Friday, June 29, 2012

Vigogo Jiji la Arusha wahojiwa kwa wizi

POLISI mkoani Arusha imewashikilia kwa muda na kuwahoji watumishi sita wa halmashauri ya Jiji la Arusha, kwa tuhuma za wizi wa mamilioni ya fedha za umma.

Habari za kuaminika zilidai kuhojiwa kwa watumishi hao ambao wengi ni viongozi wa idara mbalimbali, kumetokana na matokeo ya tume maalumu iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo, kuchunguza taarifa za ubadhirifu iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Chanzo chetu ndani ya Polisi kilisema kushikiliwa na kuhojiwa kwa watumishi hao kumetokana na wizi wa njia mbalimbali ikiwemo ununuzi hewa wa vifaa vya halmashauri.

Ilielezwa kuwa wanaohojiwa ni pamoja na maofisa wa idara za usafirishaji, afya, ugavi na uchumi.

Wanadaiwa kuisababishia hasara ya zaidi ya sh. milioni 31 Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Habari zaidi zilisema maofisa hao walikula njama na kuiibia halmashauri kupitia ununuzi wa mafuta ya dizeli lita 3,680 zenye thamani ya sh. milioni 6.2.

Maofisa hao wanadaiwa kutumia nyaraka zisizo halali zikiwemo stakabadhi katika kumlipa mzabuni aliyesambaza mafuta hayo, ambayo hata hivyo hayakununuliwa kama ilivyoagizwa.

Miongoni mwa watumishi wanaohojiwa na polisi, wamo walioibia halmashauri hiyo kiasi cha sh. milioni 25.5 kupitia ununuzi hewa wa vifaa vya Teknohama.

Fedha hizo zinazodaiwa kuliwa na maofisa hao zilitolewa msaada na Benki ya Dunia kwa ajili ya mradi huo wa kuendeleza teknolojia na kusababisha kukwama.

Hata hivyo, taarifa zilieleza kuwa kwa sasa maofisa hao wako huru wakisubiri taratibu zingine za kuwafikisha mahakamani, ambapo kwa mujibu wa maofisa wa polisi, watafikishwa kizimbani muda wowote kuanzia sasa.

“Mambo hapa yanazidi kunoga, maofisa na watumishi walioiba fedha za umma sasa ni mahakamani tu. Wamiliki wa kampuni zilizohusika na zabuni hizo pia wameitwa kuhojiwa. Kinachosubiriwa kwa sasa ni kupandishwa kizimbani kwani kila kitu kimekamilika,” kilisema chanzo chetu hicho.

No comments: