Wednesday, February 16, 2011

Na Mwandishi Maalum. New York

Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa, ambaye ni Mwenyekiti wa Timu ya watu watatu iliyoteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kuangalia mchakato wa maandalizi na hatimaye upigaji kura ya maoni katika Sudan ya Kusini. Ameliambia Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa matokeo ya kura hiyo ni ya haki, huru na kuaminika.

Rais Mstaafu Mkapa, ameyasema hayo siku ya jumatatu wakati alipokuwa akiwasilisha taarifa yake mbele ya Baraza hilo, ikiwa ni siku mbili zimepita tangu kutangazwa rasmi matokeo ya kura hiyo yaliyoonyesha, kuwa asilimia 98.83 ya wananchi waliopiga kura wameamua kujitenga na kuwa na taifa lao.

“ Timu yetu inapenda kuhitimisha kwamba matokeo ya kura hiyo ya maoni yameonyesha matakwa ya wananchi wa Sudan ya Kusini, mchakato mzima wa upigaji wa kura ulikuwa wa uhuru, haki na wa kuaminika”. Anasema Mkapa. Akasema kukamilika kwa zoezi hilo ni moja ya hatua muhimu sana kuelekea upatikanaji wa amani ya kudumu.

Baada ya matokeo ya mwisho ya kura hiyo kutangazwa na baada ya pande zote mbili kuridhia na kuyakubali, huku Jumuia ya Kimataifa ikiyaridhia, Taifa huru la Sudan ya Kusini litakaribishwa rasmi katika Jumuia ya Kimataifa Julai 9 mwaka huu.


Mkapa ambaye timu yake ilitembelea Sudan ya Kusini mara tano katika kipindi cha kuelekea upigaji wa kura hiyo. Amelieleza Baraza hilo kwamba, katika kutathimini mchakato huo wote, timu yake ilizingatia misingi yote iliyoainishwa katika Sheria ya Kura ya Maoni ya Sudan ya Kusini. Na kwamba Timu imejiridhisha kuwa zoezi lilifanyika katika mazingira ya uwazi wa hali ya juu.

Akaendelea kusema kuwa asasi zisizo za kiserikali nazo zilishiriki kwa ukamilifu na kwamba kauli zilizotolewa na viongozi wa juu wa serikali pande zote mbili za Kaskazini na Kusini zinatia matumaini.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Timu hiyo, anasema kumekuwapo na kusuasua kwa utekelezaji wa masuala ya usalama baada ya upigaji wa kura, pamoja na vitendo vya hujuma ingawa kwa maoni ya timu hujuma hizo hazikuathiri zoezi la upigaji wa kura.
Akatumia nafasi hiyo kuwapongeza Rais Omar Bashir na Makamu wa Kwanza wa Rais Slava Kiir Mayardit kwa kuonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa wa kuhakikisha kwamba hatua muhimu kuelekea amani ya kudumi imefikiwa.
Hata hiyvo ametahadharisha kwamba kazi bado ni kubwa kwa pande zote mbili zinazohusika na mkataba wa amani wa kudumu. Na akatoa wito wa kumalizia vipengele vilivyobaki huku akisisitiza umuhimu wa kuwapo kwa ulinzi wa uhakika kwa wananchi wa Sudani bila ya kujali kama ni wa Kusini au wa Kaskazini.

Pamoja na Rais Mkapa kuwasilisha taarifa yake mbele ya Baraza hilo, wengine waliowasilisha taarifa ni pamoja na Rais mstaafu Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini aliyeongoza jopo la watu mashuhuri kwa niaba ya Umoja wa Afrika, taarifa yake ilisomwa na Balozi Mhmoud Kane, na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan Kusini Bw. Haile Menkerios.
Kwa upande wake baada ya kuzipokea taarifa hizo, ambazo zilifuatiwa na matamko mbalimbali yaliyotolewa na wajumbe 15 wa Baraza Kuu la Usalama. Baraza limeyapokea na kuridhia matokeo ya mwisho ya kura hiyo ya maoni.
Aidha Baraza likawapongeza Rais Omar Al Bashiri na Makamu wa Kwanza wa Rais Salva Kiir Mayardi kwa kuyakubali matokeo ya kura hiyo.
Baraza pia, limewapongeza na kuwashukuru, Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa na timu yake, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Thabo Mbeki na timu yake, Mwakilishi Maalum wa Katibu wa UM Bw. Menkerio, Umoja wa Afrika na Jumuia ya Kimataifa kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanikisha upigaji wa kura na matokeo yake.

Akisoma Tamko la Baraza hilo, Rais Baraza kwa mwezi huu, ambaye ni Brazil, Balozi Maria Luiza Ribeiro. Amesema Baraza linatoa wito kwa Jumuia ya Kimataifa kuwasaidia kwa hali na mali wananchi wa Sudan ya Kusini katika kuijenga nchi yao. Pamoja na kulitambua Taifa hilo ifikapo Julai

Baraza Kuu linasisitiza katika tamko lake kwamba ili amani ya kudumu na usalama iwe dhahiri katika Sudan na eneo lote kwa ujumla, ni muhimu vipengele vilivyobaki katika Mkataba wa Kudumu wa Amani vikatekelezwa haraka.
“ Wajumbe wa Baraza linazihimiza pande zote za Mkataba wa Amani kukutana haraka na kukubaliana kuhusu eneo lenye mgogoro la Abyei, suala la mipaka, mpangilio wa masuala ya usalama, uraia, deni la kitaifa, sarafu, mali na ushirikiano katika utajiri na maliasili” anasema Balozi Maria Luiza Riberio.
Aidha Baraza Kuu la Usalama limewataka na kuwahimiza viongozi wa Sudan ya Kaskazini na Kusini kuendelea na moyo na utashi ambao wamekwisha kuuonyesha na kwamba Jumuia ya Kimataifa ipo pamoja nao.


MWENYEKITI wa timu ya watu watatu iliyoteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon kuangalia mchakato wa kura ya maoni Sudan Kusini, Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa akiwasilisha taarifa yake mbele ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, jana, Ijumatano, kuhsu mchakato huo na matokeo ya kura. maataokeo ya mwsiho ya kura hiyo yaliyotangazwa Jumatatu wiki hii, yameonyesha kuwa asilimia 898.83 ya waliopiga kura wameafiki Sudani Kusini ijitenge na kuwa taifa jipya.

No comments: