Imethibitishwa kuwepo na dosari ya kuwepo kwa mafuta yaliyochakachuliwa.
Kampuni hizo zinashinikiza hatua zichukuliwe baada ya mamlaka husika kukiri kuwa shehena iliyoingizwa nchini kati ya Januari na Machi, mwaka huu, ilikuwa imechakachuliwa.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya mafuta kukosa soko na yanachangia uharibifu wa magari yaliyotumia mafuta hayo.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), katika barua yake ya hivi karibuni, ilikiri kuwa shehena ya mafuta yaliyoingizwa nchini mwanzoni mwa mwaka huu ilikuwa imechakachuliwa.
Juni 5, mwaka huu, EWURA ilimwandikia Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kuratibu Uagizaji Mafuta, PIC (T) Ltd, kueleza kuwa mafuta yaliyoingizwa nchini katika kipindi cha Januari na Machi, mwaka huu yalikuwa yamechakachuliwa kutokana na kuwa na ethanol kwa wingi.
UHURU ina nakala ya barua hiyo ambayo ilisema baada ya kupata malalamiko kuhusu ubora wa mafuta yaliyoingizwa nchini kipindi hicho, EWURA ilichukua sampuli na kuzipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Iliongeza kuwa, majibu ya Mkemia Mkuu yalionyesha katika sampuli 11 zilizopelekwa, 10 zilikutwa zina ethanol nyingi, kiwango ambacho hakikubaliki hata katika vigezo vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Sampuli hizo zilichukuliwa kwenye meli 11 zilizokuwa na shehena ya mafuta kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Katika barua hiyo, EWURA inaitaka PIC (T) Ltd kurekebisha dosari zilizojitokeza na kuhakikisha Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa pamoja unaendelea bila kuathiri jambo lolote.
“Kutokana na unyeti na umuhimu wa biashara ya mafuta, mamlaka inataka kupata mipango yako na jinsi ya kushughulikia suala hili,” ilifafanua barua hiyo ya EWURA.
Uamuzi huo wa EWURA ndiyo umefanya baadhi ya wafanyabiashara kuona suala hilo linaendeshwa kisiasa bila kujali maslahi yao, hivyo kutishia uhai wao.
“Mamlaka imekiri kuwa mafuta yaliyoingizwa nchini kipindi hicho yalikuwa yamechakachuliwa, kwa nini hatua zisichukuliwe na badala yake wahusika wanalindwa na kuombwa watoe maoni...tunakwenda wapi katika biashara ya mafuta,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao bila kutaka kutajwa jina gazetini.
Mfanyabiashara huyo ambaye alikuwa akizungumza kwa niaba ya wenzake, alisema wanaomba serikali ichukue hatua ili kurekebisha dosari hizo, badala ya wajanja wachache kutumia ubabe kujinufaisha.
Hivi karibuni, kampuni za uuzaji mafuta nchini zilishitakiana kwenye mamlaka za usimamizi baada ya kukithiri kwa vitendo vya uchakachuaji wa mafuta ya petroli na dizeli.
Kukithiri kwa uchakachuaji huo wa mafuta kumesababisha baadhi ya shehena zilizokuwa zimepelekwa nchi jirani, kukataliwa.
Hali hiyo ilisababisha Chama cha Wafanyabiashara wa Mafuta Tanzania (TOAMAC) kuandika barua kwenda kwa EWURA ili kuingilia kati na kunusuru hali hiyo.
Barua ya TAOMAC ya Aprili 5, mwaka huu kwenda EWURA ilisema wafanyabiashara wa mafuta wanahisi kuwa mafuta yaliyoingizwa nchini yamechakachuliwa kwa kuchanganywa na ethanol.
Pia, TAOMAC katika barua yao walisema wanaomba EWURA kuichunguza Kampuni ya Augusta Energy ya Uswisi kama ina nyaraka muhimu ya ubora wa bidhaa zikiwa kwenye meli na bandarini kwa shehena ya mafuta ya Januari, Februari na Machi mwaka.
Barua hiyo ya TAOMAC ilisema suala hilo ni la kibiashara, EWURA ifanye jitihada za kupata majibu kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kuhusiana na sampuli za mafuta zilizopelekwa kwake.
Kampuni ya Augusta ilishinda zabuni ya kuagiza mafuta chini ya Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPS) hadi mwezi huu.
Kampuni nane za mafuta zilitoa malalamiko kuhusiana na kuwepo kwa mafuta machafu.
Kampuni hizi ni GAPCO, ENGEN, MOGAS, TIPER, NATOIL, HASS, KOBIL, OILCOM na PUMA Energy ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama BP Tanzania.
Kwa upande wa uuzaji wa mafuta katika nchi jirani, tayari Rwanda imekataa kupokea shehena ya mafuta ya kampuni ya MOGAS kwa madai yamechakachuliwa.
Shehena nyingine ya mafuta ya Kampuni ya MOGAS ilishikiliwa mjini Lubumbashi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kusubiri matokeo ya uchunguzi.
Mbali ya MOGAS, kampuni ya HASS nayo ilisema malori yake manne yalishikiliwa mjini Kigali, Rwanda na yamezuiwa kupakua mafuta.
Kwa upande wake, Kampuni ya OILCOM ilisema malori yake 10 yalikataliwa kupakua mafuta na wateja katika vituo vyake.
No comments:
Post a Comment