Monday, August 6, 2012

Uozo Zimamoto

* Vigogo wajinufaisha kwa stika feki
* Aliyefanya madudu ahamishwa kituo


NA MWANDISHI WETU, MWANZA

SERIKALI inaibiwa mamilioni ya shilingi kutokana na uuzwaji wa stika feki za vifaa vya kuzimia moto kwenye magari, viwandani na ofisini, unaofanywa na baadhi ya vigogo wa Jeshi la Uokoaji na Zimamoto Tanzania, imefahamika.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, unaonyesha baadhi ya vigogo wa jeshi hilo makao makuu, jijini Dar es Salaam, wana mtandao wa kuuza stika hizo mikoani, ikiwemo Mwanza, Mara na Geita.

Kwa mujibu wa uchunguzi, vigogo hao wanashirikiana na watumishi wa jeshi hilo, wakiwemo maofisa kadhaa walioko kwenye mikoa hiyo.

Jijini Mwanza, uchunguzi unaonyesha stika hizo zimemwagwa na kuuzwa kwa wingi kwenye viwanda kadhaa, vikiwemo vya samaki na vinywaji na kwamba, mhusika mkuu wa biashara hiyo ni ofisa mmoja wa jeshi hilo.

Ofisa huyo anadaiwa alihusika katika biashara hiyo kwenye viwanda hivyo kabla ya kuhamishwa kituo cha kazi.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya jeshi hilo, mwishoni mwa wiki iliyopita, zilidai Machi, mwaka huu, ofisa huyo alibambwa na kitabu cha stika feki akiwa katika harakati ya kuziuza kwa wenye magari.

“Alitozwa faini ya sh. 800,000 na alizilipa pale pale,” kilidai chanzo chetu cha habari na kuhoji alizipata wapi fedha hizo, ambazo ni nyingi ikilinganishwa na kipato cha mtumishi huyo.

Habari kutoka kwa mtu aliye karibu na ofisa huyo zilisema fedha hizo alitumiwa na kigogo anayedaiwa kuendesha mtandao huo.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, mkoani Geita, stika hizo zimeuzwa katika migodi kupitia kwa ofisa (jina linahifadhiwa) anayefanya kazi katika mgodi wa Geita Gold Mine (GGM).

Mkoani Mara, uchunguzi unaonyesha zinasambazwa na ofisa wa jeshi hilo (jina tunalo) ambaye inadaiwa hutumiwa moja kwa moja na kigogo aliye makao makuu, Dar es Salaam.

Julai 18, mwaka huu, dereva wa idara hiyo makao makuu alikamatwa na kitabu cha stika feki akikisafirisha kwenda uwanja wa ndege kwa ajili ya kukisafirisha kwenda mkoani Mara, kupitia Mwanza.

“Dereva huyo alipobanwa alikiri kuwa katumwa na kigogo mmoja kukituma kitabu hicho kwenda kwa... mkoani Mara, kupitia Mwanza,” kilidai chanzo kingine kutoka idara hiyo mkoani humu.

Chanzo hicho kilidai bosi huyo alipopata taarifa za kukamatwa kwa dereva, aliwajia juu askari wa idara hiyo waliomkamata, huku akitamba hawana mamlaka ya kuhoji kitu kinachotumwa na bosi wao.

Mkuu wa Zimamoto jijini Mwanza, aliyejitambulisha kwa jina moja la Bulambo, hivi karibuni akizungumza kwa simu, alishindwa kukanusha tuhuma za kukamatwa kwa mtumishi huyo na kudai suala hilo hawezi kulizungumza kwenye simu hata kama lipo.

Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili, Naibu Kamishna wa Zimamoto Makao Makuu Dar es Salaam, aliyefahamika kwa jina moja la Shija, alikiri kuwepo kwa dosari kama hizo.

Alisema kutokana na kasoro mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza, waliamua kubadili utaratibu ambapo hivi sasa stika hizo zinasimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

"Hivi sasa sisi hatuhusiki tena na uuzaji wa stika kutokana na kasoro mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza, kazi hiyo hivi sasa inafanywa na TRA," alisema.

Hata hivyo, TRA inahusika na uuzaji wa stika kwa ajili ya vyombo vya moto pekee, wakati zingine kama vile za viwanda bado zinauzwa na jeshi hilo.

CHANZO GAZETI LA UHURU AGOST 6, 2012

No comments: