Friday, July 27, 2012

KEPTENI KOMBA AREJEA KUTOKA INDIA



Kepteni John Komba akiwa na mkewe Salome, nyumbani kwake Mbezi, Dar es Salaam.

MKURUGENZI wa Kundi la Tanzania One Theatre (TOT), ambaye pia ni Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba amerejea nchini kutoka India, ambako alikwenda kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kumtibu ugonjwa wa nyonga uliokuwa ukimsumbua upande wa mguu wake wa kulia.


Akizungumza na waandishi wa habari leo, nyumbani kwake Mbezi kwa Komba, mjini Dar es Salaam, Komba alisema alirejea nchini juzi baada ya kupatiwa matibabu hayo kwenye hospitali ya Appolo iliyopo Hydrabad nchini India tangu mwanzoni mwa wezi huu.


Komba alisema, aliondoka nchini Julai 2, 2012 baada ya kupelekwa na serikali kwa maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete, Spika wa Bunge Anna Makinda na Katibu wa Bunge John Kashilila na kwamba alikwenda baada ya kukosa matibabu hapa nchini kwa sababu ya mgomo wa madaktari.


"Siku napelekwa Muhimbili tu, tayari madaktari walikuwa wameanza siku ya kwanza ya mgomo wao, nikawa sina namna ila kuujulisha uongozi wa Bunge na kisha nikamuomba Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, naye kwa mamlaka yake akanisaidia haraka kama ambavyo huwasaidia wengine kwenda kutibiwa nje", alisema Komba.


Alisema uzito ulichangia sana kusababisha mifupa kusagana kwenye nyonga upande wa mguu wa kulia, ambapo hadi anakwenda India, alikuwa na uzindo wa kilo 138 wakati wastani wa uzito aliotakiwa kuwa nao kulingana na ukubwa wa mwili wake ni kilo 90 au 100 tu.


Komba alisema baada ya matibabu, amerejea nchini akiwa na uzito wa kilo 128, ambao hata hivyo ametakiwa kuudhibiti na kuupunguza katika siku ambazo atalazimika kupumzika nyumbani kabla ya kuanza kazi Septemba mwaka huu kama alivyoelekezwa na madaktari.

Akizungumzia upasuaji ulivyoendeshwa, Komba alisema ulichukua saa tano na kukamilika bila matatizo. Alisema katika upasuaji huo, sehemu iliyopasuliwa ni ya ukubwa wa futi moja.

Hata hivyo, alisema baada ya upasuaji huo, hakuweza kurejea katika wodi ya kawaida kwa sababu magonjwa kadhaa yaliibuka, ikiwemo homa kali na presha hivyo akalazimika kulazwa katika wodi ya wagonjwa waliopo kwenye uangalizi maalum (ICU) kwa siku tano.

"Sasa nimerejea nikiwa mzima, kwa sasa natumia fimbo hii, ili kuwezesha uzito usielemee upande wa kulia nilikopanyiwa upasuaji, lakini sijambo kabisa," alisema Komba.

Komba alilaani baadhi ya vyombo vya habari, ambavyo viliripoti kwamba katika kuugua kwake alikuwa mahututi na kwamba alikuwa anaugua figo.

"Jamani ninyi waandishi wa habari, jizoesheni kuandika habari zilizokamilika siyo kurashia-rashia tu na kuzusha uongo. Mfano gazeti moja liliandika eti naugua figo, nipo mahututi wakati si kweli kabisa, ilikuwa jambo rahisi tu, kuja hapa nyumbani na kuniuliza au kuuliza mke wangu lingepata kwa uhakika ninachoumwa", alisema Komba.

NGASA ANG'ANG'ANIA KURUDI NYUMBANI YANGA

Ngasa akiondoka kwenye jukwaa la mashabiki wa Yanga baada ya kuzawadiwa jezi


Ngasa akielekea kwenye mlango wa kuingia uwanjani baada ya kuvaa jezi ya Yanga (Picha na Emmanuel Ndege Mdau wa AMKA MTANZANIA blog.)

Mshambuliaji Mrisho Ngasa juzi alifanya vitendo vya ajabu wakati timu yake ya Azam ilipokuwa ikimenyana na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Kagame.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Ngasa aliingia uwanjani kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Kipre Tchetche.

Kituko chake cha kwanza ni kwenda kushangilia bao la pili aliloifungua Azam katika mechi hiyo kwenye jukwaa wanalokaa mashabiki wa Yanga.

Muda wote wa pambano hilo, mashabiki hao walikuwa wakiizomea Azam, lakini baada ya mchezaji huyo kufunga bao na kuwafuata, walianza kumshangilia kwa mayowe mengi.

Kama hiyo haikutosha, mara baada ya pambano hilo kumalizika, Ngasa alikwenda kuungana na wachezaji wenzake kushangilia ushindi, badala yake alikwenda tena kwenye jukwaa la mashabiki wa Yanga, ambao walizidi kumshangilia.

Mbali na kumshangilia, mashabiki hao wa tawi la Yanga Bomba, walimzawadia Ngasa jezi yenye rangi ya kijani na njano, ambayo aliipokea na kuivaa mara moja na kisha kutokomea nayo nje ya uwanja, akipitia mlango maalumu wa dharula, mahali linapoegeshwa gari la wagonjwa.

Wakati Ngasa akitokomea nje ya uwanja, wachezaji wenzake pamoja na viongozi waliunda duara uwanjani wakiomba dua na kumshukuru Mungu kwa kuweza kushinda pambano hilo.

Mmoja wa maofisa wa Azam, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, alikiri kuwa, uongozi umekerwa na kitendo hicho cha Ngasa na huenda ukamchukulia hatua za kinidhamu.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Ngasa tangu michuano ya Kombe la Kagame ilipoanza wiki mbili zilizopita.

Kocha Stewart Hall hakuwa anamchezesha kwa madai kwamba, alikuwa hajitumi mazoezini na kuonyesha dalili za kutaka kucheza.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya soka wamekielezea kitendo hicho cha Ngasa kuwa kilikuwa ishara ya kumwonyesha Stewart kwamba uwezo wake bado upo juu.

Wengine wamekitafsiri kuwa, kilikuwa ishara ya kuitaka Azam imruhusu arejee Yanga, timu aliyoichezea kwa miaka kadhaa kabla ya kununuliwa na wana rambaramba kwa kitita cha zaidi ya sh. milioni 50.

RAIS JAKAYA KIKWETE AZINDUA KARAKANA (HANGA) YA NDEGE ZA SHIRIKA LA NDEGE LA PRECISION AIR


Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la ndege la Precision Air Bw. Michael Shirima akimkabidhi zawadi Mh Rais Dk. Jakaya Kikwete mara baada ya kuzinduz rasmi karakana na ndege za shirika hili (Hanga) kwenye uwanja wa ndege wa Mwalimu J.K.Nyerere leo jijini Dar es salaam, Karakana hiyo itakuwa na ikihudumia ndege za shirika hilo la mashirika mengine pia lakini pia itapokea wanafunzi walio kwenye mafunzo ya Uinjini wa ndege kutoka katika vuo vya ndani.


Rais Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe pamoja na wakuu mbalimbali wa shirika la ndege la Precision Air na wafanyakazi wa shirika hilo mara baada ya uzinduzi wa (Hanga) hiyo.

Rais Jakaya Kikwete akiweka mkasi mara baada ya kukata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Karakana na ndege za shirika la ndege la Precision Air leo kwenye uwanja wa ndege wa Mwalimu J.K.Nyerere jijini Dar es salaam kulia ni Bw Bw. Michael Shirima
Wafayakazi wa Precision Air wakiwa katika hafla hiyo ya uzinduzi.
Hili ndilo jengo la Karakana yenyewe (Hanga) kama linavoonekana



WATAKIWA KUWAJENGEA UWEZO WASICHANA

Na Mwandishi Maalum, Abuja

Wake wa Marais wa Afrika wametakiwa kuwajengea uwezo wanawake na watoto wa kike kwa kuhakikisha kuwa wanapata elimu ya kutosha ambayo itawawezesha kushika nafasi za juu katika uongozi na hivyo kupunguza ukatilia wa kijinsia dhidi yao.
Wito huo umetolewa jana na Rais wa Malawi Joyce Banda wakati akifungua mkutano wa saba wa wake wa marais wa Afrika uliozungumzia masuala ya amani barani Afrika uliofanyika mjini Abuja nchini Nigeria.
Rais Banda alisema kuwa ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ni matokeo ya kukosekana kwa elimu na amani katika nchi, jambo la muhimu ni kuwajengea uwezo wa kielimu na kiuchumi ili waweze kutambua haki zao za msingi.
“Kila mmoja wenu katika nchi yake anafanya kazi ya kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanapata elimu lakini hiyo pekee haitoshi bali mnatakiwa kuweka nguvu zaidi katika kuimarisha amani ndani ya nchi zenu kwani bila nchi kuwa na amani ukatili wa kijinsia utazidi kuendelea”, alisema Banda. Rais Banda aliendelea kusema kuwa wanawake wapewe nafasi katika usuluhishi na utatuzi wa migogoro wasiachwe wanaume peke yao kufanya kazi hiyo kwani nchi ikikosa amani waathirika wakuu ni wanawake na watoto ambao wengi wao wanauawa na wengine wanafanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwemo kubakwa.

Kwa upande wake Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan alisema kuwa nchi za Afrika lazima zifanye jitihada kubwa za kuondoa vikwazo ambavyo vinawazuia wanawake na watoto wa kike kushindwa kutimiza ndoto zao.
Wanawake wanatakiwa kutobaguliwa bali kupewa fursa sawa ya kushiriki katika elimu, siasa na uchumi. Aliendelea kusema kuwa usawa wa kijinsia unatakiwa kuwepo barani Afrika kwa kuunga mkono na kutengeneza mazingira ya kuwainua wanawake kiuchumi na kuhakikisha kuwa wanawake hao wanaishi mazingira salama.

Mkutano huo wa siku mbili unahudhuriwa na wake wa marais kutoka nchi mbalimbali Barani Afrika akiwemo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete.

JOSE CHAMELEONE AVAMIA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI UGANDA


Chameleone akiteta jambo na mmoja kati ya wafuasi wake nje ya ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Uganda.

Chameleone akipiga gita huku wafuasi wake wakiwa wamebeba mabango nje ya ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Uganda.

Polisi wa Uganda wakimtuliza Chameleone na wafuasi wake wakati walipofanya maandamano ya amani nje ya ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Uganda.


Mwanamuziki Jose Chameleone na wafuasi wake jana asubuhi walivamia kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Uganda na kushinikiza arejeshewe pasi yake ya kusafiria.

Jose, mmoja wa wanamuziki tajiri katika nchi za ukanda wa Afrika, aliendesha gari lake aina ya Range Rover Sport na kuliegesha karibu na ubalozi huo.

Mwanamuziki huyo pamoja na wafuasi wake walikuwa na mabango yaliyokuwa na maandishi yanayomtaka mfanyabiashara Eric Shigongo arejeshe hati yake ya kusafiria.

Jose aliweka kambi kwa muda nje ya ubalozi huo na kupiga gita lake huku akiimba nyimbo mbali mbali. Wafuasi wake walikuwa wamebeba mabango ya kupinga kitendo cha Shigongo kumnyang'anya hati yake ya kusafiria.

Baadhi ya mabango yalisomeka: 'Shigongo upo juu ya sheria?' , 'Tafadhali Tanzania nisaidieni', 'Nahitaji nirejeshewe hati yangu ya kusafiria'.

Shigongo ndiye aliyemwalika Jose kufanya onyesho wakati wa tamasha la matumaini lililofanyika hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Jose alifanya onyesho wakati wa tamasha hilo, lakini inasemekana kuwa Shigongo alikataa kumlipa pesa zake kwa madai kuwa, tayari alishamlipa meneja wa mwanamuziki huyo, aliyejulikana kwa jina la George.

Imeelezwa kuwa, Shigongo alimlipa George dola 3,500 za Marekani kwa ajili ya Jose kufanya onyesho hilo, lakini mwanamuziki huyo alikana kumtambua meneja huyo.

Jose alifanikiwa kuondoka nchini baada ya kupewa hati ya muda ya kusafiria katika ofisi za ubalozi wa Uganda hapa nchini.

Uamuzi wa Jose kuvamia ubalozi wa Tanzania nchini Uganda, ulifanyika saa chache baada ya kutoka kufanya onyesho kwenye Uwanja wa Amahoro mjini Kigali, Rwanda.

Maofisa kadhaa wa polisi wa Uganda walifika kwenye ofisi za ubalozi huo wakiwa na gari yenye namba UP-2627 kwa ajili ya kulinda usalama.

Hata hivyo, Jose aliwaeleza polisi hao kuwa, yeye na wenzake waliamua kufanya maandamano ya amani kwa lengo la kushinikiza arejeshewe hati yake ya kusafiria.

Baadaye, nyota huyo wa muziki alikutana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Uganda, ambaye alimuahidi kwamba atalifanyia kazi suala lake kwa kuwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi la Tanzania, Inspekta Saidi Mwema.

No comments: