BAADA YA KUSAFIRI NA TRENI
Fagio la Mwakyembe
lamkumba mtumishi TRL
*Aagiza afukuzwe kazi mara moja
*Amnasa akitoza nauli isiyo halali
*Abaini madudu chungu tele
WAZIRI wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe, amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), kumfukuza kazi mmoja wa wafanyakazi wa shirika hilo kwa kumtoza mmoja wa abiria nauli ya kubwa.
Dk. Mwakyembe aliyasema hayo jana asubuhi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kuwasili mjini hapa kwa treni kutoka Dar es Salaam.
Waziri huyo, alisema amegundua madudu mengi yanayofanywa na wafanyakazi wa kampuni hiyo dhidi ya abiria, baada ya kusafiri na treni hiyo.
Alisema mmoja wa watumishi wa kampuni hiyo bila kumtaja jina, alimtoza abiria fedha nyingi ya mizigo, huku akimpa stakabadhi inayoonyesha kiwango tofauti na alicholipa.
Dk. Mwakyembe alisema vitendo vya ulanguzi wa tiketi kwa abiria na rushwa toka kwa watumishi wa kampuni hiyo, vimekithiri.
“Nimetembelea behewa moja hadi jingine, nimeyaona mambo mengi ikiwemo uchakavu wa mabehewa na nimezungumza na abiria wameniambia mambo mengi ya kusikitisha,’’ alisema.
“Ndani ya treni hii, hakuna tofauti kati ya ‘First Class na Third Class’, yaani daraja kwa kwanza na la tatu yote hovyo tu,” alisema Waziri huyo.
Waziri Dk. Mwakyembe ambaye aliwasili mjini hapa saa 1.30 asubuhi jana akitokea jijini Dar es Salaam, alisema inashangaza kuona abiria wakilipishwa fedha kwa ajili ya mizigo yao kinyume na sheria.
Alisema kufuatia madudu hayo, ameuagiza uongozi wa TRL kumbaini mtu huyo mara moja ili hatua za kinidhamu zikuchukuliwe dhidi yake.
Kero nyingine aliyoishuhudia ni watoto wa miaka mitatu kukatiwa tiketi ya mtu mzima wakati si sahihi.
No comments:
Post a Comment