Thursday, June 14, 2012

Mtuhumiwa

wa Al-Qaeda

akamatwa Dar

JESHI la Polisi nchini, limemtia mbaroni mtuhumiwa wa ugaidi wa kundi la Al-Qaeda anayedaiwa kuwa mshirika wa kundi la kivita la Al-Shabab la Somalia.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamishna wa Makosa ya Jinai nchini, (DCP), Issaya Mugulu, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Juni 10, mwaka huu.

Mugulu alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni raia wa Ujerumani aliyezaliwa nchini Uturuki, amefahamika kwa jina la Emrah Erdogan (24), ambaye pia anajulikana kwa jina la Abdulrahaman Othman, alikamatwa jijini Dar es Salaam.

“Mtuhumiwa huyu ni mpiganaji wa Al-Qaeda ambaye ameshiriki mapambano nchini Afghanistan na hivi karibuni nchini Somalia ambako alikuwa akishirikiana na kikundi cha Al-Shabab,” alisema Mugulu.

Alisema mtuhumiwa huyo ambaye kwa sasa anahojiwa na vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania, Ujerumani, Kenya na Uganda, anadaiwa aliingia nchini kwa njia za panya akitokea Nairobi nchini Kenya.

Naibu Kamishna huyo, alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano walioutoa kwa polisi hadi kufanikisha kukamatwa kwake.

Pia, Mugulu aliwahakikishia wananchi kwamba, vyombo vya ulinzi na usalama nchini, viko imara kukabiliana na matishio yote ya uhalifu yakiwemo ya kigaidi.

Aliwaomba kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vyao vya ulinzi na usalama ili kuimarisha amani nchini.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, Erdogan anatafutwa pia na serikali ya Kenya kwa madai ya kufanya shambulizi la kigaidi mjini Nairobi lililoua mtu mmoja na kujeruhi zaidi ya watu 30, Mei 28, mwaka huu.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, polisi wa Kenya walitoa picha ya Erdogan kwenye vyombo vya habari vya nchi hiyo ikiwa na maelezo kuwa aliingia nchini humo akitokea Somalia, Mei mwaka huu.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, Erdogan, aliwahi kusafiri hadi eneo maarufu la Waziristan, lililoko Kaskazini mwa Pakistan ambalo linatumiwa na magaidi kupanga mikakati yao.

Taarifa za vyombo hivyo, zinasema alikuwa nchini humo mwaka juzi na inaaminika alijiunga na kundi la kidini lenye msimamo mkali, kabla hajasafiri hadi Somalia, mwaka jana, inakoaminika alijiunga na kundi la Al-Shabaab.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Jeshi la Polisi la Uganda lilitoa taarifa likimsaka Erdogan na raia mwingine wa Ujerumani wanaotakiwa kujibu tuhuma za ugaidi.

Nchi hiyo, imekuwa ikiwasaka watu hao wakiwa katika kundi la watuhumiwa wanaodaiwa kutekeleza mashambulizi ya kigaidi yaliyouawa zaidi ya watu 30, mwaka juzi, ambao walikuwa katika klabu moja ya usiku wakiangalia mojawapo ya mechi za Kombe la Dunia lililofanyika Afrika Kusini.


Ufisadi watingisha Longido

*Kigogo ajiuzia gari kwa bei chee

*RAS aduwaa kupokwa madaraka

NA SHAABAN MDOE, ARUSHA

UFISADI wa kutisha umegundulika katika wilaya ya Longido, ambapo kigogo mmoja anadaiwa kujiuzia gari kwa bei ya kutupwa.

Kigogo anayedaiwa kuhusika na ufisadi huo ni Ofisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Steven Laizer, ambaye anadaiwa kujiuzia gari kwa sh. milioni 1.4 muda mfupi baada ya kufanyiwa matengenezo ya sh. milioni 17.

Habari zilizopatikana wilayani hapa zinasema kitendo hicho kimemkera Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo, aliyeagiza ofisi ya katibu tawala wa mkoa kufuatilia suala hilo.

Kuwepo ufisadi huo kulibainika katika kikao cha Kamati ya Fedha ya halmashauri, kilihudhuriwa na Mulongo na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo.

Suala hilo liliibuka baada ya Mulongo kuulizia kuhusu gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser Pick-up, lenye namba ya usajili STH 3352. Mkuu huyo wa mkoa aliagiza ofisa huyo ambaye hakuwepo kwenye kikao afike ofisini kwake.

Laizer baada ya kufika na kuhojiwa, alikiri kuuziwa gari hilo na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Tumaini Msuya, ambaye sasa ni marehemu.

Kwa mujibu wa Laizer, aliuuziwa gari hilo baada ya kumweleza aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga, kuwa ni chakavu na la muda mrefu, kwa kuwa walipewa baada ya wilaya ya Monduli kugawanywa.

Longido ilikuwa sehemu ya wilaya ya Monduli kabla ya kugawanywa mwaka 2000.

Alisema baada ya waziri kuelezwa hilo, alimwagiza mkurugenzi wa halmashauri kuandika taarifa kuwa ni chakavu ili wapelekewe lingine na kwamba, Tumaini alifanya hivyo.

“Baada ya taarifa kuandikiwa, gari hilo lilipelekwa gereji ya Mwanzo, iliyoko Arusha kwa matengenezo na likiwa huko, niliandika dokezo la kuomba kuuziwa,” alisema.

Laizer alisema wakati gari hilo likiwa karibu kumalizika matengenezo ya injini na kuwekwa magurudumu mapya, yaliyogharimu sh. milioni 17, alijibiwa barua na kutakiwa kulipia sh. milioni 1.4 ili kulinunua.

Alisema anatambua gari hilo ni mali yake na kwamba, anapaswa kulipwa na halmashauri kwa kipindi chote ambacho limekuwa likitumiwa kwa kazi za halmashauri.

Kutokana na maelezo hayo, Mulongo alimwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Evelyne Itanisa, kuandika barua Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kujua kama ununuzi huo ulifuata utaratibu.

Pia alimtaka Evelyne kujiridhisha iwapo inawezekana gari kufanyiwa matengenezo kwa gharama kubwa na baadaye mtu kuuziwa kwa bei ya kutupwa.

Katika hatua nyingine, baadhi ya watumishi wa ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Arusha, wamedaiwa kukiuka kanuni na utaratibu wa utumishi kwa kuchukua madaraka ya bosi wao na kufanya mambo kinyemela.

Watumishi hao wanadaiwa kuwahamisha wenzao huko katibu tawala aikiwa hajui.

Hayo yalibainika jana mjini hapa baada ya mmoja wa watumishi hao, Muchunguzi Kabonaki, ambaye ni mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kuhamishwa.

Kuhamishwa kwa Kabonaki, kulibainika jana wakati wa ziara ya ghafla ya Mulongo wilayani Longido, iliyolenga kufuatilia masuala ya pembejeo na watumishi waliohamishiwa wilayani humo Septemba na Oktoba, mwaka jana, kama wako kazini au la.

Baada ya kuhoji wahasibu hao kama wapo sehemu zao za kazi, alijibiwa na Ofisa Utumishi wa Wilaya, Furahisha Magubira kuwa, tangu walipohamishwa kutoka Arusha kwenda Longido mmoja wa wahasibu, Gabriel Mkonyi, aliripoti lakini baada ya miezi miwili alitoweka bila taarifa na hajulikani alikokwenda.

Alisema Kabonaki alifika na kuonyesha barua iliyotiwa saini na Elgin Nkya, kutoka ofisi ya RAS Arusha kuwa anatakiwa kwenda Tanga, kusimamia kazi maalumu.

Furahisha alisema baada ya kuonyeshwa barua hiyo, alifanya mawasiliano na ofisi ya RAS kufahamu iwapo Kabonaki amehamishwa kihalali kwa sababu ofisi yao ilikuwa na uhaba wa wahasibu. Alijibiwa haina taarifa na wanashangaa kusikia hivyo.

Hatua hiyo ilimfanya Evelyne kushituka na kuhamaki mbele ya kikao cha zaidi ya watu 40 kuwa hajui kama wahasibu hao hawapo kazini na hajatoa barua ya kuwapangia watumishi majukumu mengine ya kazi.

Alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na Mulongo kama anafahamu lolote juu ya hilo.

Evelyne alisema hajawahi kuona barua kutoka kwa Kabonaki na anashangaa ofisa utumishi kusema Nkya ndiye ametoa barua hiyo, wakati yeye hana taarifa yoyote, jambo linalomtia hofu kuwa ofisi yake imegeuzwa kijiwe na baadhi ya watumishi na kuhodhi madaraka yasiyo yao.

Majibu hayo ya RAS yalimfanya Mulongo kusema: “Ninachosema si kushituka hapa na kushangaa haya yanayofanyika. Ni aibu kwako kwamba huna taarifa, matokeo yake yatakuharibia kazi, fanyia kazi na nipate taarifa ifikapo mwishoni mwa wiki ijayo.”

CHANZO CHA HABARI ZOTE GAZETI LA UHURU


Serikali iufanyie kazi utafiti wa viongozi wa Dini

NA LILIAN TIMBUKA
JANA vyombo vya habari viliripoti habari iliyohusiana na utafiti uliofanywa na Kamati ya Kudumu ya Viongozi wa Dini ya Haki za Kiuchumi na Kijamii na Uadilifu katika Uumbaji, kuhusiana na upotevu wa mapato ya serikali.
Katika utafiti huo, ilibainika jumla ya dola za Kimarekani bilioni mbili (Sh. trilioni tatu) za mapato ya nchi, hupotea kutokana na ukwepaji wa kodi.

Viongozi hao walibainisha chanzo cha upotevu huo kuwa ni kutokana na misamaha ya kodi kwa baadhi ya makampuni, sambamba na utoroshwaji wa mali zikiwemo fedha na rasilimali nyinginezo za nchi, nje ya nchi.

Walibainisha mambo mengi ambayo kama serikali itayachukua na kuyafanyia kazi, itaweza kudhibiti mapato yake yanayoendelea kutafunwa na wajanja wachache ambao wanaacha mamilioni ya Watanzania wakiteseka.
Viongozi hao walizungumzia suala la sera mbovu ya ukusanyaji mapato inayoendelea kutumika nchini sambamba na sera ya kodi ya Mwaka 2004.
Sheria hiyo licha ya kufanyiwa marekebisho, bado inaonekana kuwa na upungufu mkubwa.
Nami naungana nao kuwa muda wa kuifanyia marekebisho umefika, watendaji wasilifumbie macho suala hili, hii ni kwa siha ya Watanzania.
Sheria hiyo ina vipengele ambavyo vinaruhusu misamaha ya kodi kwa wawekezaji ambayo imeonekana kutokuwa na tija kwa sasa.

Badala ya kuwabebesha mzigo wafanyakazi ambao wameonekana vinara wa kuiingizia serikali mapato kila mwaka, hali hiyo igeuziwe kwenye makampuni na wafanyabiashara wenye vipato zaidi ya mfanyakazi.
Kama walivyoeleza viongozi hao, kuna haja ya kupanga mikakati mipya ya ukusanyaji mapato kutoka kwa makampuni yanayoendesha biashara nchini.
Hali hiyo itaihakikishia serikali mapato yakutosha kwa kuendeshea shughuli zake za maendeleo.
Kwani muda wa kuwategemea wahisani kuchangia bajeti ya nchi, umepita.
Iwapo Serikali ingedhibiti mianya ya ukwepaji wa makusanyo hayo, huenda mazuri mengi yangefanyika na kusingekuwa na malalamiko.

Fedha hizo zingeweza kupelekwa katika huduma za jamii, ambazo kwa sasa zina mahitaji makubwa.

Wakati mjadala wa bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 unapoanza rasmi leo, wabunge na watendaji wengine wa serikali wanapaswa kutazama ni kwa jinsi gani serikali itaweza kujiongezea mapato, sambamba na kubana mianya ya upotevu wa mapato.
Pia, itazame upya utaratibu wa kuvutia wawekezaji na makampuni katika kutoa misamaha ya kodi na kubainisha namna ya kuipunguza kama siyo kuiondoa kabisa.
Imefika wakati kwa Serikali kujiwekea utaratibu wa kutathimini kila mwaka gharama za matumizi yatokanayo na misamaha ya kodi, ili kubaini wanaonufaika na mtindo huo.

Leo Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, anatarajia kuwasilisha bungeni bajeti ya serikali ya mwaka mpya wa fedha 2012/2013, ya Sh. Trilioni 15.


No comments: