Monday, January 18, 2010

viongozi wa dini watishiwa maisha
Watu wasiojulikana wameanza kuwatisha baadhi ya viongozi wa dini waliohusika kuchunguza tuhuma za migodi hiyo.
Akithibitisha jambo hili, Mchungaji Magafu amesema, amepokea baadhi ya simu zikimtaka aache kusambaza mikanda ya filamu inayoonesha unnyama waliotendewa wananchi wanaoishi jirani na migodi hiyo.
“Bila aibu watu hawa nao wanajaribu kututisha sisi viongozi wa dini na wanataka eti hata filamu hizi zisitolewe. Sisi katika kufanya kazi ya Mungu, hatuogopi vitisho na afadhali kufa kwa kulinda kondoo wa Mungu kuliko kuishi”
Amesema tangu awali walipata vikwazo hata walipokuwa katika ziara hiyo, lakini hawakuvitilia maananani sana. “Lakini kadri siku zinavyoongezeka, hali inabadilika. Nataka niwambie, wasijaribu kututisha. Tunajua wanaofanya hivi wanataka kuwagopesha watu ili wasiseme na wao wapate nafasi ya kuendeleza ukatili wao kwa Watanzania.
Kadhalika, anasema” viongozi wa dini kwanza hawakuelewa sababu zilizowafanya baadhi ya viongozi wa Serikali kuficha ukweli wa kile kilichotokea katika mgodi huo na hata kuwatisha wale waliojaribu kueleza ukweli. Kwa hatua yao ya kutaka kututisha, sasa tumejua sababu yake wanataka kuficha uozo.
Mchungaji Magafu, amesema filamu zote mbili, ile ya Tarime na Shinyanga, zitasambazwa nchi nzima kwa watu wa kada mbalimbali ili watu wajue ukweli wote na wasikubali kudanganywa tena.
“Tunataka watu wajue kilichotokea na kinachoendelea kuwakuta watanzania wenzetu wa huko. Tunataka wajue namna baadhi ya wawekezaji wanavyokuja kuchota mali za Watanzania na kwenda kuzitumia nchini mwao”
Pamoja na kusambaza kwa filamu hizo, wameitaka serikali, kuwakamata na kuwashitaki viongozi wote waliohusika na unyama huu kama wanavyofanyiwa wahalifu wa kimataifa.
“Nabii Isaya alitabiri vema kabisa aliposema ..nchi yenu inaliwa na wageni mbele ya macho yenu, na hata kumbukumbu la Torati limesema litakuja taifa geni tusilojua ulimi wake, ambalo litachuma mali na kuteketeza mali zetu na watu wetu hadi tutakapoisha kabisa. Haya ndiyo tuliyoyaona huko Tarime na Sinyanga” anasema Mchungaji Magafu.
Anasema viongozi wa dini, wameshangazwa na ujasiri wa ajabu uliooneshwa na viongozi na wasomi waliopewa dhamana ya kulinda maisha ya watu na mali zao kwa kukosa huruma na kushirikiana na wawekezaji walio tayari kuangamiza maisha ya watu bila huruma.
“Kama wawekezaji hawa wanafikia hatua ya kumdanganya waziri, kwa kumtembeza katika maeneo mengine na kuficha kule maji yalikokuwa yanatiririka, kuna sababu gani ya kuwaamini tena wao na waliowasaidia? Anasema Mchungaji huyo akikumbushia tukio la Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Khamis Kagasheki, ambaye katika ziara ya kufuatialia tukio hilo, alioneshwa na uongozi wa Barick sehemu tofauti na kufichwa kule kulikokuwa kunatiririsha maji yenye kemikali zenye sumu hadi pale alipoelezwa ukweli na wenyeji na kujionea hali halisi.
Sakata la migodi hiyo, limevuma sana mapema mwaka jana kabla halijatulia kwa muda. KIONGOZI, litachapisha ripoti kamili ya kamati ya viongozi hao katika matoleo yake hajayo.

No comments: