Tuesday, July 31, 2012

Viongozi CWT

watisha walimu

* Wahamasisha wanafunzi kufanya vurugu

* Mali na majengo ya serikali yaharibiwa

* Walimu wagawanyika, waendelea na kazi

* Serikali yatoa onyo kali, korti kuamua leo

* CWT wataka mazungumzo na Serikali


NA WAANDISHI, DAR NA MIKOANI

BAADHI ya walimu wamelalamikia vitendo vichafu vinavyofanywa na viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kuwatisha ili washiriki mgomo ulioanza jana.

Pia wamelalamikia viongozi hao kuwanyanyasa kwa kuwatumia vijana wa mitaani kuwavamia na kuwashambulia wanapowakuta wakiendelea kufundisha darasani, jambo linalowashushia hadhi mbele ya wanafunzi.

Hatua hiyo imetokana na walimu hao kuhudhuria kazini na kuendelea na kazi kama kawaida, lakini katika hali ya kushangaza walikuwa wakivamiwa na kushambuliwa ili waungane na wenzao kushiriki mgomo.

Licha ya kulalamikia unyama huo, ambao wamedai unaratibiwa na viongozi wa CWT, pia wamesema hawajapewa tamko rasmi la kushiriki mgomo huo, bali wanausikia kupitia vyombo vya habari.

Baadhi ya walimu wameutaka uongozi wa CWT kuwasomea taarifa ya mapato na matumizi ya chama hicho, badala ya kuhamasisha mgomo tu.

“Hatufahamu chochote kuhusu mgomo huu, tunasikia kwenye vyombo vya habari na hatujapata notisi ya kututaka kugoma kutoka CWT, sasa ni kwa nini wanatutisha bila sababu,” alihoji mwalimu ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini kwa sababu ya usalama wake.

Kutokana na hatua hiyo, serikali imetoa onyo kali kwa walimu wanaowanyanyasa, kuwapiga na kuwaharibia mali walimu ambao hawashiriki mgomo huo.

Imesema itawachukulia hatua kali walimu watakaobainika kuwashawishi wengine kuingia kwenye mgomo na wanaoharibu mali za serikali.

Akitoa tamko la serikali jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema wamepokea taarifa za watu kunyanyaswa, kupigwa na kuharibiwa mali zao na za serikali, kunakofanywa na baadhi ya walimu ambao wanataka kususia kufundisha.

Dk. Kawambwa alisema jambo la aina hiyo si sawa na si busara kwa mtu mwenye taaluma ya ualimu kujihusisha na vitendo vinavyokwenda kinyume cha sheria na utaratibu kwa maslahi binafsi.

Alisema serikali inawahakikishia walimu ambao hawajajihusisha na vitendo vya aina hiyo kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama vitawalinda.

"Tunapenda kuwatahadharisha wote wanaojihusisha na vitendo viovu kama kuwatishia wenzao, kuwapiga, kuwaharibia mali, kuwanyanyasa kwa sababu hawajaunga mkono mgomo huo serikali itachukua hatua kali dhidi yao," alisema.

Alisema serikali inatoa onyo kali kwa baadhi ya walimu, ambao wanashawishi na kuwatumia wanafunzi katika mgogoro huo na kwamba, jambo hilo si sawa wala haki.

Waziri alisema wanafunzi wasihusishwe wala kutumiwa, kwani mgogoro huo ni kati ya serikali na walimu.

"Napenda kutoa wito kwa wazazi na walezi kuwa wasikubali, wawazuie na wawakataze watoto wao kutumiwa au kuhusishwa kwenye mgogoro huo, ambao utawahatarishia usalama wao," alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Kawambwa, mapema jana asubuhi alifanya ziara ya kushitukiza kwenye baadhi ya shule mkoani Dar es Salaam, kujionea hali halisi, ambapo shule nyingi walimu walikuwa wanaendelea na kazi.

RC DAR ATOA ONYO

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Sadiki, amewaonya viongozi wa CWT kuacha kuwatisha walimu na ameagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuwakamata viongozi hao na kuwachukulia hatua.

Alisema walimu ambao walifika shuleni na kutia saini daftari la mahudhurio bila kufanya kazi, watachukuliwa hatua, ikiwemo ya kufukuzwa.

Sadiki aliwaonya baadhi ya walimu na viongozi wa CWT, akiwataka kuacha kuwashawishi na kuwatumia wanafunzi kama ngao ya mgomo huo.

Kuhusu mahudhurio ya walimu, alisema kwa shule za msingi walikuwa asilimia 85, huku wa sekondari walikuwa zaidi ya asilimia 96, wakiwemo baadhi ya viongozi wa CWT, licha ya kuwashawishi wenzao kugoma.

Katika Shule ya Msingi Olympio, walimu walisema hawakuingia kwenye mgomo, kwani hawana madai ya msingi yanayowafanya wagome.

Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina, walisema hawawezi kugoma kwa kusikia matangazo kupitia kwenye vyombo vya habari na kwamba, wanaweza kugoma kwa kupata notisi kutoka CWT.

Mmoja wa walimu hao alisema wote wapo kazini, kwani hawana madai yanayosababisha wagome. Alisema wanatambua kuwa, nyongeza ya mshahara ya asilimia 100 haiwezekani, hivyo wanaendelea kufundisha kama kawaida.

"Tulidhani CWT inalalamikia walimu kufundisha wanafunzi wengi, uhaba wa madawati na ukosefu wa vitendea kazi. Tunaona kwa hilo la nyongeza ya mshahara halijawa sababu ya kutufanya tugome," alisema.

Katika Shule ya Msingi Bunge, walimu walikuwa wakiendelea na kazi, huku Shule ya Msingi Gilman Rutihinda, iliyopo Kigogo, baadhi ya walimu walikuwa kwenye mgomo.

Shule ya Sekondari Manzese, walimu wengi walikuwa darasani wakiendelea na kazi, baadhi ya waliohojiwa walisema hawaoni sababu ya kugoma.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Uongozi ya Bunge, ilisema jana kuwa, suala la mgomo wa walimu haliwezi kujadiliwa bungeni kwa kuwa lipo mahakamani.

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema hayo alipojibu mwongozo ulioombwa na Yahaya Kassim Issa (Chwaka -CCM), aliyetaka bunge lijadili kwa dharura mgomo huo, kwa kuwa una athari kubwa kwa jamii.

VIONGOZI CWT MBARONI

Katika hatua nyingine, viongozi watano wa CWT wilayani Mpanda, mkoani Katavi, wanashikiliwa na polisi wakituhumiwa kuhamasisha mgomo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi,

Dhahiri Kidavashari, alisema walimu hao walikamatwa juzi jioni, walipokuwa wakipita mitaani na gari la matangazo kuhamasisha walimu kushiriki mgomo.

Katibu wa CWT Mkoa wa Rukwa na Katavi, Dweesdeur Zambi, aliwataja wanaoshikiliwa kuwa, Mwenyekiti wa CWT wilayani Mpanda, Isaack Martine, Katibu wake, Nicodemus Waivyala, Mwakilishi wa Wanawake, Asha Juma na walimu wengine wawili.

OFISI ZA SERIKALI, MALI ZAHARIBIWA

Kutokana na kampeni chafu zinazofanywa kukoleza mgomo wa walimu, kundi la vijana kwa kuwatumia wanafunzi kama ngao, limevamia ofisi za Halmashauri ya Mji wa Mbozi, mkoani Mbeya na kufanya uharibifu mkubwa.

Shughuli za kijamii zilisimama kwa muda kutokana na hofu ya kuzagaa kwa vurugu hizo, huku baadhi ya wafanyabiashara wakiporwa mali.

Vurugu hizo zilianza jana saa mbili asubuhi, wakati wanafunzi wa shule 14 za msingi walipokusanyika na kufanya maandamano hadi kituo cha polisi cha Tunduma, kabla ya kufika ofisi za halmashauri ya mji.

Ilielezwa awali wanafunzi hao walikwenda nyumbani kwa diwani wa kata ya Tunduma, Frank Mwakajoka (CHADEMA) na baada ya mazungumzo naye waliandamana hadi kituo cha polisi.

Katika tukio hilo, ofisi za halmashauri zilichomwa moto, huku kompyuta tano, pikipiki yenye namba ya usajili STK 6264 na nyaraka mbalimbali ziliibwa.

Milango ya ofisi zote, vioo vya magari ya kubebea taka aina FAW lenye namba ya usajili SM 8726, na gari dogo aina ya Nissan lenye namba SM 2858, yalivunjwa na kuharibiwa.

Mkurugenzi wa halmashauri, Aidan Mwanshiga, alisema ni mapema kuelezea uharibifu huo, huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Athumani Diwani, akisema tukio hilo haliwezi kuvumiliwa.

Alisema maandamano ya wanafunzi hayawezi kusababisha kuvunjwa ofisi za serikali na kufanyika wizi, bali kuna watu wametumia mwanya huo ili kupora.

SHULE ZAFUNGWA KUFULI

Baadhi ya shule wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma, zimefungwa kwa makufuli na walimu kuwarudisha wanafunzi nyumbani, huku shule zingine zikiendelea na ufundishaji kama kawaida.

Shule chache jana ziliwarejesha wanafunzi nyumbani, huku zingine nyingi walimu wakiendelea na kazi.

Licha ya CWT kutangaza mgomo huo, walimu katika shule mbalimbali za msingi na sekondari mkoani Kilimanjaro waliendelea na kazi.

Baadhi ya shule za msingi na sekondari katika wilaya za Mwanga, Rombo, Moshi na Hai, wanafunzi walikuwa wakiendelea na masomo kama kawaida.

WANAFUNZI WAVAMIA OFISI

Ofisi za serikali katika Manispaa ya Mtwara jana zilivamiwa na kundi la wanafunzi walioandamana.

Hata hivyo, walinzi wa ofisi hizo waliwazuia kuingia ndani, hivyo kuishia kwenye uzio.

Wanafunzi hao walishinda nje ya uzio huo mchana kutwa wakiwa na vibao vilivyoandikwa 'Tunataka haki yetu'.

Katika hatua nyingine, walimu jijini Mwanza, walifika shuleni na baada ya kutia saini vitabu vya mahudhurio hawakuingia darasani, hivyo wanafunzi kuzagaa nje.

Sekondari na shule za msingi za Igoma, Nyakato, Pamba, Mkuyuni, Butimba, Nyanza, Mirongo na Buhongwa, wanafunzi walikuwa nje wakicheza, huku walimu wakiwa wamekaa na kupiga stori.

Mkoani Arusha, walimu wamegoma, ambapo wengi baada ya kutia saini vitabu vya mahudhurio waliondoka, huku wengine hawakufika kabisa kazini.

CWT WATAKA MAZUNGUMZO

Akizungumza jana kwa niaba ya Rais wa CWT, Gratian Mukoba, Katibu wa chama hicho, mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Mkaula, alisema wako tayari kuzungumza na serikali na kumaliza mgogoro huo.

Mkaula alisema mgomo upo kwa asilimia 85 na kwamba, shule nyingi za serikali na vyuo vya ualimu vimefungwa. Alisema wako tayari kusitisha mgomo iwapo serikali itatekeleza madai yao, yakiwemo ya nyongeza ya mshahara ya asilimia 100.

Katibu huyo alisema mgomo huo upo kisheria na kwamba, utaendelea mpaka watakapofikia makubaliano na serikali na kuyapatia ufumbuzi madai yao.

Wakati huo huo, baadhi ya walimu wa shule za msingi mjini Iringa, wameigeuzia kibao CWT wakipinga mgomo, badala yake wametaka waelezwe kwanza mapato na matumizi ya michango yao ya kila mwezi kwa chama hicho.

“Tunasikia kuna majengo ya walimu yanajengwa nchi nzima, makatibu wa CWT wananuliwa magari, sasa kuna mpango wa kuanzisha benki, lakini hatupewi taarifa ya mapato na matumizi.

“Hata magari waliyopewa makatibu hayana msaada kwa walimu, ambao ndio wenye mali hata kama wakiumwa,” alisema Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mtwivilla, Sidified Mapunda.

Alisema mgomo huo unawapa umaarufu viongozi wa chama hicho na hauna maana yoyote kwa walimu wa kawaida, kwa sababu utaratibu wa kuongeza mishahara ya walimu hauna tofauti na wa watumishi wengine wa umma.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Wilolesi, George Kameka, ambayo pia walimu wake wamesusia mgomo huo, alisema kabla ya kumgomea mwajiri, wanataka kufahamu mapato na matumizi ya chama hicho.

Alisema kuna taarifa zisizo rasmi kwamba CWT iko katika mstari wa mbele kudai maslahi ya walimu ili mishahara yao ikipandishwa na wao wapandishe michango.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chemichemi, Demetrius Mgohamwende, alisema walimu wote 20 wa shule hiyo wamegoma.

CHANZO GAZETI LA UHURU, JULAI 31, 2012

No comments: