MKURUGENZI Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Dk. Clemence Tesha, amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumuajiri ofisa mwandamizi anayesimamia taaluma hiyo ambaye hana cheti wala hajasajiliwa.
Dk. Tesha alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Faisal Kahamba, pamoja na Ofisa Mwandamizi wa Rasilimali Watu, Winfrida Igogo na mwajiriwa Amani Ngonyani.
Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Salha Abdallah, alidai kuwa Ngonyani aliajiriwa kwa wadhifa wa Meneja Maendeleo ya Biashara, akiwa anawajibika na kusimamia maendeleo ya taaluma ya ununuzi na vifaa wa bodi hiyo.
Katika shitaka la kwanza, Dk. Tesha na Winfrida, wanadaiwa Juni 22, mwaka 2010, katika ofisi za bodi hiyo, zilizopo jijini Dar es Salaam, walitumia madaraka yao vibaya kwa kumuajiri ofisa huyo mwandamizi.
“Amani Raymond Ngonyani, hakuwa na cheti katika ununuzi na ugavi, hakusajiliwa kama mtaalam mwandamizi na mtendaji, jambo ambalo ni kukiuka kifungu cha 46(1) cha Sheria ya Bodi ya Ununuzi na Vifaa, sheria namba 23 ya mwaka 2007,” alidai Salha.
Katika shitaka la pili, Dk. Tesha na Winifrida, wanadaiwa Juni 22, mwaka 2010, katika ofisi za bodi hiyo, walimuajiri Ngonyani ikiwa ni kinyume na sheria zinazosimamia ajira za wataalam katika fani hiyo inayosimamiwa na bodi hiyo.
Ngonyani anadaiwa kukubali kuajiriwa katika kazi inayohusiana na taaluma ya ununuzi na ugavi katika bodi inayosimamia taaluma hiyo kinyume na sheria inayosimamia taaluma hiyo.
Washitakiwa hao walikana mashitaka na upande wa mashitaka ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa kwa shauri hilo.
Hakimu Kahamba, alisema dhamana ni haki ya mshitakiwa na mashitaka yanayowakabili yanadhaminika.
Alitaja masharti ya dhamana kuwa kila mshitakiwa awe na wadhamini wawili wenye vitambulisho kutoka serikalini au taasisi inayotambulika.
Pia, alisema kila mdhamini atatia saini bondi ya sh. milioni 10. Washitakiwa walitimiza masharti ya dhamana na hivyo kuachiwa huru kwa dhamana hadi Julai 26, mwaka huu, kesi itakapotajwa.
No comments:
Post a Comment