Tunalilia katiba mpya
wakati iliyopo hatuijui
Na Lilian Timbuka
TANGU mwishoni mwa mwaka jana, Watanzania wamefungua ukurasa mpya wa kutaka mabadiliko katika mfumo wa uongozi wa kuwa na katiba mpya.
Baada ya vuguvugu la kudai katiba mpya kushika kasi, siku chache baadaye, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, aliahidi kuwasilisha madai hayo ya wananchi kuhusu Katiba mpya kwa Rais.
"Nitamshauri Rais na nitaweka nguvu zangu huko, watu wasifikiri kuwa serikali inaona kama madai ya katiba mpya si ya msingi,”alisema Pinda.
Baada ya siku kadhaa kupita, Rais Jakaya Kikwete alitoa kauli ambayo iliungana na ile ya Waziri Mkuu pale alipotangaza kuanza mchakato wa kuundwa kwa Tume itakayosimamia suala hilo na hatimaye kuiteua na tayari imeanza kazi.
Ingawa karibu kila Mtanzania hivi sasa anazungumza na kushinikiza kuandikwa kwa katiba hiyo mpya, binafsi nimekuwa najiuliza je ni Watanzania wangapi ambao wanaelewa kile kilichomo ndani ya katiba tunayoitumia hivi sasa?
Ni wazi kuwa kiwango cha uelewa wa wananchi kuhusu katiba iliyopo hivi sasa ni mdogo, hilo tukubali - tukatae.
Lazima tulichukulie hili pia kama changamoto ya msingi, wakati tunapoingia katika mchakato huo alioutangaza Rais Kikwete.
Na ili tuweze kujenga mazingira ambayo yataendana na kauli ya Rais Kikwete ya kutafuta maoni kutoka kwa wananchi, basi kazi ya ziada lazima ifanyike na ilipaswa kufanyika muida mrefu, ingawa hatujachelewa.
Na hili linatakiwa kufanywa na kuchukuliwa kwa uzito wa aina yake na wanasiasa, wanaharakati, asasi za kiraia na zile za kiserikali, ili kutafuta namna nzuri ya kuwaelewesha wananchi juu ya katiba ya sasa, upungufu wake na jinsi taifa linavyoendelea kunufaika nayo na kuathiriwa nayo pia.
Wananchi pia waelezwe ni kwa namna gani, uandishi wa katiba mpya hautatoa mwanya kwa kundi fulani la watu kupenyeza na kuweka vipengele ambavyo kwa namna yoyote vitalisaidia kupata maslahi binafsi.
Hoja hiyo inatokana na ukweli kuwa, wakati Katiba ya sasa ikiandikwa, chini ya uongozi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, maadili ya viongozi wa umma yalikuwa ya kiwango cha juu ikilinganishwa na sasa.
Nasema hivyo kwa sababu, kuna baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wajanja wajanja, wanaongoza kwa kupindisha kile ambacho Taifa linakihitaji kwa watu wake.
Uandikwaji wa katiba mpya unapaswa kufanywa kwa umakini wa hali ya juu, kwani unaweza kuharibu na kubomoa kabisa misingi tuliyojiwekea tangu uhuru, kama itaonekana kulibeba kundi moja na mengine kuachwa nje.
Ninaona hili ni jukumu lingine linalotakiwa kutekelezwa hususani na wadau ambao wanaona ni vyema kutekelezwa kwa kilio hicho cha kuandikwa katiba mpya.
Hata hivyo, umakini unatakiwa katika utekelezaji wa uandikwaji wa katiba hiyo. Haitakuwa busara kuyaacha yale ambayo yamo katika katiba ya sasa yalionekana kukidhi haja za Watanzania.
Kwani kutaka kuandikwa upya kwa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha yaliyomo kwenye sasa yanatekelezwa.
Mathalan, katika eneo la umiliki wa ardhi. Watanzania wanafahamu kuwa ni kinyume cha katiba kwa raia wa kigeni kumiliki ardhi.
Ingawa sheria ya uwekezaji inaruhusu mwekezaji kumiliki ardhi baada ya kufuata taratibu zilizowekwa, ikiwemo ya kupata kibali kutoka Kituo Cha Uwekezaji cha Taifa (TIC) kwa kuwa na mbia mzalendo, kuna wawekezaji wanaomilikishwa ardhi bila kuzingatia taratibu hizo.
Huu ni moja tu ya mfano wa mambo ambao watanzania hawahitaji uwepo wa Katiba mpya ndipo yatekelezwe.
Ni wazi kuwa, mabadiliko haya ambayo tunayadai, hata kama yatakuja lakini tukashindwa kubadilika katika utendaji wetu, sijui kama tutakuwa tumekidhi kile kinachokusudiwa.
Mabadiliko haya hata kama yatakuja kwa sura nyingine, kama hayatatekelezwa itakuwa ni kazi bure.
Ndiyo maana ninajiuliza tunataka katiba mpya sawa, je ni Watanzania wangapi ambao wanayajua upungufu uliomo katika katika ya sasa?
Je wanaijua vyema katiba ya sasa? Haya kazi kwetu kusuka ama kunyoa maana Rais karidhia, tume imeundwa na inafanya kazi, tuigie uwanjani tuicheze ngoma.
No comments:
Post a Comment