Monday, July 30, 2012

Uzalendo waubwaga ufisadi bungeni

*Ulaji wa kutisha TANESCO hadharani

* ‘Sinema’ ya mabosi, wabunge wanavyoshiriki kuhujumu yaanikwa

* Kamati ya Nishati na Madini yavunjwa, uchunguzi kuanza

* Zimwi la kula mlungula lawatesa wabunge, SMS za vitisho zawa gumzo

MCHEZO mchafu kuhusiana na vitendo vya ufisadi katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) umeibuka bungeni ambapo baadhi yao wamebainika kujinufaisha
binafsi.

Wakati uoza huo ukianikwa, zimwi la baadhi ya wabunge kupokea mlungula limeendelea kuwatesa kiasi cha kupendekezwa kamati za bunge zivunjwe na kuundwa
upya, pendekezo ambalo limenza kufanyiwa kazi kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuvunjwa na Spika Anne Makinda, huku uchunguzi ukiendelea.

ULAJI TANESCO

Akijibu hoja za wabunge wakati wa kuhitimisha Bajeti ya Wizara ya Madini na Nishati, Waziri Profesa Sospeter Muhongo, alisema anayetetea TANESCO, anatetea
upuuzi.

Muhongo alisema utendaji wa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Injini William Mhando, tangu kuteuliwa kwake haukidhi matakwa ya kanuni za utumishi katika uendeshaji
wa shirika hilo.

Alisema uamuzi wa kumsimamisha mkurugenzi huyo ulifikiwa katika kikao cha Bodi ya Shirika hilo kilichofanyika Julai 13 mwaka huu, na kwa mujibu wa maelezo
ya bodi alisimamishwa kwa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Alisema Bodi ya TANESCO imemuomba Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa baadhi ya tuhuma zilizodhihirika.

Profesa Muhongo alisema moja ya sababu za ukaguzi huo ni kutokana na Mhando kukiuka maadili ya utumishi wa umma kwa kuingia mkataba na kampuni ambayo
mwenyewe na mke wake Eva, wana maslahi nayo.

Muhongo alisema hata wakurugenzi wengine wa kampuni hiyo ni watoto wake ambao ni Fred Mhando na Veronica Mhando.

Waziri alisema kampuni yao, Santa Clara Supplies Co Limited, ilianza kazi Aprili mwaka huu ikiwa na mtaji wa sh. milioni 10, na baadae ilipata mkataba wa thamani ya
zaidi ya sh. milioni 800.

Pia Waziri Muhongo alisema chini ya uongozi wa Injia Mhando, kulikuwa na manunuzi mengine yasiyokidhi vigezo.

‘’Kashfa zilizotolewa dhidi yake ni nyingi na moja iliyonifurahisha sana ni kwamba waliagiza 'spea parts' (vipuri) kutoka Uingereza, wakalipia pauni 50,000 (sh. milioni 120) kumbe ilikuwa sanduku la misumari," alisema.

Aliongeza kuwa: "Waheshimiwa wabunge, kuna wabunge wengine ambao siwezi kuwataja hapana wanafanya biashara na TANESCO."

"Tunao ushahidi usio na shaka kwa baadhi ya wabunge, hasa walio katika Kamati ya Nishati na Madini, kwamba wanafanya biashara na TANESCO, ni kazi ngumu kweli
kweli," aliongeza kusema na kuwa baadhi ya wabunge wameingia mkataba wa biashara ya matairi na TANESCO kwa kuuziana matairi yasiyokuwa na ubora.

"Naomba niwashauri wabunge waache kufanya biashara na TANESCO ili wawe na uhuru wa kuisimamia na kuiwajibisha,’’ alisema Profesa Muhongo.

Alisema kwa sasa hakuna haja ya kuundwa kwa Tume, kwani tayari CAG ameshapewa jukumu hilo, hivyo ni bora mjadala kuhusu TANESCO ufungwe na kuendelea na
mambo mengine.

WABUNGE NA MLUNGULA

Katika hatua nyingine, suala la baadhi ya wabunge kupokea mlungula ili kufanikisha ‘miradi’ ya watu wengine kwa maslahi yao binafsi lilitawala kikao cha Bunge.

Baadhi ya wabunge (majina tunayo) ilidaiwa walipokea fedha kutoka kwa wafanyabiashara wa mafuta na watu wengine, ili kujaribu kuzuia utendaji wa maofisa wa
Wizara ya Nishati na Madini.

Habari za nje ya bunge zilisema baadhi ya wabunge hao walipewa kuanzia dola za Marekani 10,000 (sh. milioni 16) na wengine zaidi ya hapo kutokana na uwezo wao
wa ushawishi.

Wabunge hao baada ya kupewa fedha hizo, wanadai walikuwa wakipita kwa wabunge wenzao na kuwashawishi kukataa kuipitisha bajeti ya wizara hiyo kwa ahadi
kuwa watawapatia fedha.

Joseph Selasini (Rombo–CHADEMA), juzi wakati akichangia alikiri kuwepo kwa baadhi ya wabunge wanaoshawishi wenzao kupinga makadirio hayo kwa ahadi ya
kuwapa fedha. Hoja kama hiyo ilitolewa na wabunge wengi waliochangia.

Kwa upande wake, Ally Kessy (Nkasi –CCM) akiwa nje ya bunge, alitaja majina ya baadhi ya wabunge kuwa walipokea mlungula.

Wabunge hao (majina tunayahifadhi) ni wawili wa viti maalumu na mmoja kutoka moja ya majimbo ya Kanda ya Kskazini. Mbunge mwingine anayetajwa kwenye duru
hizo ni mwenyekiti wa moja ya kamati za bunge.

UJUMBE WA VITISHO

MZALENDO ilifanikiwa kunasa moja ya vitisho vilivyotumwa kwa ujumbe mfupi wa simu (SMS) ambao ulitumwa kwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakim Maswi.

Ujumbe huo unasomeka: "Maswi sijawahi kugombana na wewe kwa kuwa nakuheshimu sana, tuhuma ambazo wewe na waziri wako mnatoa dhidi yangu ni uongo, uzushi na wa kupikwa. Mwambie waziri wako na wewe binafsi, sijawahi kushindwa vita ya kulinda CREDIBILITY (hadhi) yangu. Sipendi ujinga hata kidogo, mimi nina uhuru wa kusema ninachoamini, sina bei. Tupambane tu tuone nani ataumia.’’

Ujumbe huo unadaiwa kutumwa na mmoja wa wabunge kabla ya Wizara ya Nishati na Madini haijawasilisha makadirio yake.

KAMATI YA BUNGE YAVUNJWA

Spika Anne Makinda ametangaza kuvunjwa kwa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, kutokana na baadhi ya wajumbe wake kuhusishwa na vitendo vinavyokwenda
kinyume na maadili na taratibu za Bunge.

Alitangaza uamuzi huo baada ya kupitishwa kwa makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini, ambayo yaliibua kashfa nzito dhidi ya baadhi ya wabunge katika mjadala wake.

Spika alisema kuna baadhi ya wabunge wamekuwa wakitokwa jasho na kuzungumza kwa nguvu wakati wa kujadili mambo, lakini kumbe wanafanya kazi za baadhi ya
watu walio nyuma ya pazia kwa maslahi binafsi.

Alisema wabunge hawawezi kusimamia serikali ilihali wenyewe wanapitapita na kuomba ‘kitu kidogo’.

Kutokana na hali hiyo, alitangaza kuivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, na kuwa madai ya wabunge kwenda kinyume na maadili yatafikishwa kwenye Kamati
ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo itatoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa wahusika.

Alisema baada ya kamati hiyo kumaliza uchunguzi wake, majina ya wahusika yatawekwa hadharani na umma utafahamishwa. Hata hivyo, hakutoa muda wa kamati
hiyo kufanya kazi.

Wajumbe wa kamati hiyo iliyovunjwa ni Selemani Zedi (Mwenyekiti), Diana Chilolo (Makamu Mwenyekiti), Yussuf Haji Khamis, Catherine Magige, Abia Nyabakari, Charles
Mwijage, Yusuph Nassir, Christopher Ole Sendeka, Festus Limbu, Shafin Sumar, Injinia Athuman Mfutakamba, Lucy Mayenga, Josephin Chagulla, Mwanamrisho
Taratibu Abama, David Silinde, Suleiman Nchambis Suleiman, Ali Mbarouk Salim, Vicky Kamata, Kisyeri Chambiri, Sarah Msafiri, Munde Tambwe, John Mnyika
(Waziri Kivuli) na Mariam Kisangi.

Awali, Vita Kawawa (Namtumbo – CCM) alipendekeza Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ivunjwe kwa mujibu wa kanuni ya 53 (2) inayompa mamlaka Spika kufanya
hivyo.

Alisema hatua hiyo ichukuliwe kwa kuwa wabunge wanaodaiwa kula ‘mlungula’ wamo ndani ya kamati hiyo, na kwa sasa bunge halina imani na kamati hiyo kutokana
na kutumiwa na mafisadi.

Mbunge huyo pia alitaka wachunguzwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na baadae wachukuliwe hatua. Aliwasilisha hoja binafsi kutaka hatua
zichukuliwe dhidi ya wabunge waliotuhumiwa kupokea ‘kitu kidogo’ na hivyo kwenda kinyume na maadili.

Kwa upande wake, Profesa Muhongo alisema Bodi ya TANESCO inapaswa kuvunjwa kutokana na baadhi ya wajumbe wake kuwa na maslahi binafsi katika TANESCO.

Alifafanua kuwa baada ya kuvunjwa kwa bodi hiyo na Rais kufanya uteuzi wa mwenyekiti, licha ya kupewa mamlaka ya kuteua wajumbe wengine wa bodi kisheria,
atatangaza nafasi hiyo kwenye vyombo vya habari ili wananchi wenye uwezo wajitokeze kuwania.

WEZI WA UMEME

Katika hatua nyingine, Waziri Muhongo aliwataja baadhi ya wateja wa TANESCO ambao wamekutwa wakiiba umeme.

Aliwataja wateja hao na thamani ya umeme waliokutwa wakiiba kuwa ni St. Mary’s International School inayomilikiwa na Mbunge wa Viti Maalum, Mchungaji Getrude
Rwakatare, ambayo imekutwa ikiiba umeme wa sh. milioni 10.5.

Wengine ni Acces Bank katika tawi lake lililopo eneo la Matumbi, Tabata, ambao walikutwa wakiiba umeme wa sh. milioni 13.8 na Philipo Gunda, mmiliki wa hoteli ya
Akubu Paradise iliyopo eneo la Kariakoo (sh. milioni 25.3) na Shree Sign sh. milioni 8.1.

Kwa mujibu wa Waziri Muhongo, msako dhidi ya wezi wa umeme unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini, na watakaobainika sheria itachukua
mkondo wake.

MICHANGO YA WABUNGE

Wakichangia hoja ya makadirio na matumizi ya wizara hiyo, wabunge waliendelea kuwakalia kooni wabunge waliokula `mlungula’ wazomewe, na bunge liwasusie
michango yao kwenye vyombo.

Subira Mgalu (Viti Maalumu - CCM) aliwaonya wabunge na kuwataka waache kuwa mawakala wa mafisadi.

“Hatuwezi kuwavumilia, mmeweka mbele maslahi yenu, mmetudhalilisha, naomba wabunge tupitishe azimio tuwasusie michango yao, wakichangia bungeni na kwenye
vyama tutawazomea,” alisema.

Mbunge huyo alivishukia vyombo vya habari vilivyotumika kupotosha umma kwa kuandika habari za wizara kudaiwa kukiuka kanuni bila kueleza upande wa pili
unasema nini, na kuwa tabia hiyo ya waandishi wasiofuata maadili inapaswa kukomeshwa na waandishi waache kutumiwa.

Kwa upande wake, mbunge wa Maswa Mashariki (CHADEMA), John Shibuda, alitaka wabunge waliokula ‘mlungula’ watajwe ili watu waepuke kushutumiana kwa hisia.

Alisema wabunge hao wanaotetea ufisadi ni sawa na watumishi wanaolihujumu TANESCO ambao aliwafananisha na kunguru asiyefugika.

Shibuda aliwapongeza viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini na kuwaita 'ni watu waliokuja na utukufu', na kuwaasa wawe makini wasiondolewe udhu.

Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige, alisema mtindo wa wabunge kutetea ufisadi umeanza siku nyingi na kuwa watu wakikosa zabuni ama jambo fulani, wanawatumia
wabunge ambao wanakwenda kupaza sauti bungeni kuwatetea.

Maige ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii hadi Juni mwaka huu, alinukuu maandiko matakatifu katika Kitabu cha Wafalme, usemao 'Wataumbuka mmoja baada ya mwingine' akilinganisha na wabunge waliohongwa.

Mbunge mwingine, Said Mussa Zuberi (Fuoni-CCM) alitaka wananchi wapendekeze mabadiliko ya sheria katika mchakato wa kukusanya maoni ya katiba unaoendele ili
itungwe sheria itakayowezesha mafisadi kupigwa risasi.

“Wakati wa Mwalimu Julius Nyerere watu walikuwa wakiambiwa wanasikia na kujirekebisha, lakini sasa hawasikii, hivyo ni afadhali wapigwe risasi na walipie
gharama za risasi na watakaofanya kazi ya kuwaua,” alisema.

Alisema afadhali wauawe mafisadi wasiozidi 200 ili kunusuru maefu ya watu ambao wangine wamepoteza maisha kutokana na mgao feki wa umeme.

“Umeme unapozimwa watu waliolazwa hospitali, wanaopumua kwa mashine, dawa zinaharibika na wakati mwingine zinatumiwa kutibu watu kwa mashaka na kuleta
madhara, ni kheri wauawe kisailensa kama walivyohongwa kisailensa,” alisema.

Kwa upende wake Prudensiana Kikwembe wa CCM, alisema wabunge wamesahau majukumu yao, wanakula rushwa na kugeuka kuwa Yuda aliyemsaliti Yesu na hao
wamewasiliti wananchi na serikali.

“Hawa waliokula rushwa nafsi zao sasa zinawasuta, watawezaje kukemea rushwa wakati wenyewe ndio vinara," alisema.

Bunge jana liliidhinisha makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini ya sh. bilioni 641.

CHANZO GAZETI LA MZALENDO JULAI 29-AGOSTI 4, 2012

No comments: