Sunday, December 5, 2010

TANZANIA YAOMBA NCHI ZINAZOENDELEA ZISAIDIWE UBORESHAJI WA MAISHA YA WATU WENYE WALEMAVU



NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK


Wakati Jumuia ya Kimataifa ikiadhimisha siku ya walemavu hapo desemba tatu.Tanzania imewaomba wadau wa maendeleo na mashirika ya kimataifa kuzisadia nchi zinazoendelea ili ziweze kutekeleza kwa ufanisi ushiriki wa watu wenye ulemavu katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya millennia.
Ombi hilo limetolewa na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,Balozi Ombeni Sefue wakati wa hafla ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya walemavu yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini New York.
Balozi za Tanzania na Ufilipino kwa kushirikiana na Idara ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii (DESA), ndizo zilizoandaa hafla ya maadhimisho hayo. Yaliyohudhuriwa nawadau mbalimbali wakiwamo watu wenye ulemavu, mashirika ya kimataifa na Asasi zisizo za kiserikali.
Ameyataja maeneo ambayo nchi zinazoendelea zinahitaji kusaidiwa ni pamoja na misaada ya kifedha, uboreshaji wa raslimali watu ili siyo tu waweze kuchanganua na kutambua mahitaji na ushiriki wa watu wenye ulemavu katika kujikwamua na umaskini . Lakini pia kutambua vipaumbele vyao katika maeneo ya elimu, afya na ajira.
Akasema yako ikiwa nchi zinazoendelea zitaongezewa nguvu yapo maeneo mengi ambayo serikali zinaweza kutekeleza katika kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu ,na kwa kuzingatia ushirikishwaji wa kundi hilo la jamii.
Akizungumzia namna ambavyo serikali ya Tanzania inavyojielekeza katika kuingiza masuala ya walemavu katika mipango ya MDGs, Balozie Sefue, ambaye alikuwa mmoja wa wazungumzaji katika hafala hiyo, amesema Tanzania imejitahidi kwa kiasi chake katika kuanda sera na program zinazosisitiza ushirikishaji wa watu wenye ulemavu katika vyombo mbalimbali vya maamuzi kama vile Bunge.
Akasisitiza kuwa ni jambo la muhimu sana kwa Jumuia ya Kimataifa kuzingatia maslahi ya kundi hilo la jamii umuhimu na haja ya jumuia , kwakile alichosema ni wadau muhimu ambao hawawezi kuachwa nyuma.Katika salamu zake kwenye maadhimisho hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amesema kundi hilo la jamii bado linaishi katika mazingira magumu na jumuia ya kimataifa haijafanya juhudi za kuridhisha kusaidia..
Amesema ili kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu, viongozi wakuu wa nchi na serikali ni lazima watekeleze kwa vitendo Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Walemavu.
Kama hiyo haitoshi Ban Ki Moon, anawakumbusha viongozi hao kutekeleza ahadi yao waliyoitoka ya kuwashirikisha walemavu katika utekelezaji wa MDGs, wakati walipokutana mwezi septemba wakati wa mkutano wao wa kilele uliorejea utekelezaji wa MDGs.
Kwa mujibu wa Ban Ki Moon, watu wenye ulemavu ni sehemu ya asilimia 20 ya watu wanaoishi katika umaskini wa kupindukia hasa katika nchi zinazoendelea. Aidha ni sehemu ya kundi kubwa la watu wasiokuwa na ajira huku wakikosa fursa za elimu na huduma za afya. Huku wakitengwa na familia zao na katika jamii kwa ujumla.
Ujumbe wa mwaka huu katika maadhimisho hayo ulikuwa ‘utimizaji wa ahadi na uhusishwaji wa masuala ya walemavu katika malengo ya maendeleo ya milenia’.
“ Tunapoadhimisha siku hii ya kimataifa ya watu wenye ulemavu, ni vema tukatambua kwamba hatutaweza kushinda vita dhidi ya umaskini, magonjwa na ubaguzi bila ya kuwa na sheria, sera na program zinazolenga kuwawezesha.
Pamoja na kuanda hafla hiyo, Tanzania na Ufilipino pia zilisimamia majadiliano ya maandalizi ya Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu ushiriki wa watu wenye ulemavu katika utekelezaji wa malengo ya millennia na mipango mingine ya maendeleo. kwa watu wenye ulemavu. Azimio hilo lilipitishwa na nchi wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

No comments: