Monday, October 11, 2010

Oktoba 31, kila mgombea atavuna alichopanda!
Na Lilian Timbuka
HAKUNA ubishi kwamba matarajio ya Watanzania wengi katika uchaguzi mkuu ujao ni kuona mabadiliko makubwa yakitokea katika nafasi mbalimbali za uongozi wa nchi.Mabadiliko ni muhimu ili nchi iweze kujisafisha na kujipanga upya na kuanza mwelekeo mpya katika kuwakwamua Watanzania kutoka katika lindi la umaskini uliokithiri na kurejesha matumaini mapya ya maisha bora kwa kila Mtanzania.Bila ya mabadiliko ya kifikra, dhamira, mbinu na mikakati, umakini na uadilifu katika kuheshimu na kuzingatia viapo vya uongozi kwa mujibu wa Katiba ya nchi, kamwe mabadiliko katika hali ya maisha ya Watanzania, hususan wale wote wenye kipato duni na cha chini, yatabakia kuwa ndoto za mchana na simulizi za majaliwa.Moja ya nyenzo muhimu kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi na uwakilishi, hususani ile ya urais, kupitia mikutano yao ya kampeni, ni kutoa hotuba zitakazo jenga matarajio na matumaini mapya ya kuzaliwa upya kiuchumi na kiroho, kujiamini zaidi kwa wale waliokata tamaa ya maisha. Vile vile ni kuwa na nguvu mpya ya upendo kwa wale walio tumbukia katika lindi la hofu na mashaka kwa hisia za woga na kutothaminiwa katika jamii, kwa wale waliopoteza dira na mwelekeo sahihi katika maisha yao kutokana na kipato duni na mfumo chakavu na uliotindiuka kimaadili katika safu za uongozi.
Hotuba za kampeni za wagombea wote zinatarajiwa kuwa zitaendelea kujenga upendo na mshikamano zaidi na kuondoa woga na hofu ya aina yoyote ile miongoni mwa watanzania na kila mpiga kura.Kama desturi, kila mgombea atapimwa kwa vigezo mbalimbali.
Mojawapo ni pamoja na rekodi yake ya uongozi na mahusiano katika jamii, uadilifu wake, ucha Mungu wake, umahiri wake katika kuzifafanua na kunadi sera za chama chake.Wapiga kura kwa upande mwingine, awali ya yote ni vema wakatambua kuwa wanakabiliwa na jukumu la kujitathmini wao wenyewe katika maisha yao binafsi pamoja na mustakabali wa nchi nzima kimaendeleo katika nyanja mbalimbali.
wapiga kura pia wanapaswa watafakari na kupambanua ni sababu zipi zilizo wafikisha hapo walipo sasa. Majibu yake ndiyo yatakayo waunganisha na sera za vyama mbalimbali vya siasa kwa mujibu wa Ilani zao za uchaguzi.Hatimaye wapiga kura watapata fursa ya kupambanua sera za chama kipi zimejaa ahadi zinazo tekelezeka na zisizo tekelezeka.Watapambanua ni wagombea wapi waliojificha chini ya kivuli cha chama, wakitumaini dezo ya kubebwa na umaarufu na ukongwe wa chama, lakini wao wenyewe wakiwa wamekosa hata chembe ya sifa za uongozi bora na adilifu, kwa mujibu wa rekodi zao za uongozi na mahusiano ya umma.
Miongoni mwa wagombea, wapo watakao lazimisha hoja zao zikubalike iwe isiwe, na kushangiliwa kwa mayowe na wapiga kura au wapambe wao katika mikutano ya kampeni. Hata ikilazimu kwa kuingiza ulaghai wa kisiasa na kutoa ahadi hewa na zisizo tekelezeka.Lakini baya kuliko yote kwa wagombea, ni kujisahau na kuanza kutoa hotuba za kutishia na kujenga hofu na kutojiamini miongoni mwa wapiga kura. Uongo kuhusu hali halisi ya uchumi wetu, hali halisi ya kiwango cha umaskini wa watu wetu, uongo kuhusu uvunaji wa rasilimali za nchi na uongo kuhusu mafanikio na mapungufu yetu katika nyanja mbalimbali za uchumi na kijamii.Aina moja ya hotuba za aina hiyo, ni ile ya kuonyesha waziwazi dhamira ya kulipa kisasi kwa viongozi waliopita au waliokuwepo madarakani, kwa mapungufu na makosa mbalimbali yaliyofanyika nchini wakati wa uongozi wao.Mara nyingi, hotuba za aina hiyo hazimjengi mgombea, bali humtenganisha zaidi na wapiga kura na wafuasi wake wenye dhamira na nia njema ya kupata viongozi walio bora na adilifu.Wagombea wasikurupuke kutoa hotuba za vitisho na za kulipiza kisasi zitakazo jenga woga, hofu na wasiwasi wa kutojiamini miongoni mwa wapiga kura na Watanzania wote kwa jumla.Jukumu lao la kwanza, ni kujenga matumaini mapya na moyo wa kujiamini zaidi kuhusu kesho yenye mafanikio na fursa nyingi zaidi, kwa wale waliokata tamaa ya maisha. Hakuna ubaya kwa wagombea kuwajulisha wale wote waliokata tamaa na wenye maisha duni, kuhusu chanzo na sababu zilizo wafikisha hapo walipo au kupelekea maisha yao kuwa duni.Katika kufanikisha hilo, wagombea wanapaswa kuwa wakweli na wenye kumuogopa Mungu.
Kwa sababu, wapiga kura wengi wenye dhamira na nia njema tayari wameshaanza kubaini njama za kupakana matope na udhaifu wa wagombea kwa mujibu wa vigezo mbalimbali vya uongozi bora na uadilifu.Mapungufu ya mgombea lazima yaainishwe na uhalisia wa mazingira ya uongozi yaliyo mzunguka. Asitolewe kafara kwa sababu zilikuwa nje ya uwezo wake.
Maana yake ni kwamba, lazima haki itendeke katika kumhukumu mgombea kabla ya kupitisha uamuzi wa kumpa kura.
Kila mgombea atavuna alichopanda. Na kila chama cha siasa kisitarajie mteremko au ushindi wa miujiza katika uchaguzi mkuu huu. Ushindi wa mizengwe hautokuwepo.Ushindi wa kila mgombea mmoja mmoja ndio utakao kihakikishia chama chochote kile kupata wabunge wengi zaidi na hatimaye kupata ridhaa ya Watanzania kuunda serikali mpya itakayo liongoza taifa letu kwa miaka mitano mingine.
Uchaguzi Mkuu sio kupiga kura tu, bali ni pamoja na kulinda masanduku ya kura yasije yakahujumiwa. Ili hatimaye kura za kila kituo cha kupigia kura zihesabiwe palepale kituoni na matokeo yake kutangazwa katika njia ya haki na uwazi.Yote hayo yakizingatiwa, yataufanya uchaguzi mkuu ufanyike katika hali ya amani na utulivu, na matokeo yake kukidhi matarajio ya Watanzania wengi.
MUNGU IBARIKI TANZANIA!

1 comment:

Anonymous said...

Hello dear mwombaji Mimi ni Mheshimiwa Stephen Brown kwa jina na i ni mmiliki wa Trust Fedha World Loan Company. Kwa heshima ya matendo yangu kubwa, mimi itabidi kama wewe kujua kwamba i kutoa kila aina ya mkopo unaweza milele kufikiria katika tu kiwango cha riba ya 3%. Harakisha sasa na kuomba kwa ajili ya mkopo wako haraka ili tuweze kupata mkopo wako mbio. Wasiliana nasi leo saa: trustfunds402@yahoo.com Omba kwa ajili ya mkopo wako leo na kupata hivyo kwa haraka kama unataka hivyo. * STEPHEN BROWN *