hiyo ni danganya toto? Na kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) watakuwa imara kuwashughulikia watoaji wa rushwa katika kampeni na uchaguzi Mkuu wa Mwezi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31 mwaka huu, je ni wangapi watabaki? Ni swali ambalo tunapaswa kujiuliza mimi na wewe ambao hatujaingia katika mchakato, bali tunasubiri kuwachagua hao ambao wanapigana vikumbo hivi sasa.
Nimeshangaa kuona hata wazee waliokuwa wametoswa miaka kumi iiliyopita na wengine kustaafu, wameamua kurudi ulingoni, najiuliza ni kitu gani kinawasukuma. je, ni kweli wanataka kutumikia wananchi au wanataka kujitumikia wenyewe?
Bunge lililomaliza muda wake hivi sasa, kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wanasema wamekuwa na mafanikio makubwa sana. Hotuba ya Rais ya kuvunja Bunge pia ilijaa mafanikio tu, ningependa kusikia mapungufu pia ambayo yalipatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ili tuweze kupata picha halisi.
Inaonekana hakuna mtu aliyetayari kuongelea mapungufu hayo. Baadhi ya Watanzania wamelalamikia ukosefu wa nguvu ya kushughulikia maovu kama vile wizi wa pesa za Richmond, EPA nakadhalika. Kunaweza kuwa na mafanikio mengi lakini unapoacha maovu yanayogusa jamii yaendelee kwa uhuru wote, basi yanatia doa.
Wengi wanaona kuna baadhi ya wabunge walikosa uzalendo wa kushughulikia baadhi ya masuala ya msingi ambayo yanawakabili wananchi wao. Inaonekana kama vile bunge lilikuwa na woga wa kuchukua maamuzi mazito katika utendaji wake.
Unajua ukweli ni kwamba, Watanzania sasa ni waelewa wa mambo mengi, wewe hubiri unavyotaka lakini wao wanavigezo vyao vya kupima yale unayoyahubiri.
Malalamiko yamekuwa mengi pia katika jamii yetu yakiashiria kwamba kuna kero bado hazijapatiwa ufumbuzi. Je, hawa ndugu zetu wanaofoleni kugombea ubunge wapo tayari kushughulikia masuala mazito katika bunge lijalo? Ningependa kufahamu ni kitu gani kinawasukuma kugombea ubunge huo?
Huenda sijatoa jibu la swali langu na hivi nawaomba wenzangu tuendelee kutafakari pamoja na hasa kuwahoji waheshimiwa watarajiwa kuwa ni "kwa nini wanapenda kuwa wabunge ama Madiwani?"
Napenda kurudia swali langu, "Kwa nini watu wengi wanapenda kugombea ubunge siku hizi? Je, kitu kinachowasukuma sisi tunakijua na kwa nini tuwape kura zetu, je tumeridhika nao? na mwisho tujiulize wanauzalendo wa Kitanzania kwa mfano wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere? au wanao ule wa kibinafsi yaani wa kifisadi?
Mtazamo wangu ni kwamba, kama wanauzalendo wa kibinafsi yaani wa kifisadi, basi hatuna sababu ya kuwapa kura zetu. Ni vema tukaifanya hii kama sera yetu sisi wapiga kura. Mungu ibariki Tanzania na watu wake. Tuonane katika mada ijayo.

No comments: