kumbeba bosi TANESCO
*Kukwamisha bajeti Nishani na Madini
*Mbatia amkomalia Injinia Mhando
*Bodi ya TANESCO nayo kitanzini
MKAKATI unaofanywa na baadhi ya wabunge kuendesha kampeni za chini kwa chini, zenye lengo la kumtetea aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Injinia William Mhando (pichani), umebainika.
Wabunge hao wanaoshutumiwa kuwa, huenda walikuwa wakinufaika na matatizo na vitendo vya ubadhirifu ndani ya TANESCO, wanadaiwa kufanya kampeni chafu kwa lengo la kukwamisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini, inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni leo.
Kutokana na kubainika kwa mkakati huo, wabunge hao wametakiwa kuacha kutetea vitendo vya kifisadi vinavyofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali na mashirika yake, bali waungane na wengine katika kusimamia maslahi ya taifa.
Pia wametakiwa kuwaunga mkono viongozi wanaochukua hatua za kupambana na ufisadi.
Mwenyekiti wa NCCR -Mageuzi na mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, alisema madudu na wizi uliojitokeza TANESCO haupaswi kufumbiwa macho.
Ameitaka serikali kuivunja Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, akidai kuna baadhi ya wajumbe wamekuwa wakishiriki kufanya hujuma ndani ya shirika hilo.
“Kitendo cha kuwepo wabunge ndani ya bodi ya TANESCO ni changamoto kwa kuwa kuna wengine wameonja asali inayotokana na ubadhirifu, jambo ambalo ni hatari kwa maslahi ya taifa," alisema.
Mbatia akizungumzia mkakati wa baadhi ya wabunge na watendaji wengine kumtetea Injinia Mhando, alisema ni watu ambao ‘wamevuta’ na kwamba, hawana budi kufunika kombe ili mwanaharamu apite kwa kusimamia haki, sheria na maslahi ya nchi kwanza.
Akionyesha kukerwa na mkakati huo, Mbatia alisema Bunge litatenda haki kwa kuvunja mtandao wa wizi na ujambazi ndani ya TANESCO na si kutetea kikundi cha watu wachache wanaolitafuna shirika hilo na kutaka life kama ilivyokuwa kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATC).
“Tuna taarifa kuna wabunge wanapita na kuwaomba wenzetu wengine kwa lengo la kumtetea Mhando na kampuni za mafuta, huku wakimtuhumu Katibu Mkuu wa Nishati na Madini Eliakim Maswi, kuwa amevunja kanuni kwa kuipa zabuni kampuni ya Puma Energy Tanzania Ltd kuuza mafuta kwa TANESCO.
“Hata Kamati ya Nishati na Madini imekosa uhalali wake, kwani baadhi yao wanashiriki kushawishi wabunge wamtetee mkurugenzi huyo. Hii ni aibu, ni lazima tufanye kazi iliyotuleta bungeni na si vinginevyo,’’ alisema.
Mbatia alitumia fursa hiyo kuweka hadharani mkataba mbovu wa ununuzi wa vifaa vya ofisi, ambao alidai ulitiwa saini katika mazingira yenye utata kati ya kigogo huyo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Santa Clara Supplies Co Ltd, ambaye ni mkewe.
Alisema katika mkataba huo, Injinia Mhando alifahamu kuwa mtaji wa kampuni hiyo ulikuwa sh. milioni 10 lakini akapewa mkataba wa sh. milioni 884.
“Nashangaa baadhi yetu wabunge wako mstari wa mbele kumtetea Mhando wakati amefanya ufisadi bila aibu, anatia saini mkataba wa mamilioni na mkewe kwa kutumia fedha za umma,” alisema.
Mbatia alisema kampeni nyingine ya chini kwa chini inayoendelea miongoni mwa wabunge ni ya kutaka kuzitetea kampuni za mafuta zilizotoswa katika zabuni ya kuuza mafuta mazito kwa mitambo ya IPTL, ambapo kuna wajumbe wa bodi ya shirika hilo wanashiriki.
Akifafanua kuhusu mkataba huo, alisema Kanuni ya 42 ya Ununuzi wa Umma ya 2005 inampa mamlaka katibu mkuu wa wizara kufanya uamuzi kama ataona inafaa kwa maslahi ya taifa.
“Kifungu cha 42 kimempa mamlaka na hata ikiangaliwa tofauti ya bei kati ya sh. 1,460 na sh. 1,800 iliyotolewa na kampuni zingine za mafuta, kwa mkataba huu serikali itaokoa mabilioni ya shilingi kila mwezi, hivyo kupunguza machungu kwa Watanzania.
“Kama Maswi angekubali kufuata matakwa ya mtandao huu wa wezi, basi serikali ingepoteza zaidi ya sh. bilioni sita kwa mwezi," alisema.
Hivi karibuni Injinia Mhando alinukuliwa na gazeti moja akisema hahusiki na kampuni ya Santa Clara Supplies Co Ltd, lakini alikiri kuwa inamilikiwa na mkewe.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wakiwemo wa upinzani wameweka bayana kuwa, wanaridhishwa na hatua zinazochukuliwa na serikali katika kusafisha uozo ndani ya TANESCO na kwamba, wanaunga mkono kutimuliwa kwa vigogo.
"Tunajua kila kitu na tutaiunga mkono serikali kwa hatua inazochukua. Leo bajeti itawasilishwa na tutaunga mkono kwa nguvu zote bila kujali itikadi na wale watakaotetea ufisadi tutawasema hadharani," alisema mbunge ambaye hakupenda kuandikwa jina gazetini.
Ruksa wenye uelewa
kujijazia fomu -NIDA
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imeruhusu wananchi wenye uelewa kujijazia fomu za usajili kwa ajili ya vitambulisho vya taifa.
Hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano katika vituo vya uandikishaji.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa NIDA, Dickson Maimu, katika mahojiano na kituo cha radio cha Clouds, jijini Dar es Salaam.
Alisema msongamano uliopo hivi sasa unasababishwa na uchache wa waandikishaji katika baadhi ya mitaa.
Maimu alisema NIDA imetoa ruhusa kwa wahudumu wa kazi hiyo, kutoa fomu kwa wananchi wenye uelewa ili wazijazie nyumbani na kuzirejesha katika vituo hivyo kwa lengo la kupunguza msongamano katika vituo.
Hata hivyo, alisema wanakabiliwa na changamoto ya muda, ambao alisema haijulikani ni muda gani ambapo watu hujitokeza kwa wingi katika vituo.
Alisema mkoa wa Dar es Salaam una vituo 452 vya kujisajili na wasajili waliopo ni 2,279.
Kufuatia uwingi wa watu, wanatarajia kuongeza wasajili katika vituo vyenye watu wengi.
“Mchakato huu ni mpya, naomba watu watoe ushirikiano, jukumu hili ni la kila mtu, sisi NIDA ni waratibu tu,” alisisitiza Mkurugenzi mtendaji huyo.
Akizungumzia suala la wanafunzi wa vyuo vikuu ambao mara nyingi huwa nje ya maeneo yao ya makazi, Maimu alisema unaandaliwa utaratibu maalumu kwa kushirikiana na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ili nao wapatiwe vitambulisho hivyo kwa wakati.
CHANZO: GAZETI LA UHURU
No comments:
Post a Comment